Bei ya Mbaazi Tunduru, Wakulima Wananyonywa. Uchunguzi Ufanyike.

TAARIFA KWA UMMA

UTOFAUTI WA BEI YA MBAAZI TUNDURU NA MASASI UCHUNGUZWE

Jana tarehe 16 Novemba 2022, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe, alimaliza ziara yake ya kuwasikiliza Wananchi na kuimarisha Chama katika mkoa wa kichama wa Selous kwa kuyatembelea majimbo mawili ya Tunduru Kaskazini na Tunduru Kusini.

Katika ziara hiyo, Kiongozi wa Chama ameambatana na Mawaziri Vivuli watatu: Ndugu Mtutura Abdallah Mtutura (Waziri Kivuli wa Kilimo), Ndugu Isihaka Rashid Mchinjita (Waziri Kivuli wa Nishati) na Ndugu Halima Nabalang'anya (Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara) hii ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku sita katika mikoa mitatu ya kusini mwa nchi ambayo ni Mkoa wa Kichama wa Selous, Mtwara na Lindi.

Baada ya kumaliza ziara hiyo kwenye Mkoa wa Kichama wa Selous hapo jana, Kiongozi wa Chama Zitto Kabwe leo Novemba 17, 2022 ataanza ziara kwenye mkoa wa Mtwara kwa kutembelea jimbo la Tandahimba kwa ajili ya shughuli za Ujenzi wa Chama na kuwasikiliza wananchi.

Katika ziara hiyo ya mkoa wa Kichama wa Selous, Kiongozi Zitto Kabwe na msafara wake wamepokea malalamiko mbalimbali ya wananchi yakiwa ni pamoja na wananchi kusumbuliwa na Tembo, migogoro ya Wakulima na Wafugaji, ukosefu wa wa maji kwa matumizi muhimu ya kibinadamu na kilio cha wakulima wa zao la Mbaazi kulazimishwa kuuza mazao yao katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa bei ya shilingi kati ya shilingi 600 na 700 kwa kilo tofauti na wilaya jirani ya Masasi wanaouza kilo moja kwa shilingi 1200.

Pia, katika ziara hiyo Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe alipokea malalamiko ya wanachi wa kijiji cha Likwesu Kata ya Mchoteka juu ya kutelekezwa kumaliziwa ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho kwa zaidi ya miaka tisa baada ya wanachi kushiriki ujenzi wa kuanzia hatua ya msingi hadi kwenye linta, pamoja na madai ya kuondolewa watumishi zaidi ya saba kwenye kata ya Mchoteka na kupelekwa maeneo mengine tukio linalohusishwa na sababu za kisiasa.

Akitolea ufafanuzi baadhi ya malalamiko hayo Ndugu Zitto alisema; “ACT Wazalendo, itagharamia umaliziaji ujenzi wa Zahanati ya Likwesu, iliyo katika kata ya Mchoteka kwa kuwa wananchi wa eneo hilo wanataabika kufuata huduma ya afya mbali na maeneo yao.”

Kuhusu Tembo kuvamia makazi ya wananchi Ndugu Zitto aliitaka serikali kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na hali hiyo pamoja na kuwalipa waathirika kwa mujibu wa sheria kulingana na ukubwa wa athari walizopata kutoka kwa wanyama hao.

Kwenye suala la bei ya Mbaazi Ndugu Zitto alitoa wito Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalum wa sababu za kibiashara kutofautiana kwa kiasi kikubwa katika maeneo hayo mawili ilihali wanunuzi wa zao hilo katika wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakiwa ndio hao hao wanaoununua kwenye masoko ya Tunduru.

Amesema wakulima wa Tunduru wanazalisha wastani wa tani milioni 30 za Mbaazi kwa mwaka na wanapolazimishwa kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa bei ya shilingi 700 kwa kilo kwa ujumla wao wanapoteza zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa mwaka ambayo ni zaidi ya pato la ndani la wilaya ya Tunduru.

Kiongozi wa Chama pia Alitumia ziara hii kuwaeleza wananchi kuhusu Muswada wa Bima ya Afya ambao umeondolewa Bungeni kufuatia ushauri wa ACT Wazalendo na wadau wengine ili kuuboresha na uwe na faida kwa Watanzania. ACT Wazalendo imeendelea kusisitiza umuhimu wa kutumia Hifadhi ya Jamii katika kutatua changamoto ya Bima ya Afya kwa wote.

Kiongozi wa Chama ameitaka Serikali kupitia wizara ya Afya na Wizara ya Fedha kuandaa Mkutano wa Kitaifa ili kufanya mjadala wa kina kuhusu mfumo sahihi wa Bima ya Afya kwa Wote.

Kiongozi wa Chama pia alitoa ufafanuzi kwa Wanachama wa ACT Wazalendo kuhusu suala la kutoridhishwa kwa Chama kwa mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kueleza kuhusu Maamuzi ya Kikao cha Kamati Maalumu ya Chama Zanzibar kuamua kushauriana na Wanachama wa Matawi yote zaidi ya 600 ya Unguja na Pemba kuhusu mustakabali wa Chama kuendelea au kutoendelea kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 
Imetolewa na:

Janeth Joel Rithe
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma,
ACT Wazalendo,
17 Novemba, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK