Hatari ya Jeshi letu Kuingizwa kwenye Siasa iko wazi. Idhibitiwe.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA ULINZI ACT WAZALENDO NDG. MASOUD ABDALLAH KUHUSU UTEKELZAJI WA BAJETI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

Utangulizi
Leo Alhamisi, tarehe 19 Mei 2022 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amewasilisha Bungeni hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23. Sisi, ACT Wazalendo tumefuatilia kupitia Msemaji wa sekta ya Ulinzi, ili tuweze kuimulika, kuichambua na kutoa maoni mbadala wa bajeti hiyo kwa lengo la kuisimamia Serikali na kuhakikisha maslahi ya wananchi yanazingatiwa. Baada ya kupitia hotuba ya bajeti, tumekuja na maeneo makuu matatu; Ufanisi wa taasisi chini ya wizara, maslahi ya wafanyakazi na askari wetu na uhusiano wa taasisi za wizara na wananchi na mwisho utekelezaji wa bajeti. Kwa kuangazia maeneo hayo, hotuba hii imebeba hoja saba(7) kuhusu bajeti ya wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Zifuatazo ni hoja saba (7) za ACT Wazalendo kuhusu Hotuba ya bajeti ya wizara ya Ulinzi na JKT.
1. Madeni ya muda mrefu ya Wizara na taasisi zake.
Uchambuzi tulioufanya katika utekelezaji wa bajeti tumebaini kuwa Wizara pamoja na taasisi zake zinadaiwa na watoa huduma, wakandarasi na wauzaji wa bidhaa, madeni yanayotokana na kupokea bidhaa na huduma mbalimbali. Madeni haya ni ya muda mrefu yanayodaiwa ndani ya miezi 12 hadi miaka 3 yanayofikia kiasi cha Shilingi Trilioni 1.406 kwa ujumla wake. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG 2020/21 deni hili ni jumla ya thamani ya fedha zinazodaiwa kutoka kwenye Fungu 57 (Wizara) kiasi cha Shilingi trilioni 1.014, Fungu na 38 Jeshi la wananchi (JWTZ) kiasi cha Shilingi bilioni 314.5 Shirika la Mzinga kiasi cha Shilingi bilioni 51.38 na Fungu la 39 Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Shilingi Bilioni 25.81.
Hiki ni kiwango kikubwa sana cha Fedha za watu ambazo Serikali kupitia wizara inazishikilia mkononi baada ya kupokea huduma za watoa huduma. Kutolipwa kwa madeni haya kwa wakati yanasababisha kuongezeka kwa madeni ya muda mrefu ambayo yanaweza kuathiri sifa ya Serikali na wauzaji bidhaa. Pia, yanasababisha mdororo wa uchumi na kupoteza ajira na mitaji.
Ongezeko la deni linachangiwa na kutotengewa bajeti ya kutosha kwenye taasisi hizi zilizo chini ya wizara pamoja na kuchelewa kutolewa kwa fedha na Wizara ya Fedha na Mipango. Katika makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2022/23 yaliyowasilishwa leo (tarehe 19 Mei, 2022) Bungeni na Waziri kwa kutazama mgawanyo wake kwenye mafungu hayo ni dhahiri kuwa taasisi hizi hazitaenda kulipa madeni yote kwa mwaka huu. Deni hili litaendelea kukua tena na kuweka mzigo mzito kwa walipa kodi.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kupitia wizara itenge bajeti ya kutosha ili kulipa madeni yote kwa mkupuo, pia kuwa na utaratibu na mfumo wa kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya madeni yanayoongezeka kutokana na riba na fidia.
2. Hasara za kutofuatwa kwa sheria ya ununuzi ni kubwa sana ndani ya wizara.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ni kuwa kuna upungufu mkubwa kwenye taasisi na wizara ya Ulinzi na JKT pamoja na mapungufu mengine aliyoyataja ni kuwa, taaisi hazifuati taratibu za kisheria katika kutoa huduma nje ya mfumo wa TANePS, ununuzi wa bidhaa na huduma bila ya ushindanishi, ununuzi uliofanywa bila kibali cha Bodi ya Zabuni, ucheleweshaji katika kupokea bidhaa na utoaji wa huduma.
Kila mwaka wizara inaomba kuidhinishiwa bajeti kwa ajili ya matumizi mbalimbali, wizara kupitia fungu 38 (fungu la Ngome), Jeshi la kujenga Taifa (JKT) fungu 39 na fungu 57 (Wizara) zilifanya manunuzi bila kufuata sheria ya manunuzi. Jambo hili limesababishia hasara Serikali ya Shilingi Bilioni 2.54, kwa mchanganuo ufuato; Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kiasi cha Shilingi 123,820,158.00,Jeshi la Kujenga Taifa kiasi cha Shilingi 60,925,000.00 na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa kiasi cha Shilingi 2,362,135,896.29.
Hasara hii, ingewezwa kuepukika ikiwa Serikali kupitia taasisi zake ingefuata sheria na taratibu za manunuzi.
3. Madai ya watumishi yasiyolipwa Shilingi Bilioni 202.7
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/21 imebainisha kuwa wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imelimbikiza madai ya watumishi yanayotokana na malimbikizo ya mishahara ya waajiriwa wapya, upandishwaji wa madaraja na vyeo, makato na posho yamefikia Shilingi bilioni 202.71 sawa na Ongezeko la asilimia 16 Kutoka mwaka 2019/20 ambapo madai yanayotokana na malimbikizo ya mishahara, likizo na stahiki zingine yalikuwa ni Shilingi bilioni 174. 57.
Wakati wa kuwasilishwa hotuba ya bajeti leo Bungeni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa Dkt. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) alilieleza bunge kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kulipa, lakini ukiitazama bajeti kwa mafungu yote Fungu la 38, 39 na 57 bado yanajielekeza kwa matumizi ya kawaida na kiasi kidogo tu kwa ajili kulipa madai hayo.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza bajeti yake ili iweze kuwalipa watumishi wote malimbikizo ya madai yao kwa mkupuo ili kuwawezesha kukabiliana na gharama za maisha ambazo zimepanda sana hivi sasa.
Aidha ili kutekeleza wajibu wa kuwalipa kwa mkupuo madai yote tunaitaka Serikali itazame uwezekano wa kuweka sokoni Bondi maalumu.
4. Bima ya Afya kwa wanajeshi na wastaafu wa jeshi.
Tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, limekuwa likitumia utaratibu wa wanajeshi wote kupata huduma ya matibabu kupitia vituo na hospitali zilizochini ya Jeshi lenyewe kwa gharama za Serikali. Utaratibu huo unatekelezwa kwa mujibu wa sheria ya Ulinzi wa Taifa na kanuni zake (kifungu na 26 & 27) inayosema kuwa huduma za matibabu kwa maofisa, askari na wategemezi wao zitagharamiwa na Serikali na zitakoma pale watakapostaafu.
Utaratibu huu umelalamikiwa na wanajeshi kwa muda mrefu sana kutokana na upungufu unaonyeshwa kwa ukosefu wa ufanisi wa utendaji wa hospitali hizo kwa kutokuwa na dawa, vifaa, vifaa tiba na matibabu na kupata huduma zisizoridhisha. Jambo linalowalazimisha kutumia fedha zao kutoka mifukoni mwao kwa ajili ya kugharamia huduma ya afya kwa ajili yao na wategemezi wao. Licha ya malalamiko na ahadi ya Serikali ya kuanzisha bima ya afya kwa ajili ya wanajeshi lakini hadi sasa bado Serikali haijawaunganisha wanajeshi katika mfumo wa bima ya afya ya taifa (NHIF).
Aidha, athari za utaratibu huu unakuwa na madhara makubwa zaidi kwa wastaafu wa Jeshi ambao kwa mujibu wa sheria na kanuni, Serikali inagharamia matibabu kwa wanajeshi waliopo kazi pekee kupitia vituo na hospitali maalumu za jeshi. Wastaafu wa jeshi wanaishi katika hali ya mashaka sana linapokuja suala la matibabu yao, licha ya kutumia muda mrefu.
Tunaitaka Serikali kukamilisha utaratibu wa kuwaunganisha wanajeshi wote kwenye mfumo wa bima ya afya ili kuwaweka sehemu salama zaidi. Pia, tunaishauri Serikali kuwaunganisha wastaafu wa jeshi na wategemezi wao kwenye mfumo wa bima ya afya.
5. Shirika la Mzinga; harufu za ubadhirifu katika Ununuzi wa silaha za kijeshi zenye thamani ya Bilioni 1.38.
Shirika la Mzinga lilianzishwa Januari 1971 kama Mradi chini ya Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa jina la Kiwanda cha Mzinga. Tarehe 13 Septemba 1974, Mzinga JWTZ Ilitangazwa kisheria kuwa Shirika la Umma kwa Agizo la Serikali Na. 219. Hii ilibadilisha jina la Mzinga JWTZ kuwa Shirika la sasa la Mzinga.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG mwaka 2020/21 Shirika la Mzinga lilifanya malipo yenye mashaka kwa ajili ya ya ununuzi wa silaha za kijeshi ambazo hazijapokelewa – thamani ya silaha hizo ni Shilingi. Bilioni 1.38. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) anasema kuwa “niligundua kuwa Shirika la Mzinga lilimlipa msambazaji jumla ya Euro 486,577 (Sh. 1,385,599,550), sawa na asilimia 85 ya bei ya mkataba, bila kupata ushahidi wa upakiaji na usafirishaji wa silaha.”
Hadi kufikia tarehe 07 Februari CAG anabainisha kuwa Shirika la Mzinga bado halijapokea silaha zilizolipiwa kutoka kwa wasambazaji huku muda uliopangwa kupokelewa ni tarehe 26 Novemba 2020. Hii ni wazi kuwa kuna uzembe unaofanywa na wasimamizi na hali hii inaweza kupelekea kupotea kwa fedha hizo.
Ni muhimu Serikali kuingilia kati kuhakikisha SMT Security Ltd kama iliyopewa mikataba wa usambazaji huo kukamilisha usambazaji wa silaha hizo kama mikataba unavyomtaka bila kuchelewa zaidi.
6. Migogoro ya Mipaka kati ya Jeshi la Wananchi Tanzania na Wananchi
Kumekua migogoro ya mipaka ya ardhi kati ya jeshi la Wananchi na wananchi na katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu hususani katika maeneo ya kambi ya jeshi inayozungukwa na makazi ya wananchi. Wapo wananchi wengi sana ambao wameathiriwa na migogoro hii ikiwa ni pamoja na kubomolewa makazi yao, kunyang’anywa ardhi zao, kuteswa kwa vitesho au kupoteza mifugo yao.
Pamoja na kuwepo kwa malalamiko makubwa ya wananchi kwa muda mrefu dhidi ya taasisi za kijeshi kuchukua maeneo yao na kujimilikisha au kuipa taasisi nyingine bila kufanya malipo kwa wananchi wahanga wa matukio hayo, kwa sasa kasi ya Serikali katika kushughulikia changamoto hiyo ni ndogo sana.
Kwa mujibu taarifa ya Waziri leo (Katika hotuba ya Bajeti kwa mwaka 2022/23) Bungeni amebainisha kuwa katika maeneo yenye migogoro 58 yaliyobainishwa ni jumla ya maeneo 9 pekee yamepatiwa ufumbuzi na wananchi wameshapewa fidia. Kwa taarifa hii ni wazi kuwa safari ya kumaliza migogoro hiyo ni ndefu sana.
ACT Wazalendo tunasisitiza kuwa Serikali itenge bajeti maalumu kwa ajili ya kupitia upya mipaka ya Jeshi na Wananchi katika maeneo yote yenye migogoro na kuiweka bayana ili wananchi watambue maeneo ya Jeshi na hivyo kutoyaingilia maeneo hayo.
Aidha, alama za utambulisho wa mipaka kati ya nchi na nchi tunazopakana nazo ni vyema Serikali ikaweka mkakati wa kukamilisha zoezi la alama za mipaka (beacons) ambapo kuna maeneo zimetolewa au zimearibika Serikali kupitia wizara ya ulinzi, TAMISEMI na wizara ya mambo ya nje kukamilisha zoezi hilo mara maoja.

7. Jeshi kujihusisha na siasa na uteuzi wa wanajeshi kwenye nafasi za kisiasa
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi na vyama vya siasa juu ya jeshi letu pendwa kuhusishwa na siasa hasa nyakati za uchaguzi mkuu mfano uchaguzi wa 2005,2015 na 2020 wananchi wamelalamikia sana jeshi letu JWTZ kuingilia baadhi ya maamuzi ya matokeo ya uchaguzi. ACT Wazalendo inaitaka Serikali kutoruhusu jeshi letu kuchafuliwa na mambao ya siasa.
Serikali imekuwa na utamaduni wa kuwateua maafisa wa vyombo vya dola waliopo kazini na wastaafu kushika nafasi za kisiasa kama vile wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya. Uzoefu na uchambuzi wa majukumu na vitendo vya wakuu wa wilaya na mikoa ni vigumu kutenganisha wajibu wao na viongozi wa chama tawala. Kuwateua wanajeshi kwenye nafasi hizo, inatoa picha kuwa upo uhusiano wa karibu wa jeshi katika kutumikia chama tawala ili kujiimarisha.
Aidha, kuwateua wanajeshi kushika nafasi za siasa wanapostaafu, kunaweza kutafsiriwa na wengine waliopo kazini kutozingatia maadili yao ya kazi na kuanza kujipendekeza kwa watawala kwa imani kwamba pengine na wao watateuliwa kuwa wakuu wa mikoa au wilaya watakapostaafu.

ACT Wazalendo tunaishauri Serikali na mamlaka za uteuzi kwamba wanajeshi waachwe wafanye kazi za Jeshi kwa mujibu wa taaluma na ujuzi wao wa kijeshi kwa kuwa utawala wa nchi kwa mujibu wa Katiba ni wa kiraia, sio wa kijeshi.
Hitimisho.
Tunatambua wajibu na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la wananchi Tanzania, na kwa umuhimu wake tumeweza kuonyesha kwa kiasi gani bajeti ya Serikali inavyopaswa kuzingatia inaondosha changamoto za muda mrefu za askari na maofisa wa jeshi hususani kuhusu maslahi yao na uwezo wao wa kupata huduma za matibabu, pia Serikali kuongeza bajeti kwa ajili kulipa madai ya watumishi. Aidha, tunaitaka wizara kupitia Jeshi la Wananchi kujiepusha kutumika kisiasa jambo ambalo linaweza kupunguza umuhimu na heshima lililojijengea kwa wananchi nchini na nje ya mipaka ya nchi katika nyakati mbalimbali.

 

 

Imetolewa na;
Ndg. Masoud Abdallah
Msemaji wa Sekta ya Ulinzi-ACT Wazalendo
19 Mei, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK