HOTUBA YA KIONGOZI WA ACT WAZALENDO NDG. KABWE ZUBERI RUYAGWA ZITTO KWA WATANZANIA KUPITIA MKUTANO WA KAMATI KUU YA ACT WAZALENDO- ZANZIBAR TAREHE 8 AGOSTI 2021

1. UTANGULIZI
Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo,

Ndugu Watanzania wenzangu,

Kwa takribani mwezi mzima sasa, nimekuwa nikitafakari, kushauriana na viongozi wenzangu, pamoja na kujisaili, juu ya mambo kadhaa yanayoendelea nchini, ya kiuongozi, kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Nimekuwa nikipitia njia na mienendo yetu kama Taifa kwa miaka karibu kumi iliyopita, nikiyatazama mapungufu na mafanikio yetu, changamoto na fursa zetu, mafunzo na majuto yetu.

Nimefanya yote hayo kwa lengo la kutumia uzoefu na mapito yetu hayo kushauriana na viongozi na wananchi wenzangu juu ya njia sahihi na bora zaidi za kuondoa mikwamo tuliyonayo sasa katika Taifa letu.

Hii ndio sababu iliyonifanya nitumie nafasi hii ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati Kuu ya chama kuzungumza nanyi pamoja na Taifa. Nina mambo matatu tu ya kuzungumza nanyi siku ya leo.


2. JANGA LA KORONA (UVIKO-19)

Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo,

Ndugu Watanzania wenzangu,

Dunia imeendelea kuathiriwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO -19). Janga hili tayari limeleta madhara kwa dunia nzima kwa kuharibu uchumi wa nchi mbalimbali, na kusababisha vifo vya watu wapatao milioni 4.2 duniani.

Madhara ya korona kwa wananchi wetu hapa Tanzania ni makubwa pia. Pamoja na taarifa za hospitali zetu kuzidiwa, vitanda kujaa, kukosekana kwa mitungi ya hewa ya oksijeni na kadhalika, watu wanaoendelea kupoteza maisha ni wengi sana.

Taarifa ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ya mwaka 2020 inaonyesha kuwa maombi ya kusajili vifo kupitia mfumo wa E-Huduma yameongezeka kufikia vifo 112,487 mwaka 2020 ukilinganisha na vifo 35,000 mwaka 2019. Hili ni ongezeko la zaidi ya 200% kwa mwaka.

Mtakumbuka kuwa mwaka 2020 ndio mwaka ambao ugonjwa wa Korona uliingia nchini na Serikali ya wakati huo ilizuia kutolewa kwa takwimu za wagonjwa wa Korona.

Hivi sasa hali ni mbaya zaidi, Korona inaua watu wengi kuliko wakati mwingine wowote ule. Takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa kulikuwa na wastani wa vifo 132 kwa wiki vinavyosababishwa na Korona mwezi Aprili 2021.

Mwezi uliopita, Julai 2021, kumekuwa na wastani wa vifo 507 kwa wiki. Hili ni ongezeko la vifo vinavyosababishwa na Korona la takribani 300% ndani ya miezi mitatu tu.

Korona haijaharibu maisha tu, imeharibu uchumi wetu pia. Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia zilizotolewa wiki iliyopita, Kasi ya Ukuaji wa pato la taifa imeporomoka kutoka 7% mwaka 2019 mpaka 2% mwaka 2020. Kwa upande wa Zanzibar hali ni mbaya zaidi kwani kasi ya ukuaji wa pato la taifa iliporomoka mpaka 1.3% tu mwaka 2020.

Korona pia imeathiri biashara na ajira, 35% ya makampuni yamefungwa kati ya Janauri 2020 na Januari 2021, na 17% ya wafanyakazi katika sekta ya Utalii wamepoteza kazi zao kutokana na biashara ya utalii kuanguka.

Hata hivyo Serikali haijachukua hatua za maana kuwalinda watu na sekta zilizoathirika.
Ninaisihi Serikali kuwasilisha Bungeni mpango maalumu wa kunusuru sekta ambazo zimeumizwa na ugonjwa wa korona hususani sekta ya utalii.

Ninafarijika kwamba, baada ya Rais mpya kuingia madarakani kumekuwa na muelekeo mpya wa kisera wa namna ya kukabiliana na janga hili la UVIKO-19 nchini. Takwimu zimeanza kutoka japo sio kwa ukamilifu na baadhi ya hatua za kujikinga zimeanza kuchukuliwa, ingawa bado hatua hizo haziridhishi, lakini si haba. Napenda kuipongeza Serikali kwa maamuzi hayo muhimu.

Napongeza maamuzi sahihi ya Serikali ya kuruhusu chanjo ziingizwe nchini ili kuwapa kinga Watanzania na kuulinda mfumo wetu wa afya dhidi ya wagonjwa wengi ambao bila kinga hautaweza kuhimili.

Hata hivyo, bado kuna kazi kubwa zaidi ya kufanya kwenye uhamasishaji wa watu kujitokeza kupata chanjo. Nitoe rai kwa kila mmoja wenu, nikianza na wanachama wa ACT Wazalendo kufuata taratibu na kupata chanjo mapema iwezekanavyo.

Napenda kuwahakikishia kuwa nimejiridhisha chanjo zilizoruhusiwa kuingia nchini ni salama na mimi pia nimekwisha chanjwa na niko salama salimini. Nipende kuwaasa kuwa kuchanjwa ni swala la hiari lakini tunapoangalia usalama wa wapendwa wetu, jamii yetu na watanzania wenzetu basi hatuna budi kuhakikisha tunafanya maamuzi sahihi.

Niweke bayana kuwa ni lazima kuwepo na mkakati maalum wa uhamasishaji dhidi ya Korona ambao utaongozwa na watu wanaoaminika kwenye jamii, na sio watu wale wale ambao walituambia kuwa Tanzania imeishinda Korona, ama watu wale wale ambao walituaminisha kunywa malimau na tangawizi ni kutibu korona.

Hatuwezi kuwa na utekelezaji bora wa sera mpya za kupambana na Korona iwapo tutaendelea kuwa na sura zile zile zilizotuaminisha kutumia njia zisizoshauriwa kisayansi. Ni maoni yangu kuwa Waziri wa sasa wa Afya na Naibu wake na Waziri wa sasa wa Katiba na Sheria ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi (aliyebeba ndege ya Serikali kwenda Madagaska kutuletea kilichoitwa dawa ya kutibu Korona), wanapaswa kuwajibika au kuwajibishwa kwa kuwadanganya wananchi na kuleta maafa makubwa nchini.

Vile vile niendelee kusisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote ikiwemo kuepuka mikusanyiko, kuvaa barakoa na kunawa kwa maji tiririka na sabuni kila wakati pamoja na kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na maambukizi na pia kuzuia kusambaa kwa maambukizi.

Kwa upande wa Serikali zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, hatua madhubuti zichukuliwe kuongeza elimu kwa wananchi kwani kwa mwaka mzima walikuwa wanaambiwa hakuna Korona, hivyo kuwaambia kuwa sasa ipo sio jambo rahisi kueleweka. Jitihada zifanyike kwenye kutoa elimu sahihi kwa Umma.

3. UMOJA WA KITAIFA na UCHUMI

Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu,

Ndugu Watanzania wenzangu,

Miezi minne iliyopita tulipata Rais mpya, Rais Samia Suluhu Hassan. Mara baada ya kuapishwa kwake, kwa muktadha wa mambo mabaya tuliyopitia ndani ya miaka mitano na nusu iliyopita, ya kutekana, kupigana risasi hadharani, kufilisiana, kupotezana, kuuana, kubambikiana makosa kwa sababu za kisiasa, kubambikia kodi wafanyabiashara, kuchoma nyavu za wavuvi, kupora mazao ya wakulima n.k, ambayo kilele chake kilikuwa ni kuvurugwa uchaguzi mkuu wa 2020, wengi wetu tuliona ipo haja ya kurejesha mazungumzo ya Kitaifa pamoja na mchakato wa Katiba mpya, ili tuutumie kujadiliana kama Taifa juu ya athari za miaka mitano na nusu iliyopita, na kutafuta muafaka wa Kitaifa juu ya namna njema ya kuendelea kutoka hapa tulipo, lengo hasa likiwa ni kurejesha UMOJA wa Kitaifa ambao ulimomonyoka.

Serikali mpya imefanya mambo kadhaa tangu iingie madarakani, ambayo ni kinyume na yale mabaya yaliyomomonyoa umoja wa kitaifa ya miaka mitano na nusu iliyopita, ikiwemo kuruhusu uhuru wa habari, kuondoa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mabavu na vikosi kazi, kuzifuta kesi kadhaa walizobambikiwa watu, pamoja na kuwaachia huru wahusika nk.

Hatua hizi si haba, lakini kwa uharibifu uliofanyika si hatua za kutosha. Kwetu tuliopo kwenye siasa, jambo kubwa ambalo Serikali mpya ya Jamhuri ya Muungano haijalifanya vizuri ni uhuru wa kisiasa. Bado Sheria ya Vyama vya Siasa ni ile ile ya mwaka 2019, bado Sheria za uchaguzi ni zile zile zilizotumika kuharibu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni ile ile inayoendelea kuharibu chaguzi kwa kutumia Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri (maDED) wale wale ambao wengi ni Makada wa CCM.

Vile vile Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni ile ile iliyoharibu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Tunayo mifano ya Chaguzi ndogo za Majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma, na wa karibuni hapa wa Jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba n.k inayothibitisha kuwa mwenendo wa uendeshaji wa siasa za kiuchaguzi bado ni ule ule.

Rais aliahidi kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na kuhusu mchakato wa Katiba mpya, aliomba apewe muda ili “asimamishe uchumi”. Wakati tukisubiri ahadi hiyo ya wadau wa siasa kukutana na uongozi wa Serikali, bado uongozi wa chama chetu unaona ipo haja ya uwepo wa mchakato wa Katiba Mpya, maana ni mchakato huo ndio utakaotusaidia kwa kina katika hiyo kazi ya kujenga uchumi.

Tunatambua kwamba, Serikali ya awamu ya Sita imerithi Uchumi ulio kwenye hali tete. Taarifa ya Benki ya Dunia (Tanzania Economic Update) Na.16 ya Mwezi Julai 2021, imeonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ilikuwa 2% katika mwaka 2020 kutoka 7% mwaka 2019.

Hii ni kasi ndogo zaidi ukuaji wa uchumi kupata kutokea tangu mwaka 1994, karibu kipindi miaka 30 iliyopita. Ni dhahiri kuwa ipo kazi kubwa sana mbele yetu katika kurejesha uchumi wetu katika hali nzuri, lakini ni kazi ambayo haitafanyika vyema kama hatutatibu kwanza majeraha ya kisiasa ya miaka mitano na nusu iliyopita.

Sisi viongozi wa ACT Wazalendo hatuoni kama kunaweza kuwepo kwa mafanikio katika juhudi za ufufuaji uchumi bila kwanza kujenga umoja wa Kitaifa uliomomonyolewa kwa ubaguzi wa kisiasa uliofanyika katika miaka mitano na nusu iliyopita, ndio maana mazungumzo ya wadau wa siasa ni jambo muhimu mno, maana ndiyo yatakayoweka msingi wa kuwa na hatua za kuondoa mpasuko wa Kitaifa na kuleta UMOJA – nyenzo muhimu ya kujenga UCHUMI wa Kitaifa ni UMOJA.

Ni Rai yangu na Viongozi wenzangu kuwa tuwe na Majadiliano ya Kitaifa (Inter-Parties Dialogue) ili kwanza kuganga yaliyopita na kukubaliana namna ya kwenda mbele katika kujenga upya demokrasia yetu.

Ninamsihi Rais Samia kuweka mazungumzo haya kama kipaumbele kikubwa cha kuponya Taifa na kuleta Nchi pamoja.

MASHTAKA DHIDI YA MBOWE NA VIONGOZI WENGINE YAONDOLEWE

Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu,

Ndugu wananchi wenzangu,

Sisi Viongozi, Wanachama na Wafuasi wa Vyama vya Upinzani tuliishi kwa mateso sana ndani ya miaka mitano na nusu iliyopita, tukifilisiwa mali na kufungiwa Akaunti zetu (ndugu Freeman Aikaeli Mbowe akiwa ni kielelezo cha hili), tukipigwa risasi zaidi ya 30 na mpaka leo hakuna hata uchunguzi dhidi ya vitendo hivyo vya kinyangáu (ndugu Tundu Lissu ni Kielelezo cha hili), tukibambikiwa kesi na kuhukumiwa Mahakamani (mimi na mamia ya Viongozi wenzangu wa kisiasa ni kielelezo cha hili).

Kilele cha hili ni matukio mabaya na yenye uchungu mwingi ya Oktoba 28 – 30 mwaka 2020 hapa Zanzibar, wananchi wenzetu 20 waliuawa Unguja na Pemba na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, mamia ya wafuasi wetu walitekwa na kuwekwa kwenye kambi za majeshi na vikosi, mamia ya wanachama wetu wamepata ulemavu wa kudumu kwa vipigo (humu kwenye Kamati Kuu tunao kina Nur, Jussa na Mazrui). Unaweza kusema bila kupepesa maneno kuwa wapinzani walitendewa UGAIDI mkubwa mno na vyombo vya Dola.

Sasa vyombo vile vile vya Dola vilivyotufanyia UGAIDI huo mkubwa wa kutututeka, kutuua, kutubambikia kesi, kutufilisi, na kutupa ulemavu wa kudumu ndivyo vinavyomfungulia ndugu Mbowe mashtaka ya UGAIDI, kwenye mahakama zile zile ambazo zimetumika kwa miaka mitano na nusu iliyopita kutufungulia mashtaka ya aina hiyo hiyo yasiyo na dhamana, kwa nia ya kutubughudhi na kutupotezea muda.

Jambo hili la mashtaka dhidi ya ndugu Freeman Aikaeli Mbowe linaondoa uwezekano murua wa kuwa na majadiliano mema ya kisiasa nchini. Ni jambo linalokumbusha machungu makubwa sana, ni jambo linaloipasua zaidi, ni jambo linalochochea zaidi chuki, ni jambo ambalo tukiliacha na tusilipinge basi litaondoa kabisa fursa iliyopo mbele yetu ya “kuanza upya”, litazidisha chuki kubwa ya kisiasa iliyopo, na litavunja imani, matumaini na matarajio kiasi ambayo yaliwekwa kwa Serikali hii mpya.

Niikumbushe Serikali kuwa Mashtaka yasiyo na dhamana si mbinu mpya ya kudhibiti washindani wa kisiasa, ni mbinu ambayo imetumika ndani ya miaka hii 6 iliyopita na Serikali za CCM kuwaziba midomo wale wote ambao hawakukubaliana nao kisiasa, na ni mbinu ambayo iliishia tu kutesa watu, kuziumiza familia zao, kuligawa Taifa na kuchochea chuki kati yetu.

Wanaotumia mbinu hii sasa dhidi ya ndugu Mbowe dhamira yao ni hiyo hiyo – Kuligawa Taifa, kuchochea chuki, pamoja na kuondoa kabisa uwezekano wa kuwepo kwa mjadala wa Kitaifa.

Hawamkomoi Mbowe, wala hawatuvunji moyo wa kupambania Tanzania yenye usawa wa kisiasa na kuheshimu utofauti wetu wa mawazo.

Wanalichelewesha tu Taifa letu kupata Umoja na Maendeleo ya Kiuchumi. Wanataka turudi kule kule ambapo hatupaswi kurudi.

Wito wangu na Viongozi wenzangu kwa ndugu Rais, ni kuingilia kati na kumaliza jambo hili la kisiasa kwa njia za kisiasa. Tunao uzoefu wa namna baadhi ya watendaji wanavyotumiwa kisiasa kutumia kesi kama fimbo kwa viongozi wa kisiasa wa Upinzani.

Rais asikubali jambo hili, awazuie WASAIDIZI wake wanaotaka tuendelee kuishi KIGAIDI kama ilivyokuwa ndani ya miaka mitano na nusu iliyopita. Tunajua anao uwezo huo. Tunajua akitaka anaweza kulizuia jambo hili.

Tunajua yeye hataki tuendelee kuishi KIGAIDI. Ninaomba Rais Samia aingilie jambo hili na kuhakikisha ndugu Freeman Aikaeli Mbowe anaachiwa huru na mashtaka dhidi yake yanafutwa kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Ni nasaha zangu pia Viongozi na wanachama wengine wa Vyama vya Siasa na wanasiasa waliokamatwa kwa makosa yanayotokana na shughuli za kisiasa waachiwe huru ikiwemo wananchi wengine wanaosota mahabusu kwa miaka kadhaa kwa mashtaka ya kubambikiwa. Kwa mfano, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo wa Mkoa wa Tanga Ndugu Kidege aliyebambikiwa kesi ya ugaidi.

6. HITIMISHO: TWENDE KWENYE MEZA YA MAJADILIANO

Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo,

Ndugu Watanzania wenzangu,

Ninapoelekea kuhitimisha hotuba yangu, ningependa kutoa ushauri kwa Rais Samia na kumuomba atoe uongozi katika kipindi hiki ambacho Taifa linapita katika kipindi kigumu sana cha kiuchumi.

Katika kipindi hiki Taifa letu linatakiwa kuwa moja na sio kuwa vipandevipande. Hakuna sababu ya Taifa letu kugawanyika kwa sababu ya Katiba ambayo mchakato wake ulishaanza, na yeye Rais Samia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.

Ninapendekeza kuwa wadau wa siasa tukae na kukubaliana namna bora ya kufikia malengo ya kuwa na Katiba mpya. Kupitia mazungumzo ya vyama vya siasa (Inter-Parties Dialogue) hakuna kinachoshindikana. Ni lazima tuanze kujenga utamaduni wa kusikilizana na kukubaliana, au hata kukubaliana kutokubaliana, lakini ni lazima tukae kwanza. Haitakuwa na maana kuendelea kujenga nchi wakati Taifa linaporomoka.

Mwisho, nimwombe sana Rais Samia asikubali na asiingie kwenye mtego wa kuendeshwa na watu wanaotaka kuturudisha tulipotoka, watu wanaotaka turudi gizani. Aidha, ni vema hawa wanaotaka turudi gizani, (regressive forces), wampe nafasi Rais atupe uongozi na maono yake badala ya kuendelea kuishi ndoto zao za miaka ambayo haitarudi tena kwa uwezo wake Mola wetu.

Mungu Ibariki Zanzibar,

Mungu Ibariki Tanzania,

Mungu Ibariki Afrika,

Asanteni sana kunisikiliza.

 

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Jumapili Agosti 8, 2021
Zanzibar.

Reactions

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK