HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII- ACT WAZALENDO NDG. JULIANA DONALD KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWA MWAKA 2022/23.
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII- ACT WAZALENDO NDG. JULIANA DONALD KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWA MWAKA 2022/23.
Utangulizi
Kufuatiwa na taarifa ya utekelezaji wa mujukumu na mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2022/23 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi H. Chana (Mb.) siku ya jana Ijumaa tarehe 3 Juni, 2022 ambapo ilipokelewa na kujadiliwa na Bunge kwa siku moja pekee (jana). Sisi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii tumeisoma, kuichambua na kuimulika ili kuona kwa namna gani ina akisi matarajio na matamanio ya wananchi.
Aidha, kupitia uchambuzi wetu, tumeweza kutoa mapendekezo kuhusu maeneo ya vipaumbele ambayo tunaona yanafaa kuwa sehemu ya mipango na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka huu wa fedha na kwa miaka inayofuata. Katika kufanya hivyo, hotuba hii ya Msemaji wa Maliasili na Utalii wa ACT Wazalendo Ndg. Juliana Donald imebaba hoja saba (7) kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Zifuatazo ni hoja saba (7) za ACT Wazalendo kuhusu bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/23:
1. Serikali kushindwa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi.
Moja ya majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kusimamia misitu, maeneo ya hifadhi, mapori tengefu, mbuga za wanyama na mapori ya akiba. Katika usimamizi wa maeneo haya mara nyingi kumekuwepo na changamoto za kutokea migogoro ya mara kwa mara na kwa muda mrefu migogoro hiyo imekuwa baina ya wanavijiji na mamlaka za hifadhi. Migogoro hii haipatiwi utatuzi badala yake inaibuka mipya kutokana na maamuzi ya wahifadhi dhidi ya wananchi.
Kuhuisha na kupanuliwa kwa maeneo ya hifadhi za wanyamapori kama hifadhi za taifa, mapori tengefu, mapori ya akiba, na maeneo ya hifadhi za jamii ambayo kwa pamoja yanazuia kuendelezwa kwa maeneo ya wakulima na wafugaji. Hii imesababisha hifadhi za wanyamapori kuwa karibu na wananchi na hivyo kusababisha migogoro ya wanyama na binadamu hasa pale wanyama wanapoingia kwenye mashamba ya wananchi na kula mazao au mifugo yao.
Hivi karibuni, migogoro iliyojitokeza baina ya wanavijiji vinavyozunguka hifadhi ya Sayaka, Magu, Mwanza dhidi ya maafisa wa mamlaka ya misitu (TFS) kutokana na mamlaka kusogeza vigingi vya mipaka ya hifadhi kwa wananchi. Mgogoro wa hifadhi ya Selous na vijiji vya Kilwa (Mtepera, Zingakibaoni, Ngarambe) nao umetokana na mipaka. Pia, migogoro ya mipaka kwenye vijiji 45 vinavyopatikana kwenye wilaya za Simanjiro, Karatu, Kondoa, Bariadi na Bunda.
Uhalisia unaonyesha kuwa migogoro hii inatokana na kukosekana kwa mifumo imara inayolinda haki na maslahi mapana ya wazalishaji wadogo (wakulima na wafugaji) katika ardhi. Mfano, mfumo wa umilikaji wa ardhi, changamoto za upatikanaji wa rasilimali za maji na malisho zinazoathiri wazalishaji wadogo. Katika migogoro hii, tumeshuhudia vitendo vya kinyama kama vile kuuawa kwa wafugaji, kuteswa, kuwekwa kuzuizini na kuumizwa katika maeneo mengi yenye migogoro baina ya pande hizi mbili, kwa kifupi kunaonyesha matumizi makubwa ya nguvu na hata risasi za moto.
2. Fidia ndogo na kukithiri kwa migogoro kati ya wanyamapori na wananchi
Mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa (PAs) katika Tanzania huchukua asilimia 28 ya ardhi yote. Kati ya asilimia hiyo, asilimia 4 ni Hifadhi za Taifa (NP) 12, asilimia 1 ni Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), asilimia 15 ni Mapori ya Akiba (GRs) 31, na asilimia 8 ni Mapori Tengefu (GCAs) 38. Kutokana na hali hiyo asilimia 19 ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya Wanyamapori katika maeneo yaliyohifadhiwa (PAs) ambako makazi ya binadamu hayaruhusiwi (NPs na GRs), na asilimia 9 ya ardhi kwa ajili ya maeneo yaliyohifadhiwa (PAs) ambako maisha ya wanyamapori ni sambamba na maisha ya binadamu.
Kumekuwepo kwa migogoro baina ya wananchi na wanyapori. Wananchi wanaoishi pembezoni au maeneo yanayozunguka hifadhi za wanyama au mbuga za wanyama kama vile Selous, Nyasaka, Mkomazi, Biharamulo wamekabiliwa na migogoro dhidi ya wanyama wakali au waharibifu. Uzoefu unaonyesha kuwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori hutokea pindi wanyamapori wanapoharibu mali za wananchi (mashamba, mazao, mifugo na makazi) au kuwaua watu pamoja na watu kutaka kuwaua wanyama hao kwa lengo la kujihami na kulinda mali zao.
Malalamiko ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi hujitokeza mara kwa mara lakini hatuoni jitihada za makusudi za Serikali kukabiliana na changamoto hizo.
Kwa upande wa fidia, kumekuwepo kwa viwango vidogo vya fidia (vifuta jasho na machozi) za uharibifu unaofanywa na wanyama hao kama vile tembo, nguruwe, simba, fisi na chui. Viwango vya sasa kwa mujibu wa kanuni ni Shilingi 200,000 hutolewa kwa aliyepata majeraha yasiyo ya kudumu na Shilingi 500,000 kwa majeraha au kilema cha kudumu huku wakitoa kifuta jasho cha Shilingi 100,000 ekari kwa wale ambao mazao yao yameharibiwa na wanyama pori na Shilingi 1,000,000 kwa mwananchi aliyeuwawa na wanyama.
Wakati mwingine wananchi hawapatiwi fidia kabisa na pindi wanapojaribu kuidai Serikali fidia, mrejesho wanaoupata ni kuwatuhumu wananchi wanaoishi kando ya hifadhi kuwa wanavamia maeneo ya hifadhi za wanyama kinyume cha sheria, hivyo wanapaswa kuondoka. Ni wazi kuwa mtazamo wa Serikali katika suala hili umeegemea zaidi kwenye kuangalia maslahi ya wanyapori kuliko watu. Wananchi hawa wanatazamwa kama wahalifu, wavamizi na maadui wa uhifadhi.
ACT Wazalendo tunapendekeza, Serikali iweke viwango vipya kwa ajili ya waathirika wa matukio ya ajali au majanga yanayohusisha wananchi na wanyamapori kwa kuzingatia hali halisi ya maisha pamoja na thamani ya uharibifu au madhara yaliyotokea.
3. Masalia ya Mjusi mkubwa wa Dinosa kurejeshwa nchini.
Ni miaka mingi imepita tangu watanzania (wananchi wa kawaida na wanasiasa) wakidai masalia ya Mjusi Mkubwa (Dinosa) kurejeshwa nchini na kuona kwa namna ya kulinufaisha Taifa letu, bado hakuna juhudi zilizofanywa na Serikali katika kutambua umuhimu na faida zitokanazo na rasilimali ili kuweza kumrejesha Mjusi huyo. Sehemu ya masalia hayo kwa kipindi cha sasa ni mjusi mkubwa anayeoneshwa katika Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Naturkunde Berlin, Ujerumani. Taarifa za kitaalam zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya mjusi huyo ni masalia halisi kutoka Tendaguru Tanzania na asilimia 40 ni malighafi za kibunifu kwa ajili ya kupata umbo halisi la mjusi.
Katika hotuba ya bajeti kwa mwaka 2021/22 Serikali iliahidi kuwa itaanzisha mazungumzo kupitia Makumbusho ya Taifa na Makumbusho ya Naturkunde ya jiji la Berlin, Ujerumani, ili kuweka mazingira wezeshi ya kuanzisha mjadala kati ya nchi ya Ujerumani na Tanzania ili kurejesha au kunufaika na masalio hayo, lakini Serikali ipo kimya hadi sasa ni wazi hakuna hatua za uhakika zilizochukuliwa.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuweka wazi hatua zilizofikiwa katika kumrejesha mjusi na namna ambayo tunaweza kupata gawio la manufaa ya kipindi chote ambacho Ujerumani imekuwa ikinufaika kutokana na mjusi huyo. Aidha, tunaitaka Serikali kushughulikia suala hili kwa kutumia mwakilishi wetu (Balozi), badala ya kutumia idara ya Makumbusho.
4. Serikali haitoi kipaumbele cha kutangaza maeneo ya mambo ya kale (Utalii wa utamaduni)
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Utalii na Bodi ya Taifa ya Utalii haijawezesha ipasavyo maendeleo na utangazaji wa sekta ya utalii wa utamaduni (malikale) ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi, huku ikijikita zaidi kuimarisha huduma za utalii wa wanyamapori na upandaji wa milima. Ingawa sekta ya Utalii huchangia wastani wa asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni, mchango wa sekta ndogo ya utalii wa mambo ya kale (hususani, makumbusho, maeneo ya kihistoria) huchangia kiwango kidogo sana.
Mwenendo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/17 ilichangia Shilingi Milioni 110.6, mwaka wa fedha 2017/18 ilichangia Shs. 120, mwaka 2018/19 ilichangia Shs. Milioni 175.04, mwaka 2019/20 ilichangia 232 na mwaka 2020/21 ilichangia Sh. Milioni 136.9. Kutokana na Mwenendo huu ni wazi kuwa, Wizara haijasimamia ipasavyo Makumbusho ya Taifa na maeneo ya urithi wa utamaduni ili kudumisha makusanyo na malikale na kuimarisha sekta ya urithi wa utamaduni wa taifa.
Aidha, taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/21 zinaonyesha kuwa kuna uendelezaji na utendaji usioridhisha wa makumbusho na maeneo ya urithi wa utamaduni.
CAG anabainisha kuwa asilimia 14 pekee ya maeneo ya urithi wa utamaduni nchini ndiyo yalikuwa na watumishi wenye ujuzi na yaliendesha shughuli zake za kuhudumia umma kwa ajili ya kukuza utalii na urithi wa utamaduni.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kutenga fedha kwa ajili kuiwezesha bodi ya Utalii nchini kununua vitendea kazi na kuajiri watumishi ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake yaliyoidhinishwa.
5. Tozo za huduma na mazao ya misitu
Tozo za mazao na huduma za Misitu zinasimamiwa kwa mujibu wa Kanuni ya Misitu iliyotolewa katika Gazeti la Serikali Na. 627 la mwaka 2020. Tozo hizi husimamiwa kwa kuzingatia Sheria ya Misitu Sura 323. Katika utekelezaji wa kanuni hizo, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu malipo ya tozo kulingana na thamani ya mazao na huduma itolewayo.
Katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana Serikali ilikiri kuwepo kwa viwango vya juu vya tozo na kodi kwenye mazao na huduma za misitu jambo ambalo linafanya ustawi na uendelezaji wa sekta hiyo kutoridhisha. Serikali iliweka wazi azma ya Wizara kushirikiana na wadau katika kufanya mapitio ya kanuni zinazongoza sekta ya misitu ili wananchi waendelee kunufaika kibiashara na mazao na huduma za misitu na Serikali kupata mapato yake.
Uchambuzi tulioufanya katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu hakuna mabadiliko yaliyofanywa licha ya wadau kutoa malalamiko na mapendekezo kwa ajili ya kuboresha mifumo na viwango vya tozo za huduma na mazao ya misitu.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuharakisha na kuwashirikisha wadau katika mapitio ya kanuni za sekta ndogo ya misitu ili kuondoa kero za muda mrefu kwenye sekta hiyo. Pia, ili kufanya biashara ya mazao ya misitu ni muhimu kwa Serikali na kuondoa dhana ya biashara ya mazao ya misitu ni ujangiri unaohitaji kudhibitiwa.
6. Usimamizi wa maliasili na uendelezaji wa utalii kanda ya kusini
Sekta ya utalii ina nafasi kubwa sana katika kukuza pato la taifa, kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii inaanza kwenye kutengeneza ajira, kuingiza fedha za kigeni na kuuza bidhaa za kijamii kutokana na watalii.
Katika nchini yetu, pamoja na kuwa na vivutio vingi vya utalii ukanda wa kusini bado haujaendelezwa vya kutosha ili kunufaika na sekta hii ya utalii. Mara zote Serikali inaandaa mikakati ya kusimamia na kuendeleza Utalii kanda ya kusini (Ruvuma, Iringa, Lindi, Mtwara) lakini mikakati hiyo haijatafsiriwi kwenye vitendo. Ni wazi kuwa Serikali kupitia Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) imeitenga mikoa hiyo kwa vile katika maonesho ya Utalii ya Nje za nchi, TTB imekuwa haivitangazi vivutio vilivyoko ukanda wa Kusini na juu kusini.
Kwa Mkoa wa Lindi uwepo wa magofu ya kale Kilwa kisiwani na Songo Mnara ambayo yameorodheshwa kwenye urithi wa dunia Lakini bado hayajatangazwa vya kutosha kuvutia watalii wengi zaidi. Mbuga ya Selous iliyoenea mikoa ya Pwani, Iringa, Lindi na Ruvuma nayo haijawekewa Miundombinu ya kutosha ili kuimarisha utalii wa kutazama wanayama kama ilivyo kwa Serengeti, Mikumi na Ngorongoro; Aidha, Iringa ni moja ya mikoa yenye vivutio mbalimbali vya kitalii ikiwa pamoja na mbuga za wanyama pori za Ruaha na Udzungwa. Mkoa pia una vivutio vya kihistoria na kitamaduni kama vile eneo la mali kale la Isimila (Isimila Stone Age) na makumbusho ya Mkwawa ya Kalenga
Mradi wa kusimamia na kuendeleza Utalii nyanda za juu kusini (REGROW) hautengewi fedha za kutosha kuhakikisha azma ya kuyaendeleza maeneo haya inafanikiwa kwa ufanisi mkubwa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Shilingi 30,495,601,578 ziliidhinishwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za mradi. Hadi mwezi Aprili 2021, Shilingi 5,776,178,445 zimetolewa na kutumika sawa na asilimia 18.9.
ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali Mradi wa kusimamia na kuendeleza Utalii ujikite zaidi kwenye kutengeneza Miundombinu ya usafiri, Barabara na viwanja vya ndege, kuzalisha matangazo ya video/filamu fupi fupi na mitandao ya kijamii. Pia, Serikali ihakikishe inatoa kwa wakati fedha zote zilizotengwa kwa ajili kuendeleza na kutangaza vivutio vilivyopo kusini.
7. Matumizi mseto katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambayo ina jukumu la kusimamia shughuli za uhifadhi, uendelezaji wa utalii na ustawi wa jamii zinazoishi ndani ya eneo la Hifadhi. Hivi karibu, kinyume na kuanzishwa kwake Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Serikali imeonyesha nia na kuanza kwa vitendo kuwaondosha wanajamii wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo kwa madai ya kulinda urithi wa dunia katika eneo hilo kutokana na uharibu unaofanywa na wananchi (wafugaji jamii ya Kimasai).
Mwaka jana Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utaliii ilionyesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa agizo la kushughulikia changamoto za matumizi mseto katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro. Wizara alisema kuwa imeanza kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa kwa hatua za awali. Mathalani, kwa upande wa changamoto ya matumizi mseto katika eneo la Ngorongoro, tarehe 08 Aprili, 2021 chini ya uenyekiti wa aliyekuwa waziri wa Wizara hii, Ndg. Damas Ndumbaro, Wizara ilifanya kikao na uongozi wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kuanza kutekeleza maelekezo hayo.
Athari za maagizo haya, tumeyashuhudia wazi mwaka huu tumeona Serikali inafanya kila njama za kuwaondosha wafugaji jamii ya wamasai katika eneo lao la asili kwa madai ya kulinda masharti ya kimataifa ya kulifanya eneo hilo kuwa ni urithi wa Dunia ambao uwepo wa wakazi hao kuna hatarisha uendelevu wa hifadhi hiyo.
Sisi, ACT Wazalendo tulitoa kauli na mapendekezo ya namna ya kushughulikia changamoto hiyo ili kulinda maslahi ya wananchi na uhifadhi kwa ujumla kupitia matamko ya Msemaji wa sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Tunasisitiza kuwa maslahi ya wazalishaji wadogo yanapaswa kuzingatiwa katika jitihada zozote za kulinda uhifadhi.
Hitimisho:
Sekta ya utalii ina nafasi kubwa sana ya kuzalisha ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla. Pia mnyororo wa thamani wa sekta utalii ni mrefu na kwa kuwa nchi imejaaliwa vivutio vingi vya utalii inaweza kuleta fedha nyingi za kigeni kuweza kununua mashine na vipuri tusivyoweza kuzalisha wenyewe katika kipindi cha mpito. Thamani ya fedha za kigeni katika utalii lazima ziendane na thamani ya manunuzi yetu nje ya nchi na hasa mafuta ambayo yanatumia sehemu kubwa ya akiba yetu ya fedha za kigeni. Aidha, ni muhimu Serikali kusimamia na kuendeleza maeneo ambayo kwa muda mrefu hayajapewa kipaumbele licha ya kuwa na vivutio vingi.
Pia. kasi ya kuhuisha na kupanuliwa kwa maeneo ya hifadhi za wanyamapori kama hifadhi za taifa, mapori tengefu, mapori ya akiba, na maeneo ya hifadhi za jamii ambayo kwa pamoja yanazuia kuendelezwa kwa maeneo ya wakulima na wafugaji. Hii imesababisha hifadhi za wanyamapori kuwa karibu na wananchi na hivyo kusababisha migogoro ya wanyama na binadamu hasa pale wanyama wanapoingia kwenye mashamba ya wananchi na kula mazao au mifugo yao. Serikali inapaswa kuzingatia haki za wazawa katika kulinda maslahi yao kwa ajili ya uendelevu wa jamii.
Juliana Donald Mwakan’gwali
jmwakan’[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii- ACT Wazalendo
04 Juni, 2022
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter