Tunachokisimamia

Ajira Milioni 10 katika miaka 5

Ajira Milioni 10 katika miaka 5

Changamoto kubwa inayokabili nchi yetu kwa sasa ni ukosefu wa Ajira kwa jeshi kubwa la Vijana ambao wanaingia kwenye nguvu kazi ya Taifa. Katika Watanzania Milioni 25 walio kwenye nguvu kazi ya Taifa, ni Watanzania Milioni 2.3 tu sawa na 9% ambao wameajiriwa katika ajira rasmi ambazo ni bora, zitambulika, Waajiriwa wana hifadhi ya Jamii na Pia kulipa Kodi ya Mapato Serikalini. 91% ya Watanzania wenye uwezo wa Kufanya Kazi hawamo kwenye Mfumo rasmi wakiwemo Wakulima, Wafanyabiashara wadogo, wafugaji, Wavuvi nk.

Kila Mwaka wastani wa Watoto 900,000 humaliza Elimu ya Msingi na nusu tu ya hao huendelea na Kidato cha Nne ambapo Wastani wa Vijana 430,000 huhitimu ya Elimu ya Sekondari ya Awali. Wastani wa Vijana 90,000 humaliza masomo ya Kidato cha Sita kila Mwaka. Wastani wa Vijana 60,000 humaliza masomo ya Elimu ya Juu na vyuo vya ufundi nchini.

Wahitimu wote hawa wanapaswa kupata ajira ili kuendeleza maisha Yao na kutumia nguvu kazi kuendeleza Taifa letu.

Serikali itakayoongozwa na ACT Wazalendo itafanya yafuatayo ili kuongeza ajira kwa Watanzania

1. Itaweka mazingira bora ya kuongeza shughuli za uzalishaji kiuchumi ili kutengeneza ajira zenye tija milioni kumi (10) katika miaka mitano.

  • Ajira million tano zitatoka kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo kufuatia utekelezaji wa Miradi 5 kabambe ya Umwagiliaji itakayoongeza eneo la Kilimo cha Umwagiliaji Kwa Hekta 1m, kuimarisha Ushirika Kwa kuanzisha Ushirika wa kisasa unaojenga Utajiri wa Jamii ( Community Wealth Building) na Urasmishaji wa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii.
  • Ajira million 2 kutoka sekta rasmi kufuatia utekelezaji wa Miradi Mkakati itakayochochea shughuli za uchumi nchini, kuongezeka kwa uwekezaji wa Mitaji ya ndani na nje ( FDI ) na kuweka vivutio vya kurasmisha shughuli za Vijana ikiwemo mazingira bora ya Biashara, mitaji Kwa wabunifu nk. Sekta kiongozi katika kuzalisha ajira hizi itakuwa Sekta ya Utalii, Usafirishaji na fungamanisho la sekta ya uziduaji ( Madini, Mafuta na Gesi Asilia ) na sekta nyengjne za Uchumi
  • Ajira milioni 3 kutoka sekta isiyo rasmi kutokana na kuongezeka kwa vyuo vya ufundi stadi na kupanuka kwa shughuli za uchumi za huduma ( services sector ) ikiwemo kuboreshwa kwa shughuli za Sanaa, Michezo na Burudani.

2. Itaimarisha ubora na kutafuta soko la nje kwa kazi za ubunifu kama uhunzi, uchongaji, uchoraji na bidhaa zingine zitokanazo na kazi za mikono.

3. Itaweka mifumo mizuri ya kisera na uwekezaji katika soko la sanaa na michezo.

4. Itarasimisha na kulipia mafunzo kwa vitendo (paid internship), kwa fani zote kwa kipindi kisichopungua miezi sita ili wahitimu wote wapitie mafunzo kwa vitendo kikamilifu na kuweka utaratibu wa kutumia matokeo ya mafunzo kwa vitendo katika utoaji ajira. Vile vile Serikali Itaweka vivutio maalum vya kikodi kwa makampuni binafsi yatakayotoa nafasi kwa vijana waliohitimu kufanya mafunzo kwa vitendo.

5. Itaboresha maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya umma na kusimamia maslahi stahiki ya wafanyakazi wa sekta binafsi ili ajira zote zitakazozalishwa kipindi cha uongozi wetu ziwe ajira zenye tija na zenye kukidhi mahitaji ya wafanyakazi na kupatiwa hifadhi ya jamii stahiki.

6. Itapunguza Makato ya kodi za Wafanyakazi (PAYE), lengo likiwa kuwaongezea wafanyakazi kipato ili waweze kumudu mahitaji katika maisha, kujiwekea akiba au kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji kipato cha ziada.

7. Itatengeneza mazingira mazuri ya kisera yatakayowezesha vyama vya wafanyakazi kuwa huru, kuimarika na kusimamia maslahi ya wafanyakazi kwa ufanisi.

8. Kulipa mafao ya watumishi kwa wakati na kuboresha maslahi na huduma kwa wastaafu.

9. Itapunguza gharama za kuajiri Kwa waajiri kwa kupunguza tozo ya Ujuzi ( Skills Development Levy ) mpaka 2% kutoka 4% ya sasa.

10. Itapunguza makato ya michango ya Hifadhi ya Jamii mpaka 12% kutoka 20% ya mshahara Kwa Mfanyakazi ambapo Mwajiri atachangia 7% na Mwajiriwa 5% kwenda Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.

Rudi kwenye ilani

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK