BURIANI PROF. NGOWI. KIFO CHAKO KIMEACHA FUNZO SEKTA YA USAFIRISHAJI NCHINI

BURIANI PROF. NGOWI. KIFO CHAKO KIMEACHA FUNZO SEKTA YA USAFIRISHAJI NCHINI

Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Prof. Honest Ngowi kilichotokea siku jana tarehe 28 Machi 2022 baada ya gari aliyokuwa akisafiri nayo kuangukiwa na kontena. Kifo cha Prof. Ngowi kimeacha pengo kubwa katika jamii yetu na nchi kwa ujumla.
Kwa masikitiko makubwa chama chetu kimetafakari matukio ya ajali katika sekta hii ya uchukuzi hususan katika suala la usafirishaji wa mizigo katika makontena na magari ya mafuta kuuwa watu wengi na kuendelea kuhatarisha usalama wa wananchi. Serikali bado haijaonyesha juhudi za kumaliza matukio haya kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi.
Tukio hili linatokea katika nyakati ambazo sekta ya usafirishaji iko katika ukuaji kufuatia kufunguka kwa fursa katika sekta ya biashara na nchi jirani kuitegemea Tanzania katika kupitisha mizigo yao.
Kwa sasa, kiasi kikubwa cha makontena hapa nchini husafirishwa kwa njia ya magari maalum ya kubeba makontena. Hata hivyo magari hayo hutumia njia ya barabara za kawaida sambamba na magari, mabasi ya abiria na magari madogo ya watu binafsi.
Katika nchi nyingi, sehemu kubwa ya makontena husafirishwa kwa njia ya reli na tukio hili linatukumbusha umuhimu wa kumaliza na kuanza kutumika kwa reli ya Standard Gauge (SGR) na ili kuwezesha reli ya kati kuweza kubeba mizigo ya makontena.
Tafiti na takwimu kutoka nchi zenye uzoefu kwenye sekta ya usafirishaji ya mizigo mikubwa, zimeonyesha kuwa ni gharama nafuu zaidi kusafirisha mizigo pamoja na makontena kwa njia ya reli kulinganisha na kwa magari.

Pia, usafiri kwa njia ya reli ni rafiki zaidi kimazingira kwa sababu ya kuunguza kiwango kidogo cha mafuta yanayotumika kwa kila tani moja inayosafirishwa.
Ajali ya Professa Ngowi umewashtua wadau wote wa usafiri na wananchi juu ya usalama barabarani katika sekta ya usafirishaji wa mizigo hasa katika kuhoji sera ya ukaguzi wa mara kwa mara kutumia mifumo ya teknolojia za kisasa. Upo ulazima wa kutengeneza program itakayohakikisha ukaguzi wa uhakika na kufaa hali za vyombo vya usafiri vya ndani ya nchi.
ACT Wazalendo inamuombea marehemu Professa Ngowi na Dereva wake makazi mema katika safari aliyotangulia kuenda na ambayo sote itatuwajibikia.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo katika kuepusha ajali barabarani:
i. Sera ya usafirishaji ipitiwe upya na kutizama namna ya kufanya mabadiliko ili asilimia kubwa ya usafirishaji wa makontena ufanywe kwa njia ya reli.
ii. Kuondoshwa kabisa uchukuzi wa makontena ndani na katikati ya miji na badala yake; makontena yasafirishwe kwa reli hadi kwenye vituo vilivyopangwa vya ICD. Ikibidi makontena kusafirishwa kwa magari, usafirishaji huu ufanywe nyakati za usiku.
iii. Mamlaka huzika zitumie sayansi ya kisasa itumike katika kuimarisha na kufuatilia usalama wa sekta ya usafirishaji.
iv. ACT Wazalendo inatoa wito wa kuharakisha kumalizwa kwa Mradi wa Reli ya kisasa (SGR) na ili ziweze kubeba makontena yendayo ndani na nje nchi kwa sababu reli ni usafiri nafuu na salama kwa wananchi na kwa mazingira.
Mwisho, wakati taifa linapomlilia Prof Honest Ngowi ni wakati muafaka kwa watanzania kutathmini sekta yetu ya usafirisha kupunguza ajali zinazotokana na maandalizi hafifu ya kukabiliana na changamoto za teknolojia ya uchukuzi.

Imetolewa na:

Ally Saleh
Msemaji wa Kisekta ya Habari, Teknolojia, Mawasiliano na Usafirishaji [email protected]
29 Machi, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK