BEI ZA MBOLEA NI HATARI KWA KILIMO NA UHAKIKA WA CHAKULA. SERIKALI ISIPUUZE KILIO CHA WAKULIMA
BEI ZA MBOLEA NI HATARI KWA KILIMO NA UHAKIKA WA CHAKULA. SERIKALI ISIPUUZE KILIO CHA WAKULIMA
Msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 tumeshuhudia kupaa kwa bei za mbolea hali hii ilianza mnamo mwezi Juni na Julai mwaka jana ambapo bei zilianza kupanda kwa wastani wa asilimi 20 hadi asilimia 38 na kuadimika katika mzunguko sokoni, ilipofika Disemba hali ilikuwa mbaya zaidi licha ya kuwa mbolea ilikuwa inapatikana sokoni lakini bei ilikuwa ya juu zaidi kwa asilimia 90 hadi 150. Chama cha ACT Wazalendo kimesikitishwa sana na mwenendo mbaya usiodhibitiwa wa bei ya mbolea nchini. ACT Wazalendo tumefuatilia suala hili taarifa zinaonyesha Wastani wa bei za mbolea kwa Mwezi huu March 2022 kwa kilogramu hamsini (50Kgs) kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Mwanza, Tabora, Arusha, Ruvuma, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Geita, Njombe, Rukwa na Katavi ni kama ufuatao;
UREA TShs. 110000 hadi 13,0000 kutoka bei ya Tsh. 50000 hadi 55,000 mwezi Machi mwaka jana, ni ongezeko la shilingi 60,000 hadi 75,000 sawa na 120% hadi 136%,
Huku bei ya mbolea ya CAN(50Kgs) TShs. 84,000- 125,000 kutoka kwenye bei ya shilingi 50,000 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la shilingi 34,000 hadi 75,000 sawa na 68% hadi 150% kwa baadhi ya maeneo.
Mbolea ya DAP kwa sasa ni TShs.118,000 hadi 150,000, kutoka bei ya shilingi 62.000 sawa na ongezeko la asilimia 90 hadi 142.
NPK Tsh. 120,000 hadi 130,000 kutoka bei ya shilingi 60,000, ongezeko ni kiasi cha shilingi 60,000 hadi 70,000 sawa na asilimia 100 hadi asilimia 117.
Pia bei ya mbolea ya SA TShs. 75,000 hadi 90,000 kutoka bei ya Machi 2021 ya shilingi 38,000 ikiwa ni ongezeko la shilingi 37,000 hadi 52,000 sawa na ongezeko la asilimia 97 hadi 136.
Kabla ya hali hii ya sasa, sisi ACT Wazalendo kupitia Katibu Mkuu wa chama akiwa katika ziara Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara tarehe 22-31 Disemba 2021, tulishauri njia na hatua zitakazoenda kuwasaidia wakulima na kuokoa kilimo kutokana na athari zitokanazo kupanda kwa kasi isiyo ya kawaida ya bei za mbolea.
*Serikali imefanya nini?*
Tangu mwenendo huu ulipojitokeza hakuna hatua za maana zilizochukuliwa na serikali katika kukabiliana na mwenendo wa kupaa kwa kasi kwa bei hizo katika maeneo mbalimbali tofauti na ahadi za Serikali zilizotolewa kwa nyakati mbalimbali. Mathalani, hatua zilizochukuliwa na Serikali za kusimamisha mfumo wa ununuzi wa pamoja (bulk procument system) na kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mbolea kwa madai ya kuongeza ushindani haujasaidia kushusha kwa bei ya mbolea. Kuharakisha meli zinazobeba mbolea kushusha mzigo zinapofika bandarnii, nayo haijasaidia kupunguza bei za mbolea.
Badala yake Serikali imeliacha suala hili bila kuchukua hatua madhubuti na za maana, imebaki kulalamika na kutafuta kichaka cha kujificha kwa kuwaeleza wananchi sababu za kupanda kwa bei ni kutokana na bei ya soko la dunia.
Sababu zinazotolewa kila mara na Serikali ni dalili kuwa Serikali inakimbia wajibu wake wa msingi katika kuwasadia wananchi na kuokoa kilimo. Serikali imeamua kukichezea kilimo ambacho ndio kimeajiri nguvu kazi kubwa ya watanzania kwa wastani wa asilimia 61.
*ACT tumebaini nini?*
Utafiti tulioufanya tumebaini kuwa sababu za kupanda kwa bei ya mbolea kwenye soko la dunia sio sababu pekee inayopelekea kupaa kwa mbolea nchini kwetu.
Kwanza, taarifa zinaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na bei kubwa ya mbolea ukilinganisha nchi jirani za maziwa makuu ikiwemo Rwanda, Burundi, Malawi, DR Congo, Zambia, Uganda na Kenya, licha ya kuwa hali ya utegemezi wa mbolea kutoka nje kwa nchi hizi unakaribia kulingana.Ingetarajiwa kuwa kutokana na Tanzania kujaaliwa kuwa na bandari yake bei ya mbolea ingelikuwa chini kulinganisha na nchi zingine kama ilivyo kwa wenzetu Kenya.
Pili, serikali kufanya soko la mbolea ni soko holela lisilojali maslahi ya wananchi wake, kwa madai kuwa nguvu za mahitaji na uzalishaji ndio zitaamua hatima ya bei za mbolea nchini. Na ndio maana hata mbolea inayozalishwa ndani ya nchi bei zake zimepanda kwa kiasi kikubwa zaidi. Hakuna bei elekezi.
Vilevile, Serikali haijachukua hatua za kikodi za kudhibiti kupanda kwa mbolea nchini. Mjengeko wa gharama au bei za mbolea huchagizwa pia na tozo, ushuru wa Serikali na mamlaka za bandari. Hadi sasa hakuna hatua iliyochukulia aidha kutoa ruzuku au kufuta kodi za usafirishaji wa mbolea.
Pia, Serikali kusimamisha mfumo wa ununuzi wa pamoja wa mbolea (Bulk procument system) na kuruhusu mfanyabiashara mmoja mmoja kuagiza kadri ya uwezo wake, kumechangia ongezeko kubwa la gharama na bei ya mbolea.
*Mapendekezo ya ACT Wazalendo*
ACT Wazalendo tunaendelea kutoa rai zetu kwa kuitaka Serikali kuwanusuru wakulima kutokana na kadhia ya kupanda kwa bei ya mbolea kiholela kwa kuchukua hatua zifuatazo;
1. Serikali itoe ruzuku kwenye mbolea ili kushusha gharama na bei ya mbolea kwa wakulima wetu.
2. Kuwezesha vyama vya ushirika kununua mbolea kwa mfumo wa pamoja, kila mfanyabiashara akiingiza mbolea mwenyewe hufanya meli ziwe zinachukua uzito mdogo kwa wakati mmoja na hivyo gharama za usafiri baharini kuwa kubwa na kusababisha bei za mbolea kwa wakulima kuwa kubwa pia.
3. Serikali ipunguze au iondoshe ushuru na tozo mbalimbali za usafirishaji na uingizaji wa mbolea.Serikali irahisishe mfumo wa mamlaka ya kutoza kodi ambao unahusisha mamlaka zaidi ya moja katika kutoza kodi ya mbolea.
4. Serikali kuweka Bei elekezi ya usambazaji wa mbolea hiyo hadi kwa mlaji wa mwisho
5. Serikali kupitia shirika la Mbolea (TFC) isimamie uagizaji wa mbolea kutoka kwa wazalishaji moja kwa moja ili kunusuru wakulima.
Hatua za muda mrefu;
1. Kuweka msisitizo wa matumizi ya mbolea mbadala (mbolea zisizo na kemikali) kutoka kwa wakulima wenyewe.
2. Kuondoa utegemezi wa mbolea kutoka nje, kwa kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji ili watu waweze kujengwa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini na kuimarisha uzalishaji kwa viwanda vilivypo.
Mwisho, iwapo serikali hatochukua hatua kwa haraka, athari zinazotarajiwa kutokana na ongezeko hili la bei ya mbolea ni kubwa sana kuanzia kwenye upatikanaji wa chakula cha kutosha katika masoko ya ndani, mfumuko wa bei za bidhaa nyingi za ndani,nguvu ya kununua ya wakulima wengi itapungua, Usalama wa chakula wa nchi utatetereshwa na matumizi makubwa ya pesa za kigeni katika kununua chakula kufidia nakisi itayotokana na kushuka kwa uzalishaji. Kwahiyo, ni muhimu Serikali kuingia suala upesi sana kabla athari hazijakuwa kubwa zaidi.
Imetolewa na;
Ndg. Mtutura Abdallah Mtutura,
Msemaji wa Kisekta wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
ACT Wazalendo.
16 Machi, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter