Taarifa ya Kaimu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa Juu ya Kuapiswa kwa Mama Samia Suluhu Hassan Kushika Madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Chama cha ACT Wazalendo tunatoa pongezi za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kwake leo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais, Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki juzi jioni Machi 17, 2021.
Sisi ACT Wazalendo tunampongeza Mama Samia Suluhu Hassan kwa heshima hii yenye dhamana kubwa na ya kipekee ya Urais ambayo leo hii Machi 19, 2021 ameapa kuanza kuitumikia kwa kipindi cha takribani miaka mitano ijayo.
Aidha kiapo alichokula leo ni dhamana kubwa. Watanzania hususani wanawake tuna imani kubwa na yeye kuweza kuliponya taifa letu kwa kujenga na kutuleta pamoja kama Taifa kwa kuongoza maridhiano ya kitaifa.
Pia sisi ACT Wazalendo tumefurahishwa na hotuba ya Mama Samia Suluhu Hassan aliyoitoa leo baada ya kula kiapo chake.
Tumeipokea hotuba hiyo kwa uzito wa kipekee pamoja na rai yake kwa vyama vya upinzani na Watanzania kuwa tushikamane, tufute machozi, tusahau yaliyopita
Mbali na hayo, Sisi ACT Wazalendo tunaamini kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa kiongozi wa mfano ambaye atatulea na kuongoza Taifa letu kwa upendo bila kuweka kando misingi ya Katiba, Sheria na Utawala Bora sambamba na kushamirisha yale mema yaliyofanywa na mtangulizi wake na kurekebisha pale palipo na upungufu ili kwa pamoja tuweze kusonga mbele na kujiletea maendeleo.
Hongera sana Mama Samia Suluhu Hassan, tunakutakia kila la heri.
Imetolewa na:
Dorothy J. Semu,
Kaimu Mwenyekiti Taifa,
ACT Wazalendo
19 Machi, 2021.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter