Hoja 5 Wananchi Mbagala: Ziara ya Sekretarieti ya Chama Taifa
Hoja Tano za Wananchi katika Ziara ya Sekretarieti Jimbo la Mbagala
UTANGULIZI
Kuanzia tarehe 29 Juni 2022 hadi tarehe 06 Julai 2022, Sekretarieti ya Chama Taifa ilifanya ziara kwenye Kata zote kumi za Jimbo la Mbagala. Ziara hiyo iliyoongozwa nami Katibu Mkuu wa Chama, ilikuwa na malengo mawili; Mosi, ziara ilijikita katika masuala ya ujenzi wa Chama kama vile kuhakiki hali ya Chama katika ngazi ya Kata; Kuhamasisha usajili wa wanachama katika mfumo wa ACT Kiganjani; Kusikiliza changamoto za wanachama na viongozi katika ngazi ya Kata na kutoa msimamo na mwelekeo wa Chama katika siasa za nchi.
Pili, ziara ilikuwa na lengo la kuwatembelea Wananchi kwenye maeneo yao ya kazi, makazi na burudani kwa malengo ya kusikiliza maoni, changamoto na ushauri wao juu ya mwelekeo wa nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kuangazia hali halisi kwenye jamii yao na taifa kwa ujumla.
Ninawashukuru sana Wanambagala kwa mapokezi mazuri na uungwana wao wa kutupokea, kutusikiliza na kutueleza masuala mbalimbali na kuwezesha malengo yote mawili ya ziara hii kufanikiwa kwa ufanisi. Mbagala imeweka msingi wa programu hii kuendelezwa kwingineko. Ninayo furaha kutangaza kuwa Programu ya Ziara ya Sekretarieti Kata kwa Kata sasa itatekelezwa katika Majimbo yote Kumi ya Mkoa wa Dar es salaam.
Kwa muhtasari, ninachukua pia fursa hii kuwasilisha masuala ya Wananchi yaliyoibuliwa kwenye ziara ya Sekretarieti Katika Jimbo la Mbagala na Mwongozo wa Ofisi ya Katibu Mkuu katika kuyashughulikia masuala hayo na mengine ya namna hiyo nchi nzima.
MASUALA YALIYOIBULIWA
1. Kupanda kwa Gharama za Maisha na Hali Ngumu ya Kiuchumi
Kote tulikopita, kilio kikubwa cha Wananchi ni hali ngumu ya maisha kunakotokana hasa na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama vile bidhaa za chakula, mafuta ya petroli na dizeli, bidhaa za ujenzi na nauli za usafiri wa daladala na za kwenda mikoani.
Mathalani uchambuzi wa bei ya vyakula muhimu kama vile mchele, unga wa mahindi, mafuta ya kupikia na maharage imepanda sana ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka jana.
Kwa mfano:
Mchele umepanda kutoka Sh. 1,200 hadi 2,400
Unga wa mahindi KUTOKA Sh. 1,000 hadi 1,600
Mafuta ya kupikia kutoka Sh. 3,000 hadi 9,000
Unga wa ngano kutoka Sh. 1,200 hadi 2,000
Sukari kutoka Sh. 1,500 hadi 3,000
Nyama kutoka Sh. 6,500 hadi 9,000
Pia, licha ya Serikali kutangaza kuingiza Tsh. Bilioni 100 kama ruzuku kwenye ununuzi wa mafuta ili kupunguza bei, kwenye vituo vya mafuta Mbagala na kwingineko nchini bei ya mafuta inazidi kupaa. Mathalani, bei ya mafuta ya petrol na imepanda kutoka Tsh. 3,100 mwezi uliopita hadi Tsh. 3,220 mwezi huu.
ACT Wazalendo tunarejea ushauri wetu uliotolewa na Msemaji wa Sekta ya Nishati Ndugu Isihaka Mchinjita kuishauri Serikali kuondosha Tsh. 500 kwa kila lita zinazokusanywa kama tozo ambapo itahakikisha kuwa Serikali inaweka ruzuku ya Tsh. bilioni 152.5 kila mwezi badala ya bilioni 100. Aidha, tunasisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwa kuyawezesha mashirika ya TIPER na TPDC kuagiza mafuta ili kuhakikisha unafuu zaidi unapatikana.
Vile vile, Serikali itenge fedha haraka kwa ajili ya kuongeza uwezo wa hifadhi ya mafuta ya petroli ambapo itaongeza siku zaidi tofauti na utaratibu wa sasa wa kuagiza kila mwezi.
Kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli ndiko kunakochochea kwa sehemu kubwa kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na nauli.
2. Janga la Ajira na Changamoto Mahsusi za Wamachinga, Bodaboda na Wafanyabiashara wa Masokoni
Kwenye Kata zote tulizopita, Wananchi wanalia juu ya changamoto ya ajira. Vijana wasomi wanaendelea kumiminika mitaani huku uchumi wetu ukiwa hauzalishi fursa za kutosha kuwawezesha wahitimu wote kuajiliwa na kujiajiri.
Mbali na hayo, vijana waliojiajiri kwenye sekta za bodaboda, wamachinga na wafanyabiashara masokoni, sekta ambazo zimeajiri vijana wengi, wametueleza kuwa Serikali haijaweka mazingira rafiki kwa wao kufanya shughuli zao.
Mathalani, Wamachinga wa maeneo ya Mbagala Rangi Tatu wametueleza kuwa Serikali inawashinikiza kuondoka kuhamia maeneo ya Soko la Kampochea, Soko la Kijichi na Soko la Kilamba ambako kimsingi hakuna wateja wala mazingira rafiki ya kufanya biashara. Wengi, kwa kuinusuru mitaji yao, wamerejea tena Rangi Tatu kuendelea na biashara.
ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kufikiria upya mpango wake wa kuwapanga Wamachinga. Ni muhimu kuja na Mpango shirikishi ambao utazingatia maslahi mapana ya Wamachinga kufanya biashara kwenye maeneo yenye mzunguko mkubwa wa Biashara. Machinga ni Watanzania wanaotegemewa na familia zao. Shughuli zao za kujitafutia kipato zithaminiwe badala ya kuonekana watu wasiostahili kuwepo.
Kwa upande wa Bodaboda na Bajaji, wametueleza changamoto za bei ya mafuta, abiria kushindwa kumudu nauli halisi kutokana na ugumu wa maisha, kusumbuliwa na askari, hali duni ya usalama hasa wakati wa usiku na kuzuiliwa kuingia maeneo ya mjini.
Serikali ichukue hatua kuboresha mazingira ya bodaboda kufanya kazi ikiwemo kuwaruhusu kuingia mjini, kupunguza bei ya mafuta na kuwa na mkakati shirikishi wa kuhakikisha wanafuata sheria badala ya mahusiano ya "paka na panya" yaliyopo sasa baina yao na Askari wa Usalama Barabarani.
Kwa upande wa masoko, Serikali ichukue hatua kuimarisha miundombinu ya masoko. Ujenzi wa masoko uzingatie pia maoni ya wafanyabiashara ili kuepusha ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi ya masoko.
Kwa mfano, Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonesha kuwa sehemu kubwa ya soko la Kijichi lililogharimu Tsh 765.1 milioni halitumiki kwa sababu ujenzi wake haukuzingatia mahitaji wa wafanyabiashara. Pia, ujenzi wa soko la Zakhem uliyeyuka licha ya kutengewa fedha Tsh. 2.26 bilioni.
3. Miundombinu Mibovu na Huduma Duni za Kijamii
Wananchi wa Mbagala wametulalamikia kuhusu huduma duni za barabara, afya na elimu zisizoendana na mahitaji halisi kutokana na wingi wa watu. Ukiacha barabara za Kata ya Kijichi ambazo baadhi zimetengenezwa kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ambao kwa mujibu wa Ripoti ya CAG nao umegubikwa na ufisadi wa Tsh. 120 milioni, barabara nyingi za mitaa ya Mbagala zipo kwenye hali mbaya sana.
Barabara ambazo zipo kwenye hali mbaya zaidi ni pamoja na barabara ya Shule ya Msingi Rangi Tatu hadi Goroka Kata ya Kibondemaji, barabara ya Mzambarauni hadi Saku mwisho Kata ya Chamazi, barabara ya Thaqalain hadi Mponda na Mponda hadi Vigozi Kata ya Mianzini, barabara ya Kontena hadi Dumbalumbe Kata ya Kiburugwa na Kilungule, na barabara ya Biasi Kata ya Charambe. Pia, barabara ya Nzasa hadi Buza ambayo licha ya mkandarasi kulipwa Tsh. 19.1 bilioni na kutakiwa kukamilisha mradi mwezi Juni 2021 hadi sasa mradi haujakamilika.
Hali ya huduma za afya, maji na elimu ni duni pia. Wananchi wametulalamikia juu ya uchache wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, shule, uhaba wa vifaa vya kutosha mashuleni, uhaba wa dawa hospitali, michango mingi shuleni na gharama kubwa za matibabu.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali itekeleze pendekezo la CAG kumwajibisha mkandarasi kumaliza mradi kwa wakati na kulipa fidia. Pia, Serikali itenge fedha kujenga na kukarabati barabara za Mitaa ya Mbagala ambazo zipo kwenye hali mbaya.
4. Demokrasia, Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya
Wananchi wa Mbagala wametueleza kuridhishwa na msimamo wa ACT Wazalendo katika kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya. Kwenye Tume Huru ya Uchaguzi, Wananchi wameweka bayana kuwa iwapo Tume ya Uchaguzi haitafanyiwa maboresho, Wananchi wengi hawatapiga kura.
Kuhusu Katiba Mpya, Wananchi wamesisitiza kuwa kiporo cha Katiba Mpya kimaliziwe kwa sababu Katiba Mpya ni takwa la Watanzania.
Kwenye mazungumzo yetu na Wananchi, tumeendelea kusisitiza kuwa ACT Wazalendo itaendelea kuongoza ajenda ya mageuzi ya kisiasa nchini kupitia maridhiano.
Tutaendelea kusimamia hoja zetu za Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, Mageuzi ya Jeshi la Polisi, mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa nchini na kuachiliwa huru kwa wahanga wa utawala uliopita (wanasiasa, viongozi wa dini, wanaharakati na wafanyabiashara).
5. Uwajibikaji wa Serikali za Mitaa
Kwenye maeneo mengi tuliyoyatembelea, Wananchi wamelalamikia kuhusu uwajibikaji duni wa Serikali za Mitaa katika kutekeleza majukumu yao. Mathalani, kwenye Mitaa mingi, licha ya Serikali kukusanya michango kwa ajili ya usafi, kampuni zinazopewa tenda ya kukusanya usafi haziwajibiki kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Pia, Serikali za Mitaa zinalalamikiwa kuuza maeneo ya wazi, kutosoma mapato na matumizi, na ufujaji wa michango ya ulinzi shirikishi.
ACT Wazalendo inasisitiza kuwa Serikali iache kuwakingia kifua viongozi wa Serikali za Mitaa wanapotaka kuwajibishwa kwa umma.
MWONGOZO WA OFISI YA KATIBU MKUU
1. Kutokana na uzoefu wa ziara ya Mbagala, Ofisi ya Katibu Mkuu itatoa Mwongozo Maalum kwa viongozi wa Mikoa na Majimbo kwa ajili ya kuzisemea changamoto za maeneo yao. Viongozi wa kila eneo watapimwa kwa namna wanavyozisemea changamoto za maeneo yao na kufanya uchambuzi wa kero za Wananchi.
Viongozi watapaswa kutumia Taarifa za Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta kuiwajibisha Serikali kwenye maeneo yao.
2. Chama kitazindua hivi karibuni, kupitia Halmashauri Kuu ya Chama Taifa, Sera ya Chama ya Wamachinga. Kwenye Sera hiyo, tutaweka bayana hatua ambazo Serikali inapaswa kuzichukua kuhakikisha kuwa Wamachinga wanafanya Shughuli zao kwa uhuru.
3. Kongamano la Kitaifa la Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya. ACT Wazalendo itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya kwa njia mbalimbali ikiwemo kufanya Makongamano ya Kitaifa ya Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya.
Ninayo furaha kutangazia umma kuwa Kongamano la Nne la Kitaifa la Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya litafanyika Mkoani Tanga (Tanga Mjini) tarehe 23 Julai 2022. Kama ilivyo ada, Kongamano litawaleta pamoja viongozi, Wanachama na Wapenzi wa ACT Wazalendo kutathmini na kutoa mwelekeo wa ajenda ya mabadiliko kwenye eneo la Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya kwa kuzingatia hoja za ACT Wazalendo.
HITIMISHO
Licha ya jitihada ambazo Serikali inazichukua katika kuimarisha demokrasia, ni dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa kukabiliana na hali ngumu ya maisha ya Wananchi hazitoshi. Serikali inapaswa kuchukua hatua muafaka kuhakikisha kuwa bei ya bidhaa muhimu inadhibitiwa ili kuwanusuru Watanzania wa chini.
Imetolewa na:
Ado Shaibu
Katibu Mkuu
ACT Wazalendo
07 Julai, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter