Tunachokisimamia

Gharama ya ilani yetu

Gharama ya ilani yetu

Ahadi za ACT Wazalendo Jamhuri ya Muungano ZITATEKELEZWAJE?

1. Elimu ya Juu: Kufuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu na kuanza kutekeleza Mfumo mpya wa kugharamia Elimu ya Juu. Serikali italipia Ada ya Masomo (Tuition Fee), Fedha za Vitabu (Stationeries), na gharama za Mafunzo kwa Vitendo (Field Studies/Internship) kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye Chuo Kikuu. Wanafunzi watachukua mikopo, Kwa wanaotaka, Kwa ajili ya gharama za maisha tu ( Meals and Accommodation ). Mfumo mpya utaanza Mwaka wa Masomo 2021/2022.

FEDHA ZA KUTEKELEZA ZITATOKA WAPI?

- Gharama za Elimu Ufundi na Elimu ya Juu zitatokana na Mapato ya Tozo ya kuongeza ujuzi ( Skills Development Levy - SDL ). Tozo hii itatozwa kutoka Waajiri wa sekta binafsi na sekta ya Umma Kwa kiwango cha 2% ya gharama za mishahara. Sasa hivi tozo hii inatozwa kwa sekta binafsi peke yake Kwa kiwango cha 4% ya gharama zote kwa Wafanyakazi walioajiriwa na kampuni husika ( SDL is charged based on the gross pay of all payments made by the employer to the employees employed by such employer ). Baada ya marekebisho ya kupanua wigo wa walipaji, Serikali itakuwa na uwezo wa kukusanya shilingi Bilioni 470 kila Mwaka. Mapato haya yataongezeka kulingana na kuongezeka kwa shughuli za Uchumi Nchi na Ajira nyingi zaidi kutengenezwa.


2. Bima ya Afya kwa Wote: Kuboresha mfuko wa Bima ya Afya kwa kuunganisha na mifumo ya Hifadhi ya Jamii, ili kila Mtanzania anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya Afya moja kwa moja. Kwa mfumo huu, mfuko wa Bima ya Afya utaweza pia kupata fedha kwa wakati na kulipa watoa huduma kwa wakati. Bima ya Afya ni haki ya kila Mtanzania. Itaisimamia kikamilifu haki ya kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya yenye kumpa kinga ya matibabu bila kujali hali yake ya kiafya (wakati wa kujiunga na bima).

FEDHA ZA KUTEKELEZA ZITATOKA WAPI?

- Kupitia vyama vya Ushirika na vikundi vya uzalishaji vya Wananchi haswa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Serikali itaanzisha Mfumo wa kuchangia wananchi wanaochangia Skimu ya Hifadhi ya Jamii. Serikali itatenga Fedha kutoka kwenye Bajeti kila Mwaka kuchangia michango ya Wananchi kwenye Hifadhi ya Jamii ( matching scheme). Kwa mfano katika mchango wa Shs 30,000 kwa Mwezi, Serikali itamchangia Mwananchi Shs 10,000. Kwa njia hii kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya Kama Fao katika Skimu ya Hifadhi ya Jamii. Skimu hii itawezesha Taifa kuwa na Akiba kubwa kwa uwiano wa Pato la Taifa (savings - GDP ratio) na hivyo kuwezesha uwekezaji mkubwa na wa muda mrefu kufanyika. Kwa Makadirio ya Watu Milioni 6 watakaojiunga na Skimu ya Hifadhi ya Jamii, Mfuko utakuwa makusanyo ya Shilingi Trilioni 2.2 kwa Mwaka, katika hizo Shilingi Bilioni 648 zitachangiwa na Serikali kutoka kwenye Bajeti.

3. Maji safi na salama kwa kila Mtanzania: Kuwekeza kiasi cha  shilingi Trilioni 10 ndani ya miaka mitano, wastani wa Shilingi Trilioni 2 kwa kila mwaka, kwenye kumaliza kabisa tatizo la maji safi na salama kwa Wananchi. Hii ni pamoja na kujenga na kupanua miundombinu ya maji safi na maji taka.

FEDHA ZA KUTEKELEZA ZITATOKA WAPI?

- Gharama za Ujenzi wa Miradi ya Maji zitagharamiwa na Tozo Maalumu ya Matumizi ya Mafuta ya Petroli. Serikali itachukua Mkopo nafuu wa Muda mrefu wa Shilingi Trilioni 10 kutoka Benki za Maendeleo ili kutekeleza mradi kwa mara moja na Mapato ya ‘fuel levy’  yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa. Tozo ya shilingi 200 kwa kila lita ya Mafuta itazalisha Jumla ya shilingi Bilioni 700 kila Mwaka zinazoweza kutumika kulipa mkopo wa muda mrefu wa miaka 15.

4. Barabara ya Korosho: Kuwezesha Ujenzi wa barabara ya korosho (cashew ring road) – Nangurukuru – Liwale – Nachingwea – Masasi – Newala – Tandahimba – Mtwara – Lindi - Nangurukuru kutoka mapato ya ushuru wa korosho kwa kutumia mfumo wa “development finance” ili kufungua wilaya zinazolima korosho. Vile vile kufungua Wilaya ya Liwale kwa kufungua barabara za Songea-Liwale na Liwale-Morogoro

FEDHA ZA KUTEKELEZA ZITATOKA WAPI?

- Gharama za Ujenzi wa Barabara ya Korosho (Cashew Ring Road) zitalipiwa na 50% ya Mapato ya Ushuru wa Korosho (exports levy) ambapo Serikali itachukua mkopo nafuu wa muda wa kati ili kupata fedha za ujenzi wa barabara hiyo mara moja na mapato ya exports levy yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa. Ushuru wa Korosho unakadiriwa kuingiza mapato ya zaidi ya shilingi Bilioni 245 kila Mwaka ambazo nusu yake inaweza kulipa mkopo wa barabara hiyo na barabara za Songea-Liwale na Liwale-Morogoro kwa muda wa miaka 10.

5. Kilimo cha kimapinduzi: Kusimamia Ujenzi wa mabwawa makubwa 5 ya kuzuia mafuriko na kujenga skimu kubwa za umwagiliaji zenye jumla ya hekta 1,000,000 zitakazowezesha Kilimo cha kimapinduzi, mamilioni ya ajira, uzalishaji wa mazao ya mafuta ya kula, sukari na chakula hivyo kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza sukari na mafuta ya kula kutoka nje, na kuongeza Mapato ya Fedha za Kigeni.

FEDHA ZA KUTEKELEZA ZITATOKA WAPI?

- Gharama za Miradi mikubwa ya Umwagiliaji zitalipiwa kutoka uwekezaji wa skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima kama uwekezaji wa Skimu wa muda mrefu. Jumla ya Shilingi Trilioni 2.5 zitawekezwa kwenye miradi hii ya uwekezaji kutoka Skimu ya Hifadhi ya Jamii kama Uwekezaji wa kuongeza shughuli za uchumi Kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na Viwanda vya kuongeza mazao ya Kilimo.

Rudi kwenye ilani

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK