Hotuba Mbadala ya ACT Wazalendo ya Wizara ya Madini kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2023/2024

HOTUBA YA WAZIRI KIVULI WA MADINI-ACT WAZALENDO NDG. EDGAR FRANCIS MKOSAMALI KUHUSU MPANGO WA BAJETI WA WIZARA YA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24.

Utangulizi.
Katika mwendelezo wa kufuatilia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiendelea kupitia, kujadili na kuidhinisha bajeti mbalimbali za Serikali, juzi Alhamisi tarehe 27 April 2023, Waziri wa Madini Ndg. Dotto Biteko (Mb) aliwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Sekta ya Madini ni miongoni mwa sekta muhimu kwa nchi yetu. Sekta hii inabeba uzito na jukumu kubwa sana katika uchumi wa taifa na inastahili kupewa kipaumbele na Serikali. Ingawa nchi ina utajiri mkubwa wa rasilimali madini ya aina mbalimbali lakini bado utajiri huo haujainufaisha nchi kama inavyostahili na kuondoa umasikini wa wanachi.

Pamoja na hatua mbalimbali zilizofanyika; ambazo zimesaidia kidogo kuongeza mchango wa madini katika pato la taifa, lakini bado kuna changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii katika usimamizi, mikataba ya madini, kuongeza thamani ya madini yetu, uchimbaji na utoroshwaji wa madini.

Kwa hiyo ni muhimu kutazama kwa umakini Mpango wa Bajeti, Sheria, mikataba na taratibu za usimamizi wa shughuli za madini zinavyopaswa kutafsiri umuhimu huo. ACT Wazalendo kupitia Waziri Kivuli wa Madini imeangazia maeneo hayo na kutoa mapendekezo na hatua za kuchukuliwa ili kuondoa changamoto hizo.

Maeneo Nane (8) ya uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

1. Mchango wa mdogo wa Sekta ya Madini Katika pato la Taifa na uchumi wa nchi
Takwimu za Serikali na Wizara ya Madini zinaonesha kwamba mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia 7.2 mwaka 2021.

Aidha sekta ya madini imekuwa kinara kwa kuingiza nchini fedha za kigeni ikiwa imeingiza asilimia 56 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote nje ya nchi. Aidha Serikali imejiwekea malengo kufikia aslilima 10 ya pato la taifa kutoka katika sekta ya madini.
Pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo ya shughuli za madini nchini.

ACT Wazalendo inaamini kwamba mapato hayo yangekuwa maradufu endapo Serikali ingekuwa makini na kuwekeza katika miradi mikubwa ya madini ya chuma ya Liganga na Mchuchuma, mradi wa Kabanga Nickel, miradi ya madini muhimu na udhibiti wa utoroshwaji wa madini. Mradi wa chuma na Kabanga Nickel imesuasua kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Endapo Serikali ingewekeza kwenye miradi hii, leo tungekuwa tunazungumza asilimia 15 – 20 ya mchango wa madini kwenye pato la taifa.

2. Mikataba ya Madini na Maendeleo ya Watu
Pamoja na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na 2019, kanuni zake na mikataba ambayo Tanzania inaingia na wawekezaji kwa mfumo wa ‘Production Sharing Agreement’, lakini bado aina hii ya mikataba inamwondoa mwananchi mkaazi katika kunufaika na rasilimali madini yanayopatikana katika makaazi yake.

Sera ya madini (2009), inataka wananchi kufidiwa makaazi na ardhi yao ili kupisha shughuli za uchimbaji wa madini tu. Wananchi hufidiwa mali na makazi yao duni kwa thamani ya soko na baada ya hapo hawanufaiki tena na shughuli za uchimbaji na biashara ya madini isipokuwa kwa hisani ya mwekezaji au mchango wa mwekezaji kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

ACT Wazalendo tunaona mfumo huu wa mikataba hauwezi kuwaondolea umasikini na kuwaletea maendeleo wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguuka shughuli za uchimbaji mkubwa wa madini.

Kwa muda sasa, ACT Wazalendo tumekuwa tukipendekeza ushirikishwaji wa wananchi kabla na wakati wa uwekezaji kwa kupewa sehemu ya umiliki wa shughuli za madini yanayopatikana katika maeneo yao kwa sharti la kupata kibali kutoka kwa wananchi kupitia Serikali ya Kijiji (Free Prior Informed Consent).

Kabla ya Tume ya Madini kutoa leseni kwanza iwe imethibitisha na kusajili ridhaa za wananchi katika eneo husika ikiwemo mikataba ya namna wenyeji watafaidika. Hii itapunguza malalamiko ya wananchi na vile vile itapunguza sana migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.

Mfumo wa sasa unajenga zaidi uchumi na faida kwa mwekezaji na Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali huku ukimwacha mwananchi katika dimbwi la umasikini licha ya kuishi jirani na utajiri mkubwa wa madini.

Tarehe 17 April 2023 Serikali imesaini mikataba mitatu ya uchimbaji wa madini muhimu ya mkakati ya Kinywe (Graphite) na makampuni kutoka nchini Australia (Evolution Energy Minerals Ltd, Ecograf Limited na Peak Rare Earth Ltd) yenye jumla ya thamani ya dola za Kimarekani milioni 667.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kueleza ni kwa kiwango gani uwekezaji huu utakuwa na maslahi kwa maendeleo ya moja kwa moja kwa watu wa maeneo ya Chilalo, Wilayani Ruagwa; Epanko, Wilayani Mahenge na Ngwala (Songea). Aidha Serikali ieleze namna mikoa ya Lindi, Morogoro na Songwe itanufaika moja kwa moja na uwekezaji huu.

3. Wizi na Utoroshwaji wa Madini
Utoroshwaji na wizi wa madini umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Taarifa za Wizara ya Madini katika mwaka wa fedha 2021/2022, zinaonyesha kwamba Tume ya Madini iliokoa kiasi cha Shilingi milioni 501.2 baada ya kukamata madini yaliyokuwa yakitoroshwa.

Aidha katika hotuba yake Bungeni, Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko ameliambia Bunge kwamba katika kipindi cha 2022/2023 madini yenye thamani ya Shilingi milioni 532.44 yalikamatwa yakitoroshwa. Hiki ni kiwango cha thamani ya madini yaliyokamatwa. Hatujui kiwango cha madini yaliyofanikiwa kutoroshwa.

Kutokana na kuendelea kuongezeka kwa vitendo vya utoroshwaji wa madini yetu, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuchukua hatua zifuatazo;

Mosi, kufanya utafiti maalumu na kubaini sababu zinazopelekea wafanyabiashara ya madini kuvutiwa na vitendo vya utoroshaji kuliko kupitisha madini kwenye masoko halali yaliyopo. Je! ni kwa sababu ya sheria kandamizi? Je! Ni kwa sababu ya tozo na kodi kubwa, Je! ni kwa sababu ya wizi madini machimboni au ni kwa sababu ya tamaa ya kupata faida kubwa kwa baadhi ya wafanya biashara?

Pili, tangu mwaka jana iliporipotiwa na wafanyabiasha wa kigeni wakinadi madini aina ya Ruby kwenye mnada wa kimataifa nchini Dubai kwa mabilioni ya shilingi, Wizara ya madini haijatueleza nini ilikuwa hatma ya madini hayo yaliyodaiwa kutokea nchini Tanzania. Je! Serikali ilikubalina na ofa ya mgao wa bilioni 20 iliyotaka kutolewa na wauzaji kama ilivyoripotiwa na Waziri Dotto Biteko? Nini kilijiri na ni hatua zipi zilizofikiwa kutokana na madini hayo yaliyotoroshwa?

Tatu, tunarudia wito kwa Wizara ya Madini na Serikali kwa ujumla kuendelea kuzuia mianya ya utoroshwaji wa madini na kuchukua hatua kali kwa wahusika wa vitendo hivyo. Na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ya madini na kanuni zake zinaipa Serikali 16% ya umiliki kwenye makampuni ya madini

4. Malalamiko ya Wachimbaji Wadogo nchini.
Pamoja na mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo hapa nchini lakini hakuna jitihada za wazi za Serikali kuwasaidia, kuwawezesha na kuwainua wachimbaji wadogo wa Tanzania.

Wakati migodi mikubwa inachangia asilimia 60 ya mapato yote ya madini na kuajiri watu 14,742 tu, kwa upande mwingine hadi kufikia mwaka 2021 jumla leseni 6,381 zilitolewa na Tume ya Madini kwa wachimbaji wadogo ambao wameajiri moja kwa moja wastani wa watu laki mbili kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na wafanya biashara ya madini bila kuhesabu idadi wa watoa huduma na bidhaa kwenye maeneo ya machimbo. Wachimbaji wadogo wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato yote yatokanayo na madini hapa nchini.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali isiishie kutoa elimu na maelekezo tu kwa wachimbaji wadogo. Ni lazima serikali ijihusishe moja kwa moja kuwawezesha vifaa na fedha ili wafikie uwezo wa kumiliki na kuendesha migodi ya kati na hatimaye mikubwa.

Katika hotuba yangu mbadala kwa waandishi wa habari mwaka jana, niliitaka na kuishauri Serikali kutenga walau asilimia 5 ya mapato yanayotokana na madini kwa ajili ya uwezeshaji wa fedha na mitambo midogo kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki maalumu ya madini itakayokuwa rafiki kwa mazingira ya wachimbaji wadogo. Serikali haijatekeleza maoni haya zaidi ya kuhamasisha mikopo ya kibiashara ya kibenki ambayo ina masharti ya dhamana na kibiashara ambayo haiwezi kuwa rafiki kwa wachimbaji wachanga.

Akisoma bajeti yake Bungeni Aprili 27 Waziri Dotto Biteko ameeleza kwamba Serikali imenunua mitambo 3 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa hapa nchini. Pamoja na umuhimu wa mitambo kwa wachimbaji wadogo, maamuzi ya kununua mitambo hiyo inazua maswali mengi yanayohitaji majibu. Miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na;

i. Hapa nchini kuna migodi zaidi ya 80 ya wachimbaji wadogowadogo na migodi mingi ina wachimbaji zaidi ya 100. Je! Mitambo 3 itawasaidia vipi wachimbaji zaidi ya 800 waliotawanyika mikoa na maeneo tofauti tofauti hapa nchini?

ii. Je! Wizara imenunua mitambo hiyo 3 kwa gharama gani? Ni mitambo kwa ajili ya shughuli gani shughuli za madini na ni ya aina gani?

iii. Je! Wizara imefanya upembuzi yakinifu na kubaini ufanisi na tija ya kuwa na mitambo hiyo kwa ajili ya sekta binafsi? Kuna ufanisi unaotarajiwa katika hili?

iv. Je! Wizara inataka kujiingiza kwenye biashara ya kukodisha mitambo? Kwa gharama na utaratibu gani?

Aidha, ACT Wazalendo inazipongeza benki za NMB, CRDB, NBC, Azania na KCB kwa kuunga mkono hoja yetu ya mikopo kwa wachimbaji wadogo na wale wa kati. Aidha tunazipongeza taasisi hizi kwa kukuza kiwango cha ukopeshaji kwa wachimbaji wadogo kutoka shilingi bilioni 36 mwaka 2022 hadi bilioni 145 mwaka 2023. Hata hivyo mabenki yamependekeza kuundwakwa kikosi kazi ili kuandaa miongozo ya ukopeshaji na kwamba kikosi kazi kiundwe kutoka miongoni mwao, Wizara na STAMICO.

5. Masoko ya Madini
Masoko ya madini yenye bei nzuri ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya madini ili kupata faida nzuri na kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo. STAMICO ina wajibu wa kutafuta masoko ya madini ndani na nje ya nchi ili kuleta tija kwa wachimbaji na hatimaye kuvutia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu waweze kujiajiri huko na hatimaye kutibu tatizo sugu la ukosefu wa ajira nchini.

Wachimbaji wadogo wa Longido walitoa ombi hili kwa Serikali kuhusu madini yao ya Ruby, Spessartite, Sunstone na Quartz.

ACT Wazalendo kwa niaba ya wachimbaji kote nchini tunaihoji STAMICO kuhusu utekelezwaji wa suala hilo na kuitaka kuongeza jitihada za kutafuta masoko ya uhakika yenye kutoa bei nzuri kwa madini yetu badala ya kutegemea madalali wa madini wanaonunua madini kwa bei poa na kuyauza kwa bei nzuri kwenye masoko ya kimataifa.

6. Uwekezaji Katika Madini Muhimu ya Kimkakati
Kwa sasa dunia inahama kutoka katika matumizi ya nishati zinazochafua mazingira kwa kutoa hewa ya ukaa kwa wingi na kuhamia kwenye vifaa vya kielekroniki kama kompyuta, vyombo vya moto kama magari na mitambo inayotumia nishati jadidifu (renewable energies) inayotokana na mionzi ya jua (solar energy), mabetri ya kuchaji (rechargeable batteries), na gesi asilia (natural gas) na magari yanayotumia umeme.

Tanzania imebarikiwa kuwa na madini muhimu na ya kimkakati yanayotakiwa duniani kwa ajili hiyo madini kama vile graphite, lithium, nickel, cobalt na mengine mengi. Madini haya ni machache duniani na mengine yana bei kubwa kuliko hata madini makuu (major metals)
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuwa na mpango maalumu wa utafutaji na uchimbaji wa madini haya kwa umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na sera na kanuni maalumu zitakazoongoza biashara nzima ya madini haya.

Aidha, tunataka maslahi ya taifa yalindwe kwa kuongeza uwazi na kuingia katika mikataba yenye tija kwa kuanza na mikataba ya uchimbaji wa graphite katika mikoa ya Lindi, Morogoro na Songwe na mikataba itakayosainiwa ya uchimbaji na uchakataji wa madini ya lithium katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

7. Uchimbaji wa Madini na Uhifadhi wa Mazingira
Kulingana na tafiti na taarifa ya taasisi ya Natural Resources Governance Institute (NRGI) na Policy Analysis Development Organization (PADO), shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini huchangia kwa asilimia 4 – 7 katika uharibifu wa mazingira nchini Tanzania.
Na kwa utafiti uliofanywa na ACT Wazalendo kwenye migodi 5 ya wachimbaji wadogo mkoani Mwanza na Geita, tumegundua kwamba kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya nishati na magogo ya miti yanayosimikwa ili kusapoti njia za uchuimbaji chini ya ardhi.

Tofauti na migiodi mikubwa inayotumia zege, wachimbaji wadogo hutumia maelfu ya magogo ya miti kwa ajili hiyo. Ukifika katika migodi ya wachimbaji wadogo utadhani umefika katika kiwanda cha kuchakata magogo.

Kwa bahati mbaya Wizara ya Madini haina jitihada zozote katika jambo hili. Waziri wa Madini Ndg. Dotto Biteko wala hakugusia jambo hili nyeti katika hotuba yake ya Bajeti ya 2023/2024.

Katika kukabiliana na uhaibifu na mazingira katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuwa makini (serious) na kuja na njia mbadala na miradi ya kuhami uharibifu wa mazingira katika shughuli za madini ikiwa ni pamoja na:

Mosi, Wizara ya Madini ishirikiane na Wizara zinazoshughulika na mazingira, nishati, maji, ujenzi na afya katika kusimamia changamoto za miundombinu katika maeneo ya machimbo hasa ya wachimbaji wadogo na kuja na njia ya kutatua changamoto hizo.

Pili, kushirikisha sekta binafsi juu ya kupata suluhisho ya changamoto ya nishati katika migodi ili kuachana na matumizi ya diesel katika kuendesha mitambo migodini.
Tatu, kuhamasisha na kuvutia uwekezaji na matumizi ya nishati jadidifu na hasa uwekezaji wa umemejua (Stand alone solar power systems) katika migodi yote, mikubwa, ya kati na midogo hasa ile ambayo haijaunganishwa na gridi ya taifa. Iwe ni marufuku kwa migodi mikubwa kuendesha shughuli zake kwa kutumia nishati ya mafuta.

8. STAMICO na Mradi wa Makaa ya Mawe (Rafiki Briquettes)
Pamoja na tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira linalotokana na ukosefu wa nishati ya uhakika ya kupikia, kampuni tanzu ya Serikali (STAMICO) bado inajivuta sana na kutumia muda mwingi katika kukamilisha taratibu na kuanza uzalishaji na usambazaji wa makaa ya mawe maarufu kwa jina la ‘Rafiki Briquettes’ kwa ajili ya matumizi ya kupikia majumbani.

ACT Wazalendo tunaamini kwamba matumizi ya gesi na makaa ya mawe kwa wingi kungeokoa mamilioni ya miti inayokatwa kila mwaka kwa ajili ya kutengeneza mkaa wa kupikia. Tunaitaka Serikali, STAMICO na Wizara ya Madini kufanya mchakato huu kwa haraka ili kuiokoa misitu na mazingira. Na kama STAMICO haiwezi kutokana na urasimu wa Kiserikali basi itafutwe namna ya kutelekeleza mradi huu kupitia ushirikiano na sekta binafsi kwa njia ya PPP. Ukataji miti kwa ajili ya nishati ya kupikia na matumizi ya magogo viwandani na migodini ni janga kubwa lisilopata msukumo stahiki na Serikali.

Hitimisho
Kutokana na Uchambuzi wetu wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 tunaona bado kuna changamoto ya sekta ya madini kutochangia vya kutosha katika maendeleo ya nchi hasa ya kiuchumi na kijamii. Kuwepo kwa usiri mkubwa wa mikataba na ushirikishwaji mdogo wa wananchi. Kutotekelezwa ipaswavyo kwa sheria ya madini iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, wananchi kutolipwa fidia stahiki wanapohamishwa kupisha miradi ya uchimbaji wa madini na jamii kutonufaika na uwekezaji huo. Aidha, uharibifu wa mazingira katika maeneo ya migodi mikubwa ukilinganisha na jitihadi zinazofanywa kudhibiti.

ACT Wazalendo inaamini kwamba sekta ya madini inaweza kufanya vizuri zaidi na kuchangia maradufu katika uchumi wa nchi kama Serikali itajikita katika kutatua changamoto hizo na kuweka vipaumbele katika uchimbaji wa madini ya kimkakati na kuwashirikisha wananchi katika uchumi na biashara ya madini.

Imetolewa na;
Ndg. Edgar Francis Mkosamali,
Twitter: @EMkosamali
Waziri Kivuli wa Madini
ACT Wazalendo.
29 April 2023.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK