Buriani Benald Membe, mwanademokrasia

Buriani Bernard Membe, Mwanademokrasia

Mama Dorcas Membe pamoja na wanao
Ndugu Wafiwa
Viongozi na Waombolezaji wenzangu
Ndugu Watanzania

Nimepewa nafasi niseme machache ya kumuaga mzee wangu Bernard K. Membe, ni mzee wangu sana. Nimepata tabu kutafuta la kusema kati ya mingi ninayomjua kwayo, naamini wengine watayasema mengi kati ya vipawa vyake. Mimi nitajikita kwenye jambo moja tu, kumuelezea Bernard Membe MWANADEMOKRASIA.

Mwanamakakati wa Demokrasia

Mzee wangu Bernard Membe, BM, ulikuwa mwanasiasa mwanamikakati. Nilikufahamu mara ya kwanza kwa sifa yako hii, pale mwaka 2005 mlipokuwa mnapambana kwa ajili ya kupata mgombea atakayemrithi Rais Mzee Benjamin Mkapa kulikuwa na maneno na minong’ono ya chini ya kapeti kuwa mgombea wenu asingeteuliwa mngejiunga nasi tuliokuwa upande wa upinzani.

Ni hali ya kawaida kuwa na maneno ya namna hii kila nyakati za uchaguzi. Wakati mwengine maneno ya namna hii huwa kweli na wakati mwengine haitokei. Wakati wenu huo haikutokea, nadhani kwa sababu mgombea wenu alishinda.

Hata hivyo kitendo cha wewe kuja kupaki gari yako mbele ya ofisi ya makao makuu ya chama changu cha wakati huo, na kuzungumza na mmoja wa waliokuwa wabunge wa chama hicho na kumpa salamu za kumletea mwenyekiti wetu, “kwamba tujiandae mnakwenda Dodoma, demokrasia ikikanyagwa tuwapokee”, kilikuwa ni kitendo cha kimkakati mno.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa ulikifanya mchana hadharani, ukijua kuwa ni lazima macho mengi yalikuwa yanakuona, lengo ni kutengeneza mazingira ya wakubwa wa chama chako kupata ujumbe mahususi uliokusudia. Tukio hili kwangu lilikuwa ni mafunzo ya mwanzo ya uanademokrasia na uanamikakati wako. Ni wanasiasa wachache sana wana kipaji cha kukusanya kwa wakati mmoja uanasiasa na uanamipango ya kisiasa. Wewe uliweza kuwa nazo hizo sifa zote.

Mtetezi wa Watu, Haki na Demokrasia

Mzee wangu, BM, ulikuwa mstari wa mbele kutetea haki za Watanzania wote. Nakumbuka mwaka 2006, nikiwa ndio tu nimechaguliwa kuwa mbunge na wewe ukiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi yetu, mkoa wa Kigoma ulikumbana na operesheni ya idara ya Uhamiaji, ambapo familia moja katika kijiji cha Kigalye, Jimbo la Kigoma Kaskazini ilituhumiwa kwamba sio raia wa Tanzania. Familia nzima ikawekwa kwenye meli kurudishwa kulikoitwa kwao, huko DRC Congo.

Familia hii ilitendewa hayo kwa kuonewa tu kwa sababu ilisapoti upinzani, ilinisapoti mimi. Nilikuletea malalamiko kwa njia ya simu kuwa familia ile ilisakiziwa tu kwa sababu za kisiasa na ndio maana huko DRC kwenyewe Serikali imekataa kuwapokea, maana sio raia wao.

Hukusita kuchukua hatua mara moja ya kuitendea haki familia hii, licha ya kwamba ulipaswa kukanyaga miguu ya wakubwa wa chama chako ndani ya mkoa wa Kigoma. Ulijali haki za watu zaidi kuliko maslahi finyu ya kisiasa. Watu wengi wana mifano mingi ya namna uliwatazama Watanzania kwa Utanzania wao na sio kwa vyama vyao.

Una Misimamo, Ulitupigania Sote

Mzee wangu, BM, ulikuwa ni mtu mwenye misimamo. Hukuogopa kusema lile uliloliamini, ulikuwa na ‘pride’ ya kutokubali kutii mambo kwa sababu tu mkubwa kataka, na hukujali madhara ya kusimamia hayo. Wakati mgumu sana wa maisha yako kisiasa ulikuwa ndio wakati mgumu sana wa kisiasa hapa nchini. Ulisimama na watetezi wa demokrasia na watetezi wa haki za binaadam bila kupepesa macho.

Ulikuwa nasi kila tulipopata maswahibu, kiasi cha kukuingiza wewe mwenyewe kwenye maswahibu uliyokabiliana nayo kwa namna unayojua wewe mwenyewe. Mpaka umauti unakufika hukuacha kulionyesha Taifa na dunia namna tunapaswa kuhusiana hata kama tunapingana kimawazo na mirengo ya kisiasa.

Ulipambana kulinda heshima yako dhidi ya watu waoga ambao badala ya kukabili hoja zako waliamua kutuma mtu kukuchafua wewe pamoja na wote tuliokuwa na mawazo mbadala, kwa Lengo la kutunyamazisha sote. Kesi yako kupinga kuchafuliwa ulitusemea na sisi wenzako wote.

Ulitupigania sisi wote dhidi ya tabia ya hovyo kabisa iliyojitokeza katika nchi yetu. Tabia ya watu wenye mamlaka kutuma wahuni kutukana viongozi wenzao. Tabia ya vyombo vya dola, vingine vyombo vya usalama, kuendekeza upuuzi na hata kuwezesha tabia hiyo chafu kabisa. Ni aibu kuwa mitambo ya baadhi ya “vyombo” vyetu ilitumika kuchapisha mambo ya namna ile.

Wapo hapa watu ambao walifadhili na kushabikia upuuzi uliopigana kuupinga mpaka mahakamani na ukashinda. Nao eti wanakulilia. Nao eti wanakuaga. Naamini kifo chako hiki na mazishi yako haya yatazika tabia zile ambazo hukukubali kamwe ziwe ni sehemu ya utamaduni wetu wa kisiasa. Nataraji hata kwa mioyoni mwao watu wale watajuta na kukuomba radhi ukiwa kwenye umauti.

Mzee wangu BM, Jambo moja kubwa umetufunza ni kuishi nasaha za Mtume Muhammad (SAW) kwamba “uonapo jambo baya lizuie kwa mikono yako, ama ulikemee kwa mdomo wako, na kama huwezi basi angalau unune”. Wewe sio tu ulizuia na ulikemea upuuzi ule bali ulihakikisha unatoa mfano kwa mpuuzi aliyebebeshwa upuuzi ule ili kuwa funzo kwa wapuuzi wengine.

Bernard Membe wa ACT Wazalendo, Mwanademokrasia
Mzee wangu BM, mimi na wewe ni wapenzi wa kusoma vitabu kuongeza maarifa, mara zote ulipenda kunialika kwenye maktaba yako kubwa ya kijijini kwako Rondo, mahali ambapo pamoja na kuongeza maarifa ulipatumia kunieleza dhamira yako ya kutaka kujiunga nasi ACT Wazalendo, ukivutiwa na namna chama chetu kilivyotoa mapokezi ya heshima kwa mzee wangu mwengine, Maalim Seif Sharif Hamad, na wenzake kutoka chama cha CUF.

Nilipenda utaratibu uliotumia kujiunga nasi, ukituandikia barua ya kueleza kwa kina kwanini umeichagua ACT Wazalendo, pamoja na mengine, ukituhimiza tusiache kutengeneza mazingira ya kutoa fursa wa kila mhanga wa Siasa na Demokrasia kupata nafasi ya kuendelea kufanya siasa kupitia ACT Wazalendo. Tukio hili lilikuwa kilele cha Uanademokrasia wako.

Ulikaa nasi katika ACT Wazalendo kwa muda mfupi sana wa maisha yako ya kisiasa. Lakini muda huo mfupi ulikuwa na mafunzo makubwa sana kwetu. Ucheshi wako uliamsha ari zetu za kazi. Kila jambo lililokuwa linatokea ulikuwa hukosi mfano wa kutupatia kulinganisha mazingira ya sasa na wakati ukiwa ama serikalini au katika majukumu yako ya nje ya nchi.

Namna ulivyoamua kujiunga nasi ilikuwa ni mchakato wa mafunzo makubwa na pia hata namna ulivyoamua kutoka na hatimaye kurejea chama chako ulichokuwapo ilikuwa na mafunzo pia. Waandishi wa habari walipokuandama kutaka useme sababu za kuondoka chama chetu na kurejea chama chako cha muda wote uliwaambia kuwa umetuandikia barua yenye kila kitu.

Ni kweli ulituandikia barua yenye mahusio ya namna ya kujenga Chama cha Siasa cha kitaifa kitakachoweza kushika Dola siku za usoni. Tunafuata mahusio hayo na kwa uwezo wake mola tutakupa tabasamu siku moja tutakaposhika na kuongoza dola la nchi yetu hii nzuri ya Tanzania.

Umetimiza Wajibu, Upumzike Pema Membe

Mzee wangu BM, tuko hapa tunakuaga wewe, mwanademokrasia na mwanasiasa mahiri katika Taifa letu, ambaye umekuwa sehemu ya mijadala ya kitaifa katika nchi yetu. Umetumikia nchi yako kwa uwezo wako wote katika nafasi zote ulizopewa bila ubaguzi wa kisiasa. Umekuwa mtetezi wa haki na demorasia ya vyama vingi, haki za binaadam na mzalendo wa kweli wa nchi yako.
Tangulia BM. Umeacha simanzi kubwa kwa Watanzania na Waafrika. Umeacha simanzi kwa Jumuiya ya Kimataifa ambayo uliitumikia kwa weledi wa hali ya juu. Zaidi umeacha simanzi kubwa kwa Mama yangu Dorcas na wadogo zangu Cecy, Richard na Dennis. Umeacha simanzi kwa wanaLindi wenzako ambao walikupenda sana.Wajibu wetu ni kusherehea maisha yako. Maisha yako yanaeleza urathi wako kwa uwazi kabisa. Tutaenzi kazi zako na misimamo yako ya kutetea watu bila kujali itikadi zao na bila ubaguzi. Ni wajibu wetu vijana na marafiki zako kuhakikisha kuwa MWANADEMOKRASIA MEMBE HAUSAHAULIKI.
 
Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.

Upumzike kwa amani mzee wangu, Bernard Membe.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Viwanja Vya Karimjee, Dar es salaam
Mei 14, 2023

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK