Asilimia 85 ya Watanzania Hawana Bima ya Afya! - Dr. Nasra

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA AFYA DR. NASRA OMAR – ACT WAZALENDO KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

Utangulizi:
Leo ya tarehe 16 Mei 2022, Waziri wa Afya Mh Ummy Ali Mwalimu (Mb.), amewasilisha Bungeni mpango wa Wizara na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na maeneo ya kipaumbele ambayo wizara itajielekeza nayo kwa mwaka huu. Sisi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Afya tumeisikiliza, kuichambua na kuimulika ili kuona kwa namna gani inaakisi matarajio na matamanio ya wananchi. Katika kufanya hivyo, hotuba hii ya Msemaji wa Afya wa ACT Wazalendo imekuja na hoja kumi (10) kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Zifuatazo ni hoja kumi (10) za ACT Wazalendo kuhusu bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2022/23:
1. Upungufu mkubwa wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali za Umma:
Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya. Hali ya vituo vya afya nchini hairidhishi kabisa, bado kuna upungufu na matatizo ya upatikanaji wa dawa, vifaa na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora. Uwekezaji wa ujenzi wa vituo vya afya unapaswa kwenda sambamba na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma ya afya kwa wananchi.
Tafiti za viashiria vya utoaji wa huduma za afya nchini (2018), zinaonyesha hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya vya umma ni wastani usiozidi asilimia 60. Pia, zinaonyesha kuwa ni chini ya nusu (49 %) ya dawa muhimu za wanawake wazazi zilipatikana; ni 8% tu ya vituo vilikuwa na dawa zote 14 muhimu kwa afya ya binadamu; na ni 1% tu ya vituo vya vijijini ndio walikuwa na dawa hizo.
Kwa mujibu wa takwimu za wizara (2021), hali ya upatikanaji wa dawa aina 312 katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ilifika asilimia 71 na katika maghala ya MSD ni asilimia 51 ikilinganishwa na hali ya upatikanaji wa dawa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2019/20, ambapo upatikanaji ulikuwa ni asilimia 80 katika vituo vya kutolea huduma na asilimia 56 katika maghala ya Bohari ya Dawa. Upatikanaji wa dawa kwa ngazi ya zahanati ni asilimia 43, vituo vya afya ni asilimia 42, hospitali za wilaya ni asilimia 50, hospitali za rufaa za Mikoa 76 na hospitali za kanda ni asilimia 71.
Hali hii inathibitishwa pia na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2020/21 (CAG) inaonyesha ufanisi mdogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwani ilishindwa kwa asilimia 66 kutimiza mahitaji ya bidhaa za dawa na vifaatiba kwa wateja. Hadi tarehe 30 Juni 2021, Bohari Kuu ya Dawa iliweza kutimiza asilimia 34 tu ya jumla ya bidhaa 43,180,884 za dawa na vifaa tiba zilizoagizwa na wateja (vituo vya afya).
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye vituo vya afya vyote nchini. Pili, Serikali iijengee uwezo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Tatu, Serikali ifuatilie kwa umakini utaratibu wa ugavi wa dawa katika hospitali za wilaya na rufaa za mikoa ili kudhibiti ubadhirifu na wizi wa dawa unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu na kuwachukulia hatua stahiki.
2. Utendaji usioridhisha wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) unaongeza ukosefu wa dawa na vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma:
Athari za utendaji mbovu wa MSD ni kubwa kwa taifa. Kuna mlundikano wa bidhaa 7,676,436 zilizoagizwa kwa fedha za walipa kodi ambazo sasa hazifai tena kwa matumizi ya binadamu. Ripoti CAG 2020/21 imebaini uwepo wa jumla ya bidhaa hizo za thamani ya Shilingi bilioni 22.80 zilizopitwa na muda ambazo zilikuwa kwenye maghala ya Bohari Kuu ya Dawa kuanzia tarehe 16 Aprili 2000 hadi 30 Juni 2021 (miaka 20).
Aidha, MSD imeshindwa kuteketeza dawa zilizopitwa na muda za kufubaza VVU-UKIMWI hata baada ya kulipwa na kupewa ruhusa ya kufanya hivyo. Ripoti ya CAG 2020/221 inaeleza “nilibaini Bohari Kuu ya Dawa ilipokea fedha kutoka kwa wafadhili ambazo ni dola za Marekani 239,023.92 ili kugharamia zoezi la kuharibu dawa za kufubaza VVU-UKIMWI. Hata hivyo, ingawa ruhusa ya kuteketeza dawa hizo ilishatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango tangu tarehe 7 Oktoba 2021, dawa hizo hazikuharibiwa hadi wakati wa ukaguzi mwezi Disemba 2021”.
ACT Wazalendo tunapendekeza, Serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuiwezesha Bohari ya Dawa (MSD) kufanya kazi zake kwa uhuru na kuiwajibisha.
Aidha, Bohari Kuu ya Dawa iongezewe watafiti na wataalamu wa ugavi kuhakikisha hakuna upoteaji au ukosekanaji wa dawa kiholela.
3. Uhaba wa miundombinu, ubadhirifu na ucheleweshwaji wa ujenzi wa vituo vya afya:
Uwiano uliopo kati ya vituo vya afya kwa maana ya Zahanati, vituo vya afya na Hospitali za rufaa bado hauridhishi. Sera ya kuwa na zahanati kila Kijiji na kituo cha afya kila kata, haijatekelezwa kwa maeneo yote. Pia kuna uhaba wa miundombinu ya afya kama vile vitanda na huduma za maeneo ya mapumziko ya wagonjwa, maabara za kiuchunguzi na vyumba vya upasuaji. Taarifa za Ofisi ya takwimu ya taifa inaonyesha kuna jumla ya hospitali za serikali 185, vituo vya afya 779, zahanati 5395 tu.
Pia, kwenye baadhi ya vituo vya afya kuna ukosefu wa miundominu msingi kama vile maji safi, vyoo bora na umeme. Utafiti wa viashiria vya utoaji wa huduma za afya (2016) ulionyesha nusu tu (50%) ya vituo vya afya ndivyo vyenye maji safi, vyoo bora na umeme. Hata hivyo, kuna tofauti kubwa kati ya vituo vya vijijini na mijini (36% kwa umma dhidi ya 79% ya vituo vya mijini). Mathalani, vituo vya afya vya vijijini vinakosa huduma za umeme na maji safi, ambazo ni rasilimali muhimu katika sekta ya afya. Hali hii inaendelea hata sasa kwenye maeneo mengi ndani ya nchi yetu.
Vilevile, kuna hila na ubadhirifu katika utekelezaji wa ujenzi wa vituo vya afya kupitia fedha za Uviko–19. Kuna malalamiko mengi kuwa utekelezaji wake umegubikwa na hila na viashiria vya ubadhirifu.
Katika ziara ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo mwezi Desemba 2021 na Januari 2022 kwenye mikoa ya Kusini, tulikutana na changamoto ya migogoro inayotokana na utekelezwaji wa miradi hiyo wenye wa hila za kisiasa.
Maeneo yaliyopaswa kujengwa vituo vya afya yalibadilishwa licha ya wananchi kufanya jitihada za awali za kujitolea, mathalani katika Kata ya Mikoma II, wilayani Newala Mtwara, kituo cha Afya kimejengwa kwenye Kijiji anachotokea Mbunge badala ya Mikoma II ambapo tayari kuna nguvu kubwa za wananchi. Vilevile, Mkoani Lindi katika wilaya ya Kilwa, tulikutana na migogoro kwenye vijiji viwili; Kijiji cha Mandawa ambapo ilipopaswa kujengwa kituo cha afya kimehamishiwa Hotel Tatu; Pili katika Kijiji cha Njinjo kituo cha afya kimehamishiwa Kipindimbi badala ya kujengwa Njinjo. Hila za kisiasa katika utekelezaji wa miradi zimetokea maeneo mengi nchini, hii ni mifano michache sana.
Aidha, CAG katika ripoti yake 2020/21 amebaini kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa majengo ikiwemo hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati katika mamlaka 54 za Serikali za mitaa zilizopokea kiasi cha shilingi bilioni 31.10. Uchelewehaji huo umekuwa kwa kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi miaka mitatu.
4. Upungufu wa Watumishi wa afya katika hospitali za umma:
Uhaba wa watumishi wa afya katika vituo vya afya umekuwa ni tatizo sugu na la muda mrefu hali inayopunguza ufanisi wa wafanyakazi na kupunguza ubora wa huduma za afya kwa wananchi. Idadi ya chini kabisa ya watumishi wa afya inayohitajika katika kutoa huduma bora katika sekta ya afya ni watumishi 145,454 lakini waliopo sasa hawazidi 70,244; na hivyo kuna upungufu wa watumishi 75,211 sawa na asilimia 52.
Mfano tutazame ukubwa wa tatizo hili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Ikama ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mwaka wa fedha 2020/21 inaonesha uhitaji wa wafanyakazi 4567, hadi kufikia Novemba 2021. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG 2020/21 Hospitali hii ilikua na jumla ya watumishi 2734 ikiwa na upungufu wa watumishi 1833 sawa na asilimia 40. Idara inayoongoza kwa upungufu wa watumishi ni Maternity Block 1, eneo linalohusika na kinamama na uzazi ambapo kuna upungufu wa watumishi 171. Hii ni idara inayoshughulikia watu wawili kwa wakati mmoja yaani mama na mtoto aliye tumboni. Kwa hali hii, vifo vya mama na mtoto haviwezi kupungua kwa kasi tunayoitaka ikiwa upungufu huu utaendelea, pamoja na hayo matatizo yanayosabishwa na mazingira mabovu au kushindwa kupata huduma za haraka kwa wajawazito kunaongeza kasi ya maradhi yanayoweza kuepukika kwa watoto wachanga kama vile Utindio wa Ubongo (Cerebral Pasly).
Serikali inatakiwa kuajiri wahudumu wa afya ili kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto. Kuweka mifumo mizuri inayosimamia haki na wajibu wa mfanyakazi wa afya, ili kuwawajibisha endapo atafanya uzembe wakati wa kuhudumia jamii.
Vilevile, wahudumu wa afya wanatakiwa kupewa mafunzo ya mara kwa mara ikiwemo, mafunzo ya huduma kwa wateja, mafunzo ya huduma za dharura kwa mama wajawazito, na mafunzo ya uwajibikaji ili kuongeza ufanisi kwenye kazi zao.
5. Utendaji mbovu wa Mfuko wa Bima ya afya (NHIF)
Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) una jukumu la kutoa huduma ya afya bora kwa wanachama wake bila ya kujali hali ya ugonjwa au kipato cha mchangiaji. Hadi Machi 2020 mfuko wa NHIF ulikuwa umesajili wanachama 1,127,956 na wanufaika 4,341,993 sawa na asilimia 8 ya watanzania wote, ikiwa ni pungufu kwa asilimia 1 kutoka asilimia 9 ya mwaka 2020. Mfuko huu wa NHIF kwa sasa unaendeshwa kwa hasara, na kwa mwaka 2020/21 mfuko umepata hasara ya shilingi bilioni 109.71.
Gharama za uendeshaji na ulipaji wa mafao ulikua zaidi ya makusanyo ya michango. Licha ya kuja na matabaka ya uchangiaji, mfuko huu hauna fedha za kutosha kuwahudumia wanachama wake. Katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali 2020/21 kumeonekana udhaifu wa kiutendaji wa NHIF, uliosababisha hasara ya mabilioni ya fedha yanayotokana na ukusanyaji hafifu wa madeni, utoaji mikopo na uwekezaji mbovu wa fedha za umma.
Mfuko wa Bima ya Afya umeendeshwa kwa hasara kwa miaka takribani mitatu mfululizo kuanzia 2018/19 hadi 2021/22. Hasara zinatokana na madeni yaliyokopwa na Serikali umepelekea mfuko wa bima kuleta vifurushi vipya kufidia makosa yake kwa kutoza wananchi gharama zaidi na kupunguza mafao wanayopata wananchi wanapoumwa. Wananchi hawapswi kutumika kulipa gharama za maamuzi mabovu ya Serikali.
ACT Wazalendo katika Ilani ya Chaguzi 2020 tuliahidi kuhakikisha suala changamoto za afya kuwa historia “Serikali ya ACT Wazalendo itafanya yafuatayo; Itaboresha mfuko wa Bima ya Afya kwa kuunganisha na mifumo ya Hifadhi ya Jamii, ili kila Mtanzania anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya Afya moja kwa moja. Kwa mfumo huu, mfuko wa Bima ya Afya utaweza pia kupata fedha kwa wakati na kulipa watoa huduma kwa wakati. Bima ya Afya ni haki ya kila Mtanzania.”
ACT Wazalendo inaitaka Serikali kupitia wizara ya fedha ihakikishe mikopo inayodaiwa kupitia mashirika ya Umma na Wizara inarudishwa haraka ili kuujengea Uwezo Mfuko wa Bima wa Afya.
6. Utendaji usioridhisha wa hospitali za kanda na hospitali za rufaa za mikoa:
Wizara kwa kushirikiana na wadau wake ilifanya tathmini katika halmashauri zote 184 na hospitali za rufaa za mikoa kuhusu ufanisi wa mfumo wa ugavi wa dawa na kubaini kuwa, karibia kila kituo kinakabiliwa na tuhuma za usimamizi duni wa mnyororo wa ugavi jambo linalosababisha kiasi cha kutosha cha bidhaa za afya kutowafikia wagonjwa hususan dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Aidha, sambamba na tathmini hiyo, yapo matukio mbalimbali ya ubadhirifu na wizi wa bidhaa hizi ambayo yameripotiwa. Licha ya kuonekana kuimarika kidogo kwa huduma za uchunguzi na vipimo kwa ngazi ya hospitali za kanda na rufaa za mikoa, bado ubora wa huduma unalazimisha mifumo ya rufaa mara kwa mara kwenda kwenye hospitali za taifa jambo ambalo linasababisha msongamano wa wagonjwa na kuzorota kwa utoaji wa huduma kutokana na kuzidi uwezo.
ACT Wazalendo tunaendelea kutoa rai kwa wizara ya afya kuhakikisha zinaboresha huduma na kusimamia utendaji wa watumishi katika hospitali za umma.
7. Mfumo wa sasa wa kugharamia afya, unatengeneza na kukuza matabaka nchini:
Tangu Serikali ilipoanza kutekeleza sera ya uchangiaji wa huduma muhimu kama vile za Afya na Elimu kutokana na sera ya urekebishaji wa uchumi na soko huria, mwanzoni mwa miaka 1990, kumeongeza pengo kubwa la wenye nacho na wasio nacho katika kupata huduma za afya. Upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa unategemewa na uwezo wa mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa wenyewe. Jitihada za Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa usawa zinazuiwa na gharama kubwa na mifumo mibovu ya kuunganisha nguvu za wananchi ili kupanua wigo na uwezo wa Serikali kugharamia huduma.
Mfumo wa sasa wa ugharamiaji wa huduma za afya umeachwa kwenye mabega ya mwananchi aidha kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya. Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya Afya, jumla ya Watanzania 8,224,271 sawa na asilimia 14.7 ya watanzania wote (takriban milioni 59.4) ndiyo wanaonufaika na huduma za bima ya afya. Mfuko wa NHIF kwa sasa unahudumia wanachama 1,127,956 na wanufaika 4,341,993 sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote, huku asilimia 5.4 wanahudumiwa na Bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF), asilimia 0.3 wanufaika wamejiunga kupita SHIB-NSSF na asilimia 1 wanatumia bima za makampuni binafsi. Kwa hiyo, 85.3% ya nguvu ya Watanzania haimo kwenye Mfumo wa Bima ya Afya.
Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2020 zilizotolewa Juni 2021, zinaonyesha kuwa mwaka 2020 jumla ya Watanzania milioni 42 walikuwa wagonjwa wa nje kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati Nchi nzima. Hii ina maana kuwa 68.4% ya Watanzania waliumwa mwaka 2020. Katika Nchi ambayo raia wake wanaumwa kwa kiwango hiki suala la Afya linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa sana. Kitendo cha Serikali kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa namna yoyote ni kuumiza wananchi wake.
Wote ni mashahidi namna watu wanavyopoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu, Ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua maiti katika hospitali kutokana na marehemu kuwa na deni linalotokana na gharama za matibabu. Utu wetu unafifia kutokana na kukosa mfumo wa afya wa kujaliana, kuthaminiana. Kukosekana kwa mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii umewafanya watu wengi wasiwe na uwezo wa kupata huduma za matibabu.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuhakikisha kila mtanzania anakuwa kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuwawezesha wananchi wote kupata bima ya afya ya taifa.


8. Sera ya matibabu bure kwa watoto, wajawazito na wazee haitekelezwi kwa ufanisi:
Katika nukta za hapo juu nimelezea na kuonyesha udhaifu wa mfumo wetu wa ugharamiaji unaochangia kudunisha utu wa watanzania na kutengeneza matabaka. Pamoja na hali hiyo, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wenye miaka zaidi ya 60 wana haki ya kupata matibabu bure kwa mujibu wa sera ya matibabu bure kutoka katika vituo vya afya vya Serikali.
Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa na changamoto kubwa, tathmini yetu inaonyesha kuwa wastani wa asilimia 40 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanalazimika kulipia matibabu. Vilevile, kwa wajawazito wanalipishwa matibabu na inatokea hivyo kwa watu wenye miaka zaidi ya 60 hulazimika kulipia huduma hizo tofauti na utaratibu uliopo.
Tunaitaka Serikali ifuatilie kwa makini utekelezwaji wa sera hii ili kuhakikisha kuwa walengwa – ambao ni watoto, wajawazito na wazee wanapata haki zao za msingi.
9. Utegemezi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka nje ya nchi:
Sera ya Afya ya Taifa ya mwaka 2007, iliweka malengo ya kukabiliana na utegemezi wa dawa na vifaa vingine vya afya kutoka nje ya nchi. Changamoto hii bado ingalipo, mwenendo wa utegemezi wa nchi yetu unazidi kukua. Bohari ya Dawa ya Serikali (MSD) imekuwa ni wakala tu wa makampuni ya madawa kutoka nje.
Bajeti ya Serikali katika sekta ya afya kwa sehemu kubwa inaenda nje kwa ajili ya kugharamia dawa, vifaa na vitendanishi, hali ya utegemezi inaenda kuathiri bei za dawa, vifaa na vitendashi kwa kuwa nchi haina uwezo wa kudhibiti. Pia, utegemezi unapunguza uwezo wa kujikimu kwa mahitaji ya afya na kuongeza gharama ya huduma ya afya kwa kadri ya maamuzi ya soko linavyoamuliwa na makampuni hayo. Vilevile, wakati mwingine inaathiri ubora wa dawa na vifaa tiba vinavyoingia nchini, kulingana na mahitaji mbalimbali nchini.
Sisi ACT Wazalendo tunatambua umuhimu wa taifa kuwa uwezo wa kujikimu kwa dawa na vifaatiba hivyo inalenga kuwekeza kwenye utafiti na uzalishaji wa dawa salama ndani ya nchi pamoja na vifaa tiba. Hivyo basi, tunapendekeza Serikali kuweka utaratibu maalumu wa kuwezesha kimitaji viwanda vya ndani na vyuo vya ufundi ili viweze kuzalisha dawa na vifaa tiba kwa kiwango cha kimataifa, ili kukidhi soko la ndani na kushindana katika soko la nje.
Aidha, tunaitaka Serikali kuimarisha mfumo wa usambazaji dawa na vifaa tiba kwa kutumia teknolojia mbalimbali za mawasiliano, na kudhibiti ubora wa dawa na vifaa vya afya vinavyotumika nchini.
10. Lishe duni ni janga kwa taifa letu:

Utapiamlo unaendelea kudhoofisha maendeleo katika uhakika wa chakula, uboreshaji wa elimu, na afya bora ya mama na mtoto nchini. Kwa mujibu wa utafiti wa Idadi ya watu na Afya ya mwaka 2016, takriban theluthi ya watoto wote chini ya miaka mitano wana udumavu na asilimia 14 wana upungufu wa uzito. Sababu kuu zinazoongoza kuleta utapiamlo ni ukosefu wa lishe mchanganyiko na bora kwa kila kaya, upatikanaji mbovu wa huduma za afya (pamoja na maji safi na salama, usafi wa mazingira), na mienendo duni ya lishe.
Tanzania inakadiriwa kutumia gharama yenye thamani ya asilimia 2.6 ya Pato la Taifa kila mwaka kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya udumavu na utapiamlo. Upotezaji huu wa mapato ni mkubwa sana, lazima hatua Madhubuti zichukuliwe. Athari za utapiamlo kwa watoto wadogo ni ukuaji duni kimwili na kiakili. Aidha, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa utapiamlo unachangia zaidi ya asilimia 50 ya vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Utapiamlo unasababisha wanawake wajawazito kuzaa watoto wenye uzito pungufu na pia, unaweza kusababisha vifo miongoni mwao.
Hitimisho:
Kupungua kwa bajeti ya wizara mwaka hadi mwaka kunaonyesha itatuchukua muda mrefu sana kufikia lengo la kuwa na jamii yenye afya kwa wote. Pia, mfumo wetu wa ugharamiaji unawaacha wananchi wetu kwenye maumivu makubwa. Bajeti ya Serikali inapaswa kuakisi mahitaji ya wananchi katika kupata ‘haki ya afya kwa wote’. Lakini mwaka hadi mwaka tunaona deni la Serikali na ruzuku finyu kwenda kwa Bohari Kuu ya Dawa kunaifanya taasisi hii kuzidiwa na majukumu.

 

Imetolewa na:

Dr. Nasra Omar
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Afya- ACT Wazalendo
16 Mei, 2022

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK