Hotuba Mbadala ya ACT Wazalendo Wizara ya Afya. Gharama kubwa za matibabu: Tunataka Mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa Wote

GHARAMA KUBWA ZA AFYA NCHINI; TUNATAKA KILA MTANZANIA KUWA KWENYE HIFADHI YA JAMII

[Uchambuzi wa Bajeti ya Afya kwa mwaka wa fedha 2023/24]
Utangulizi.
Ijumaa Mei 12, 2023 Waziri wa Afya Ndugu Ummy Ali Mwalimu (Mb.) aliwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa fedha 2023/24 ambayo ulianza kujadiliwa Ijumaa na kesho Jumatatu utaendelea na kuidhinishwa na bunge. Bajeti ya afya ni miongoni mwa bajeti zinazofuatiliwa kwa karibu sana na wananchi kutoka na uhusiano wake wa karibu na maisha ya watu.

Sisi, ACT Wazalendo kupitia Waziri Kivuli wa afya tumeisikiliza na kuichambua bajeti hiyo kwa kuangalia; taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa Mwaka wa fedha 2022/23; taarifa ya Ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22; Mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 ili kuona kwa namna gani bajeti ya Wizara ya Afya inaakisi mahitaji, matarajio na matamanio ya wananchi.

Uchambuzi wetu kwa ujumla tumebaini mwelekeo wa bajeti ya afya bado ni finyu katika kutimiza lengo la kutoa huduma bora ya afya kwa Watanzania. Bajeti hii imeendela kuwa chini ya 3% ya bajeti ya taifa kwa miaka kumi (10) mfululizo. Mwelekeo huu ni chini zaidi ya kiwango kinachokubali miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ya kutenga bajeti ya afya 15% ya bajeti ya Taifa kwa nchi zao. Kwa kiasi hiki (Shilingi Trioni 1.2 ambayo ni sawa na 2.8 ya Shilingi Trilioni 44.38 ya bajeti ya Taifa) cha bajeti ya Wizara ya Afya, lengo la bajeti ya afya kufikia makubaliano ya Abuja bado ni ndoto.

Aidha, hali ya upatikanaji wa fedha kwa ajili utekelezaji wa miradi bado ni changamoto kubwa, kwa kutolewa pungufu ya kiasi kilichoidhinishwa. Katika Mwaka wa fedha 2022/23 Miradi ya Maendeleo ilitengewa kiasi cha Shilingi bilioni 555.1. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 Wizara ilipokea Shilingi bilioni 284. 4 sawa na asilimia 51 pekee ya fedha za bajeti zilizoidhinishwa, hali hii imekuwa ikijirudia mwaka hadi mwaka.

Vilevile, bajeti inaonyesha ongezeko kubwa la matumizi na miradi kwa hospitali za rufaa za mikoa, kanda, maalumu na taifa ikilinganishwa na hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati ambazo ndio zinahudumia wananchi wengi. Bajeti inaonyesha hospitali za wilaya zinatengewa asilimia 34 huku zahanati na vituo vya afya kwa ujumla vimepewa asilimia 10 tu.

Jambo, jingine ni kuwa mwelekeo wa bajeti kwa mwaka 2023/24 unaonyesha kujikita zaidi kwenye tiba kuliko kinga. Uchambuzi wetu wa vitabu vya bajeti (randama) umebaini kuwa matumizi yote ya fedha zilizotengwa zinazoenda kwenye huduma za tiba ni 39% huku huduma za kinga zimepewa asilimia 13 pekee. Sisi tunaona, huduma bora ya afya ya msingi kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya ni muhimu ili kupunguza idadi ya wagonjwa watakaohitaji matibabu bingwa yenye gharama kubwa.

Mwelekeo huu wa Serikali katika kuitazama Sekta ya afya inapalilia matumizi makubwa ya fedha za umma kwenye matibabu na kuzima mwelekeo wa kukabiliana na magonjwa (kinga).

Pamoja na uchambuzi huu wa jumla, katika Uchambuzi wetu tumebainisha maeneo kumi (10) kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2023/24 kama ifuatavyo;

1. Kupanda kwa gharama za afya na Mfumo usiofaa wa kugharamia huduma ya afya
Tangu Serikali ilipoanza kutekeleza sera ya uchangiaji wa huduma muhimu kama vile za Afya na Elimu kutokana na sera ya urekebishaji wa uchumi na soko huria, mwanzoni mwa miaka 1990, kumeongeza pengo kubwa la wenye nacho na wasio nacho katika kupata huduma ya afya.

Upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa unategemewa na uwezo wa mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa wenyewe. Jitihada za Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya afya kwa usawa zinazuiwa na gharama kubwa na mifumo mibovu ya kuunganisha nguvu za wananchi ili kupanua wigo na uwezo wa Serikali kugharamia huduma.

Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2021 zilizotolewa Juni 2022, zinaonyesha kuwa mwaka 2020 jumla ya Watanzania milioni 43 walikuwa wagonjwa kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati Nchi nzima. Hii ina maana kuwa 70.5% ya Watanzania walihitaji huduma ya afya mwaka 2021. Katika huduma ya afya kuhitajika kwa kiwango hiki inadhihirisha kuwa suala la Afya linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa sana. Kitendo cha Serikali kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa namna yoyote ile ni kuumiza wananchi wake.

Mfumo wa sasa wa ugharamiaji huduma ya afya umeachwa kwenye mabega ya mwananchi kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya. Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya Afya, jumla ya Watanzania 8,224,271 sawa na asilimia 14.7 ya Watanzania wote (takriban milioni 61) ndiyo wanaonufaika na huduma za bima ya afya. Mfuko wa NHIF kwa sasa unahudumia wanachama 1,327,001 na wanufaika 4,921,040 sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote, huku asilimia 5.4 wanahudumiwa na Bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF), asilimia 0.3 wanufaika wamejiunga kupita SHIB-NSSF na asilimia 1 wanatumia bima za makampuni binafsi. Kwa hivyo, 85.3% ya Watanzania haimo kwenye Mfumo wa Bima ya Afya.

Sote ni mashahidi namna watu wanavyopoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu, Ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua maiti katika hospitali kutokana na marehemu kuwa na deni linalotokana na gharama za matibabu. Utu wetu unafifia kutokana na kukosa mfumo wa afya wa kujaliana, kuthaminiana. Kukosekana kwa mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii umewafanya watu wengi wasiwe na uwezo wa kupata huduma za matibabu.

ACT Wazalendo tunapendekeza kwamba Serikali ihakikishe kila mtanzania anakuwa kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuwawezesha wananchi wote kupata bima ya afya ya taifa. 20% ya Michango ya wanachama wa Mifuko ya hifadhi ya jamii iwasilishwe NHIF. NHIF itapata wanachama wapya milioni 1.9 na makusanyo ya bilioni 530 kwa mwaka.
Pili, Serikali itumie 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri kuwaingiza wananchi kwenye hifadhi ya jamii na NHIFkwa kuchangia theluthi ya mchango wao baada ya kujiunga na hifadhi ya jamii kwa hiyari, takribani wanachama milioni 7.4 wanaweza kujiunga na NHIF na makusanyo ya Bilioni 620.

Tatu, Serikali iwalipie 100% wanufaika wa TASAF kwenye hifadhi ya jamii na NHIF. Takribani watu milioni 6.3 na makusanyo ya bilioni 470. Nne ili kutekeleza mapendekezo yote hapo juu, Serikali itenge kwenye bajeti ya kila mwaka asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia matibabu na hivyo kuwezesha wananchi milioni 11 kuwa na Bima ya Afya pamoja na wategemezi wao.

2. Upungufu mkubwa wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
Hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu katika utoaji wa huduma ya afya. Taarifa za vituo vya afya na hospitali zinaonyesha upungufu na matatizo ya upatikanaji wa dawa, vifaa na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora. Uwekezaji wa Serikali katika ujenzi wa vituo vya afya hauendi sambamba na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma ya afya kwa wananchi.
Kwa miaka mitatu mfululizo inaonyesha bajeti inayotengwa kununua dawa inazidi kushuka; katika Mwaka wa fedha 2021/2022 ziliidhinishwa Shilingi bilioni 218.1; Mwaka 2022/2023 ziliidhinishwa Shilingi bilioni 200.0 sawa na asilimia 0.48 ya bajeti ya taifa; mwaka 2023/24 zinaombwa Shilingi bilioni 205.0 sawa na asilimia 0.46.

Ufinyu wa bajeti ya fedha kwenye kununua dawa unathibitishwa na taarifa ya bajeti ya wizara ya afya 2023 inaonyesha upatikanaji wa aina 290 za dawa muhimu, vifaa tiba na vitendanishi muhimu kufikia asilimia 59 katika ngazi ya MSD na asilimia 52 ngazi ya Zahanati, asilimia 47 kwa ngazi ya Vituo vya Afya, asilimia 67 kwa ngazi ya hospitali za Wilaya, asilimia 98 kwa Hospitali za Rufaa za Mikoa, na 94% kwa hospitali za Kanda, Maalum na Taifa. Kiasi hiki cha dawa hakitoshelezi kabisa mahitaji wa wananchi.

Pamoja na ufinyu wa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, ripoti ya CAG 2021-2022 imeonyesha hasara iliyotokana na dawa ambazo muda wa matumizi yake ulikwisha kwa kipindi cha kuanzia miezi mitatu hadi miaka 10 ambazo hazikuwa zimeteketezwa. Hasara hiyo ni ya shilingi bilioni 2.24 katika Hospitali za rufaa na Hospitali maalumu na Sh milioni 976.5 katika hospitali, vituo vya afya na zahanati katika mamlaka 16 ya Serikali za Mitaa.

Aidha, changamoto ya upatikanaji wa dawa inatokana na ufanisi mdogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Ripoti ya CAG 2021-2022 inaonyesha ufanisi mdogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa kushindwa kwa asilimia 66 kutimiza mahitaji ya bidhaa za dawa na vifaatiba kwa wateja. Hadi tarehe 30 Juni 2022, Bohari Kuu ya Dawa iliweza kutimiza asilimia 34 tu ya jumla ya bidhaa 43,180,884 za dawa na vifaa tiba zilizoagizwa na wateja (vituo vya afya) ambazo zilikuwa zimelipiwa. Fedha za vituo vya huduma ya afya zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 20.66 zinashikiliwa na Bohari Kuu ya Dawa licha ya kukosekana kwa dawa na vifaa tiba. Vilevile, kuna matumizi mabaya ya fedha za umma Sh Milioni 455.7, kwa baadhi ya halmashauri kutumia fedha za manunuzi ya dawa kulipa posho na matumizi mengine ya kawaida.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza bajeti na usimamizi wa bajeti kwa ajili ya usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye vituo vya huduma ya afya hasa kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya vijijini.
Pili, tunarudia wito wa kuitaka Serikali kuiwezeshaji kimtaji angalau Shilingi Bilioni 567 Bohari ya Dawa (MSD) ili iweze kununua dawa za kutosha na bidhaa zingine za afya.
Tatu, Serikali ihakikishe dawa zilizoisha muda wake zinateketezwa kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kanuni za uagizaji na matumizi ya dawa vinazingatiwa.

3. Uhaba wa miundombinu ya afya unazorotesha huduma ya afya
Pamoja na ongezeko la ujenzi wa vituo vya huduma ya afya, Idadi ya vituo vya kutoa huduma ya afya bado haikidhi mahitaji ya umma. Pia kuna uhaba wa miundombinu kama vile vitanda vya kulaza wagonjwa, vyumba vya kujifungulia wajawazito, vyoo na vifaa vya kunawia mikono, viteketezi taka, huduma za maeneo ya wagonjwa kusubiri huduma, maabara za kiuchunguzi na vyumba vya upasuaji. Pia, vituo vingi vya huduma ya afya vina ukosefu wa miundominu msingi kama vile maji safi, na umeme.

Kwa kipindi cha July 2022 hadi Machi 2023, asilimia 67.6 ya wagonjwa wote wa nje walienda kwenye zahanati na vituo vya afya kupatiwa matibabu. Hii inamulika umuhimu wa kugharamia mfumo bora wa huduma ya afya ya msingi kama suluhisho la kupambana na kuzuia na magonjwa yasiyoambukiza na ya kuambukiza.

Sera ya kuwa na zahanati kila Kijiji na kituo cha afya kila kata, haijatekelezwa kwa maeneo yote. Idadi ya vituo vya kutolea huduma ya afya nchini vilivyosajiliwa ni 11,040. Kati ya hivyo, Hospitali ni 430, Vituo vya Afya ni 1030, Zahanati ni 7,458 na Kliniki 906, maeneo ya mijini yakiwa na vituo vingi vya kutoa huduma ya afya kuliko vijijini. Kati ya vituo 11,040 vituo vinavyomilikiwa na Serikali ni 6682 tu sawa na 60% ya vituo vyote. Taarifa za Serikali zinaonyesha kuna jumla ya kata 3956 na vijiji 12,319 nchi nzima. Idadi iliyopo ya vituo vya huduma ya afya haitoshelezi mahitaji ya Watanzania.

Aidha, Ripoti ya CAG ya mwaka 2021-2022 inaonyesha uchelewashaji wa ujenzi wa majengo ya hospitali yenye thamani ya Sh biliioni 74.1. CAG alibaini ujenzi wa majengo ulikuwa ukicheleshwa kwa miezi mitatu hadi miaka mitatu. Baadhi ya sababu za kuchelewa kwa ujenzi huo ni kuchelewa kutolewa fedha kwa wakati kutoka Wizara ya Afya kwenda hospitalini, kuchelewa kwa usambazaji wa vifaa vya ujenzi, uhaba wa watumishi wa kiufundi na ufadhili usioridhisha.

ACT Wazalendo tunaiitaka Serikali kuongeza bajeti ya huduma ya afya hasa kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Bajeti ya sasa ya wastani wa 5% ya bajeti ya Taifa haiendani na mahitaji ya wananchi. Pili, kuimarisha usimamizi wa fedha dhidi ya ubadhilifu. Aidha wote waliohusika na matendo ya matumizi mabaya ya fedha kama ilivyoainishwa kwenye Ripoti ya CAG wachukuliwe hatua kali za kisheria.

4. Matumizi mabaya ya fedha za Miradi inayogharamiwa na fedha za UVIKO-19
Tarehe 7 Septemba 2021 Shilika la Fedha Duniani IMF) ilikopesha Serikali ya Tanzania Sh bilioni 1291.74 ili kutekeleza mpango wa Kupambana na Ugonjwa wa UVIKO19. Wizara ya Afya ilipokea sehemu ya fedha hizo Sh bilioni 401.32 kwa madhumuni ya kujenga miundombinu ya afya, kununua vifaatiba na vitendanishi kwa huduma ya afya na kuongeza wafanyakazi wa afya.

Ubadhirifu wa fedha hizi umeonekana katika maeneo mbalimbali kama usimamizi wa matumizi ya fedha, manunuzi na mikataba, na utendaji. Jumla ya Sh bilioni 91 zilizotumiwa na Wizara zina ubadhilifu na matumizi yenye mashaka.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika katika ubadhirifu wa fedha hizi.

5. Sera ya matibabu bure kwa watoto, wajawazito na wazee haitekelezwi kwa ufanisi
Katika nukta za hapo juu nimelezea na kuonyesha udhaifu wa mfumo wetu wa ugharamiaji unaochangia kudunisha utu wa Watanzania na kutengeneza matabaka. Pamoja na hali hiyo, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wenye miaka zaidi ya 60 wana haki ya kupata matibabu bure kwa mujibu wa sera ya matibabu bure kutoka katika vituo vya afya vya Serikali.

Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa na changamoto kubwa, tathmini yetu inaonyesha kuwa wastani wa asilimia 40 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanalazimika kulipia matibabu. Vilevile, kwa wajawazito wanalipishwa matibabu na inatokea hivyo kwa watu wenye miaka zaidi ya 60 hulazimika kulipia huduma hizo kinyume na mwongozo uliwekwa na Wizara ya Afya.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ifuatilie kwa makini utekelezwaji wa sera hii ili kuhakikisha kuwa walengwa – ambao ni watoto, wajawazito na wazee wanapata haki zao za matibabu.

6. Changamoto uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeshindwa kutatua tatizo la ugharamiaji wa bima ya afya licha ya kuwepo kwa matabaka ya uanachama wa mfuko. Mfuko huu hauna fedha za kutosha kuwahudumia wanachama wake. NHIF imekuwa ikiendeshwa kwa hasara kwa miaka takribani minne mfululizo. Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali 2020 -2021 na 2021/22 zimeonyesha mfuko huu unaendeshwa kwa hasara zaidi sasa kuliko miaka iliyopita. Mwaka 2020/21 Mfuko ulipata hasara ya Sh bilioni 104 na mwaka 2021/22 hasara ya bilioni 205.

Hasara hii imetokana na kukosekana kwa njia bora za kudhibiti na kuendesha mfuko na matumizi mabaya ya fedha. Mwaka 2021/22 wafanyakazi wa NHIF walikopa hela za mfuko Sh bilioni 41.4 kinyume na utaratibu, kutolewa kwa malipo hewa yaliyotokana na madai ya uongo na kughushi, wategemezi waliokosa sifa, mfuko una wategemezi 104729 wenye umri zaidi ya miaka 18 kinyume na sifa za kuwa tegemezi, mwaka 2021/22 kadi 21,042 za watu wasiochangia kwenye mfuko zilitumika kwa matibabu. Aidha taarifa za mwaka hadi mwaka za ukusanyaji hafifu wa madeni yanayokopwa na Serikali na uwekezaji mbaya wa fedha za Mfuko bado hazijapatiwa ufumbuzi.

Hasara za mwaka hadi mwaka zimepelekea Serikali kuchukua hatua mbalimbali kuunusuru mfuko, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuondoa bima zote za gharama nafuu za VIKOA, kudhibiti huduma zinazotolewa kwa kuweka vifurushi vya kujiunga vyenye gharama zinazotofautiana, kupandisha gharama za uanachama, kupunguza mafao kwa huduma zenye gharama kubwa kama magonjwa ya moyo, saratani, ini, sukari na huduma za operesheni za uzazi, kuzuia matumizi kwa baadhi ya hospitali na kuondoa bima ya afya ya bei nafuu kwa watoto yaani TOTO Afya. Juhudi hizi zinapelekea kuongeza mzigo kwa mwananchi kwa kumtoza mwananchi gharama zaidi na kupunguza mafao anayopata mwananchi anapoumwa. Wananchi hawapaswi kutumika kulipa gharama za maamuzi mabovu ya Serikali.

ACT Wazalendo katika Ilani ya Uchaguzi 2020 tuliahidi kuhakikisha suala changamoto za afya kuwa historia “Serikali ya ACT Wazalendo itafanya yafuatayo; Itaboresha mfuko wa Bima ya Afya kwa kuunganisha na mifumo ya Hifadhi ya Jamii, ili kila Mtanzania anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya Afya moja kwa moja. Kwa mfumo huu, mfuko wa Bima ya Afya utaweza pia kupata fedha kwa wakati na kulipa watoa huduma kwa wakati. Bima ya Afya ni haki ya kila Mtanzania.”

ACT wazalendo tunapendekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe na Fao la Matibabu, mwanachama wa Mifuko hiyo awe moja kwa moja mwanachama wa NHIF. Pili, Bodi na Menejiment yote ya NHIF ibadilishwe, Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote uandikwe upya kuzingatia mapendekezo ya ACT wazalendo na sheria mpya ya NHIF itungwe ili kuimarisha mifumo ya huduma ya afya

7. Upungufu wa Watumishi wa afya katika hospitali za umma:
Uhaba wa watumishi wa afya katika vituo vya afya umekuwa ni tatizo sugu na la muda mrefu hali inayopunguza ufanisi wa wafanyakazi na kupunguza ubora wa huduma ya afya kwa wananchi. Juhudi za kuongeza watumishi wa Sekta ya Afya haziendani na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu nchini. Hadi kufikia mwezi Machi 2023, Sekta ya Afya ilikuwa na jumla ya watumishi wa afya wapatao 109,616 ambao ni sawa na asilimia 50 tu ya watumishi wote wanaohitajika katika sekta ya afya. Kati yao idadi ya madaktari na wauguzi ni ndogo zaidi.

Idadi ya chini kabisa ya wafanyakazi wa afya yaani madaktari, wauguzi na wakunga waliosajiliwa inayohitajika ili kuweza kutoa huduma ya afya ya msingi kwa jamii ni wafanyakazi 2.5 kwa watu 1000. Hadi kufikia Machi, 2022, Jumla ya madaktari 26,090 wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, ikiwa ni idadi ya madaktari 0.4 kwa kwa watu alfu moja. Jumla ya wauguzi na wakunga waliosajiliwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania ni 47,973, au wakunga 0.8 kwa watu 1000. Aidha kuna tatizo la mgawanyiko wa wafanyakazi wa afya, zahanati na vituo vya afya vijijini na maeneo ya pembezoni vikiwa na uwiano mdogo zaidi wa idadi ya wafanyakazi wa afya na wagonjwa kulinganisha na hospitali na vituo vya vingine vya huduma ya afya vilivyopo mijini.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kubuni njia endelevu za kuandaa na kuajiri wahudumu wa afya ili kimarisha huduma ya afya kwenye ngazi zote za vituo vya huduma ya afya, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha madaktari, wauguzi na wakunga kufanya kazi kwenye maeneo ya vijijini. Pili, wahudumu wa afya wanatakiwa kupewa mafunzo ya mara kwa mara (Refresher course) ikiwemo, mafunzo ya huduma kwa wateja, mafunzo ya huduma za dharura na uwajibikaji ili kuongeza ufanisi kwenye kazi
8. Hatua za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga haziridhishi
Mwaka 2021/2022 halmashauri 13, zimekuwa na ongezeko la vifo vya wajawazito kwa asilimia 12 hadi 48 kulinganisha na mwaka uliopita, Vifo vya watoto wachanga vimeongezeka katika halmashauri 11. Ripoti ya One Plan iii inaonyesha kila mwaka watoto wachanga zaidi ya 44,000 wanafariki. Idadi hii haijumuishi vifo vinavyotokea kwenye jamii.

Sababu kuu za vifo vya watoto wachanga ni kuzaliwa kabla ya wakati na kukosa hewa na maambukizi ya bakteria. Matatizo haya yanaweza kuepukika kabisa kwa kuimarisha huduma ya wajawazito na huduma ya mama na mtoto baada ya kujifungua katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya.

Vihatarishi vikuu vya afya ya wajawazito na watoto wachanga ni huduma ya afya za wajawazito kabla na wakati na huduma ya mama na mtoto baada ya kujifungua kutokutolewa kwa wakati na kukosekana kwa watoa huduma wenye ujuzi. Kuchelewa kwa wajawazito katika vituo vya afya ili kupata huduma ya matibabu wakati wa uchungu, watoa huduma ya afya ya msingi kutokuwa na ujuzi wa kutosha wa kutoa huduma za kujifungua, na uhaba wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya katika zahanati na vituo vya afya ni vikwazo vya juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Inakadiriwa kuwa kila mwaka wanawake wapatao milioni 2.3 hutarajiwa kupata ujauzito nchini Tanzania, kati yao ni Wajawazito ni 632,930 tu sawa na 27.5% walioanza kupata huduma za wajawazito chini ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito. Kuanza kliniki katika umri chini ya wiki 12 ni wakati muafaka kwa matokeo chanya ya ujauzito kipindi hiki kinatoa fursa muhimu ya kutambua na kutibu changamoto mbalimbali zinazoweza kuhatarisha maisha ya mama au mtoto aliyeko tumboni. Kati ya kina mama milioni 2.3 waliotarajiwa kupata ujauzito mwaka 2022/23, wajawazito milioni 1.4 walijifungua kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya sawa na asilimia 61. Kati yao wajawazito 1.3 milioni au asilimia 56 tu walipatiwa huduma ya kujifungua na watoa huduma wenye ujuzi. Idadi hii bado ni ndogo, na inatokana na upatikanaji wa huduma ya afya usioridhisha kwenye ngazi za zahanati na vituo vya afya.

ACT wazalendo, tunaitaka Serikali ikusanye takwimu za afya ya mama na mtoto kwenye jamii sambamba na zile zinazokusanywa kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ili kuwa na picha halisi ya huduma ya afya ya mama na mtoto. Pili, tunaitaka Serikali ihakikishe huduma bora za afya zinatolewa katika vituo vya afya ikiwa ni pamoja na kuwajengea wahudumu wa afya ya msingi maarifa na ujuzi wa kutosha kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga
9.

Kukosekana kwa mipango madhubuti ya kupambana na tatizo la afya ya akili
Matatizo ya afya ya akili ni tatizo linalokua kwa kasi hasa kwa vijana. Zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania ni vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 25. Watu takribani milioni 7 wanaishi na magonjwa ya akili nchini. Mgawanyo wa fedha ya Bajeti ya Wizara ya Afya 2023 -2024 haujatoa kipaumbele kwenye huduma ya afya ya akili.

Ripoti ya Ramani ya Afya ya akili Tanzania ya mwaka 2020 inaonyesha idadi ya wafanyakazi wa afya waliobobea kwenye ugunduzi na matibabu ya matatizo ya afya ya akili yaani wataalamu wa magonjwa ya akili (pychiatrists) ni 38 yaani waatalamu 0.07 kwa watu 100000 na wataalamu wa saikolojia (pyschologists) ni 0.03 kwa watu 100000, idadi hii ni ndogo kwa rika zote, kulinganisha na idadi kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, na idadi ya chini kabisa inayotakiwa na shirika la Afya Duniani la walau mtaalamu mmoja kwa watu 100000.
Huduma kwa waliopatwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto haziridhishi wala hazikidhi mahitaji ya nchi.

Katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022 jumla ya watu 97,479 walitoa taarifa katika vituo vya kutolea huduma ya afya, kati yao waliotoa taarifa ndani ya saa sabini na mbili (72) walikuwa 26,364 sawa na asilimia 27. vituo vya kutolea huduma jumuishi kwa waliofanyiwa vitendo vya ukatili ni 18, idadi hii ni ndogo sana kulinganisha na mahitaji makubwa nchini. Aidha, ni watoa huduma wa afya 745 na watoa huduma wa ngazi ya jamii 155 tu ndio wamejengewa uwezo wa namna ya kutoa huduma za kitabibu na kisaikolojia pamoja na utoaji wa elimu kwenye ngazi ya jamii. Idadi hii ni ndogo sana; haikidhi kabisa mahitaji ya jamii.

ACT Wazalendo, tunapendekeza Wizara ya Afya iweke kipaumbele kwenye tafiti za matatizo ya afya ya akili ili kubaini ukubwa wa tatizo, visababishi na njia za kutatua tatizo kwenye ngazi ya jamii.

Pili, Wafanyakazi wote wa afya kuanzia ngazi ya zahanati wajengewe uwezo wa kutoa huduma za kitabibu na kisaikolojia, na kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kutoa huduma ya afya ya akili na elimu kwa jamii.

Tatu, Bajeti maalumu itengwe ili kuongeza huduma ya afya ya akili kwenye ngazi ya jamii.

Nne, Wizara ya Afya iweke mpango mahususi wa kuboresha huduma ya afya ya akili kwa watu wazima, vijana na watoto.

Hitimisho:
Bajeti ya wizara ya afya kama asilimia ya pato la taifa ni ndogo na haikidhi mahitaji ya kufikia lengo la kuwa na jamii yenye afya bora kwa wote. Pia, mfumo wa ugharamiaji wa afya uliopo haufai, unamtwisha mwananchi mzigo mkubwa wa ugharamiaji wa huduma ya afya, ni mfumo ambao hauwezi kutufikisha kwenye lengo la Afya kwa wote. Bajeti ya Serikali inapaswa kuweka mkazo huduma ya afya kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya ili kuakisi mahitaji ya wananchi katika kupata ‘haki ya afya kwa wote’.
Imetolewa na;

Dr. Elizabeth Sanga
Twitter: @DrBsanga
Waziri Kivuli wa Afya
ACT Wazalendo.
14 Me, 2023.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK