Hotuba Mbadala ya ACT Wazalendo Wizara ya Maji na Mazingira katika mwaka wa fedha 2023/24

UBADHIRIFU WA MIRADI YA MAJI NCHINI; CHANZO CHA HALI DUNI YA UPATIKANAJI WA MAJI.

[Uchambuzi wa Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2023/24]

Utangulizi.
Jana jumatano tarehe 10 Mei 2022, Waziri wa Maji, Ndugu Jumaa Hamidu Aweso aliwasilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za wizara ya maji kwa mwaka wa fedha 2023/24. Katika mwaka huu wa fedha Serikali imeomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni 756. 2 kwa Wizara ya maji. Kati ya fedha hizo, kwa ajili ya maendeleo zimetengwa Shilingi bilioni 695. 8 na fedha za matumizi ya kawaida ni Shilingi bilioni 60.3.

Pamoja na makadirio ya mapato na matumizi, Hotuba ya Wizara ya Maji hutazama maeneo ya hali ya sekta ya maji (upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini, ubora wa maji na hali ya rasilimali ya maji), utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha uliopita na vipaumbele na mpango wa utekelezaji kwa mwaka huu.

Sisi ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Maji na Mazingira tumeifuatilia hotuba ya wizara na kuisoma ili kuweza kuitazama kwa kiasi gani imeweza kubeba matarajio au kutatua changamoto katika sekta hii nyeti kwa maisha ya wananchi. Pia, huu ni mwendelezo wetu wa kuzichambua hotuba za bajeti za wizara zote na kutoa mtazamo mbadala wa bajeti na vipaumbele.

Katika uchambuzi wetu wa hotuba ya bajeti, tumeona tuangazie maeneo nane (8) kutoka kwenye hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24

1. Kasi kubwa ya ubadhirifu wa fedha za miradi ya Maji.
Kumekuwa na wimbi kubwa sana la ubadhirifu wa fedha za miradi ya maji inayopelekea ucheleweshwaji wa upatikanaji wa huduma za maji katika maeneo husika. Kila mwaka wa ukaguzi wa matumizi ya fedha zinazoidhinishwa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali, wizara hii imekuwa ikikutwa na hoja zenye thamani ya mabilioni ya Shilingi zilizotafunwa.

Tukichukulia mifano ya ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG za mwaka 2021 ilionyesha kulikuwa na fedha kiasi cha shilingi bilioni 37.1 na dola za kimarekani milioni 6.05 ambazo zilikuwa zimefanyiwa ubadhirifu. Katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za Serikali ya mwaka 2022 Wizara ya maji na taasisi zilizochini yake imekutwa na matatizo mengi yanayoweza kusomeka kama ubadhilifu wa fedha za umma.

Kwanza, imeonyesha hoja zenye thamani ya Shilingi bilioni 56.27 kutoka kwenye mamlaka za maji nchini.

Pili, CAG ameonyesha ubadhirifu wa shilingi bilioni 82.8 wa fedha za Mkopo wa Uviko 19 kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Hiki ni kiwango kikubwa cha ubadhilifu katika sekta ya maji, Maendeleo ya sekta hii na upatikanaji wa maji hauwezi kufanikiwa kwa ubabe na maneno matupu bali kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo, kutokana na Kasoro zilizojitokeza katika matumizi mabaya ya Fedha za Umma tunamtaka waziri wa maji na timu yake wajitathmini kama wanafaa kuendelea kuiongoza wizara hii muhimu kwa maslahi mapana ya wananchi.
ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuwawajibisha wakandarasi, watendaji na watumishi wote waliohusika na uzembe huu.

2. Tatizo la mgao na upatikanaji duni wa maji Mijini na Vijijini
Mahitaji ya maji kwa umma yanaongezeka kwa 7% kila mwaka, lakini uzalishaji wetu wa maji unaongezeka kwa 2% kwa mwaka. Sababu kubwa ya uzalishaji kuwa chini sana tofauti na uhitaji, ni uwezo mdogo wa Wizara ya Maji kusimamia miradi mbalimbali ya maji, jambo linalochangia miradi mingi kutotoa maji kabisa ama kuzalisha kiwango kidogo. Kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 uzalishaji wa maji nchini ni 56% tu ya uhitaji wa maji wa wananchi, hivyo kupelekea wananchi kutumia muda mwingi na gharama kubwa kutafuta maji.

Asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijijini, licha ya idadi kubwa ya watu kuonekana wanaishi vijijini na mchango wao katika pato la taifa kupitia shughuli za kilimo, uvuvi, madini na mazao ya misitu. Hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni asilimia 77 tu na asilimia hizo zinatajwa kwa maana miradi iliyofika sio upatikanaji wa huduma ya maji, uhalisia unaonyesha kuwa kutokana na kutofanyika kwa ukarabati na uwekezaji mdogo kati ya miradi ya maji iliyowekezwa vijijini takribani asilimia 30, haifanyi kazi kwa ufanisi au imekoma kabisa kutoa huduma ya maji na zaidi ya vijiji 300 nchini Tanzania havijafikiwa na mradi wowote wa maji.

Hali ya upatikanaji wa maji maeneo ya mijini ni asilimia 88 tu huku kukishuhudiwa upotevu mkubwa wa maji na udhibiti mdogo wa majitaka kutokana na ubovu wa miundombinu na usimamizi usioridhisha.

Katika hotuba za waziri wa maji za kila mwaka zinaishia kutaja orodha ndefu ya miradi iliyotekelezwa lakini kila mwaka inatajwa miradi ambayo ukamilishwaji wake unachukua wastani miaka mitatu hadi kumi. kutokamilika kwa Mradi wa Maji wa Kagongwa – Isaka kwenda katika Vijiji vya Mwalugulu, Kilimbu, Jana, Butondolo na Itogwanholo, Mradi wa Maji Ruangwa - Nachingwea, Mradi wa Maji Mkinga - Horohoro, Mradi wa Maji Morunganya – Morogoro Vijijini, Mradi wa Maji Ukiliguru, Sumve hadi Koromije ni miongoni mwa miradi ambayo kama ingekamilika kwa wakati ingepunguza uhaba wa upatikanaji wa maji kwa wanavijiji.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza bajeti ya miradi ya maendeleo ili kutanua mitandao ya maji kwenda vijijini zaidi.
Pili, tunaitaka Serikali ianzishe Gridi ya Taifa ya maji kwa lengo la kuongeza kasi ya usambazaji maji.

3. Maji ni Mtego wa Umasikini wa Watanzania.
Mwenendo wa upatikanaji wa maji vijijini upo nyuma ya maelengo ya muda wa kati ambayo yanasema kufikia asilimia 80 ya wananchi vijijini watapata huduma ya maji ifikapo 2020 na sasa tupo 2022 huku bado tukiwa kwenye asilimia 77 tu.

Changamoto ya upatikanaji wa Maji inachangia sana kuwashikilia watu wa vijijini kwenye dimbwi la umasikini. Gharama za maji wanazotumiwa wananchi ili waweze kuishi ni kubwa mno maeneo ya vijijini kiasi kwamba zinazidi wastani wa pato la mtu mmoja (per capital income) kwa siku nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi ya Taifa ya Juni 2021, “Pato la Taifa mwaka 2020 lilikuwa shilingi trilioni 148.5, huku idadi ya watu Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa watu milioni 55.9 mwaka 2016. Hivyo, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa Shilingi 2,653,790 mwaka 2020.”

Kwa kipato hicho, nitatoa mfano wa Kijiji cha Gehandu huko Mbulu, mkoani Manyara ambako mwananchi ananunua maji pipa moja la lita 200 kwa shilingi 7000 na familia moja inahitaji angalau pipa moja kwa siku kwa matumizi ya kujibana kabisa ya maji. Kwa hiyo mwananchi huyu atahitaji takribani shilingi milioni 2.5 kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu ya kutumia yeye na familia yake. Kwa familia ya Watu 6, huu ni wastani wa 16% ya kipato cha kila mwanafamilia hata mtoto mdogo wa siku moja kutumika kununua Maji.

Hivyo familia moja inatumia wastani wa kipato cha mtu mmoja kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu. Lazima familia hii iendelee kushikwa kwenye mtego wa umasikini. Zaidi muda unaotumika kutafuta maji ni mkubwa sana, na hupatikana kwa mateso ya kuyabeba kwa kutumia wanyama kama punda, lakini maji yenyewe yakiwa ni chanzo cha maradhi kwa kuwa si safi na salama.

ACT Wazalendo tunaamini Tanzania tunao uwezo wa kuondoa kabisa hali hii ikiwa Wizara ya Maji itapewa bajeti ya kutosha kutekeleza miradi ya maji, itaongeza umakini na ufanisi kwenye usimamizi wa miradi hiyo na kuhakikisha inazalisha kiwango cha juu cha maji kama ilivyokusudiwa, pamoja na kuondoa upotevu wa mapato kwenye usimamizi wa miradi husika oamoja na uendeshaji wa mamlaka za maji nchini.

4. Mwendelezo wa hasara kubwa kutokana na upotevu wa maji Shilingi bilioni 162.14
Upotevu wa maji ni kipimo muhimu cha ufanisi na utendaji wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira. Kwa kutathmini kiasi cha maji kinachozalishwa au kununuliwa lakini hupotea kabla ya kufikia wateja. Upotevu wa maji huwasilishwa kwa asilimia na hutathminiwa kwa kutoa kiasi cha maji kilichouzwa kwa watumiaji kutoka kwenye jumla ya kiasi kilichozalishwa au kununuliwa.

Sababu zinazochangia upotevu wa maji ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ya zamani inayosababisha uvujaji wa maji, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji imeweka kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika kuwa kisizidi asilimia 20. Kwa miaka minne mfululizo mpaka sasa bado kuna kiasi kikubwa cha maji kinapotea na kusababisha hasara kubwa Bukoba 43.00%, Morogoro 40.48% Arusha 37.00% , Dar es salaam 39.43% Korogwe 38.00% CAG ameonesha upotevu huu umekua ukijirudiarudia na kuongezeka hali iliyoisababishia Serikali hasara ya shilingi Bilioni 162.14

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kufanya ukaguzi na ukarabati wa miundombinu ya maji kama vile, mita, mabomba, matanki, kuzuia upotevu wa maji na pia kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa wananchi unafika kwa wakati.
Pia, Bajeti ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu bora zaidi inapaswa kutengwa ili kuzuia gharama tunazozipata kutokana na upotevu wa maji.

5. Ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji.
Licha ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwa miaka mingi imeonekana kuwa Wizara ya Maji bado haijaweza kutatua changamoto zilizopo kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa katika Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 na Malengo ya Maendeleo ya Milenia.

Baadhi ya changamoto zilizopo ni pamoja na kuhakikisha wananchi wote wanapata maji, kudumisha ubora na viwango vya maji, kuweka miundombinu endelevu ya maji, na kuwezesha mipango na maamuzi shirikishi. Changamoto hizi zinahitaji hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa rasilimali maji nchini zinasimamiwa kwa ufanisi na kwa njia endelevu.

i. Mradi wa Uboreshaji Usambazaji Maji Same–Mwanga-Korogwe (SMKWSIP)
Mkataba huo uliosainiwa tarehe 20 Novemba 2014, ulitarajiwa kukamilika tarehe 16 Julai 2017 kwa thamani ya mkataba wa awali wa Dola za Marekani milioni 41.36. Mkataba huo ulisitishwa tarehe 29 Desemba 2020 kutokana na mkandarasi kushindwa kuwasilisha Dhamana ya Mradi na kuhakikisha inakuwa hai kwa kipindi cha utekelezaji wa mkataba kinyume na Kifungu Na. 4.2 cha Masharti ya Jumla ya Mkataba.

Tangu mwaka 2014 mradi huu haukamilika, kumekua na kizungumkuti katika ukamilikaji wake, katika hotuba ya bajeti Waziri wa maji Ndg. Jumaa Aweso (Mb) ameliambia bunge kuwa Wizara na mkandarasi wameingia Mkataba wa Makubaliano tarehe 13, Machi 2023. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2024.

ii. Mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama Wenye Thamani ya Sh. bilioni 56.35
Tarehe 17 Novemba 2020, Wizara ya Maji ilisaini mkataba Na. ME-011/2020-2021/CONTRA/W/01 na M/s Unik Construction Engineering (Lesotho) Ltd kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Mugango-Kiabakari-Butiama kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 24.44 sawa na Sh. bilioni 56.35. Mradi huo ulipangwa kuanza tarehe 17 Desemba 2020 na kukamilika tarehe 17 Desemba, 2022.

Hadi kufikia tarehe 28 Desemba 2022, utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 69 tu, ukionesha ucheleweshaji wa asilimia 24 dhidi ya lengo lililopangwa la asilimia 93 wakati dola za Marekani milioni 12.04 sawa na Sh. bilioni 27.76, ikiwa ni asilimia 49 ya kiasi cha mkataba kilikuwa kimelipwa kwa mkandarasi na mshauri.

CAG katika ripoti yake ya 2022 anasema "Nilibaini kuwa kazi kubwa kama vile sehemu ya kuchujia maji, na ujenzi wa vituo vya kusukuma maji, zilikuwa nyuma sana ya mpango uliokubaliwa. Kituo cha kusukuma maji cha juu kilikuwa kimekamilika kwa asilimia 10 ikilinganishwa na asilimia 95 iliyopangwa, wakati Kituo cha Kusukuma Maji cha Chini kilikuwa kwa asilimia 78 ikilinganishwa na asilimia 95 iliyokubaliwa.

Aidha, hadi wakati wa ukaguzi kazi za kielekitroniki na mitambo (electromechanical works) na vifaa ambavyo vinachangia asilimia 25 ya kiasi cha mkataba, vilikuwa bado havijanunuliwa na kufungwa, na vilitarajiwa kukamilika kwa asilimia 95 kufikia Novemba 2022.

Kuchelewa kwa miradi hii mikubwa kunasababisha wananchi wa maeneo husika kukosa uhakika wa maji na kuendelea kuteseka, hata hivyo kuchelewa kwa miradi hii kunatengeneza mazingira ya ubadhilifu katika fedha za umma, mathalani katika mradi wa Same-Mwanga-Korogwe Serikali iliingia nyongeza ya mkataba uliosababisha ongezeko la takribani dola za kimarekani Milioni 2.3 bila idhini na bila kufuata sheria ya manunuzi
ACT Wazalendo, tunataka utekelezaji wa miradi hii miwili ichunguzwe kwani katika utekelezwaji wake kuna harufu ya ubadhilifu mkubwa na uhujumu kwa wananchi wa maeneo hayo, aidha Serikali ihakikishe miradi hii inakamilika mapema na endapo itachelewa hatua madhubuti za kimkataba zichukuliwe dhidi ya mkandarasi.

6. Upungufu wa uzalishaji wa maji kwa mamlaka za maji nchini.
Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira, Sura 272 inaelekeza mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira kutoa huduma ya maji safi na majitaka katika miji. Hata hivyo, miongoni mwa kero kubwa kwa wananchi nchini ni kukatikakatika kwa maji, sehemu kubwa ya nchi kumekua na mgao wa kimyakimya wa maji. jambo hili limekuwa kero kubwa sana na aibu kubwa kwa taifa hili lenye maji lita za ujazo Bilioni 126 na mahitaji ya lita za ujazo Bilioni 62 tu, hii inaonesha kuwa kuna uzembe mkubwa kwa mamlaka za maji na usafi wa mazingira katika utoaji wa huduma, mkazo wa mamlaka nyingi nchini ni kukusanya mapato zaidi na si kuboresha huduma.

Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) anasema katika ukaguzi wa mwaka 2021/22 nilibaini mamlaka za maji 25 zilikuwa na upungufu wa uzalishaji na usambazaji wa maji kiasi cha kuanzia asilimia 10 hadi asilimia 80 kwa siku mfano mamlaka ya maji zinazozalisha maji pungufu ni Bariadi upungufu wa 80.40%, Karatu upungufu 79.71% Dodoma 40.64%, Moshi 39.45% Mbeya 26.11%, Mwanza 46.78% Lindi 50.78, Tanga 20.96%
ACT wazalendo tunaitaka Serikali na mamlaka zake kuhakikisha huduma za maji kwa Watanzania zinapatikana muda wote, mamlaka zinazozalisha maji pungufu zieleze sababu ya changamoto hiyo na mikakati yake hadharani kwani mwka 2021 uzalishaji pungufu ulikua katika mamlaka 23 tu ongezeko hili linathibitisha uzembe na kutowajibika ipasavyo kwa baadhi ya mamlaka za maji, hatuna sababu yoyote ya msingi ya kukatakata maji kwa maeneo kama mwanza, Moshi na maeneo mengine hapa nchini, nchi yetu ina utajiri wa maji.

7. Mifumo mibovu ya uondoaji wa maji taka katika miji.
Huduma ya usafi na mazingira ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira bora na kuepusha maradhi yanayoweza kusababishwa na uwepo wa majitaka katika mazingira yetu. Ili kuweza kuondokana na milipuko ya magonjwa kama vile magonjwa ya matumbo na kipindupindu mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira zinalazimika kutoa huduma za usafi wa mazingira pamoja na kuhakikisha matibabu salama na utupaji wa majitaka katika maeneo yao ya huduma angalau kufika asilimia 40.
Hali ya sasa kwenye miji yetu, inatia shaka sana, kuna miundombinu mibovu ya kuweza kuondosha majitaka. Ni jambo la kawaida kukuta majitaka yanatiririshwa mitaani, mitaro kutofunikwa, uvujaji wa mitaro na matenki ya majitaka.

Mfumo wa sasa wa uondoaji wa maji taka kwa kubeba na magari ya bowser sio mfumo salama kabisa. Hakuna miundombinu imara iliyojengwa kwa ajili ya kuondokana na changamoto ya majitaka kusambaa mitaani na kusababisha milipuko ya magonjwa.

Kwa namna hali ilivyokuwa mbaya, ipo haja ya kuwa na udhibiti na usimamizi mzuri wa mifumo yetu ya taka lakini Serikali haijafanya juhudi za kutosha kuwekeza kwenye kujenga miundombinu ya kuondoa majitaka majumbani, sehemu za taasisi za Serikali.

Tafiti zinaonyesha ili kupata ufanisi katika usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji wa taka kunahitaji bajeti ya kutosha, bajeti ya Serikali ya mwaka huu iliyotengwa kwa ajili ya usimamizi wa mifumo ya taka ni finyu sana.

Ni wakati sasa Serikali iongeze jitihada ya kibajeti na kiusimamizi kwenye uboreshaji wa miundombinu katika miji ili kuwezesha mifumo ya maji taka ya mojakwamoja kwa kujenga mitaro mikubwa itakayopita mijini, aidha hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wabebaji wa maji taka watakapobainika kutirirsha maji taka mitaani.

Hitimisho:
Mwisho, Tanzania ni nchi pekee barani Afrika iliyozungukwa na Maziwa makuu na yenye jumla ya mabonde 9. Hifadhi ya maji kwa Mwaka kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Wizara ya Maji mwaka 2019 ni mita za ujazo billion 126 huku maji ya juu ya Ardhi yakiwa na mita za ujazo billion 105 na chini ya Ardhi yakiwa ni mita za ujazo billion 11

Hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira unachora mstari mkubwa wa usawa wa kimaendeleo uliopo kati ya mijini na vijijini. Kwa takribani miaka 61 ya uhuru wa nchi yetu wanakijiji zaidi ya asilimia thelathini hawajawahi kuona maji ya bomba na kuyatumia, ni wazi watu hawa hawajanufaika na matunda ya uhuru wa nchi yao. Ili kuweza kuwaondoa wananchi kwenye unyonge na manungúniko haya hatuhitaji kuwa na mbwembwe nyingi bali vitendo. Vitendo ni kutenga fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maji. Maji ni uhai.

Imetolewa na;
Ndg. Ester A. Thomas
Twitter: @Ester_Thomas1
Waziri Kivuli wa Maji na Mazingira
ACT Wazalendo.
11 Mei, 2023

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK