August 05, 2020 1:57 PM

Hotuba ya Kiongozi wa Chama Ndg. Zitto Kabwe kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa ACT Wazalendo

Hotuba ya Kiongozi wa Chama Ndg. Zitto Kabwe kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa ACT Wazalendo, Agosti 5, 2020 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Ndugu Wajumbe Mkutano Mkuu,

Ndugu Wananchi wa Tanzania,

Ninafuraha kubwa sana kuwa leo tupo tumejumuika hapa kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Chama chetu hichi chenye miaka 6 tokea kuanzishwa kwake. Ni chama kichanga kuliko vyama vyote vilivyopo Tanzania kwa umri wake. Taaswira ya Mkutano huu ni tofauti kabisa na umri wa chama chenyewe. Mkutano huu umejumuisha Wajumbe kutoka kila kona ya nchi yetu. Hongereni sana wana ACT kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kujenga Chama imara. Kwa taaswira hii sina mashaka baada ya October 2020, ACT kitakuwa ni chama kinachoongoza Serikali.

Ndugu Wananchi wa Tanzania,

Wiki chache zijazo tutaanza kuzunguka nchi yetu, kila Kijiji, kila Kata na kila Jimbo kuzungumza na Wananchi kuhusu maono yetu juu ya nchi yetu. Tutawapa Wananchi machaguo ya aina ya Watanzania wanayotaka kuishi katika miaka mitano inayokuja – Wananchi watakuwa na chaguo la wazi kati ya Tanzania wanayoishi sasa au Tanzania mbadala ambayo sisi ACT Wazalendo tunataka kushirikiana nao kuijenga. Sisi tunakwenda kuwashirikisha Watanzania, wabara na wa Zanzibar, aina ya Taifa tunalotamani kuwa nalo - Tanzania yenye watu wenye hali bora kijamii na furaha ya kweli, yenye kujali utu, yenye mfumo mzuri wa utoaji haki, yenye demokrasia ya kweli, yenye uhuru na yenye uchumi jumuishi, imara na unaostawi”

Katika Miezi 2 ya kuzunguka huko tutakuwa tunakamilisha zoezi muhimu la kikatiba la kila miaka 5 Watanzania kupata fursa adhimu ya kuchagua viongozi wao. Uchaguzi wa mwak huu ni uchaguzi muhimu sana katika maisha ya Taifa letu. Kiongozi Mkuu wa Taifa tunayekwenda kumchagua na Wawakilishi wetu katika Baraza la Kutunga sharia na mabaraza ya madiwani ndiye atakayetuongoza kuingiza nchi katika muongo wa sita tangu Tanganyika ipate uhuru na tangu Jamhuri ya Muungano iundwe. Vile vile tunakwenda kuchagua Kiongozi ambaye ataiongoza Zanzibar kuingia muongo wa sita tangu Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa uzoefu wa miaka mitano iliyopita Watanzania wanakwenda kufanya maamuzi muhimu sana.

Uchaguzi wa mwaka 2020 ni uchaguzi wa kuchagua

- Uhuru wa kweli kwa kila mtu dhidi ya ukandamizwaji,
- Matumaini dhidi ya hofu,
- Amani na usalama kwa kila mtanzania dhidi ya tafrani na misukosuko
- Siasa safi dhidi ya siasa za chuki na za kizandiki
- Utaifa na mahusiano yenye tija kimataifa dhidi ya mgawanyiko na kujitenga
- Maendeleo Jumuishi ya watu dhidi ya maendeleo ya vitu,
- Utajiri wa watu dhidi ya utajiri wa serikali,
Muhimu zaidi ni uchaguzi wa kuchagua kurudisha utu na heshima kwa kila mtanzania hasa wanawake na watoto dhidi ya kejeli, manyanyaso ya makundi fulani ya jamii yetu. Ni uchaguzi wa Watu dhidi ya Uchaguzi wa Vitu

Mkutano Mkuu huu wa chama chetu leo utafanya maamuzi muhimu ya ajenda hizi za uchaguzi wa mwaka huu na watu watakaobeba ajenda hizi. Ni matumaini yangu kuwa mtawapa Watanzania wagombea ambao kwa kuwatazama tu watarejesha nyuso za furaha na matumaini ambayo yamepotezwa katika miaka mitano iliyopita.

ACT wazalendo imedhamiria na kujiandaa kikamilifu kujenga na kuongoza Tanzania ya Watanzania. Tanzania ambayo kila mtanzania, mtoto, kijana, mwanamke, mwanamume, mzee, wa kijijini na mjini ana haki sawa mbele ya sheria na ana fursa stahiki za kujenga na kuzifikia ndoto zake. Tanzania ambayo, watanzania wanajivunia kuwa watanzania na sio Tanzania hii ya sasa ambayo mamilioni ya watanzania wanavumilia kuwa watanzania.

Chama cha ACT Wazelendo kinaamini kwa yakini, miongo inayokaribia sita tangu tupate uhuru wetu kutoka kwa mkoloni, watanzania na Wazanzibari, hawapaswi na hawastahili kuishi kwa hofu na kufifishwa ndoto zao, bali wanapaswa kuwa wenye raha na furaha, na matumaini yakufia na kuishi mafanikio yao binafsi na kuwa sehemu ya mafanikio ya taifa kwa ujumla.

ACT wazalendo inataka kuunda Serikali ambayo itahakikisha upatikani na ulinzi wa haki na ustawi wa wanawake ambao ndiyo ni walezi wa taifa hili, watu wenye ulemavu, watoto hasa walioko kwenye mazingira magumu, jamii na makundi yaliyopo pembezoni. Tafiti za kisayansi zimeonyesha na kuthibitisha kuwa kuwezesha na kuwekeza kwa wanawake na makundi mengine maalumu, kuna tija endelevu kiuchumi na kijamii. Muhimu zaidi, kunaleta umoja na usawa katika jamii.

Tunataka Serikali ambayo sio tu itatokomeza ubaguzi ila pia itafanya jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa kila mtanzania, bila kujali jinsia, dini, maumbile, itikadi, umri, kabila, anashiriki kikamilifu katika kuongoza taifa hili katika nyanja mbalimbali na anaishi maisha yenye mafanikio, maisha ya raha na furaha. Kauli mbiu yetu ya #KaziNaBata ni dhana jumuishi, kwa sababu kila Mtanzania, ana haki ya kufurahia utanzania wake, na maisha yake. Tunataka Watanzania wafanye Kazi kwa bidii na pia wafaidi matunda ya jasho lao. Wawe na Raha na Furaha. #KaziNaBata.

Kwenye Taifa lenye zaidi ya 80% ya watu wake wakiwa na umri chini ya miaka 35, ni dhamira yetu, kuwekeza na kutengeza sera, sheria na taratibu zitakazohakikisha kuwa vijana wa taifa hili wanakuwa kipaumbele na chachu ya maendeleo, kwao wao na kwa taifa. Tunataka Serikali zitakazoongozwa na ACT Wazalendo, zikatae kuona vijana wa Nchi zetu mbili wananyang’anywa fursa, wanakatishwa ndoto zao, wanakandamizwa na kufanywa watwana ndani ya taifa lao.

Tunataka kuona Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo, kuwa serikali ya vijana kwa ajili ya vijana wa Tanzania wa kike na wa kiume. Lakini pia kuandaa maisha stahiki uzeeni kwa kuwa na Mfumo Madhubuti wa Hifadhi ya Jamii kwa wote ambayo itahakikisha kuwa kila Mtanzania na kila Mzanzibari anakuwa na Bima ya Afya na Pensheni akifika umri wa kutoweza kufanya kazi.

Tunataka kuhakikisha kuwa huduma za jamii bora, zenye ufanisi zinatolewa kwa wakati stahiki hazitakuwa na upendeleo kwa viongozi au watu wachache, bali zitakuwa kwa kila Mtu.Tunataka tuwe na Elimu bora yenye kukidhi vigezo vya soko la ajira na kuwaanda wahitimu kuvumbua na kujiajiri. Hatutaki kuona vijana wamalizapo vyuo vikuu au vyuo vya ufundi kuwa na mzigo wa madeni ndio maana Serikali itachukua mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa Elimu ya Juu mpaka sasa ili kuondoa mzigo kwa vijana kuhudumia madeni hayo na kuanza upya mfumo wa kugharamia Elimu kwa kutoa ufadhili wa gharama za masomo ‘tuition fee’ bure kwa Watu wote watakaodahiliwa kwenye vyuo vya Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi Mchundo. Vijana wote watakaojiunga na Elimu ya Ufundi ya VETA watasoma bila malipo ili kuondoa kikwazo cha vijana kupata Stadi na ujuzi kuendesha maisha yao. Vijana wanaonisikiliza leo wana chaguo la wazi kabisa – kuchagua chama na mgombea wa chama ambacho kitaendelea kuwaweka katika mnyororo wa madeni au kuchagua chama na mgombea wa chama ambaye atawaondoa katika utumwa wa madeni ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani.

Tunataka Serikali ambayo itahakikisha Huduma bora za afya kwa watu wote na sio Serikali inayotamba kwa kujenga majengo. Chaguo kwa Wanawake waja wazito lipo wazi katika uchaguzi wa mwaka huu – kati ya chama na mgombea wa chama ambacho kitaendelea kulipisha huduma za afya na kugeuza afya kuwa bidhaa kama nyanya sokoni kuchagua chama na mgombea wa chama ambaye atahakikisha kila Mtanzania ana Bima ya Afya na ana hifadhi ya Jamii ambayo ina mafao yatakayomwezesha asiwe na mashaka kabisa apatapo majanga. Ni uchaguzi ulio wazi kabisa.

Tunataka Serikali ambayo itahakikisha upatikaji wa maji safi na salama kwa kila mtu. Watu wenye kipato kidogo hapa nchini wana chaguo la wazi kabisa katika uchaguzi wa mwaka huu – kati ya chama na mgombea wa chama ambacho kitaendelea kuwafanya masikini walipie maji kwa gharama kubwba zaidi kuliko watu wenye kipato kikubwa na mgombea wa chama ambaye atahakikisha kuwa ndani ya miaka mitano watu wote wanapata maji na salama kwa kutekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa miradi ya Maji yote nchini kwa pamoja kwa kutumia maarifa ya fedha za maendeleo.

Ndugu wajumbe,

Kwa Wananchi wa Zanzibar wana hiari ya kuamua kati ya chama na mgombea ambaye ataendelea kuifanya Zanzibar kuwa duni kimaendeleo kwa kukandamizwa na upande mmoja wa Muungano kwa sababu tu Mkuu wa Serikali ya Muungano hataki kutoa shikamoo; na chama na mgombea ambaye atahakikisha kuwa kwanza Zanzibar inatumia kikamilifu mamlaka yake yaliyo kwenye Katiba ya sasa ya Muungano na Katiba ya Zanzibar na pili atakaye hakikisha kuwa Muungano unaimarishwa kwa kufanya mabadiliko makubwa ya mundo wa Muungano ili kuwa na Muungano wa Haki, Usawa na wenye kuheshimiana.

Ndugu Wajumbe, Ndugu Watanzania,

Uchaguzi wa Mwaka huu unahusu pia uchumi wenu. Unahusu maisha yenu ya kila siku. Hatma ya maisha ya kila Mtanzania ipo mikononi mwake sasa na ataamua tarehe 28 Oktoba 2020.

Ninataka kuwahakikishia kuwa Uchumi wa taifa litakaloongozwa na serikali ya ACT Wazalendo utakuwa Uchumi Jumuishi;

- UCHUMI WA WATU SIO VITU.
- Uchumi wa Wananchi walio wengi na si uchumi wa Serikali na kundi la wachache.
Tunataka Serikali itakayowekeza kwenye sekta zinazoajiri watanzania wengi, hasa Kilimo, Ufugaji na uvuvi, ili kuleta kilimo cha kimapinduzi ambacho kitawaondoa Wakulima, Wavuvi na Wafugaji kutoka katika dimbwi la umasikini. Wakulima, Wavuvi na Wafugaji wa Tanzania wana uchaguzi ulio wazi kabisa – kuchagua chama na mgombea ambaye kwa miaka mitano amewadharau, kuwapora fedha zao na kuwafukarisha kwa kuchoma nyavu zao au kuwaondoa kwenye maeneo ya malisho AU kuchagua chama na mgombea ambaye anatambua umuhimu wa kilimo na atawekeza kwenye kilimo na kujenga ushirika wa kisasa wa wakulima, wavuvi na wafugaji ili kulinda haki zao na kuboresha maisha yao kutokana na shughuli zao.

Tunataka Serikali ambayo itaboresha na kuwezesha ustawi wa sekta isiyo rasmi hasa ya biashara ndogo ndogo ambazo nyingi zinafanywa na wanawake na vijana. Mifumo ya kodi na urasimishaji biashara vitalenga katika kuleta ufanisi na kukuza biashara na si kudumaza na kuleta ukiritimba. Tafiti, sayansi na tekinolojia vitakuwa chachu katika kutengeneza fursa na kukuza uchumi jumuishi. Serikali yetu itahakikisha wataalamu wa fani mbalimbali wanawekewa mazingira sawia ili walisaidie Taifa katika kukuza uchumi ambao unaboresha maisha ya mtu mmoja mmoja.

Ndugu Wajumbe na ndugu Watanzania,

Tunataka Serikali ambayo inatambua mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi yetu. Wafanyabiashara nchini wana chaguo la wazi kabisa mwaka huu. Kwa Wafanya biashara huu ni uchaguzi kati ya;

- Chama na mgombea wa chama ambaye anaweza kuamka asubuhi na kutegemea na alivyoamka na kuvunja mikataba ya kisheria dhidi ya Chama na mgombea wa chama ambaye ataheshimu mikataba na malipo na migogoro kutumia njia halali kutatua migogoro hiyo
- Chama na mgombea wa chama ambaye anakusanya kodi kwa mitutu ya bunduki dhidi ya chama na mgombea wa chama ambaye ataheshimu sheria na kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria bila kupoka uwezo wa makampuni kuzalisha mapato zaidi.
- Chama na mgombea wa chama ambaye akiamka asubuhi na kutegema na alivyoamka anaweza kuingia kwenye akaunti ya benki ya mfanyabiashara na kuchukua fedha zake dhidi ya chama na mgombea wa chama ambaye ataheshimu haki za watu kumiliki mali.

Ndugu Wajumbe na ndugu Watanzania,

Tunataka Serikali ambayo itajikita katika kufufua na kuimarisha uhusiano wetu na mataifa mengine na haswa nchi jirani. Tumedhamiria kurudisha heshima ya Tanzania kwenye medani ya kimataifa. Nikiwa Kiongozi wa chama hiki napenda kuwahakikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa chama chetu na Wagombea wote wawili watakaopitishwa na chama chetu watajitahidi kwa nguvu zao zote kuimarisha utangamano wa eneo letu la kikanda. Hapatakuwa na siasa za tit for tat, kuchoma vifaranga wala kurushiana maneno. Ninukuu maneno ya Rais John F Keneddy ya mwaka 1961 akihutubia Bunge la Kanada;

“Geography has made us neighbors. History has made us friends. Economics has made us partners, and necessity has made us allies. Those whom God has so joined together, let no man put asunder”.

ACT Wazalendo itaenzi juhudi za viongozi waliotangulia kuimarisha Afrika Mashariki moja, imara na inayoheshimiana. Watanzania wataamua hivyo mwaka huu.

Ndugu wajumbe na Watanzania,

Serikali yetu ya #KaziNaBata haitaweza kufikiwa kama wasanii na wanamichezo wataendelea kunyonywa na kufanya kazi katika mazingira magumu. Kwa kushirikiana na wasanii na wanamichezo mbalimbali, serikali yetu itawekeza kwa kiwango kikubwa kuhakikisha vipaji na vipawa vya watanzania vinakuwa vyenye tija kwao, burudani kwetu na tunu ya taifa katika majukwaa ya kimataifa. Sanaa na Michezo itakuwa ni moja ya vipaumbele vya Sera yetu ya mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa ili kujenga taswira chanya ya Nchi yetu na kuongeza Mapato ya Fedha za Kigeni. Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar zitahakikisha kuwa michezo na burudani inaimarika.

Ndugu Wajumbe,

Chama chetu cha ACT Wazalendo kimeongoza juhudi za kuona tunakuwa na mashirikiano na vyama makini katika uchaguzi huu. Mwenyekiti wetu amefanya kazi kubwa sana ya kuwasilisana na baadhi ya viongozi wa vyama kufanikisha hili. Kwetu sisi ushirikiano na vyama vyengine vya siasa vilivyo makini ni jambo muhimu sana katika kukabiliana na CCM. Tunaamini kupitia ushirikiano na vyama vyengine, kazi ya kuiondoa CCM Madarakani inakuwa rahisi mno kuliko kila chama kupigana kivyake.

Nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania kuwa ACT tumefanya na tutaenelea kufanya kila lilo ndani ya uwezo wetu kuona tunapata mashirikiano na vyama vyengine vya siasa. Tunafahamu suala la ushirikiano ni hitajio la watanzania walio wengi wanaotaka mabadiliko. Niwahakikishie Watanzania wanaonisikiliza muda huu kuwa chama ninachokiongoza mimi chini ya uwenyekiti wa Maalim Seif ambaye sote sisi wana mageuzi wa zama hizi tunachukua busara zake hakiwezi kuwa Mchawi wa ushirikiano, Niwaambie mpaka muda huu ninapozungumza bado mashauriano yanaendelea na kwenye Mkutano huu pia Wajumbe mtapokea tarifa ya mashauriano haya ili nanyi mtupe muongozo wenu.

Ndugu Wajumbe,

Leo mtapokea pia tarifa ya maandalizi ya Ilani ya uchaguzi itakayowezesha yote niliyoyataja hapo juu. Niwaambie kuwa Wajumbe wa Kamati Kuu na Halimashauri Kuu wamefanya kazi kubwa ya kutupatia ilani bora ili wagombea wetu waweze kuwa na ajenda mahususi ya kutuwezesha kushinda uchaguzi mwaka huu.

Ilani hizi ni dhamira ya chama katika kuifikia na kuijenga Tanzania ya watanzania na Zanzibar ya Wazanzibari, zaidi ni mkataba kati cha chama na watanzania na chama na Wazanzibari. Sisi, ACT Wazalendo tunaamini na tunawataka watanzania waamini pamoja nasi kuwa, INAWEZEKANA

✓ Kufanya kazi na kula Bata
✓ Kuishi Maisha ya Raha na Furaha
✓ Kuondoa Serikali dhalimu madarakani
✓ Kuwa na Serikali inayoheshimu sheria, utu, uhuru na ustawi wa watu wake
✓ Kujenga Uchumi jumuishi na endelevu
✓ Kila mtanzania kufikia ndoto zake
✓ Kuwa na umoja wa kitaifa na heshima kimataifa
Nawashukuru sana

Zitto Zuberi Kabwe

Kiongozi wa Chama

Agosti 2020

Showing 1 reaction

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK