Hakuna Elimu bila Walimu, Serikali imalize tatizo la ukosefu wa Walimu:

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA ACT WAZALENDO NDG. RIZIKI S. MNGWALI KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA SERIKALI YA WIZARA YA ELIMU KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023
Utangulizi:
Ndugu Waandishi wa Habari,

Jana tarehe 10 Mei 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipokea na kuanza kujadili hotuba ya bajeti Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo itajadiliwa kwa siku mbili (2). Bajeti ya Wizara ni nguzo muhimu katika kugharamia utoaji wa huduma ya elimu hapa nchini. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni mshauri mkuu wa Serikali kuhusu mfumo wa elimu, hivyo hutoa miongozo kwa taasisi za elimu na mashirika yanayochangia katika malengo ya Serikali kuhusiana na maendeleo ya elimu. Majukumu makuu ya Wizara ni kupanga mikakati, sera na mipango ya mageuzi na maendeleo ya elimu; na kuandaa rasimu ya kanuni na taratibu, na kusimamia utekelezaji wake.
Kutokana na umuhimu wa bajeti ya Sekta ya Elimu, wananchi na wadau wa maendeleo wameifuatilia hotuba hii na kutoa maoni yao kuhusu vipaumbele vya Wizara. Kwa umuhimu huu, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Elimu tumefanya uchambuzi wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2022/23. Katika hotuba hii, uchambuzi wetu utahusisha maeneo nane (8) kuhusu bajeti ya Elimu ya mwaka huu.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Bajeti ya Elimu kwa kawaida inashughulikiwa na Wizara mbili, Wizara iliyo chini Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mapema mwezi Aprili, chama chetu cha ACT Wazalendo kilitoa mtazamo wake na maeneo ya kipaumbele kupitia Msemaji wa Sekta ya TAMISEMI na Maendeleo Vijijini yakiwemo baadhi ya mambo yanayoangukia kwenye sekta ya Elimu. Hotuba yetu ya leo imelenga Sekta ya Elimu kwa muktadha wa majukumu na vipaumbele vinavyotokana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

1. Usimamizi mbaya kwenye Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari:
Mwaka 2016, Serikali ilianza kutekeleza mpango wa elimu ya msingi bila malipo. Katika utekelezaji wa sera hii Serikali imelegalega kwenye kusimamia utoaji wa huduma, miundombinu na gharama. Hivyo mkakati huu na sera zake kushindwa kufikia malengo ya kuhakikisha kwamba watoto wote wa kitanzania wanapata elimu ya msingi bila vikwazo vya ada.
Takwimu zinaonyesha upungufu mkubwa wa walimu, madarasa na vitabu kuanzia ngazi ya awali, shule za msingi na sekondari. Pia, kwa muda mrefu Serikali imeshindwa kufanya ukaguzi kwa ufanisi kwenye shule za msingi na sekondari ili kukagua na kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa.
Upungufu wa vitabu kwa shule za msingi na sekondari kuna athari matokeo na kitaalum ya mwanafunzi.
Waraka wa Ruzuku kwa Shule za Msingi za Serikali (elimu bila malipo) 2015 unaitaka Serikali kutoa fidia ya shilingi 10,000 na shilingi 25,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi katika shule za msingi na sekondari mtawalia; ambapo Wizara itatumia 40% kununua vitabu na kusambaza shuleni.
Kwa mujibu CAG inaonyesha kuwa ili kukidhi mahitaji ya vitabu kwa wanafunzi katika shule za msingi za Serikali vilihitajika vitabu 6,323,566 kwa mamlaka 22 za Serikali za Mitaa. Hata hivyo, ni vitabu vya kiada 1,467,829 (sawa na 23%) vilisambazwa katika mwaka huo ikionesha upungufu wa vitabu 4,855,737 vyenye thamani ya shilingi bilioni 19.42.

ACT Wazalendo katika ilani yake ya 2020, tumelenga Serikali kuhakikisha inasimamia elimu kwa kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia, kupunguza uhaba wa walimu kwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa walimu, kuondoa gharama za nyenzo na vifaa vya kufundishia kama vile vitabu na mengineyo. Pia, Serikali kuongez fedha ya ruzuku kwa wanafunzi kutokana na uhalisia wa gharama za bidhaa kwa sasa.
2. Wanafunzi kukatisha masomo kabla ya kumaliza Elimu msingi (Darasa la Saba)
Serikali imeshindwa kufuatilia vyanzo na kuondoa vikwazo vya anguko kubwa la Watoto wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi darasa la saba (7). Takwimu za Wizara zimekuwa zikionyesha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kwa ngazi ya darasa la kwanza. Ripoti ya Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha kuwa, kuanzia 2018 hadi 2021 (kwa sampuli za shule kutoka mamlaka za serikali za mitaa 27) wanafunzi wanaoshindwa kumaliza shule ya msingi kwa kukatisha masomo yao ni 2.06% ya wanafunzi walioandikishwa.
Kwa mujibu Takwimu za Utafiti za Elimu (BEST 2020), zinaonyesha kiwango cha wanafunzi kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali ni wanafunzi 166,991 sawa na 1.6% ya wanafunzi waliondikishwa ambao walikuwa 10,174,237. Huku utoro ukichukua 97.5% ya sababu zote ikifuatiwa na vifo pamoja na ujauzito kwa watoto wa kike.
Idadi hii ni kubwa na inakinzana na malengo yaliyowekwa na Serikali kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mpango huu unalenga kufikia uwiano wa uandikishaji wa elimu ya msingi kuwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2022.
Katika hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 haijawekea mkazo wa namna ya kukabiliana na tatizo hili ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki yake ya elimu kama malengo tulivyojiwekea.

ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kike aliyepata mimba akiwa shule anamaliza elimu yake kama ilivyokusudiwa kwa kusimamia utekelezaji wa ahadi ya kuruhusu kumrejesha mtoto wa shule shuleni. Pili, kukomesha adhabu kali dhidi ya watoto ili kuhakikisha watoto wanakuwa huru kushiriki na kupata elimu.

Pia ilani ya ACT Wazalendo ya 2020 ililenga kuboresha miundombinu ya kujifunzia kwa kujenga shule maeneo ya karibu ili kupunguza umbali kwa wanafunzi.

3. Ubora wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi havipewi kipaumbele nchini:
Wizara ya Elimu kupitia Baraza la Taifa la Elimu limepewa mamlaka kusimamia elimu ya ufundi nchini. Katika uchambuzi wetu wa hotuba ya wizara tumeona kuwa Serikali haijaweka udhibiti wa ubora wa Elimu ya mafunzo ya ufundi. Kiasi cha fedha kinachotengwa na Wizara kwa ajili ukaguzi hakiliwezeshi Baraza la Taifa la Elimu kutekeleza majukumu yake. Tangu 2016 hadi sasa kiasi cha bajeti kinachotengwa kwa ajili ukaguzi kimekuwa ni hafifu na ndiyo sababu ya vyuo vya elimu ya ufundi kukosa ubora.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAG 2020/21, Serikali imefanya ukaguzi wa ubora katika vituo 73 vya ufundi kati ya vyuo 779. Hii ni kinyume na sheria na kanuni za usimamizi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Serikali imesababisha uwepo wa vyuo visivyokaguliwa na kupelekea hatari ya kuwepo kwa vyuo visivyokidhi viwango vinavyotakiwa.

Aidha, ubora wa vyuo vya ufundi unaathiriwa kutokana na upungufu mkubwa wa wakufunzi na walimu ukilinganisha na idadi ya wanafunzi. Pia, vyuo hivi vya elimu na mafunzo ya ufundi vina uwezo mdogo wa kudahili wanafunzi ikilinganishwa na uhitaji uliopo. Kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaokosa fursa ya kuendelea na masomo wanapohitimu elimu ya shule ya msingi na sekondari. Takwimu zinaonyesha ni wastani wa wanafunzi milioni moja wanahitaji kujiunga na vyo hivi huku uwezo wa vyuo kudahili wanafunzi ni 266,000 tu kwa mwaka.
Ili kuweza kukabilia na tatizo hili, ilani ya ACT Wazalendo 2020, ilibainisha:

i. Kuwepo kwa angalau Chuo kimoja cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) katika Kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji).
ii. Kuondoa malipo ya ada kwa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA).
iii. Kuweka mfumo utakaomuwezesha muhitimu wa chuo cha VETA kuweza kujiunga na mifumo mingine ya elimu.
iv. Kuhakikisha katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, kuna vyuo vya Ufundi Mchundo (Technical Schools) vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi Zaidi ya 10,000.

4. Hakuna Elimu bila Walimu, Serikali imalize tatizo la ukosefu wa Walimu:
Kasi na jitihada za Serikali kuajiri walimu imekuwa ni ndogo ikilinganishwa na uhitaji katika taasisi za elimu nchini. Uwiano wa wanafunzi wanaogharamiwa na serikali kusomea Ualimu na mahitaji halisi haushabihiani na kasi ya ajira zinazotolewa na Serikali. Ni dhahiri kuwa idadi ya wahitimu wa masomo ya ualimu ingeweza kupunguza uhaba wa walimu katika shule za awali, msingi na sekondari.

Tatizo la upungufu wa walimu liko pia katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, ambako pia Serikali haijaweka wazi jitihada zake kukabiliana na katika mkwamo huo.
Kwa mujibu wa taarifa za udahili wa walimu kupitia Wizara, Serikali imeweza kudahili jumla ya:
• Wanafunzi wa Astashahada ya Elimu ya Msingi kuwa 10,975 (wanawake 5,824 na wanaume 5,151)
• Stashahada ya Ualimu Sekondari miaka miwili 2,663 (wanawake 1,037 na wanaume 1,626)
• Stashahada maalum ya ualimu sekondari sayansi miaka mitatu 5,540 (wanawake 1,973 na wanaume 3,567)
Hii imefanya vyuo vya Ualimu vya Serikali kuwa na jumla ya wanafunzi 19,178; Ikiwa ni ngazi ya astashahada na stashahada pekee, bado wanafunzi wanaodahiliwa kwa ngazi ya shahada.
ACT Wazalendo tunaendelea kutoa rai kwa Serikali kurejesha mfumo wa ajira za walimu za moja kwa moja ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa na walimu na kuboresha elimu yetu.
Kwa kufahamu changamoto za uhaba wa walimu hususani vyuo vikuu ACT Wazalendo katika Ilani ya Uchaguzi 2020 tulisema kuwa “Serikali ya ACT itaajiri wahadhiri wasiopungua 5,000 kwa miaka mitano ili kupunguza uwiano mkubwa uliopo kati ya wahadhiri na wanafunzi.”

Serikali makini na yenye dira inatakiwa kufanya juhudi hizi ili kuboresha Elimu yetu.

5. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inaendeleza ubaguzi:
Mfumo wa ugharamiaji wa elimu yetu hususani katika ngazi ya elimu ya Ufundi, Elimu ya juu na vyuo vya utabibu bado inaweka vikwazo kwa watoto wetu kupata elimu kwa kadri ya vipawa, vipaji na uwezo wao. Tunatambua jitihada za serikali za kuongeza bajeti kwa ajili kutoa mikopo kwa elimu ya juu lakini bado wastani wa 28% hadi 36% ya wanafunzi wanashindwa kupata mikopo hiyo na wengine wanalazimika kusitisha masomo.

Yamekuwepo malalamiko na taarifa zenye ushahidi juu ya changamoto zinazowapata wanafunzi na wazazi katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya juu. Uwezo na ufasi katika utambuzi, vigezo na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji umekuwa na mjadala na hata wakati mwingine umewahi kusababisha migomo na maandamano.

Licha ya hayo yote Serikali ya CCM, imeshindwa kufanya juhudi za makusudi kupata jawabu la kudumu ili kuondokana na tatizo hili. ACT Wazalendo tunaamini kuwa, ili kupanua wigo wa wanafunzi kuendelea na masomo Elimu ya juu inapaswa kugharamiwa serikali hususani ada, malipo ya mafunzo kwa vitendo, fedha za vitabu na viandikwa. Kwa kufanya hivi tutaondosha minyukano na kutoa fursa ya kupata elimu bila kujali kipato cha mtu bali uwezo. Tutaondosha matabaka ya watoto wa wenye nacho na wasio nacho kwenye haki ya elimu.

Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020, chama cha ACT Wazalendo kilibanisha kuwa “ Serikali ya ACT Wazalendo Itafuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Italipa Ada ya Masomo (Tuition Fee), Fedha za Vitabu (Stationeries), na gharama za Mafunzo kwa Vitendo (Field Studies/Internship) kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye Chuo Kikuu. Itatunga Sheria kuhakikisha kuwa Mikopo ya Elimu ya juu itakuwa ni kwa ajili ya gharama za kujikimu tu (Meals & Accomodations).”

Serikali haijawahi kuelekeza juhudi kuhakikisha mikopo hii inawafikia wanafunzi wanao dahiliwa ngazi ya vyuo vya kati na vyuo vya ufundi. (Bodi ya mikopo) kisheria hakihusiki na mfumo wa ugharamiaji kwenye ngazi ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Lakini Serikali inatakiwa kuthamini wanafunzi wote na kutatua changamoto zao.


6. Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti fedha za Miradi ya Maendeleo ya Elimu
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kutenganisha fedha za miradi halisi ya Maendeleo na fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa kuzianzishia fungu maalum ili fedha za miradi halisi ya maendeleo ziweze kuonekana na kufuatiliwa utekelezaji wake;
Katika mwaka wa fedha 2021/22 wizara ilipitisha bajeti ya Shilingi 994,711,772,676.29 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo bilioni 570 zilikuwa kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Serikali inafanya makusudi kuchanganya fedha za mikopo ya elimu ya juu katika fedha za maendeleo kwa kuwa fedha hizo huonekana kuwa ni nyingi lakini fedha zinazokwenda kutekeleza miradi halisi ya maendeleo ni kidogo sana. Kwa kutazama fedha hizo kwa mwaka jana fedha za mikopo zinachukua asilimia 57 za fedha zote za miradi.
Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imeomba kuidhinishiwa fedha shilingi 959,547,439,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, ni fedha pungufu kwa kulinganisha na bajeti ya mwaka jana. Pia, kiasi kinachoenda kuhudumia gharama za mikopo kitaendelea kupanda kutokana kuongezeka kwa idadi ya wahitimu kidato cha sita mwaka huu.


7. Haki ya Elimu Kwa mtoto wa Kike
Serikali ilitangaza rasmi kuwa mwanafunzi wa kike akipata ujauzito apata fursa ya kurejea shule pindi atakapojifungua. Lakini kupitia Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Elimu inaonyesha kuna dalili za kuwarejesha kwa dirisha jingine na siyo kupitia mfumo rasmi.

ACT Wazalendo tunaisisitiza Serikali kusimamia haki ya watoto wa kike kwa kuwarejesha kwenye mfumo rasmi wa elimu badala ya utaratibu wa kuwarejesha nje ya mfumo rasmi.

8. Elimu ya Mafunzo kwa vitendo kwa Elimu ya juu
Mfumo wa sasa wa kutoa mfunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu (Elimu ya Juu) ni miezi 2 au wiki 56 na ugharamiaji wake bado unabebwa katika mabega ya mwanafunzi mwenyewe au mzazi. Katika kuimarisha ubora na ufanisi wa kujifunza kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ni muhimu sana wanafunzi wapate muda mrefu zaidi kuanzia miezi sita (6) hadi mwaka ili kuwajengea uzoefu na umahiri kwenye fani wanazosomea.

Katika, mabadiliko ya mitalaa na sera ya elimu, Serikali inapaswa kutazama upya utaratibu wa sasa kwa kuwa unashindwa kumuandaa mwanafunzi kumudu fani yake kutokana na kukosa muda wa kujifunza kwa vitendo.

Katika Ilani ya Uchaguzi 2020, ACT Wazalendo tuzungumzia kutoa vivutio kwa makampuni au taasisi binafsi zitakazo toa nafasi ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo. Pia, Serikali kuhakikisha inalipia kwa fani zote kwa kipindi kisichopungua miezi sita ili wanafunzi wote wapitie mafunzo kwa vitendo kikamilifu, vilevile kuweka utaratibu wa kutumia matokeo ya mafunzo kwa vitendo katika utoaji ajira ili kuhimiza wanafunzi kuona umuhimu wa mafunzo kwa vitendo.

Hitimisho.

Kwa kuhitimisha, tunaisihi Serikali kuhakikisha sekta ya Elimu inasimamiwa na wizara moja. Usimamizi wa sekta ya Elimu umegawanywa katika wizara takribani zaidi ya tatu ( Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto – kwa baadhi ya maswala). Hii imepelekea mipango ya bajeti kwenye sekta ya Elimu kuyumbishwa kwa vipaumbele vyake.

Pia, changamoto nyingi za kibajeti na kisera zinatokana na kukosekana kwa mwafaka wa kitaifa juu ya aina ya Elimu tunayoitaka, hivyo ni muhimu mchakato wa Mapitio ya Sera uwahusishe wadau wote wa elimu nchini.


Imetolewa na:
Ndg. Riziki Shahari Mngwali
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Elimu- ACT Wazalendo
11 Mei 2022. 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK