Hatua za Dharura Kuwaondoa Raia wetu Ukraine zichukuliwe

SERIKALI YA TANZANIA ICHUKUE HATUA ZA DHARURA KUWAONDOA HARAKA RAIA WETU UKRAINE NA RUSSIA

Chama cha ACT Wazalendo kinaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha Watanzania walioko nchi za Ukraine na Russia wanakuwa salama kipindi hiki cha mgogoro wa kivita ulioibuka na kuanza kusababisha maafa baina ya nchi hizo mbili.

Kulinda raia na kuhakikisha usalama wao ni jukumu la mwanzo na la kipaumbele kwa taifa lolote wakati na mahali popote wanapokuwa katika hatari hasa inapotokea majanga kama haya ya vita.

Kwa taarifa zilizopo hali ya amani na usalama katika eneo hilo imezorota kufuatia vita iliyozuka. Mpaka sasa, takribani vifo 137 na majeruhi 316 vimeripotiwa kutokea.

Tumeshuhudia katika mitandao na vyombo mbalimbali vya habari Watanzania, hasa wanafunzi waliyoko Ukraine wakiwa wamenasa eneo la vita pasipo kuwa na msaada wa maana kutoka kwa Ubalozi wetu wa Stockholm Sweden ambao ndio wenye dhamana ya kuwahudumia, jambo linalotia mashaka na wasiwasi mkubwa juu ya usalama wao.

ACT Wazalendo hatujaridhishwa na taarifa iliyotolewa na Ubalozi wetu huo wa jijini Stockholm (unaohudumia pia Ukraine) tarehe 22 , Februari ,2022 kuhusu Watanzania na wanafunzi wa Kitanzania waliopo nchini Ukraine.

Taarifa hiyo ya Ubalozi ilijikita katika ‘kuwashauri Watanzania waishio Ukraine kuondoka (wao wenyewe!) ikiwa wanadhani kubaki huko si muhimu kwa sasa.’ Pia Ubalozi uliwataka wazazi wenye watoto wanaosoma nchini Ukraine kufanya utaratibu binafsi wa kuwarudisha nyumbani kwa kutumia ndege za abiria zinazofanya safari kutokea Ukraine.

Sisi tunadhani, taarifa na hatua hiyo ya Serikali kupitia Ubalozi wake ni nyepesi, inayoonyesha ukosefu wa uwajibikaji.

Tunaona ni hatua ya kujivua majukumu juu ya maisha na usalama wa wananchi wetu waliyoko kwenye hatari katika eneo la vita. Tunapinga na kukosoa hatua hiyo isiyo muafaka na isiyo ya kiuwajibikaji kwa maisha na usalama wa raia wetu.

Licha ya hilo, kwa hali ya mambo ilivyo sasa Ukraine, hatuoni kama ni sawasawa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuachia jukumu la usalama wa Watanzania mikononi mwa Ubalozi peke yao.

Tulitarajia kuona juhudi za dharura na za makusudi za Serikali katika kuwaondoa raia wetu Ukraine na Russia katika maeneo yenye hatari ya vita haraka bila kuchelewa.

Tunapendekeza Hatua za Dharura na za Kiuwajibikaji:

1. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Ubalozi za Tanzania katika nchi hizo mbili Ukraine na Urusi ichukue hatua za dharura na za haraka kutuma ndege kwa ajili ya kuwaondoa raia wetu waliyoko eneo la vita mapema iwezekanavyo na kuwarejesha nyumbani kabla hali ya vita haijapamba moto,kama wafanyavyo nchi zingine.

2. Kama suala la kuchukua Raia wa Tanzania kwa ndege ni gumu kwa wakati huu kutokana na hali ya hatari iliyopo ni vyema jitihada zifanywe kwa kuondoa Watanzania wote waishio katika miji ya mipakani Ukraine au wote waishio Ukraine kuwasogeza katika miji inayopakana na nchi jirani kama Poland au kuwasaidia kuwaingiza Poland na nchi zingine jirani zinazopokea watu kutoka Ukraine kwa ajili ya hifadhi na usalama katika kipindi hiki .

3.Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itoe taarifa ya kulaani vita na mashambulizi yaliyoanza na iunge mkono juhudi na jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kuzitaka pande zinazopigana kusitisha mapigano mara moja na kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kuepusha athari na maafa makubwa zaidi.

Jitihada za kusitisha mapigano ni muhimu na zenye manufaa si tu kwa Ulimwengu, bali kwetu kama nchi kwani athari za mgogoro huo zitatuathiri Tanzania pia kutokana na mahusiano ya kiuchumi na kijamii yaliyopo baina ya nchi yetu na nchi zinazohusika na mgogoro huo.

Imetolewa na:

Dahlia Majid Hassan,
Naibu Msemaji wa Kisekta, Mambo ya Nje
ACT Wazalendo
25 Februari, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK