HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA FEDHA NA UCHUMI- ACT WAZALENDO NDG. EMMANUEL LAZARUS MVULA KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA FEDHA NA UCHUMI- ACT WAZALENDO NDG. EMMANUEL LAZARUS MVULA KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.
Utangulizi
Jana tarehe 07 Juni, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilihitimisha kujadili hotuba za bajeti za kisekta kwa kupokea na kujadili bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu L. Nchemba Madelu (Mb.) ambapo ilijadiliwa kwa siku moja pekee. Wizara ya Fedha na Mipango ndio yenye majukumu ya kusimamia manunuzi ya mashiriki, serikali na usimamizi wa sera za fedhkwa ujumla wake. Aidha, wizara hii ndio inayoshughulikia usimamizi wa masuala ya fedha ya Muungano, suala la deni la taifa, uendeshaji wa mashirika ya umma na vitega uchumi wa serikali, ulipaji wa mafao kwa watumishi wa umma wasio wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Pia, wizara inasimamia na kudhibiti mali za umma. Hivyobasi, bajeti ya wizara ya fedha na mipango inahusisha mafungu nane (8); Deni la taifa (Fungu.22), Ofisi ya Msajili Hazina (Fungu Na.7), Tume ya pamoja ya fedhaa (Fungu Na.10), Kitengo cha kudhibiti fedha haramu (Fungu Na.13), Hazina (21), Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali (23), Wizara ya fedha na Mipango (50) na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu (45). Ambapo Bunge limepitisha jumla shilingi Trilioni 14.9 kwa ajili ya mafungu haya yote. Kati ya hizo, Shilingi trilioni 13.6 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi trilioni 1.3. kwa ajili ya maendeleo.
Kutokana na umuhimu huu, Sisi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi tumeisoma, kuichambua na kuimulika ili kutoa mapendekezo kuhusu maeneo ya vipaumbele ambayo tunaona yanafaa kuwa sehemu ya mipango na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka huu wa fedha. Katika kufanya hivyo, hotuba hii ya Msemaji wa Sekta ya Fedha na Mipango wa ACT Wazalendo Ndg. Emmanuel Lazarus Mvula imebaba hoja sita (6) kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2022/23.
1. Serikali inaikalia Akaunti ya pamoja ya fedha za Muungano, kuinyonya Zanzibar.
Nchi yetu ni Muungano wa Nchi mbili, Zanzibar na Tanganyika, zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeelekeza kuundwe Chombo cha kusimamia Mapato yote ya Muungano ili yatumike kuendesha shughuli za Muungano zinazotajwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwa mujibu wa Ibara ya 133 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani na Sheria Na. 15 ya mwaka 1984 ilianzisha Akaunti ya fedha ya pamoja ambayo itakuwa ni sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.
Aidha, Ibara ya 134(1) ya Katiba hiyo imeanzisha Tume ya Pamoja ya Fedha na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria namba 14 ya mwaka 1996 ambayo inatekeleza kifungu hicho cha Katiba. Tume ilianzishwa mwaka 2003. Hata hivyo kanuni za kutekeleza sheria hiyo zilichelewa sana kutungwa.
Kwa miaka zaida ya 36 tangu kutungwa kwa sheria ya kuanzisha kwa akaunti ya pamoja ya fedha za Muungano, akaunti hii bado haijaanza kufanya kazi na fedha zinazotokana na makusanjo ya Jamhuri yameendelea kutumika bila kujali haki, usawa wa pande mbili za Muungano. Majibu ya serikali ya mara zote ni kuwa majadiliano baina ya pande mbili kuhusu mapendekezo ya Tume bado hayajakamilika. Inasikitisha kuona Mwenendo huu wa zaidi ya miaka 22 tangu ilipoundwa. Na kila mwaka TUME inatengewa fedha pamoja na mambo mengine ni kushauri Lakini serikali hazichukua hatua ya utekelezaji.
Kwa mujibu wa utafiti uliokasimiwa na serikali unaonyesha Zanzibar hutumia 2% tu ya Mapato ya Muungano (Mapato ya Muungano yanayokusanywa Zanzibar) na Tanganyika hutumia 98% ya Mapato ya Muungano (yanayokusanywa Tanzania Bara). Utafiti huo ulitumia Bajeti za Serikali za kuanzia mwaka 1999 – 2004.
Kanuni ya kugawa fedha inaweza kuwa ama 4.5% ama 11%. Mgawo wa 11% wa Mapato ya Muungano ni kigezo cha hisa za Zanzibar wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaanzishwa mwaka 1965 kutoka East African Currency Board. Mgawo wa 4.5% unatokana na ushauri wa IMF na kupitishwa na Serikali ya Waziri Mkuu John Samwel Malecela mwaka 1994. Mgawo huu hutumika hivi sasa kugawa Misaada kutoka nje. Kwa kutumia mgawo wa 4.5%, Wastani wa Fedha zinazopaswa kuwa mgawo halali wa Zanzibar kwa miaka 9 iliyopita ni shilingi Bilioni 660 kwa mwaka tangu 2013/14 – 2021/2022. Kwa kutumia mgawo huu wa 4.5% Zanzibar inaidai Serikali ya Jamhuri ya Muungano Jumla ya Shilingi trilioni 5.94 kama mgawo wake wa Mapato ya Muungano yanayozidi Matumizi ya shughuli za Muungano. Lakini hadi sasa, Zanzibar haipati mgawo na wala hakuna akaunti ya pamoja.
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kufanya tathmini mpya ya mgawo na kulipa madeni yote inayodaiwa na Zanzibar. Aidha, tunaitaka serikali kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha ikiwemo kuanzishwa na kufanya kazi ipasavyo na haraka Akaunti ya pamoja ya Fedha.
2. Mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha
Wizara ya fedha na mipango Ndio yenye wajibu wa kusimamia sera ya fedha kwa ujumla wake. Mwenendo wa bei za bidhaa kwa mwaka wa fedha 2021/22 umekuwa wenye kuongezeka mwezi hadi mwezi, na hali kuwa mbaya zaida katika robo tatu ya mwisho yaani kuanzia mwezi Januari hadi sasa (Juni).
Pamoja na takwimu za jumla za mfumo wa bei zikionyesha mfumuko wa bei za bidhaa kuongezeka kwa takribani asilimia 0.6 kutoka alimia 3.3 mwaka 2020/21 hadi asilimia 3.9 kwa mwaka 2021/22. Lakini katika bei za bidhaa tumeshudia mwenendo wa bei ya mafuta ya kula, mchele na ngano upandaji wake umefikia hadi asilimia 156 ikilinganishwa na mwaka. Hivyo, Mwenendo wa bei umekuwa na athari kubwa katika kupaisha mfumuko wa bei na hivyo kufanya wananchi walio wengi kutomudu gharama za maisha. Aidha, tumeshuhudia kupanda kwa bidhaa zisizo za chakula kama vile vifaa vya ujenzi (mabati na saruji), pembejeo za kilimo (Mbolea) nazo upandaji wake umepaa kwa wastani wa asilimia 90 hadi 150 kwa mbolea za UREA, CAN, DAP, SA na NPK. Pia, bidhaa za matumizi ya nyumbani kama vile sabuni.
Vilevile, kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol, Diseli na mafuta ya taa kwa zaidi ya asilimia 100, imechochea zaidi maumivu kwa wananchi. Mwenendo wa bei ya mafuta ya petroili, Diseli na mafuta ya taa, umekuwa ukiongezeka kila mwezi tangu tarehe 01 Julai, 2021. Kwa kipindi chote serikali haikuwa inachukua hatua madhubuti za kuleta unafuu au kushusha bei hizo ili kuzuia kutokea kwa mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha. Mathalani, bei za rejareja za mafuta ya Petroli, Diseli na Mafuta ya Taa kwa mwezi julai, 2021 ilikuwa shilingi 2,249 kwa kila lita ya petroli, Diseli ilikuwa shilingi 2073 na mafuta ya taa ilikuwa Shs, 1,957. Kupanda kwa bei hizi za mwezi julai kutokea mwezi Juni, 2021 kwa sehemu kubwa zilichangiwa na sera za kikodi na sheria ya fedha ya mwaka 2021/22
Pamoja na kuwepo na mabadiliko mbalimbali ya kidunia, usamamizi na udhibiti wa sera za uchumi za ndani zina mchango mkubwa sana kwenye kuongeza gharama za Maisha kutokana na mfumuko wa bei usiodbitiwa au kuratibiwa na wizara. Ni jambo la kushangaza kuona hakuna hatua Madhubuti zinazopendekezwa na wizara kibajeti.
ACT Wazalendo, inapendekeza katika sera za kodi kwa wa fedha 2022/23 itazame maeneo yote ya bidhaa tunazoingiza nchini kwa matumuzi yetu ambayo yameathirika kutokana na mabadiliko ya kidunia kupunguza kodi au kusitisha kwa muda ili kushusha gaharama ya bidhaa nchini. Tunaendelea kupendekeza kwenye bei ya mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa kuondosha shilingi 500 kwenye kila lita. Aidha, tozo ya kuingiza mafuta kulabandarini ipunguzwe kutoka asilimia 35 iliyopo sasa hadi asilimia 10. Pia, serikali iimarishe mfumo wa Usimamizi wa matumizi ya serikali na mashirika ya umma ili kudhuibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma ambazo zingeweza kutumika kufidia maumivu yanayotokana na mfumo wa bei.
3. Serikali kutosimamia utendaji wa mashirika ya umma.
Usimamizi wa utendaji na undeshaji wa mashirika ya umma umechwa chini ya wizra ya fedha na mipango. Mwenenendo wa utendaji, uendeshaji na matumizi katika mashirika ya umma unatoa jawabu la moja kwa moja kuwa anayeyasimamia mashirika haya, hatekelezi majukumu yake ipasavyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ya mwaka 2020/21 inaonyesha mapungufu mengi yanayotokana na kutosimamiwa ipasavyo; Moja, CAG anaonyesha kuwa mashirika ya umma takribani 42 yalifanya matumizi kinyume na mapato yao. Hali ya kuwa na matumizi zaidi ya mapato kwa mashirika yasiyofanya biashara ilichangiwa zaidi na upungufu wa ruzuku kutoka Serikalini na ukosefu wa vyanzo vingine vya mapato visivyotosheleza mahitaji na kwa upande wa mashirika ya kibiashara yalisababishwa na udhibiti hafifu wa mapato na matumizi.
Pili, CAG ameibua hoja ya mashirika ya umma na taasisi za serikali kuwa na madeni makubwa. CAG anasema alibaini kuwa taasisi 16 zilikuwa na uwiano usioridhisha wa madeni kwa mtaji kwa zaidi ya asilimia 100. Hali hii inaonesha kuwa taasisi hizi zilikuwa zikitegemea zaidi madeni ili kuendesha shughuli zake, hivyo uwezo wa kifedha wa taasisi hizi unaweza kuathiriwa zaidi kutokana na gharama kubwa ya mikopo. Pia, yapo mashirika ambayo hayana kabisa uwezo wa kulipa madeni ya muda mfupi Lakini yanaendele kukopa.
Aidha, Mashirika ya umma takribani 32 haya bodi ya wakurugenzi. Bodi za wakurugenzi ni mamlaka za usimamizi wa mashirika ya umma ambazo kazi yake ni kuhakikisha utendaji wa taasisi unakuwa wa ufanisi na tija kwa maslahi ya umma. Bodi ya wakurugenzi ni chombo kinachowajibika kufanya maamuzi yanayotoa mwelekeo wa shirika kwa maslahi ya umma. Kukokesana kwa bodi katika mashirika ya umma kwa idadi kubwa hivi ni kuchelewesha utendaji na kudhoofisha Usimamizi wa manunuzi.
Wizara ya fedha na mipango kama msimamizi wa uendeshaji wa mashirika haya ni muhimu ikaona haya ya kusimamia kupatikana kwa bobi za wakurugenzi kwa mashirika yote ili nchi mashirika yasiendelee kutia hasara.
Sisi, ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuondoa mfumo wa uteuzi wa bodi za mashirika ya umma kutoka kwa Rais uende kwa Waziri wenye dhamana.
4. Ukosefu wa Mfumo wa Kuhakiki Mapato ya Michezo ya kubahatisha katika Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania
Michezo ya kubahatisha ni moja ya tasnia zinazokua kwa kasi duniani hususani katika nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania hii pia imezifanya serikali kuwa na chanzo cha mapato ya Serikali. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuanzia Julai 2016 hadi Juni 2021, jumla ya kodi iliyolipwa serikalini kutokana na uendeshaji wa michezo ya kubahatisha nchini ilifikia Sh. bilioni 428.9. Katika mwaka 2016/17 mapato yalikuwa Sh. bilioni 33.6, mwaka 2017/18 yalikuwa Sh. bilioni 78.7 na mwa-ka 2018/19 yalikua Sh bilioni 95.1. Mapato yalishuka kidogo katika mwaka 2019/20 kutokana na mlipuko wa janga la Uviko-19 ambao ulichangia kudorora kwa biashara na michezo na mapato yalikuwa Sh bilioni 89.5. Katika mwaka 2020/21 mapato yaliongezeka na kufikia Sh bilioni 132
Pamoja na kuongezeka kwa mapato kila mwaka bado kuna ufuatiliaji hafifu wa kujiridhisha mapato yanayowasilishwa na makampuni kwa serikali. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG anasema kuwa nilibaini kuwa haikuwa na mfumo wa kuhakiki na kufanya ulinganifu wa taarifa za mapato zilizowasilishwa na waendesha michezo ya kubahatisha ili kuwa na uhakika wa ushuru unaokusanywa. Bodi ilikusanya shilingi bilioni 2.88 kwa mwaka 2020/21 kwa kutoza ushuru kulingana na asilimia ya mapato ghafi iliyokubaliwa kati ya Bodi na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha. Hata hivyo, Bodi ilitegemea taarifa za mapato zilizowasilishwa na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha ili kubaini kiwango cha ushuru. Hakukuwa na njia za kuhakiki ukamilifu na usahihi wa mapato yaliyowasilishwa kila mwezi na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha.
Anaenedelea kusema kuwa “nina shaka na ukamilifu na usahihi wa kiasi cha mapato kilichowasilishwa na waendeshaji, kwani endapo waendeshaji wa michezo hiyo wangeficha baadhi ya mapato, Bodi haiwezi kubaini kwa sababu ya kukosekana mfumo wa uhakiki hivyo kusababisha upotevu wa fedha za umma”.
5. Utitiri wa kodi unaongeza gharama na mzigo kwa wananchi.
Utitiri wa kodi za serikali kwenye bidhaa zinazoingizwa nchini (tozo na kodi bandarini), zinachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko kubwa la ghrama za bidhaa hususani zile zinaingizwa kutoka nje hususani bdihaa muhimu za chakula,kama vile Mafuta ya kula, Mbolea na Ngano. Unaweza kuona mchango wa tozo na kodi katika mjengeko wa bei za bidhaa hizi unaanzia asilimia 35 hadi 50.
Vilevile bidhaa zisizokuwa za chakula kama vile Mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa, vifaa vya Ujenzi (nondo, mabati na saruji) Mfano mchanganuo wa bei ya mafuta ya petrol, diseli na mafuta ya taa baada ya gharama ya usafiri, forodha na bima mpaka yanapofika bandarini kwa mwezi septemba 2021 ilikuwa shilingi 1,162 kwa petrol, dizeli Sh1,098 na mafuta ya taa Sh1,062. Tozo na kodi mbalimbali zilizoongezwa na serikali pamoja na mamlaka zake ilikuwa shilingi 1113.48 kwa petrol na kufanya bei kuwa 2405 rejareja huku kodi na tozo za serikali ziliongeza gharama kwa asilimia 51katika kila lita moja. Hivyo hivyo kwa diseli na mafuta ya taa ongezeko kutokana na kodi na tozi lilikuwa ni zadi ya asilimia 50. Mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya Taa zinatozwa kodi na tozo zipatazo 18 kwenye kila lita moja.
Aidha, kuanzishwa kwa tozo za miamala za mitandao ya simu za mikononi umechangia kwa sehemu kubwa sana ugumu wa Maisha. Kwa kuwa mfumo wa Maisha kwa kulinga vipato vya watanzania, matumizi ya miamala ya simu za mkononi husaidia mzunguko wa fedha na ubadilishanaji wa fedha. Kuanzishwa kwake kupelekea kuongeza maumivu kwa wananchi. Sambamba na hilo, hadi sasa haijawekwa wazi fedha zinazotokana na tozo za simu zinatumikaje.
ACT Wazalendo, tunaitaka tusitishe tozo za miamala ya simu ili kuwapunguzia mzigo wananchi kwa kuwa fedha zilizopaswa kukusanywa na kwenda kutumika, zimefidia na Mkopo wa Serikali wa kuimarisha uchumi kutokana athari za Ugonjwa wa Uviko-19 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).Mapendekezo ya kupunguza kodi zingine tumeshayatoa hapo juu.
6. Manunuzi yasiyofuata sheria yenye thamani ya shilingi bilioni 645.9
Wizara ya fedha na mipango ina jukumu la kusimamia manunuzi ya mashirika ya umma na taasisi za serikali. Kwa mujibu wa Uchambuzi wetu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesbabu za serikali tumebaini kuwa jumla ya hoja zilizoibuliwa na CAG zinazotokana na Manunuzi yaliyofanywa na serikali ambayo hayakufuata sheria yalikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 645.9 kati ya hizo manunuzi yaliyofanywa na taasisi za serikali yalikuwa shilingi Bilioni 476.67 na manunuzi yaliyofanywa na mashirika ya umma yalikuwa shilingi bilioni 169.32.
Hoja kubwa zinazopelkea kuligharimu taifa kwenye upande wa manunuzi yasiyofuata sheria na taratibu ni ucheleweshaji wa miradi ya kimkakati ambayo imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 214. 54 na Ununuzi unaofanywa nje wa mfumo wa malipo ya kieletroniki na TANePS ambayo inafanya kuwa thamani ya shilingi bilioni 135.
Hivyobasi, unaishauri serikali kuzisimamia taasisi zake ili kuhakikisha zinafuta sheria kuepusha upotevu mkubwa unaolisababishia hasara taifa.
Hitimisho:
Uchambuzi wetu wa bajeti ya wizara ya fedha na mipango tunaona ni ile ile inayotenga kiasi kikubwa cha fedha kuhudumia deni la taifa bila kuweka makakati wa kupunguza kukopa nje. Aidha, hakuna mkakati Madhubuti wa kuaznishwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja. Michezo ya kubahatisha kuonekana chanzo cha mapato kisichofuatiliwa kwa karibu zaidi na kupimwa athari zake kwa jamii.
Imewasilishwa na;
Juma Kombo
[email protected]
Naibu Msemaji wa Sekta ya Fedha na Mipango- ACT Wazalendo
08 Juni, 2022
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter