- HOTUBA YA KIONGOZI WA CHAMA, NDUGU ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA HAFLA YA UZINDUZI WA OFISI MPYA ZA MAKAO MAKUU YA CHAMA, MAGOMENI DAR ES SALAAM, TAREHE 30 OKTOBA, 2022.
Salaam kwa Viongozi mbali mbali
Salaam kwa Waalikwa
Salaam kwa Wanachama na Wananchi kwa ujumla.
Ndugu Wananchi na Wageni wetu waalikwa.
Awali ya yote ninapendenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kutuwezesha leo kukushanyika tukiwa na furaha kubwa katika shughuli yetu hii adhimu ya ufunguzi wa Ofisi zetu hapa magomeni kwa salama na amani.
Aidha nichukue nafasi hii kuwashukuru nyote mliohudhuria katika shughuli hii. Wageni wetu kutoka Zambia na Zimbabwe, Wageni kutoka Vyama mbali mbali vya siasa hapa nchini, Wawakilishi wa taasisi na mashirika mbalimbali, wanachama na wananchi kwa ujumla. Nyote leo mmeamua kuacha shughuli zenu na kuja kuungana na WanaACT . Tunawashukuru sana sana.
Vile vile niwashukuru Kamati ya Maandalizi kwa kuandaa shughuli hii kwa mafanikio makubwa.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Leo hii, mimi mwenyewe binafsi na viongozi wezangu wa ACT bila shaka na Wanachama pamoja na wapenzi wa ACT popote walipo duniani tuna furaha kubwa sana, furaha isiyo na kifani kuona leo hii tunafungua ofisi yetu wenyewe hapa Magomeni, Dar es Salaam. Tumekuwa na Ofisi kwa muda wa kipindi chote cha uhai wa Chama chetu hapo Kijitonyama lakini kwa hakika haikuwa na hadhi ya Ofisi ya Chama cha siasa chenye ndoto ya kushika dola na kuongoza Serikali, muda wote tulikuwa na ndoto kuwa ifike siku moja ACT iwe na ofisi yake yenyewe, na sio Ofisi tu bali iwe ni Ofisi ya kisasa kwa haiba yake lakini pia kwa samani na vifaa mbalimbali kwa matumizi ya ofisi. Ndoto hii leo tumeitimiza mbele yenu mkiwa ni mashahidi.
Tuna furaha sio kwa sababu tumepata Jengo tu bali kwa sababu Ofisi yenyewe inawakilisha taswira ya chama chetu – Chama cha Vijana, cha kisasa, wabunifu na wachapa kazi. Chama cha watu wenye maarifa na wenye uwezo mkubwa wa kustahmili misukosuko (resilient). Muhimu Zaidi chama Kiongozi kinachotazama mbele (forward ever, backward never).
Ofisi yetu hii sio tu ni jengo, kuna majengo mengi mazuri nchini, bali ni alama ya sisi ni nani na tuna dhamira gani. Ni alama ya uwezo wa wanachama wetu kujikusanya wenyewe na kuamua kufanya jambo ambalo katika hali ya kawaida hudhani haliwezekani. Ni alama ya uwezo wa viongozi wetu kuwafikia watu wa makundi mbalimbali na kuwashawishi waamini katika ndoto yetu.
Jengo hili tunalofungua leo ni kielelezo cha kuonyesha ukubwa wa ndoto zetu. Kama hatuwezi kujenga Ofisi yetu wenyewe, tutaweza kujenga miundombinu mikubwa ya umwagiliaji? Tutaweza kujenga mashule ya watoto wetu kusoma na Vituo vya Afya vya kina mama zetu kujifungua kwa stara? Tutaweza kupambana na janga la umasikini wa watu wetu na kutengeneza uchumi unaozalisha ajira kwa vijana wetu?
Ofisi hii ni ishara ya ndoto zetu. Tutaijenga Tanzania na Zanzibar kwa ukubwa huu wa ndoto zetu. Ndoto kubwa ndio siri iliyojificha kwenye ujenzi huu wa Ofisi yetu ambayo leo tunaifungua rasmi.
Sisi ACT Wazalendo tunaamini kuwa shabaha kuu ya chama chochote cha siasa inapaswa kuwa ni kuunda sera zitakazowezesha kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi. Kutatua shida za Watanzania kunahitaji viongozi wenye muda wa kutulia na kufikiria, kuna hitaji viongozi wenye ofisi zinazoruhusu tafakari. Wanawachama wa ACT wametuwekea sisi viongozi mazingira hayo ya kufanya kazi na kutafakari vizuri ili kuimarisha chama chetu na kubuni sera mbadala za kuliongoza Taifa letu.
Kwa mnasaba huu basi, sina budi kutoa shukrani zangu za dhati kwa Viongozi wezangu ndani ya ACT kwa kuwa na dira ya pamoja katika ujenzi wa chama chetu. Aidha Wanachama wetu na wapenzi pamoja na wahisani wetu wa ndani na nje ya nchi ambao tumekuwa tukishakana mikono kwa hali na mali kukiendesha chama chetu. Kupitia kwenu ndani ya kipindi cha miaka 2 tumefanikisha kufanya Mikutano Mikuu 3 kwa gharama zenu. Na leo hii tunazindua Jengo letu linalotokana na michango yenu. Tunawashukuru sana.
Nisiwe mwizi wa fadhila kama sitowashukuru pia mafundi kuanzia Mhandisi mwenyewe, mafundi na vibarua ambao wamejitolea kwa nguvu zao zote kukamilisha ujenzi wa ofisi hii. Najua hasa wiki 3 hizi za mwisho kazi haikusita hata saa moja si usiku si mchana muda wote watu wamekuwa kazini. Ahsanteni sana.
Ndugu Wananchi na Wageni wetu Waalikwa,
Jengo hili ni sehemu ya mipango mingi tuliyonayo katika ujenzi wa chama chetu. Tunakusudia kufanya mabadiliko makubwa katika kila eneo. Kuanzia Ofisi zetu za Chama, Uongozi na Sera zetu.
Tulianza mapema mwaka huu kwa kuzindua mfumo wa kuandikisha wanachama wetu kidigitali tuliouita ACT Kiganjani. Hivi sasa maelfu ya wanachama wetu wanajisajili katika mfumo huo na tunaendelea na kampeni maalumu za kuhakikisha kuwa kila mwanachama wetu anasajiliwa katika mfumo wa ACT Kiganjani.
Vile vile mwanzoni mwa mwaka huu tulizindua Baraza Kivuli la Mawaziri kama Idara Maalumu ya Chama ya Wasemaji wa Kisekta. Mawaziri wetu, na hapa niseme kwa ufakhari kabisa, asilimia 52% ni wanawake na 45% vijana chini ya umri wa miaka 35 wakiongozwa na Waziri Mkuu Kivuli Bi Dorothy Semu, wanafanya kazi nzuri sana.
Hivi sasa kila siku unaisikia ACT Wazalendo ikipaza sauti kuibua masuala ya wananchi. Hili ndio jukumu la chama cha Siasa – muda wote kuiwajibisha Serikali kwa masuala ya wananchi na kupendekeza majawabu. Sisi tulikataa kuwa chama cha kulalamika tu. Tulikataa kushikwa mateka na madhila ya mwaka 2020. Tumeamua kuhakikisha yaliyotokea 2020 hayatokei tena kwa kupigania mageuzi ya kisheria na kikatiba na sio kwa kuwa walalamikaji.
Katika mwendelezo wa kukijenga chama chetu kimkakati tumefanya mapitio ya sera zetu na mapema mwakani tutazizindua rasmi. Tangu mwezi Aprili tumekuwa tukifanya kazi kubwa ya Ujenzi wa Chama chetu chini na kazi hiyo tunaendelea nayo. Tumedhamiria kufikia malengo yetu ya kuwa chama kinachoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar na kujenga TAIFA LA WOTE kwa MASLAHI YA WATANZANIA WOTE. Yote haya ni katika mageuzi tuliyoamua kuyafanya.
Tunayafanya haya kwa sababu ACT ni chama kinachoamini kuwa nchi yetu inahitaji mageuzi ya kweli kweli ambayo yatawanufanisha watanzania wote. Sisi tunaamini ACT ni chama kinachoweza kutimiza matarajio hayo ya wananchi.
Hivyo niwaambie basi katika mpango wetu huu mara baada ya kumalizika kwa ujenzi huu sasa nguvu zetu zinaelekea kujenga ofisi ya kisasa kule Zanzibar. Baada ya hapo tunahamia kwenye ujenzi wa Ofisi zetu za Mikioa na baadaye ofisi za Majimbo. Na hatutoishia kwenye majengo tu, ni ofisi za kisiasa pamoja na vifaa vyake ikiwa na pamoja na vitendea kazi na usafiri kwa watendaji wetu. Muhimu ni kuwa tunataka viongozi wanaowajibika kujenga chama, mageuzi haya hayatomuacha pia kiongozi goigoi. Kwa hiyo wito wangu viongozi na wanachama tuongoze juhudi za ujenzi wa chama.
Ndugu Wanachama na Wageni wetu waalikwa,
Nichukue nafasi hii kuwaeleza Watanzania kuwa tumedhamiria kujenga chama cha siasa cha kisasa, kinachoshughulika na masuala yao, kinachowajibika kwao na kinachoongoza harakati za mageuzi hapa nchini.
Tunajenga chama cha siasa kinachofanya siasa. Kwa wale Watanzania walio kwenye vyama mbalimbali na wanaona kuwa hawapati nafasi ya kufanya haswa kazi ya siasa wanayokusudia, jukwaa la kufanya Siasa lipo ACT Wazalendo.
Hii ni nchi ya kidemokrasia inayotoa uhuru kwa kila mtu kujiunga na chama cha Siasa kinachoweza kufanikisha malengo yake. Ewe Mwanasiasa ambaye unataka kufanya siasa lakini chama chako hakikupi nafasi ya kufanya hivyo, njoo ACT Wazalendo tufanye siasa.
Asanteni sana.
Zitto Kabwe
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
30 Oktoba, 2022
Magomeni, Dar es Salaam.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter