Hotuba ya Msemaji wa sekta ya Mambo ya Ndani ACT Wazalendo Ndg. Mbarala Abdallah Maharagande kuhusu bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Hotuba ya Msemaji wa sekta ya Mambo ya Ndani ACT Wazalendo Ndg. Mbarala Abdallah Maharagande kuhusu bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Utangulizi:
Jana Alhamisi tarehe 5 Mei 2022 Wizara ya Mambo ya Ndani iliwasilisha bungeni hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23. Sisi, ACT Wazalendo tulifuatilia kupitia Msemaji wa Sekta ya mambo ya ndani, ili tuweze kuimulika, kuichambua na kutoa maoni mbadala wa bajeti hiyo kwa lengo la kuisimamia Serikali na kuhakikisha maslahi ya wananchi yanazingatiwa. Baada ya kupitia hotuba ya bajeti, tumekuja na maeneo makuu manne; Mfumo wa utoaji haki chini ya jeshi la polisi, hali ya mahabusu, maslahi ya askari, mapitio ya bajeti za miradi ya maendeleo na utendaji wa mamlaka ya vitambulisho. Kwa kuangazia maeneo hayo, hotuba hii imebeba hoja kumi (10) kuhusu bajeti ya Wizara ya mambo ya ndani kwa mwaka wa fedha 2022/23.

1. Jeshi la Polisi kutumika kuminya mfumo wa utoaji wa haki.
Katika mfumo wetu wa haki jinai nchini, jeshi la polisi ni mdau ambalo linahusika kwenye kukamata watuhumiwa. Katika mnyororo huo wa haki jinai jeshi la polisi limepewa haki ya kukamata na kufanya uepelelezi. Lakini utekelezaji wa utaratibu huu unapelekea kuzuia haki za wananchi wanapokuwa kwenye mikono ya polisi. Ushiriki wa polisi kwenye hatua kadhaa ndio zinaminya utoaji wa haki.
Kwanza, Haki ya Dhamana ni hisani ya polisi (Polisi wanaweza kumshikilia mtuhumiwa kwa muda wanao utaka wao kinyume na sheria). Jeshi la Polisi kutumika kuzuia haki ya dhamana kwa watuhumiwa ambao hawajatiwa hatiani, jambo ambalo linanyima fursa ya kupatikana kwa haki kwa wananchi wanapotuhumiwa na makosa mbalimbali.
Pili, Mfumo wa ukamataji bado ni wa kikoloni, utaratibu wa ukamataji umeelezwa vyema kabisa katika sheria ya jeshi la polisi, Lakini bado ukamataji hauzingatii haki ya mshukiwa. Polisi wanavyokuja kukukamata, tayari wameshakuhukumu (wao ndio mahakama), wao ndio magereza (wanaosimamia adhabu na urekebishaji wa tabia). Jeshi la polisi bado lina sura katili mithili ya jeshi la kikaburu. Polisi wanaweza kukamata, wakazuia ndugu, jamaa na wakili kuja kukuona.
Tatu, Jeshi la Polisi kutesa watuhumiwa vituoni. Mateso wanayopewa watuhumiwa katika vituo vya polisi imekuwa ikichukuliwa kama mbinu ya uchunguzi na upelelezi, ukweli mchungu ni kuwa uchunguzi haufanywi kitaalamu au kisayansi. Wapo watu ambao wamepata ulemavu wa kudumu kutokana na mateso (vipigo) wakiwa chini ya jeshi la polisi. Kama kungekuwa na takrimu sahihi, tungeweza kubaini kuwa idadi kubwa ya mahabusu waliopo magerezani, walikiri makosa yao wakiwa kwenye mikono ya polisi kutokana na vipigo vya mbwa koko, wakasalimu amri.
Kwa hoja hizi tatu, ni dhahiri jeshi la polisi kwa tofauti tofauti zinachangia kukandamiza haki za wananchi.
2. Ukiukwaji wa haki za watuhumiwa katika vituo vya Polisi na kucheleweshwa kwa upelelezi.
Kifungu na 32 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kinawataka polisi kumfikisha mtuhumiwa mahakamani ndani masaa 24. Lakini kifungu hiki cha sheria hakifuatwi, matokeo yake jeshi la polisi linafanya kadri wanavyotaka kwa kisingizio cha agizo kutoka juu. Upo Ushahidi wa kutosha, hivi karibu wakili Peter Madeleka alikamatwa na polisi na kuchukua wastaani wa masaa 78, kuachiwa. Wapo wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani walioshikiwa na jeshi la polisi zaidi ya siku saba hadi wiki mbili wakiwa kwenye mikono ya polisi bila kuachiwa huru au kupelekwa mahakamani.
Pia, Jeshi la Polisi linafanya kazi ya kusimamia mashtaka ya watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani mbali na wajibu wao wa upelelezi. Ingawa kumekuwa na mipango ya kuhakikisha jukumu la uendeshaji wa mashtaka wanaachiwa mawakili wa serikali, kutokana na idadi ndogo ya mawakili, zipo mahakama ambazo mashtaka yamekuwa yakiendeshwa na maofisa wa polisi. Maofisa hao wa polisi hao wanafanya kazi kwa niaba ya mawakili wa serikali inapelekea kucheleweshwa kwa upelelezi.
ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuachana na polisi kuwa kama waendesha mashtaka katika mahakama mbalimbali nchini. Badala yake iongeze ajira za waendesha mashtaka.

3. Maslahi na haki za askari polisi na magereza nchini.
Maslahi ya polisi ni jambo muhimu sana katika kuhakikisha kuwa polisi wanatekeleza majukumu yao kwa uhuru na bila kuingiliwa kwa namna moja au nyingine. Hivyo basi ili kuhakikisha uhuru wa polisi ni vyema vyanzo vya mapato kwa Polisi vikawa vya uhakika, vinavofahamika na vinavyoendena na mahitaji ya jeshi la polisi.
Pia, polisi wanapopanda vyeo na madaraja wanatakiwa kuenda sambamba na kupanda kwa mishahara yao, zipo taarifa kuwa maofisa na askari wengine wa jeshi la polisi na magereza wamekuwa wakipandashwa vyeo na kuongezewa majukumu lakini inachukua muda mrefu kupandishwa mishahara.
4. Msongamano wa mahabusu na hali ya usalama katika Magereza
Takwimu zinaonyesha kuwa ulinganifu kati ya idadi ya wafungwa na mahabusu ni kuwa mahabusu ni wengi kuliko wafungwa. Kwa mujibu wa wizara (2020/21) kulikuwa na wafungwa na mahabusu 32,438 katika magereza yote nchini, Kati yao wafungwa ni 14,464 na mahabusu 17,974. Huku uwezo wa magereza ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902.
Kwa mujibu wa Mpango wa Fedha wa kipindi cha kati wa miaka 2017/18 - 2019/20 na 2020/21 – 2022/23, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Jeshi la Magereza hazikutenga bajeti yoyote kwa ajili ya ujenzi wa magereza mapya na ukarabati wa yaliyopo licha ya kujumuishwa kwenye mipango mkakati.
Ripoti ya CAG pia inathibitisha hali ya upungufu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anasema kuwa “upungufu wa fedha kwa ajili ya miundombinu ya rumande na magereza umesababisha msongamano katika magereza yaliyotembelewa ambayo yalibainika kuwa na msongamano kati ya asilimia 1 na 194 zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa. Kiwango kikubwa cha msongamano kilibainika mkoani Dar es Salaam katika Gereza la Keko, ambalo lilikuwa na msongamano wa zaidi ya asilimia 194,”
Katika makadirio ya bajeti ya mwaka huu, Waziri anasema wamefanikiwa kujenga magereza mapya Chato na Ruangwa kama sehemu za jitihada za kupunguza msongamano, katika ripoti ya CAG imebainishwa ujenzi wa majengo haya mawili (2) umefanywa bila kufuata tathmini ya mahitaji halisi ili kuhalalisha haja ya kuanzisha na kujenga magereza hayo. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG hatua hizo hazijasaidia kupunguza msongamano na ni upotevu wa fedha.

ACT Wazalendo tunasisitaza matumizi ya adhabu mbadala kama inavyobainishwa katika kifungu 3 (1) cha Sheria: The Community Services Act (Cap. 291 R.E. 2019) ili kupunguza msongamano. Ambapo inampa Afisa Ustawi wa Jamii mamlaka ya kupendekeza adhabu mbadala kwa watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo adhabu husika ni chini ya miaka 3.

 

5. Hali ya vituo vya zimamoto Nchini na vitendea kazi
Mwenendo wa utendaji wa jeshi la zima moto bado hauridhishi mathalani kwa miezi sita (6) kutokea kwa matukio ya kuungua kwa masoko ya wafanyabiashara ya Kariakoo, Karume I & II, soko la Mbuyuni Moshi, Soko la Mbeya, Mbagala yote haya hayakunusuriwa na jeshi la zima moto.
Takwimu zinaonyesha upungufu mkubwa wa askari na bajeti kidogo ya mafunzo kwa ajili ya uokoaji ndio zinazorotesha utendaji wake, bajeti ya mwaka huu ilipaswa kuwa mwarobaini wa changamoto hizi. Pia, upungufu wa vituo na magari ya kuzimia moto.
Taarifa ya wizara (2021/22) inaonyesha kuwa Jeshi la Zima moto na Uokoaji lina jumla ya vituo vya zima moto 82 Tanzania Bara wakati mahitaji halisi ya vituo ni 162. Jeshi pia lina magari 72 ya kuzimia moto na maokozi, ikilinganishwa na mahitaji halisi ya magari 324.
Katika bajeti ya mwaka huu kiasi kilichotengwa kwa ajili ununuzi wa magari ya zimamoto ni kiasi cha bilioni 1.96 kwa ajili ununuzi wa magari 19, huku kiasi cha bilioni 2.99 kwa ajili magari 3 kutoka Kampuni ya nyumbu. Kwa mujibu hotuba ya Waziri wa mambo ya ndani Ndg, Masuni viwango hivi vinaleta utatanishi. Pia, ununuzi hakuna kiasi kilichotengwa kwa ajili ujenzi wa vituo vipya.

6. Matukio ya tishio la usalama na uvunjifu wa amani.
Hali ya usalama wa wananchi kwa siku za hivi karibu, imetikishwa kwa kujitokeza kwa msululu wa matukio ya uvamizi, kujeruhi na kuporwa kwa mali za wananchi hususani katika jiji la Dar es Salaam. Matukio haya yameripotiwa kufanywa na makundi ya vijana alimaarufu kama panya road au panya buku kwa nyakati mbalimbali katika Wilaya ya Temeke maeneo ya Yombo, Buza, Mzinga Kongowe, Halmashauri ya jiji la Ilala hususani mitaa ya Zingiziwa, Chanika na Kinondo, mtaa wa mtongani kata ya Kunduchi. Tunatambua jitihada zilizofanywa na Serikali kupitia kauli ya Rais wa Nchi na hatua za jeshi la polisi Mkoa wa Dar es Salaam kuchukua hatua.
Lakini ni tunasisitiza kwa jeshi la polisi kuendelea kufanya doria kwa ajili kuhakikisha matukio ya namna hii yanakomeshwa na kutojirudia tena ili kuimarisha usalama maeneo mbalimbali nchini.

7. Mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA)
Kila mwaka wa fedha, Serikali huweka kipaumbele cha kuendelea kutambua wananchi na kuwasajili. Lakini uzoefu na uchambuzi wetu umebaini kuwa kuna utendaji usioridhisha wa mamnalaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) katika uandikishaji, usajili, uzalishaji wa namba za vitambulisho, uzalishaji wa vitambulisho vyenyewe na usambazaji wake. Kuna pengo kubwa kati ya usajili na uzalishaji wa vitambulisho, mathalani hadi 21 Machi 2022 wananchi wanaodaiwa kusajiliwa ni 22,917,859 lakini vitambulisho vilivyozalishwa ni Milioni saba pekee. Kasi ya utambuzi, usajili na uzalishaji ni ndogo mno na Serikali kila mwaka inakuja na kauli za matumaini

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 Serikali iliitaarifu umma kuwa wizara tayari imenunua mashine mbili (2) zenye uwezo wa kuchapisha vitambulisho 144,000 ili kufanikisha lengo lililowekwa la kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho kwa wakati. Lakini ni masikitiko yetu makubwa kuwa hadi sasa mashine hizi hazifanyi kazi yoyote, tatizo lipo palepale.
Utendaji mbovu wa NIDA unathibitishwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2020/21 kwa maneno yake anasema “nilibaini kuwa Mamlaka imekuwa na utendaji kazi usioridhisha katika shughuli za msingi za usajili, utengenezaji wa nambari za utambulisho na utengenezaji wa vitambulisho”
Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa NIDA ililenga kuzalisha Vitambulisho vya Taifa 13,900,000. Hata hivyo, ilifanikiwa kuzalisha vitambulisho 1,705,693 pekee, hivyo kushindwa kufikia lengo la uzalishaji wa Vitambulisho vya Taifa 12,194,307, sawa na asilimia 88. Kwenye usambazaji wa vitambulisho ni asilimia 84 tu vilisambazwa. Pia, ilizalisha namba za vitambulisho 1,900,000 kiutekelezaji ilifanikiwa kuzalisha namba za vitambulisho 1,061,295 pekee na kushindwa kufikia lengo la kuzalisha Nambari 838,705, sawa na asilimia 44.
Vilevile, kutengwa kwa mikoa ya pembezoni (Kigoma, Kagera) kwenye usajili na uzalishaji wa namba za vitambulisho vya taifa, NIDA haitoi kabisa vitambulisho kwenye mikoa hiyo kwa kisingizio cha uchambuzi. Serikali ina mpango gani kumaliza suala hili, kwasababu kuwaacha kando wananchi wa maeneo haya kunaongeza hatari ya Serikali kushindwa kuwatambua raia wake, pamoja na kushindwa kupata taarifa zao kwa matumizi mbalimbali. Pia, inapelekea kuwepo na changamoto kwa wananchi kukosa huduma mmbalimbali za kisheria zinazohitaji utambulisho wa namba za utaifa.
8. Jeshi la Polisi kutumika kukandamiza demokrasia ya vyama vingi.

Serikali ya awamu ya tano iliweka zuio haramu, linalokiuka Katiba ya nchi - kwa vyama vya siasa hususani vyama vya upinzani kutofanya mikutano ya hadhara, kichaka kilichokuwa kinatumika kutekeleza amri na zuio hilo haramu ni sheria ya vyama na sheria ya jeshi la polisi. Jeshi la polisi limekuwa likitumika kuwazuia wapinzani kufanya shughuli za kisiasa kwa hoja ya taarifa za “kiintelijensia” kwamba kufanyika kwa shughuli hizo kunaweza kuvunja amani.
Licha ya hali hii kupungua kidogo katika awamu hii ya sita ya serikali, ni muhimu kama nchi tuwe na sheria zinawaondoa kabisa polisi kwenye shughuli za siasa, ili kufanya uwanja wa siasa kuwa wa ushindani. Kwa uzoefu wa miaka mingi jeshi la polisi limekuwa likitumika kukilinda chama cha Mapinduzi. Ipo mifano mingi sana ya namna ambavyo jeshi la polisi linavyotumika kuzima mwanga wa demokrasia ya vyama vingi nchini hususani katika miaka takribani sita (6) iliyopita.

ACT Wazalendo katika ilani ya uchaguzi (2.4.4-(i) tulidhamiria kufanya mageuzi makubwa kuhusu Jeshi la Polisi na uhuru wa kukusanyika. Serikali ya ACT itafanya marekebisho sheria kandamizi ya Jeshi la Polisi Tanzania na huduma saidizi sura ya 322, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kifungu cha 43 (3), (4), na (6), inayotoa mwanya wa wazi kwa polisi kuzuia uhuru wa kujumuika bila sababu yoyote ya msingi, hivyo kukengeuka Katiba yetu ya nchi ya 1977 ibara ya 20 (1) inayoruhusu Uhuru wa Kukusanyika.

Ni rai yetu kama chama cha ACT Wazakendo, Serikali na mamlaka zitachukua hatua madhubuti ili kulifanya Jeshi la Polisi kuwa ni huduma na linalojali utu sheria ya jeshi la polisi ifanyiwe marekebisho.

9. Ufinyu wa Bajeti kwenye eneo la Miradi ya Maendeleo
Katika mapitio ya Utekelezaji wa bajeti na makadirio ya mapato na matumizi kwa miaka ya 2019/20, 2020/21, 2021/22 na mwaka huu 2022/23. Tumeona uelekeo wa wizara kutotoa kipaumbele kwenye eneo la Miradi ya Maendeleo ambayo ina nafasi kubwa sana katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ya idara mbalimbali, nyumba za askari na mabweni ya wafungwa. Kwa mwaka wa fedha 2019/20 bajeti iliyotengwa ilikuwa shilingi bilioni 31.93 ambayo ni sawa na asilimia 3.46 ya bajeti nzima ya wizara. Kwa mwaka wa fedha 2020/21 bajeti iliyotengwa ilikuwa shilingi bilioni 38.29 ambayo sawa na asilimia 4.24. Pia, kwa mwaka wa fedha 2021/22 fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ilikuwa shilingi 27,470,000,000 sawa na asilimia 2.92.
Na mwaka huu fedha zilizotengwa ni kiasi cha shilingi bilioni 140.412 sawa na asilimia 11.58. Kwa miaka minne mfululizo bajeti ya miradi ya maendeleo haijafika asilimia 15.
Ili kukabiliana na changamoto tulizozioorodhesha ACT Wazalendo tunapendekeza wizara iweke angalau ya asilimia 20 ya bajeti ya kwenye miradi ya maendeleo.


10. Serikali illipe malimbikizo ya Madeni yenye thamani ya shilingi Bilioni 751
Taasisi tatu zilizo chini ya wizara ya mambo ya ndani zilipokea huduma na bidhaa kutoka kwa wakandarasi, wauzaji na watoa huduma. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG kwa mwaka 2020/21 madeni haya yamechukua muda mrefu kuanzia mwezi mmoja hadi 12, kuchelewa kulipwa kwa madeni haya kuna litia taifa hasara zaidi kutokana na ongezeko la riba inayosababisha kukua kwa deni lenyewe. Mchanganuo wa thamani ya madeni ni kama ufuatao; FUNGU 28 Jeshi la Polisi Tanzania ina daiwa shilingi 641.79, Idara ya Magereza ya FUNGU 29 bilioni 80.1 na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa bilioni 29.03

Bajeti ya wizara ya mambo ya ndani kwa mwaka wa fedha 2022/23 haijatenga hata kiasi kidogo tu cha kulipa madeni haya. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuzisimamia idara zote ziweze kulipa madeni kabla hayakuwa makubwa zaidi.


Mwisho, bajeti ya wizara ya mambo ya ndani ni muhimu itazamwe na wadau kabla ya kupitishwa leo, tunatumai kwa mtazamo huu mbadala itasiadia kwa kiasi kikubwa kuboresha bajeti ya mwaka huu na uelekeo wa vipaumbele.


Ndg. Mbarala Abdallah Maharagande
[email protected]
Msemaji wa sekta ya Mambo ya Ndani
ACT Wazalendo
06 Mei, 2022.

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK