UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO KUHUSU RIPOTI YA CAG 2019/2020

UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO KUHUSU RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA MWEZI JUNI 2020

Tunalipia Gharama za kuendesha Nchi Gizani

A: UTANGULIZI

Leo tarehe 11 Aprili, 2021 ni Mwaka mzima kamili tangu Chama chetu kifanye uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019. ACT Wazalendo, chama ambacho kimeendelea kujipambanua kama Chama mbadala na kinachozielekeza katika kujadili masuala makubwa ya kitaifa na kupendekeza suluhu yake kinaendeleza utamaduni wake wa kufanya uchambuzi katika mambo muhimu machache kutoka kwenye Ripoti ya CAG.

Kwa kuzingatia utamaduni wetu huo, na baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha Taarifa yake kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020; Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni.

Katika uchambuzi wetu wa mwaka uliopita, tuliona ni bora pia tufanye mapitio ya Taarifa za CAG kwa miaka yote mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano (2015/16 – 2018/19). Hivyo, tulifanya uchambuzi mtambuka tangu Serikali ya Rais John Magufuli ilipoingia madarakani hadi Mwaka 2020. Uchambuzi ule uliibua ukweli mmoja tu, kwamba Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni Miaka 5 ya kushindwa kazi, na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Na Ripoti ya CAG ya mwaka huu imethibitisha ukweli huu kwamba tumekuwa na miaka ya uholela mkubwa ambao umepelekea ubadhirifu mkubwa wa Fedha za Umma.

Kwa Mujibu sa ripoti hii ya CAG, thamani ya Jumla ya Hoja za Ukaguzi katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa ujumla wake ni Shilingi Trilioni 3.6 na Dola za Marekani Milioni 596. Hoja hizi za ukaguzi hazihusishi Hoja za madai ya Kodi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 360 na Dola za Marekani Milioni 181. Hoja hizi za Ukaguzi ni Uwiano wa 16% ya Bajeti nzima iliyotekelezwa na Serikali katika Mwaka wa Fedha wa 2019/2020.

Tunatarajia kuwa Mamlaka husika zitachukua hatua mahususi za kujibu hoja zote kwa mujibu wa sheria kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na hatimaye kusafisha Hesabu za Serikali. Hoja nyingi za ukaguzi zinajirudia rudia mwaka hadi mwaka, hivyo ni muhimu pia kwa Bunge kuhakikisha kuwa Katiba na Sheria zinaheshimiwa ili kuondoa hoja sugu.

Kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku za nyuma, uchambuzi wetu utajikita kwenye mambo makubwa Kumi (10) ambayo tunaona ni muhimu Watanzania kuyatambua na kuyatolea mapendekezo ili yaweze kuchukuliwa hatua. Hii haina maana kuwa mambo muhimu ni hayo kumi tu, la hasha.

Ripoti ya Mwaka huu ya CAG ina mambo lukuki na yenye masuala mazito sana kwa nchi yetu. Hakika Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ndugu Charles Kicheere amefanya kazi kubwa na kwa ujasiri mkubwa. Hoja tisa ambazo tumezifanyia uchambuzi kwa mwaka huu kama ifuatavyo;

 


1. Makusanyo ya Kodi Yapo Chini Sana

Uchambuzi wa ACT Wazalendo kwenye Ripoti ya CAG umebaini kwamba, uwezo wa Serikali kukusanya mapato kulinganisha na Pato la Taifa bado upo chini sana. Hii inapelekea Serikali kushindwa kutekeleza Bajeti na hivyo kuathiri utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Suala hili tumekuwa tunalizungumza kila mwaka tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie Madarakani.

Duniani kote ufanisi wa Taifa kukusanya kodi hupimwa kwa kutazama uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa thamani ya shughuli za uchumi katika nchi husika, yaani Tax/GDP Ratio kwa lugha ya kiuchumi.

Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015/16 Uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa Pato la Taifa ilikuwa ni 13.68%. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka Mitano, 2015/16 mpaka 2020/2021 uliweka lengo la Uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa Pato la Taifa kuwa 20% ifikapo mwaka 2020.

Kwa mujibu wa CAG katika Ripoti yake ya Mwaka 2019/2020, Uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa Pato la Taifa ulikuwa 12.1% tu ikiwa ni ongezeko dogo kutoka 11.6% mwaka 2018/19.

Uwiano wa Kodi kwa Pato la Taifa kwa miaka mitatu iliyopita ulikuwa kama ifuatavyo:
- 2017/18 ni 12.30%
- 2018/19 ni 11.60%
- 2019/2020 ni 12.10%

Hali hii inadhidhirisha kuwa licha ya kutumia nguvu kubwa katika Makusanyo ya Kodi bado Uchumi wetu hauzalishi kwa kiwango kinachotakiwa na kwamba tumeshindwa kufikia lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa kiasi kikubwa sana. Hili ni pungufu kubwa la ufanisi wa Serikali katika kuendesha uchumi wa Nchi yetu.

Tunarejea ushauri wetu wa kila mwaka kwamba Serikali ijielekeze kwenye kuongeza shughuli za uchumi wa Wananchi ili kuongeza kipato chao na hatimaye makusanyo ya Serikali. Serikali iongozwe na filosofia kuwa katika kila kampuni inayoanzishwa na kupata faida Serikali inapata 30% ya hiyo Faida. Vile vile katika kila ‘business transaction’ inayofanyika nchini Serikali inapata makusanyo yake. Ni faida kwa Serikali iwapo Biashara nyinyi zitaanzishwa na kukua kuliko kuua Biashara.

2. Madai ya Wazabuni dhidi ya Serikali yafikia Shilingi Trilioni 3.1

Uchambuzi wetu umebaini kwamba, mwaka 2019/2020 madai dhidi ya Serikali (accumulated libalities OR Payables) yalikuwa ya Jumla ya Shilingi Trilioni 3.1 kutoka Shilingi Trilioni 2.7 mwaka 2018/19. Madai ya Wazabuni dhidi ya Serikali yaliongezeka kwa 15% kutoka mwaka uliopita.Hiki ni kiwango kikubwa sana cha Fedha za watu ambazo Serikali inazishikilia mkononi baada ya kupokea huduma za Watu hao. Hali hii inasababisha mdororo wa uchumi, kwani Serikali inashikilia Fedha za wakandarasi, wafanyabiashara na watoa huduma na hivyo kudumaza shughuli za uzalishaji mali, na wakati mwingine kufukarisha wananchi.
Mzunguko wa Fedha kwenye Uchumi wa Nchi unadumazwa na kitendo cha Serikali kutolipa watoa huduma wake. Mwenendo wa Madai ya Wazabuni na Watoa Huduma kwa Serikali kwa miaka mitatu iliyopita ni kama ifuatavyo:

- 2017/2018 Shilingi Trilioni 3
- 2018/2019 Shilingi Trilioni 2.7
- 2019/2020 Shilingi Trilioni 3.1

Tunashauri kuwa Serikali ilipe madeni yote ya watoa huduma kwa mkupuo ili kuchangamsha Uchumi kwa kuongeza mzunguko wa Fedha. Pia Serikali iweke mfumo mzuri wa kulipa watoa huduma kwa wakati ili kuwasaidia kukuza shughuli zao na hivyo kuongeza ajira na kuondoa umasikini wa Wananchi.

3. Shilingi 2.2 Trilioni Hazikupita Mfuko Mkuu wa Hazina na Hivyo Kutoidhinishwa na CAG Matumizi Yake

Katika uchambuzi tuliofanya mwaka jana tulionyesha kuwa kuna Fedha za Serikali ambazo zimetumika bila kwanza kupitia Mfumo Mkuu wa Hazina kama Katiba inavyotaka. Katika mwaka wa Fedha 2018/19 Serikali ilitumia Shilingi Trilioni 1.7 bila kwanza kupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Baadhi ya Fedha hizi kwa kiwango kikubwa zinatokana na Mikopo kutoka Nje, (Shilingi Trilioni 1.2) ambapo CAG alisema zilikwenda kulipia miradi ya Maendeleo moja kwa moja. Mwaka 2019/2020 Jumla ya Shilingi Trilioni 2.16 hazikuhesabiwa Mfuko Mkuu.

Katiba ya nchi imevunjwa kwa Serikali kupokea Fedha na kuzitumia bila kwanza kupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Ibara ya 135(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa;

“Fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa fedha za aina iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, zitawekwa katika mfuko mmoja maalumu ambao utaitwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali”.

Ibara ya 136(3) inamtaka CAG kuidhinisha kutolewa kwa Fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina. Hivyo Fedha ambazo zinatumika bila kwanza kupita Mfumo Mkuu zinakosa idhini ya CAG na hivyo zinaweza kuwa zinatumika kinyume cha Bajeti na kinyume cha Sheria iliyotungwa na Bunge. Zaidi matumizi ya aina hiyo ni kichaka cha kufichia ufisadi.

Tutaonyesha mifano ya miaka mitatu tu ya Fedha ambazo hazikupita Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, jambo la kushtusha ni kuwa kila mwaka matumizi ya Fedha bila kupitia mfuko Mkuu wa Serikali yamezidi;

- 2017/18 Shilingi Bilioni 800
- 2018/19 Shilingi Trilioni 1.7
- 2019/2020 Shilingi 2.16

Fedha hizi kutokupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ni kichaka cha kukwepa udhibiti wa CAG ili kufanya ubadhirifu. Uvunjifu huu wa Katiba umeshamiri zaidi miaka ya hivi karibuni kama alivyoonyesha CAG.

Niwakumbushe kuwa tangu mwaka 2015/16 CAG amekuwa akionyesha namna Katiba haiheshimiwi lakini pia namna mifumo ya udhibiti katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali haizingatiwi. Mwaka 2015/16 kulikuwa na tofauti ya Shilingi Trilioni 2.9 katika masalio ya fedha katika Hesabu Jumuifu lakini Serikali haikuweka wazi (no disclosure) kiasi cha kusababisha Hesabu Jumuifu za Taifa kutokuwa sahihi na kupata Hati Mbaya ya Ukaguzi.

Yote haya yanatokea kwa sababu ya kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji kwani uvunjifu wa Katiba ni kosa kubwa linalostahili adhabu kubwa.

Tunaitaka Serikali kufuata Katiba kwa kufanya matumizi ya Fedha Mara baada ya kuwa zimepitia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali.

4. Fedha Zote Alizopora DPP Kutokana na Kesi za Kubambikiaa Watu Zirejeshwe

CAG ameonyesha katika Ripoti yake kuwa alipitia uendeshwaji wa Akaunti ya fedha zinazotokana na mali zilizotaifishwa na kurejeshwa Serikalini zilizo chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini hadi kufikia tarehe 30 Juni 2020. CAG amekuta kuna fedha kiasi cha Shilingi bilioni 51.521 kutokana na kesi zilizomalizika katika mahakama mbalimbali kwa kipindi cha miaka 6. Kwa mujibu wa CAG fedha hizi hazikutumika kwa sababu ya kukosekana kwa sheria na kanuni za matumizi yake.

Ni muhimu kukumbuka kuwa kuanzia mwaka 2017 lilizuka wimbi la Serikali kushiriki uporaji dhidi ya mali za watu, wakiwemo wawekezaji kupitia kesi za kubambikiwa za Uhujumu Uchumi. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka – DPP ilianza kutaifisha fedha za watu bila ya kuwepo kwa Sheria ya plea bargain. Baada ya malalamiko ndipo sheria ikatungwa. Fedha nyingi katika hizi bilioni 51.52 ni fedha za dhulma ambazo watu waliobambikiziwa kesi walilalazimika kuzilipa ili kununua uhuru wao.

Fedha za fidia Mahakamani na hizi za plea bargain zilipaswa kulipwa kwa Akaunti ya Hazina na kutolewa risiti ya exchequer badala ya kupelekwa kwenye akaunti ya DPP.

Ni muhimu kuwakumbusha Watanzania kuwa uporaji wa aina hii pia ulifanywa kwa Wamiliki wa Maduka ya Fedha za Kigeni nchini, na kudhulumiwa Fedha zao. CAG hajaonyesha katika ukaguzi wake zilipo fedha zilizochukuliwa kutoka kwa Wamiliki wa Maduka ya Fedha za Kigeni.

Tunapendekeza Rais aunde Tume ya majaji, ili kupitia malalamiko ya watu wote ambao walilipishwa Fedha kwa mtindo wa kukiri makosa na kulipa Fedha Serikalini. Wote watakaobainika kuwa walionewa warejeshewe Fedha zao na Rekodi zao za Jinai kufutwa kisheria.

5. Madudu Mamlaka ya Bandari (TPA) Yachunguzwe Zaidi

Mamlaka ya Bandari Tanzania imetajwa kwa kiwango kikubwa katika Ripoti hii ya CAG, ambapo vilibainika vitendo vya ubadhirifu katika Bandari za Mwanza na Kigoma vya thamani ya Shilingi bilioni 3.27 ambazo ziliibiwa kutoka akaunti za Benki.

Hata hivyo, hoja hii ya CAG ni sehemu ndogo sana ya ubadhirifu mkubwa ambao umekuwa ukifanyika katika Mamlaka ya Bandari Tanzania. Miradi mingi ya uendelezaji wa Bandari kama vile Mradi wa kuchimba kina cha Bandari ya Tanga imekuwa ikilalamikiwa kugubikwa na wizi na ubadhirifu na kulitia hasara Shirika kwa kiwango kikubwa.

Tunashauri CAG afanye ukaguzi Maalumu wa Miradi yote mikubwa inayotekelezwa na Mamlaka ya Bandari ili kupata uhalisia wa ubadhirifu katika TPA. Wakati ukaguzi huo unafanyika tunapendekeza kuwa Mamlaka za Uteuzi zivunje Bodi ya Bandari na kuiunda upya ili kuweza kuweka misingi ya uwajibikaji katika Shirika.

6. Tukague Ununuzi wa Ndege, Tubadili Muundo wa Uendeshaji wa ATCL ili Kupunguza Hasara

Hoja ambayo imeleta mjadala mkubwa katika Ripoti ya CAG ni Hasara kwa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). CAG alifanya ukaguzi wa kiutendaji (Startegic and Operational Efficiency) kwenye Kampuni ya Ndege Tanzania na kubaini kuwa Serikali ilikuwa imetumia shilingi Trilioni 1.028 kununua Ndege ili kufufua Shirika la ATCL.

Kati ya Mwaka 2018/19 na 2019/2020 Mapato ghafi ya Shirika yaliongezeka kutoka Shilingi 112 bilioni kwa mwaka mpaka shilingi 158 bilioni kwa mwaka sawa na ongezeko la 41%. Katika kipindi hicho pia Matumizi ya Shirika yaliongezeka kwa 45% kutoka shilingi bilioni 134 mpaka shilingi bolioni 193.

Pamoja na kununua ndege, kwa miaka mitano yaani kuanzia 2015/16 hadi 2019/20 Serikali imeisaidia Kampuni ya Ndege kiasi cha Sh. Bilioni 153.711 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na maendeleo. Fedha hizi za Walipakodi Serikali imekuwa ikizitoa kama ruzuku kwa ATCL. Hata hivyo Shirika limekuwa na hasara (accumulated losses ) ya jumla ya shilingi 153 bilioni katika miaka mitano ikiwemo hasara ya shilingi 60.25 bilioni mwaka 2019/2020. Ruzuku yote ambayo Serikali imekuwa inadumbukiza ATCL imeliwa na hasara.

CAG hakueleza katika Ripoti yake ilikuwaje Shirika ambalo lina hasara kiasi hiki licha ya Ruzuku ya Serikali liliweza kulipa Gawio kwa Serikali. Ilikuwa ni Usanii!
Katika uchambuzi wa Ripoti ya CAG Mwaka 2017/18 tulisema haya kuhusu ukaguzi wa ATCL,

“Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege

Hatujafanikiwa kuona Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18.

Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka jana (ripoti ya mwaka wa fedha wa 2016/17) tuliwaeleza kuwa katika ripoti ile licha ya kuwa ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo muhimu kadhaa ambayo CAG aliyaacha. Na tukamtaka kwenye ripoti yake ya mwaka 2017/18 ayafanyie kazi, mojawapo ni ukaguzi wa Ununuzi wa Ndege Sita (6) zinazoendeshwa na Kampuni ya Ndege nchini, ATCL.

Mpaka sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Trilioni1 kununua ndege sita (6) na katika makadirio ya Bajeti ya mwaka 2019/20 yanayoendelea sasa bungeni Serikali imeomba Bunge liidhinishe shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kulipia ndege mpya nyengine. Ufuatiliaji wetu umegundua kuwa Serikali imekuwa ikichukua Fedha za Umma kupitia Fungu 62 (Wizara ya Uchukuzi) na kufanya manunuzi ya ndege. Ndege hizo wanakabidhiwa Wakala wa Ndege za Serikali kama wamiliki na shirika la ATCL inakodishiwa ndege hizo kwa Mkataba maalumu (ambao haujawekwa wazi popote, hata kwa Bunge).

Tulitarajia kuwa ripoti hii ya CAG ya mwaka 2017/18 kwenye ukaguzi wa fungu Namba 62 tungeweza kuona ukaguzi wa manunuzi ya ndege hizi. Lakini Serikali kwa lengo la kuficha taarifa imeamua kuhamishia kwenye Ofisi ya Rais (fungu 20) Wakala wa Ndege za Serikali kupitia tangazo la Serikali namba 252 la Juni 2018.

Tumetafuta taarifa ya ukaguzi wa fedha hizo za umma zilizofanya manunuzi ya ndege bila mafanikio. Tunamwomba CAG;
- Afanye Ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma Shilingi Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege.
- Afanye Ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa ndege za Serikali na Shirika la Ndege la ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya Fedha zao za Kodi.

Jambo hili ni muhimu sana, kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kila jambo lenye harufu ya wizi au matumizi yenye mashaka basi Serikali huliamishia jambo hilo ikulu (Kwa kuwa inajua ukaguzi wake hautawekwa wazi). Hata kwenye fedha shilingi 1.5 trilioni ambazo tulizianisha kuwa hazijulikani ziliko kutokana na uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17, baada ya kuibana Serikali na kumtaka CAG afanye uchunguzi maalum, mwishowe Serikali ilihamishia Ikulu matumizi ya Shilingi 976 bilioni kati ya hizo shilingi 1.5 trilioni ili isihojiwe.

Mafungu mawili, Fungu 20 (Ofisi ya Rais Ikulu) na Fungu 30 (Sekretariati ya Baraza la Mawaziri) yanapaswa kumulikwa sana katika matumizi ya Fedha za Umma. Tumeona mwaka huu Serikali inaomba Bunge litenge shilingi Bilioni 302 kwa Fungu 30 kwa kile kinachoitwa ‘matumizi mbalimbali ya kitaifa’. Mwaka ujao, Mungu akituweka hai, tutafuatilia kwa kina kaguzi za mafungu Haya kwani inaonyesha ndimo inakuwa kichaka Cha kuficha Taarifa za namna Fedha za Umma zinatumika.”

Tunapendekeza kuwa CAG afanye ukaguzi wa manunuzi ya Ndege ili tuweze kujiridhisha kama taratibu zote za manunuzi zilifuatwa na nchi kupata thamani ya fedha.

Pamoja na hasara iliyobainishwa na CAG kuna matumaini makubwa katika Shirika la ATCL. Kinachohitajika ni maamuzi sahihi yenye maarifa ya sekta husika. Tunapendekeza kuwa muundo wa umiliki wa ATCL ubadilishwe kwa kuhusisha mashirika ya uhifadhi na utalii kama wamiliki. Shirika la TANAPA na NCAA wamilikishwe 60% ya Kampuni na hivyo waondolewe katika orodha ya Mashirika ya kupeleka Hazina 15% ya Makusanyo yao ghafi.

Vile vile Mashirika haya ya Utalii yaachiwe kujiendesha na kukusanya mapato yao wenyewe. 40% zilizobakia zimilikiwe na Serikali ambapo Kampuni ikikaa vema 25% ya Shirika wamilikishwe wananchi kwa kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kuongeza uwazi na kuboresha misingi bora ya uendeshaji wa Kampuni (governance).

7. Utekelezaji Mradi wa Reli ya Kisasa

Katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Serikali inatekeleza miradi ya kielelezo (flagship projects) ikiwemo Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa kuzalisha Umeme wa Maji wa Mwalimu Julius Nyerere maarufu Stigler’s Gorge.

Katika mwaka wa Fedha wa 2019/2020 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekagua miradi ya kimkakati na kutoa Taarifa yake kwa Umma. Miradi hii miwili ndio miradi inayochukua Fedha nyingi zaidi za Umma kuliko miradi mingine yote.

CAG amebainisha hoja za ukaguzi zenye thamani ya shilingi 137 bilioni katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa peke yake, pamoja na hoja nyengine nzito kama vile mradi kuchelewa sana kumalizika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba na kutojengwa wa kipande cha Reli urefu wa Kilometa 3. Vile vile CAG ameonyesha udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mazingira kwamba mradi ulianza bila ya kufanya tathmini ya athari ya mazingira na hivyo kuweza kupelekea madhara makubwa kwa wananchi.

Hata hivyo CAG hajafanya ukaguzi wa manunuzi ya wakandarasi (procurement audit) wa Mradi huu. Taarifa ambazo zinazungumzwa na Wataalamu ni kuwa namna Mradi ulivyokuwa umepangwa kutekelezwa Kwa kupitia Mkopo kutoka Serikali ya China ingegharimu Dola Bilioni 7 Kwa Mradi mzima wa Reli ya Kati Kwa ukamilifu wake. Hata hivyo Gharama za Ujenzi Kwa njia ambayo Tanzania ilichagua baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kutupilia mbali Mpango wa Serikali ya Awamu ya Nne zinasemekana kuwa zitakuwa maradufu.

Hivyo mapendekezo yetu ya kwanza ni kwa CAG kufanya Ukaguzi Maalumu wa Manunuzi ya Mradi huu na kulinganisha kama ungetekelezwa tofauti ili kutambua kama ni Mradi wenye thamani ya Fedha (value for money) na namna gani ya kumalizia kuutekeleza kwa ufanisi zaidi.

8. Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere

Kwa upande wa Mradi wa kuzalisha Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere, CAG amebainisha hoja nzito ambazo zinaonyesha kuwa mradi huu wenye kugharimu shilingi trilioni 6 unatekelezwa kwa uholela mkubwa. Hoja kubwa ambayo inahitaji mjadala mpana tena mjadala wa kitaalamu ni ile ya kazi ya ushauri wa mradi kufanywa na taasisi ya Serikali. Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupitia kitengo cha (TECU) ambaye ni mhandisi mshauri anayesimamia mradi. TECU ni TANROADS.

CAG anasema “TANESCO iliingia makubaliano ya hiari badala ya mkataba na TECU kupitia kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika manunuzi yenye kiasi cha Sh. Bilioni 9. Hii ni kinyume na kifungu cha 60(7) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 ambacho kinataka wakati ambapo taasisi ya umma imefikia muafaka wa makubaliano na mkandarasi, muuzaji au mtoa huduma yeyote ni lazima mkataba rasmi usainiwe baina ya pande mbili na kazi/huduma ifanyike kwa mujibu wa makubaliano hayo. Nilibaini kuwa, TANESCO waliingia makubaliano ya hiari na TECU badala ya mkataba rasmi. Makubaliano hayo yalikuwa hayaziwajibishi kisheria pande zote mbili. Pia ilibainika kuwa tarehe 17 Aprili 2019 TANESCO ilisaini makubaliano ya hiari na Wakala wa Barabara kwa ajili ya huduma ya ushauri katika ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Julius Nyerere kwa thamani ya Shilingi 8,910,704,500. Thamani hii inajumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani, kinyume na matakwa ya sheria ya manunuzi ya umma.

Mkataba huu wa TANESCO na TANROADS haukuidhinishwa na Bodi ya TANESCO. Madhara ya mfumo huu wa utekelezaji wa mradi ni usimamizi mbovu wa Mradi ambao ulisababisha kingo za bwawa kubomoka na kusababisha mafuriko makubwa sana mikoa ya Morogoro na Pwani. Hatukuelezwa hili kwa sababu Serikali iliamua kuendesha kila kitu gizani. Pia hakuna mtu aliyewajibishwa TANESCO wala TANROADS, Ni kana kwamba Tanzania ilikuwa na kundi linaloweza kuvunja sheria bila kuguswa na linaloguswa bila hata ya kuvunja sheria.

9. Hasara TPDC kwa Serikali Kulitelekeza Bomba la Gesi la Mtwara

Ni Vema kuwakumbusha Watanzania kuwa CAG pia katika Taarifa ya Mwaka huu ameonyesha kuwa Shirika la TPDC lina mtaji hasi wa Shilingi Bilioni 332 ambao umesababishwa na Mkopo ambao Serikali yetu ilichukua kutoka China Kwa ajili ya Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Mkopo ule ni wa thamani ya Shilingi Trilioni 3.23. TPDC wameshindwa kulipa Mkopo huu Kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuachana na Mkakati wa kuzalisha Umeme Kwa Gesi Asilia na badala yake kuwekeza kwenye Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ya Mwaka 2015/16 Bomba la Gesi lenye uwezo wa kusafirisha Futi za Ujazo 737.9 Milioni hivi sasa linasafirisha Futi za Ujazo 46.61 milioni tu sawa na 6% ya uwezo wake.

Iwapo Bomba hili lingetumika Kwa uwezo wa 30% peke yake lingeweza kuzalisha Umeme 3500MW, zaidi ya Umeme wote unaotarajiwa kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, bila ya Nchi kutumia hata senti 1 Kwa kutumia Sekta Binafsi kuwekeza kwenye Mitambo ya kufua Umeme.

Tunapendekeza pia kuwa Serikali itazame upya masuala ya utawala bora katika usimamizi wa Miradi hii mikubwa kwa kuondokana na uholela unaoendelea sasa. Serikali itafute kampuni zenye weledi na uzoefu kusimamia Ujenzi wa Miradi hii kama Wakandarasi washauri. Fedha nyingi zimekwishaingizwa katika Miradi hii hivyo ni lazima kuimaliza. Hata hivyo ni muhimu kurekebisha makosa yote ambayo CAG ameyaonyesha katika Taarifa yake na mengine ambayo wataalamu wameyaanisha.

Tunapendekeza pia Serikali iliache Shirika la TPDC lifanye kazi yake kibiashara na kurudi katika Mpango kabambe wa kuzalisha na kusambaza Umeme ili Uwekezaji uliofanywa katika Bomba la Gesi uwe na manufaa Kwa Taifa letu.

10. MSD Washindwa Kusambaza Dawa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amebainisha kuwa Bohari ya Madawa Nchini (MSD) ambayo ndio Shirika lenye Jukumu la manunuzi yote ya dawa hapa Tanzania, inaidai Serikali Jumla ya Shilingi Bilioni 257.

Katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 MSD haikupewa Fedha kwa mujibu wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa 99.45%. Hili ni janga kwa Taifa. Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa inatamba kuwa imeongeza Bajeti ya Dawa kumbe inaliua Shirika la MSD. Ni aibu kubwa sana kwa MSD kushindwa kufanya kazi.

Ifahamike kwamba MSD inahitaji Mtaji wa shilingi Bilioni 500 tu ili iweje kujitegemea na kujiendesha bila kuhitaji Fedha kutoka Serikalini. Fedha hizi ni sawa na Bajeti ya Mwaka mmoja tu wa mwaka 2018/2019 ya kununua Ndege za Shirika la Ndege la Taifa – ATCL.

Tunapendekeza Serikali ilipe Deni lote la MSD, na pia Serikali itoe mtaji kamilifu kwa MSD ili iweze kujitegemea kibiashara katika shughuli ya usambazaji wa Dawa kwa Wananchi wetu.

B: Hitimisho:

1. Ushahidi wa Uholela:

Ripoti Kuu ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2020 umeibua Hoja nyingi za Ukaguzi ambazo tusingweza kuchambua zote. Kwa kuwa Ripoti hii ipo wazi kwa Umma ninawasishi Watanzania waisome kwa kina na kuendelea kuichambua kila mtu kwa namna yake anayoona inafaa. Sisi ACT Wazalendo tutaitumia kama nyenzo ya kuisimamia Serikali katika shughuli zetu kama Chama Cha Siasa cha Upinzani.

Ripoti ya Mwaka huu imeendelea kudhihirisha kiwango kikubwa cha uholela katika uendeshaji wa Serikali na haswa katika usimamizi wa Fedha za Umma na uendeshaji wa Miradi.

Miaka Sita ya Vyombo vya habari kuminywa katika kufanya shughuli zao, Bunge kuondolewa meno yake kupitia Kamati za Bunge, Asasi za Kiraia kukandamizwa na Vyama vya Upinzani kupondwapondwa kuliwezesha Nchi kuendeshwa kwenye Giza totoro.

Gharama ya uendeshaji wa Nchi kwenye Giza ndio hizi tunazoziona katika Ripoti ya CAG. Hoja hizi za Ukaguzi ni sehemu ndogo sana ya uvundo mkubwa uliopo katika nchi yetu.

2. Tujenge Taasisi:

Ni ushauri wetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kujenga mifumo madhubuti ya Uwajibikaji na kuimarisha Taasisi za Uwajibikaji. Bila Taasisi Imara Nchi yetu haitaweza kupiga hatua kubwa za Maendeleo.

Miradi mikubwa kama Mradi wa Umeme wa Bwala la Mwalimu Julius Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa na Mradi wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa inaweza kugeuka kuwa miradi yenye hasara kubwa kwa Taifa iwapo hatua mahususi hazitachukuliwa kuingiza utaalamu, weledi na maarifa katika utekelezaji wake.

Mradi wa Bwawa la Umeme ukiendelea kutekelezwa kwa namna ambavyo unatekelezwa sasa utasababisha maafa makubwa ya Wananchi Zaidi ya hasara ya Fedha. Tunashauri Mamlaka ziunde upya Bodi ya TANESCO na Menejimenti yake ikiwemo Menejiment nzima ya Mradi ili kurekebisha makosa yote ambayo yameainishwa na CAG.

Kwa namna TANROADS na watu waliokuwa Wafanyakazi wa TANROADS walivyohusika na miradi mbalimbali nchini, ni ushauri wetu kuwa Serikali ifanye uchunguzi maalumu wa Genge la TANROADS (The TANRODS Junta) katika kuifikisha nchi mahala ilipo sasa ili kuchukua hatua za kurekebisha panapostahili.

3. Ukaguzi kuhusu Akaunti ya Pamoja ya Fedha za Muungano:

Mwisho ni ushauri wetu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika mawanda yake ya ukaguzi katika siku za usoni. Katiba yetu ibara ya 133 inaelekeza kuundwa kwa Akaunti ya Pamoja ya Fedha ambayo itakuwa sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kuhifadhi Fedha za Muungano kwa madhumuni ya Shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.

Ibara hii ya Katiba haitekelezwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hajawahi kutoa Taarifa ya Ukaguzi kuhusu Mapato na Matumizi yanayotokana, na au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano. Hili ni eneo ambalo ni kero kubwa katika uendeshaji wa Muungano wetu.

Tunamuomba CAG afanye ukaguzi Maalumu wa eneo hili ili aweze kuzishauri Mamlaka kupitia Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu mfumo wa shughuli za Fedha wa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.


Asanteni sana.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
Aprili 11, 2021
Dar es Salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK