Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula, Amtembelea Katibu Mkuu ACT Wazalendo

Leo tarehe 06 Machi 2021, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu amekutana na kufanya mazungumzo na Baba Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula, ambaye ni Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian Duniani, aliyemtembelea katika Ofisi za Chama zilizoko Magomeni Dar es salaam.

Katika mazungumzo yao, Askofu Mwamakula amewasilisha pongezi zake kwa Chama cha ACT Wazalendo kwa mapendekezo makini ya jina la Ndg. Othman Masoud Othman, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Askofu Mwamakula amemweleza Katibu Mkuu Ado Shaibu kuwa ameridhishwa na uteuzi wa Ndg. Othman Masoud kwa sababu ni mtu mwenye sifa, uwezo na dhamira ya dhati kwa Zanzibar na kwamba ana imani kuwa atafuata nyayo za Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo.

Kwa upande mwingine, Askofu Mwamakula amewasilisha kwa Katibu Mkuu salamu na ujumbe wa wito wa mshikamano katika matembezi aliyoyaasisi yenye lengo mahsusi la kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Katika suala hilo, Katibu Mkuu Ndugu Ado Shaibu amemuhakikishia Baba Askofu ushirikiano wa dhati kutoka ACT Wazalendo kwa sababu suala la Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ni matakwa ya Watanzania na mambo muhimu kwa ustawi wa nchi yetu.


Imetolewa na:

Janeth Rithe,
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma,
ACT Wazalendo.
06 Machi, 2021.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK