Hadaa na Uzembe wa Serikali Unaangamiza Elimu nchini

Hadaa na uzembe wa Serikali katika utekelezaji wa Sera ya Elimu bila malipo; unaangamiza Elimu nchini.

Utangulizi

Kwa takribani wiki tatu (3) mfululizo hususani kwa mwezi Januari 2023, kumeibuka maswali, maoni, malalamiko na vilio kuhusu sekta ndogo ya Elimu nchini. Mambo yaliyopelekea kuwepo kwa mitazamo na malalamiko hayo ni pamoja na matokeo yasiyoridhisha ya mitihani ya darasa la nne, darasa la saba na kidato cha pili. Pia suala jingine ni kuongezeka kwa gharama za ada na michango kwa shule binafsi kwa upande mmoja na kukithiri kwa michango na tatizo la watoto wengi kutohudhuria shule (kidato cha kwanza) kwa kukosa mahitaji kwa shule za Serikali. Kwa kutazama changamoto hizi ni wazi kuwa ni ishara tosha za kutokuwa na mazingira bora ya utoaji wa elimu na kulegalega kwa Serikali katika kutekeleza kwa ahadi zake (hadaa).

Ingawa mambo haya yamekuwa na mjadala kwa wiki za hivi karibuni, yapo mambo mengine yanauhusiano wa karibu au ni ishara nyingine za ubovu wa mfumo wetu wa elimu na uzembe wa Serikali katika kusimamia sekta ya elimu nchini ili kutimiza shabaha ya kuwa na mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mtazamo chanya na kuleta maendeleo ya taifa.
ACT Wazalendo tumeamua kuangalia maeneo yafuatayo ambayo ni wazi Serikali inatoa ahadi hewa na kufanya uzembe unaopelekea kuangamiza hatima ya elimu yetu nchini na umma hauyatazami kwa uzito mkubwa licha ya kuwa ni tishio endapo hayatachukuliwa hatua za haraka.


1. Matokeo mabaya ya darasa la nne na kidato cha pili na idadi ya wanafunzi kuacha shule

Tumeshuhudia tambo za Serikali za kuongeza uandikishaji wa watoto kwenda kidato cha kwanza na darasa la kwanza mwaka huu na miaka yote huko nyuma. Hususani tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimu bila malipo (ada). Hata hivyo, kupanuka kwa kasi katika sekta ya elimu kumekuwa hakuendani na uboreshaji wa matokeo ya ujifunzaji.
Mwenendo wa matokeo ya mitihani kwa darasa la nne, darasa la saba na kidato cha pili yanaonyesha ingawa watoto wengi zaidi wanahudhuria shule leo kuliko wakati mwingine wowote nchini Tanzania, hawajifunzi (kuelimika na kuongeza maarifa, stadi, ujuzi na uwezo).

ACT Wazalendo tumetazama kwa kipindi cha miaka miwili kumekuwa na hali ya kushuka kwa kasi kwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la nne, darasa la saba na kidato cha pili.
Katika matokeo yaliyotolewa na Baraza la mitihani la Taifa (NECTA) kwa darasa la nne yameonesha kuporomoka kwa kasi kubwa kutoka 86.30% mwaka 2021 hadi 82.95% mwaka 2022 ambao ni sawa na wanafunzi 271,900 watarudia darasa. Ukiachilia mbali wanafunzi 120,000 ambao hawakufanya mtihadi licha kuwa walisajiliwa.
Aidha, matokeo ya darasa la saba kuna mporomoko wa 2.35% kutoka 81.9% 2021 hadi 79.6% mwaka 2022 ambapo jumla ya wanafunzi 200, 203 wameshindwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Vilevile, matokeo ya kidato cha pili yameporomoka kwa 7.14% kutoka 92.32% mwaka 2021 mpaka 85.18% mwaka 2022 huu ni mporomoko mkubwa wa matokeo ambao haujawahi kutokea katika kipindi cha hivi karibuni. Zaidi ya wanafunzi 55,211 wakiwemo wasichana 24,803 hawajafanya mitihani licha ya kusajiliwa, achilia mbali wanafunzi alfu tisini na tano ambao watatakiwa kukariri darasa kama ilivyoelekezwa na Waraka wa Elimu na. 2 wa mwaka 2018 unaoelezea kuhusu Kukariri darasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.


Hii inaonesha kuwa
 Kuna Idadi kubwa ya mdondoko wa wanafunzi kuanzia darasa la nne mfano kwa miaka miwili tu 2021 na 2022 wanafunzi zaidi ya laki mbili na arobaini (240,000) hawajafanya mitihani licha ya kusajiliwa kufanya mitihani hiyo. na kidato cha pili kwa mwaka 2022 pekee wanafunzi 55,211 hawajafanya mtihani licha ya kusajiliwa kufanya mitihani hiyo.

 Kuporomoka kwa kasi katika matokeo ya darasa la nne, darasa saba na kidato cha pili.

2. Kuhusu elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Katika jitihada za kuhakikisha Wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu bila kubaguliwa Serikali ilileta mkakati wa Elimu Jumuishi wa 2021/2022 hadi 2025/2026 ambao ulizinduliwa rasmi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka Januari 28/2022.
Kwa bahati mbaya sana mpango mkakati huu si jumuishi bali ni uunganishi kwani unawaunganisha wanafunzi darasani lakini hauwajumuishi katika kupata maarifa kutokana na mazingira na nyenzo za kufundishia na kujifunzia ambao kwa hakika hautatui tatizo la msingi la kuachwa nyuma wanafunzi wenye mahitaji maalum kwenye kupata elimu kama vile wenye uoni hafifu, wanafunzi wenye uziwi, wanafunzi wenye ulemavu wa viungo na wale wenye ulemavu wa ngozi.
Katika jamii kubwa ya kitanzania bado watoto wengi wenye ulemavu hawapati haki ya kupata elimu, kutokana kasumba za baadhi ya wazazi na wanajamii na ukosefu wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kwa hivyo hata baada ya kuwa na mkakati huu “Unganishi” ambao si Jumuishi bado watoto wengi wenye mahitaji maalum wanakosa haki ya kupata elimu kwa sawa.
Mathalani shule nyingi hazina miundombinu jumuishi inayofaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum hali inayofanya watoto wenye mahitaji maalum kusoma mbali na maeneo yao, Kutokana na uhaba wa waalimu wataalamu wa watu wenye mahitaji maalum inapelekea watoto wengi wenye mahitaji maalum kushindwa mitihani na kukariri darasa hali inayosababisha kushindwa kuendelea na masomo.
Mfano Mkoani Tanga katika shule ya Tanga Technical School ambapo wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka sehemu mbalimbali za mkoa huo zaidi ya 90% wameshindwa mtihani wa kidato cha pili 2021/2022 kutokana na uhaba wa waalimu wa kada hiyo.

3. Kukithiri kwa michango shuleni na kadhia ya watoto wengi kutohudhuria shule kwa kukosa mahitaji.

Azma ya Serikali kupanua fursa ya kupata elimu ya msingi na sekondari kwa kuondoa vikwazo vya gharama kutoka kwa mzazi ilikuwa na ni njema kwa hakikisha hata watoto kutoka familia zenye vipato vya chini wanapata elimu.
Lakini namna Serikali inavyotekeleza mpango huo ndio unaibua hofu na kuacha wasiwasi ikiwa iliahidi mpango huo ili kupata kuungwa mkono kwenye chaguzi mbalimbali bila kuwa na dhamira ya kweli inayokusudia kumuandaa mtoto wa kitanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali. Matokeo ya uzembe na utekelezaji duni wa sera hii unapelekea kuzalishia changamoto nyingi sana. Miongozi mwa changamoto hizo ni uhaba wa vyombo vya madarasa, upungufu wa walimu, upungufu mkubwa wa vitendea kazi.
Tumeshuhudia idadi kubwa ya watoto waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza Januari 2022 wanachelewa kuripoti shuleni kwa kukosa mahitaji muhimu kama vile sare, na michango mingine ambayo imeainishwa katika fomu zao za kujiunga na shule (joining instructions)
Kutokana na hali ngumu ya maisha wazazi wengi hawamudu gharama zinazoanishwa jambo linalopelekea watoto wengi hadi leo bado hawajaanza kwenda shule licha ya kupangiwa shule za kuripoti.
Mfano katika baadhi ya shule za kutwa za mkoa wa Arusha na Moshi mkoa wa Kilimanjaro mwanafunzi anatakiwa kutoa pesa ya mitihani ya kila wiki shilingi 1,000, pesa ya chakula 16,000 kwa mwezi, pesa ya kuchangia walimu wa sayansi shilingi 300 kila siku.
Mambo yote haya yanasababishwa na.

a) Upungufu mkubwa wa walimu nchini, hadi Machi, 2022 mahitaji ya walimu katika Shule za Msingi ni 274,549 kwa kutumia uwiano wa 1:60 (Mwalimu mmoja kwa wanafunzi 60) walimu waliopo ni 173,591 na upungufu ni 100,958 sawa na asimilia 36.77 ya mahitaji. Aidha, mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa Shule za Msingi ni walimu 3,631, waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,143 sawa na asilimia 59.02 ya mahitaji. Vilevile, mahitaji ya walimu kwa Shule za Sekondari ni 159,443 waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 74,743 sawa na asilimia 46.87.

b) Upungufu wa vitabu vya kiada na ziada kwa shule za Msingi na Sekondari na Changamoto ya Miundo mbinu. Kuna upungufu mkubwa wa Matundu ya Vyoo kwa mujibu wa taarifa ya BEST 2019 inaonesha kuwa upungufu ni matundu 175,732 hivyo Wavulana 60 wanatumia tundu 1 la choo na si 1:25 kama taratibu zinavyotaka na Wasichana 1:20 na Upungufu wa Nyumba za Walimu takribani 198,439.

c) Waraka wa Elimu na.3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimu msingi bila malipo unatoa mwanya wa michango mbalimbali ikiwemo nafaka au pesa, baadhi ya Shule masomo ya ziada na mitihani inachangiwa kwa kila wiki, hali inayofanya baadhi ya wazazi kushindwa kumudu na kusababisha watoto kukatisha masomo.

d) Mkakati wa Elimu Jumuishi wa 2021/2026 hautoi suluhu kwa changamoto ya kutoa fursa sawa kulingana na uhitaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum. mkakati huu kwa bahati mbaya utazidisha kupungua kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwenye mfumo rasmi wa elimu.

e) Wanafunzi wenye mahitaji maalum idadi yao ni kubwa kuliko Shule zilizo na Miundo mbinu inayoweza kukidhi mahitaji yao, mathalani shule zote zilizotengenezwa kwa pesa za UVIKO-19 hazina mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo jumla ya vyumba vya madarasa 15,000 vimetengenezwa.
Msimamo wa ACT Wazalendo kama ilivyosisitiza katika ilani ya uchaguzi, ambapo pamoja na mambo mengine ili kukabiliana na changamoto hizo;

i. ACT-Wazalendo inasisistiza vitabu na zana nyingine za kufundishia na kujifunzia vinatolewa bure kwa kila shule za Serikali kwa ubora na wakati sahihi.

ii. Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu na kuwapunguzia mzigo waalimu ACT-Wazalendo inaitaka serikali kuajiri waalimu 30,000 kila mwaka, kwa kuwa nchi haina sababu ya kuwa na uhaba wa waalimu, tunaamini ni uzembe na kutokujali kwa Serikali kwani kila mwaka kodi za wananchi zinatumika kusomesha wanafunzi katika vyuo vikuu kwa mikopo ni ajabu kuwa na uhaba wa waalimu wakati tayari tunao vijana walioandaliwa kuondoa tatizo hilo wapo mitaani, kuna upungufu wa zaidi ya walimu 100,958 kwa shule za msingi tu na upungufu wa zaidi ya waalimu wa sekondari 74,743 na upungufu wa zaidi ya waalimu 2,143 wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, na kila mwaka wanafunzi wanaongezeka. Hii inaonesha namna gani serekali haina nia ya dhati yakuendeleza sekta hii nchini.

iii. Pia ACT-Wazalendo tunasisitiza ujenzi wa Vyuo vya ufundi VETA kila mamlaka ya serikali za mitaa, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji ili watoto wanaomaliza kidato cha nne wapate elimu ya ufundi kwa urahisi na gharama zote zitagharamiwa na serikali.

iv. Kuhusu haki na stahiki za walimu ni kipaumbele cha ACT Wazalendo, hivyo tunaitaka Serikali kuhakikisha waalimu wanapata maslahi bora, mazingira mazuri ya kuishi na kufanya kazi na fursa za kuongeza taaluma na kupanda madaraja kwa wakati, kwa kuwa bila kufanya haya ari ya kufanya kazi hupungua na hivyo kudumaza utoaji wa elimu.

v. Tunaitaka Serikali ije na mkakati maalum wa kisera ambao ni jumuishi kweli utakaohakikisha watu wenye mahitaji maalum wanapata haki sawa ambapo utahusisha kuwajengea uwezo waalimu, kuajiri waalimu na kutoa zana za kutosha kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

vi. Ruzuku ya Wanafunzi iboreshwe toka 10,000/= ya Shule ya Msingi hadi 20,000/= ili kukidhi ununuzi wa Vitabu na vifaa vingine Shuleni.

vii. Serikali iharakishe mchakato wa upatikanaji Sera mpya ya Elimu itakayoendana na maendeleo ya Dunia ya sasa Mabadiliko yoyote ya Sera yaende sambamba na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa Sera hiyo hususan Walimu.
viii. Tunaitaka Serikali idhibiti wimbi kubwa la mdondoko wa wanafunzi wakiwemo watoto wa kike na wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuwaondolea mzigo wa michango mbalimbali kwani ripoti ya NPS ya mwaka 2022 inaonesha kuwa wanafunzi wanaacha shule kwasababu ya Ugumu wa maisha, ndoa, maradhi, mimba za utotoni, na umbali wa zilipo shule.

Ndg. Riziki Shahari Mngwali
Twitter:
Msemaji wa sekta ya Elimu
ACT Wazalendo
25 Januari 2023.

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK