HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MAZINGIRA ACT WAZALENDO NDG. ESTER THOMAS KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MAZINGIRA NA MUUNGANO KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MAZINGIRA ACT WAZALENDO
NDG. ESTER THOMAS KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MAZINGIRA NA MUUNGANO KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023

Utangulizi:

Jana Jumatano tarehe 27, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) amewasilisha bungeni hotuba ya makadiridio ya mapato na matumizi pamoja na malengo (vipaumbele) ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23. Katika kufuatilia hotuba hiyo, kama ilivyo kawaida ya chama cha ACT Wazalendo tumefanya uchambuzi wa mwenendo wa bajeti ya wizara hii kwa miaka mitatu mfululizo, tumetazama maeneo ya vipaumbele na kuangalia hali ya utekelezaji wa bajeti zilizopita na makadirio ya bajeti ya mwaka huu.
Vilevile, tumetazama utekelezaji wa bajeti kwenye maeneo ya miradi ya maendeleo. Pamoja na utangulizi huu, chama chetu kimeona kutofungamana kwa sekta ya Mazingira na Muungano kisera.
Kutokana na hali hiyo, Msemaji wetu wa Utumishi wa umma na Muungano, tarehe 26 April 2022 alitoa kwa mapana zaidi mtazamo wetu kuhusu suala la Muungano. Katika hotuba hii tumechambua maeneo muhimu sita (6) yanayogusa mazingira na maeneo ya Muungano, pia tumetoa mapendekezo yetu kuhusu mpango wa bajeti wa wizara ya Muungano na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2022-2023.

A: Mapitio ya hotuba sehemu ya Mazingira:

1. Utekelezaji wa Miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya Nchi kutegemea fedha za taasisi/mashirika ya nje.
Suala la uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi ni ajenda za kudumu kutokana na matokeo ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoweza kubadili maisha ya wananchi wetu kwenye sekta mahususi kama vile kilimo, maji, uvuvi na afya. Katika uchambuzi, tumeona kwa minne ya makadirio ya bajeti hauoni zikiakisi na kupewa kipaumbele kwenye eneo hili nyeti licha ya serikali kuweka mikakati mitupu.
Tunashangazwa sana licha ya kuwa Ofisi hii ya Makamu wa Rais inatambua uzito wa tatizo la mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa joto kali hadi kufikia nyuzi joto 36, upungufu wa mvua au mvua kubwa na za muda mfupi zilizosababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini, kuyeyuka kwa theluji ya mlima Kilimanjaro, kupungua kwa vina vya maji katika mabwawa, mito, maziwa, kuingia kwa maji chumvi katika nchi kavu/mashamba na vyanzo vya maji (kunakotokana na kuongezeka kwa kina cha bahari) na ukame unao jirudiarudia.
Bado kwa sehemu kubwa ya utekelezaji wa mikakati na jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi hutegemea zaidi fedha za wahisani au miradi ya mashirika ya nje, ambayo hatuna uamuzi nao wa moja kwa moja. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali yam waka 2020/21 inaonyesha miradi inayotekelezwa kwa kutegemea fedha za mashirika ya nje ni ifuatavyo;
• Mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza uhakika wa chakula katika maeneo kame Tanzania (LDFS) wenye thamani ya shilingi Bilioni 3.7 unao fadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
• Mradi wa usimamizi jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai. Mradi huo ni wa kipindi cha miaka 5 (2021 hadi 2026) na unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environment Facility – GEF) kwa gharama ya Dola za Marekani 11,205,872. Pia mradi wa uwezeshaji wa taasisi katika maswala ya hali ya Hewa na taarifa za hali ya hewa Kaskazini mwa Tanzania wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.125
• Mradi wa kujenga uwezo wa kitaasisi wa kutekeleza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Mradi huu ni wa miaka 3 (2020-2023) na unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.9 kwa ufadhili wa Serikali ya Sweden na Mradi wa kurekebisha Mfumo wa ikolojia vijijini Tanzania (EBARR) wenye thamani ya shilingi bilioni 1.21
• Mradi endelevu wa usimamizi wa ardhi kwenye chanzo cha ziwa nyasa wenye thamani ya shilingi milioni 292.62
Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu 2022/2023, tumeona mwendelezo ni ule ule wa Serikali kutoweka mkazo wa kibajeti katika kukabiliana na changamoto za tabia ya nchi, wanaweka maneno mepesi katika swala linalohitaji umakini na utaalamu. Hii ni hatari kwa mustakabali wa nchi yetu, wizara inapaswa kutenga bajeti inayotosha, kuungana na nchi nyine duniani ambazo zimeazimia na ziko kwenye juhudi katika kufanya mapambano haya kuwa endelevu na ya uhakika.

2. Utata wa uchunguzi wa uchafuzi wa mazingira katika Mto Mara
Tangu matokeo ya ripoti ya uchunguzi wa uchafuzi wa mto Mara ilipotolewa mnamo tarehe 19 Machi 2022, wananchi na wadau wa mazingira walijitokeza kujadili matokeo yaliyogubikwa na utata kutokana na kukinzana kwa taarifa ya uchuguzi ya awali na matokeo ya uchunguzi wa pili. Pia, ilionyesha wazi kuwa Serikali kupitia Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) inafanya mzaha na kuwakejeli wananchi walioatharika la uchafuzi wa Mto Mara. Tumefuatilia hotuba na vipaumbele vya Serikali kwa mwaka huu wa fedha, tumeona haijatoa uelekeo wala kipaumbele kwenye kushugulikia uchafuzi na athari zilizotokana na matokeo ya uchafuzi huo wa mazingira.
Sisi, ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza kuwa uchunguzi wa uchafuzi wa Mto Mara ufanywe upya na taasisi zingine huru, kwa kuwa tayari wananchi wameshapoteza imani na matokeo ya Serikali yenye utata mwingi.
Pili, tunaitaka Serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kutoa fidia kwa wananchi walioathirika na uchafuzi wa mazingira katika Mto Mara.
Tatu, hatubaliani na matokeo ya uchunguzi na mapendekezo yake hususani kuliingiza eneo la mto Mara katika orodha ya maeneo lindwa (protected areas).

3. Udhaifu wa Serikali katika kufuatilia ma kukagua maeneo ya miradi ya uwekezaji na mazingira ili kukabiliana na uchafuzi.
Serikali kupitia baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) kama msimamizi mkuu wa uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya usimamizi wa Mazingira limeonyesha udhaifu mkubwa sana kushughulikia changamoto za uchafuzi unaofanywa kwenye miradi ya viwanda, migodi, mabomba ya mafuta, mitambo ya gesi na mafuta, mitambo ya nishati za umeme, maghala ya kemikali na vyombo vya usafiri.
Katika hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilikiri kuwepo kwa changamoto za uchafuzi wa mazingira kwenye miradi mikubwa uchafuzi kama vile; kutiririsha majitaka kwenye mazingira ikiwemo vyanzo vya maji na makazi ya watu; Matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali kama misitu ya asili kwa ajili ya nishati na ujenzi; Ukosefu wa mifumo ya kuhifadhi taka ngumu; Uzalishaji wa hewa chafu; na Uzalishaji na usambazaji wa mifuko mbadala isiyokidhi viwango.
Serikali kupitia bajeti ya mwaka jana, iliahidi kushughulikia matatizo haya lakini bado tunaona hali hiyo ikiwa inaendelea tena kwa kasi zaidi, Serikali haijachukua hatua kali za kisheria na kuonyesha umma msimamo wake kupinga vitendo hivi hatari kwa mazingira.
Ipo mifano zaidi, magari ya usafirishaji wa kemikali yamekuwa na desturi ya kumwaga kemikali barabarani mfano maeneo ya Temeke Sandali. Hivi karibuni mnamo tarehe 6 April 2022 wananchi walilalamika kumwagika kwa kemikali aina ya Sulphur barabarani na kuathiri afya zao, na serikali ilikaa kimya bila kuchukua hatua zozote. Tumefuatalia mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/22 katika hotuba hii, hakuna mrejesho wowote wa ushughulikiaji wa suala hili.

4. Ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya mazingira
Kumekua na ucheleweshwaji wa kukamilika kwa miradi mbalimbali ya sekta ya mazingira, wakandarasi waliopewa mikataba. Hali hii inathibitishwa na ripiti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CA) mwaka 2020/21 inaonyesha kuwa mikataba yenye thamani ya Tsh. Bilioni 26.93 haikukamilika hadi tarehe ya kukamilika na hakuna fidia iliyotozwa kwa wakandarasi husika. Pia, CAG ameonyesha ucheleweshwaji wa mradi wa ujenzi wa udhibiti wa mafuriko na mifumo ya mifereji ya maji Gerezani wenye thamani ya Tshs 8,496,720,207 uliopaswa kuanza 1 julai 2019 – na kumalizika Septemba 2020 lakini haujakamilika mpaka leo na umechelewa kwa takribani mwaka mmoja.

5. Kasi ndogo ya matumizi ya Nishati mbadala
Nishati ni hitajio muhimu sana katika Maisha ya mwanadamu, kutokana na uhitaji huo inatoa msukumo mkubwa kwa uharibufu wa mazingira. Zaidi ya asilimia 85 ya wananchi vijiji wanategemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha Nishati ya kupikia majumbani. Huku Dar es Salaam ikitegemea kuni na mkaa kwa asilimia 78.2 na kutumia 70% ya mkaa wote unaozalishwa nchini. Kiwango cha ukataji wa miti kinakadiriwa hekta 372,000 kwa mwaka kiasi cha kutishia usalama wa misitu nchini.
Ukiangalia mipango ya bajeti tangu miaka ya 2016 hadi 2021, serikali ina taja kuhamisisha matumizi ya nishati mbadala kuwa ni eneo la kipaumbele kwenye wizara ya muungano na mazingira. Lakini, serikali haijaweka nguvu kuhakikisha matumizi ya kuni na mkaa yanaondoshwa kwa kuweka mazingira mazuri ya usambazaji wa gesi, kuharakisha mazungumzo na uwekezaji kwenye gesi asili ya Lindi, ambayo itashusha gharama za gesi kwa wananchi.
Pia, hadi sasa bado zipo taasisi za Serikali zinatumia kuni na mkaa kuwa ndio nishati ya kupikia, mathalani magereza, hospitali, shule na vyuo, kambi za jeshi kujenga taifa na kambi za mafunzo ya polisi.
Sisi ACT Wazalendo tuliweka wazi katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 katika kuhakikisha tunakuwa na nishati mbadala kuwa; “Serikali ya ACT Wazalendo itasambaza bomba la gesi majumbani kwa matumizi ya kupikia ili kupunguza gharama za kutumia umeme, kununua mitungi ya gesi na kuokoa mamilioni ya misitu inayopotea kila mwaka kwa matumizi ya kupikia majumbani.”
Hivyo, tunaitaka serikali isiishie kuweka kwenye hotuba tu mkakati wa kutumia nishati mbadala, badala yake iwekeze kwenye nishati ya jua, umeme wa maji, gesi asilia ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yana athari kubwa kwenye mazingira.
6. Uwekezaji na ujenzi wa miradi katika maeneo ambayo hayakufanyiwa tathmini ya athari za mazingira kimkakati.
Moja ya jukumu la Ofisi ya Makamu ya Rais ni kuhakikisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kutathmini na kukagua mazingira kabla kuanzisha miradi ili kujua athari za mazingira.
Katika kupitia taarifa ya utekelezaji wa wizara tumebaini kuwa miradi imeonekana kasoro kubwa katika usanifu na michoro ya maradi ya maendeleo ya mazingira katika miji ambayo haikidhi vigezo vya matumizi ya eneo husika na haizingatii hali ya hewa, vigezo vya kijani, pamoja na maswala ya afya usalama na mazingira.
Vilevile, kwenye ripoti ya CAG imeonyesha Miradi mingi ya maendeleo ya jamii haizingatii masharti ya misingi na athari za mazingira na jamii (ESIA). ''Katika kupitia tathimini ya athari za mazingira kwa jamii katika miradi minnee, nilibaini kuwa masharti ya msingi ya mazingira hayakuwakilishwa vizuri''.
Pia, ukiangalia barabara zetu nyingi ndani ya miji na kwingine kote haina mifereji ya kuhimili mafuriko kipindi za mvua kwenye kupitisha maji na mchanga , na pia haina miti wala bustani za miji ili kupunguza mmomonyoko wa udongo kwenye kingo za mito ambao ni moja ya ishara ya uharibifu wa mazingira.
7. Mifumo mibovu ya udhibiti wa taka nchini
Duniani kote, kiwango cha uzalishaji wa taka kimeonekana kikipanda kwa kasi sana, takwimu (Benki ya Dunia, 2019) zinaonyesha kwa mwaka uzalishaji wa taka katika miji mikubwa duniani unafikia tani bilioni 2.01. Kwa Tanzania, takwimu za taifa za mazingira (Ofisi ya Takwimu, 2019) zinaonyesha tunazalisha tani milioni 2.102 katika mikoa yetu Tanzania Bara. Lakini, tafiti hizo hizo zinaonyesha ni wastani wa asilimia 80 za taka ngumu zinazozalishwa maeneo ya miji yetu hazikusanywi na asilimia 60 ya taka hizo hutokea majumbani ambazo hukusanywa na kutupwa kwa kufukiwa, kuachwa wazi kwenye madampo au kuchomwa. Vitendo hivi huleta madhara makubwa kwa afya, usalama na mazingira. Uzagaaji wa taka hutumika kama mazalia ya vimelea vya magonjwa, huchangia mabadiliko ya hali ya hewa duniani kupitia uzalishaji wa methane, na zinaweza hata kukuza uchafuzi wa mazingira mijini.
Kwa namna hali ilivyokuwa mbaya, ipo haja ya kuwa na udhibiti na usimamizi mzuri wa mifumo yetu ya taka lakini Serikali haijafanya juhudi za kutosha kuwekeza kwenye ukusanyaji wa taka majumbani mfano, magari ya taka. Bado jamii nyingi huandaa majalala majumbani mwao na kuchoma taka jambo ambalo ni hatari kwa afya na usalama wa wananchi.
Tafiti zinaonyesha ili kupata ufanisi katika usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji wa taka kunahitaji bajeti ya kutosha, bajeti ya Serikali ya mwaka huu iliyotengwa kwa ajili ya usimamizi wa mifumo ya taka ni finyu sana.
B: Mapitio ya bajeti ya Muungano:
8. Mamlaka kamili ya Zanzibar na kero za Muungano
Kwa sababu ya kukosa dhamira ya kweli ya kisiasa, na muundo usiokidhi haja, Muungano umekuwa na matatizo mengi na mengine yakidumu kadri ya umri wa Muungano wenyewe. Muungano huu umekosa taratibu za kikatiba na kisheria za kutatua migongano, mivutano au uchukuaji wa madaraka unaofanywa na Serikali ya Muungano dhidi ya Zanzibar na kadhalika Zanzibar inapojitutumua kudai haki na stahiki zake katika Muungano ambazo hazitimizwi.

Miongoni mwa changamoto za Muungano ni kama zifuatazo;
• Zanzibar kutokuwa na Sauti Katika Uendeshaji wa Muungano, kutunga sera za mambo ya Muungano,
• Kukosekana kwa usawa na haki katika matumizi ya fursa na rasilimali ndani ya muungano.
• Mafao ya Zanzibar Katika Mapato ya Muungano kama yalivyofanyiwa uchambuzi na tume ya pamoja ya fedha
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania irejeshe malimbikizo yote ya haki za mapato ya Zanzibar kutokana na mapato ya ziada ya Muungano kama ilivyochambuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha.
Pili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurejesha Mamlaka stahiki kwa Zanzibar (Kodi, Fedha, na Ushirikiano wa Kimataifa)
9. Madeni ya Zanzibar kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Nchi yetu ni Muungano wa Nchi mbili, Zanzibar na Tanganyika, zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeelekeza kuundwe Chombo cha kusimamia Mapato yote ya Muungano ili yatumike kuendesha shughuli za Muungano zinazotajwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Ibara ya 134(1) ya Katiba hiyo imeanzisha Tume ya Pamoja ya Fedha. Vile vile, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria namba 14 ya mwaka 1996 ambayo inatekeleza kifungu hicho cha Katiba. Tume ilianzishwa mwaka 2003. Hata hivyo kanuni za kutekeleza sheria hiyo zilichelewa sana kutungwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliokasimiwa na serikali unaonyesha Zanzibar hutumia 2% tu ya Mapato ya Muungano (Mapato ya Muungano yanayokusanywa Zanzibar ) na Tanganyika hutumia 98% ya Mapato ya Muungano ( yanayokusanywa Tanzania Bara ). Utafiti huo ulitumia Bajeti za Serikali za kuanzia mwaka 1999 – 2004.
Kanuni ya kugawa fedha inaweza kuwa ama 4.5% ama 11%. Mgawo wa 11% wa Mapato ya Muungano ni kigezo cha hisa za Zanzibar wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaanzishwa mwaka 1965 kutoka East African Currency Board. Mgawo wa 4.5% unatokana na ushauri wa IMF na kupitishwa na Serikali ya Waziri Mkuu John Samwel Malecela mwaka 1994. Mgawo huu hutumika hivi sasa kugawa Misaada kutoka nje. Kwa kutumia mgawo wa 4.5%, Wastani wa Fedha zinazopaswa kuwa mgawo halali wa Zanzibar kwa miaka 9 iliyopita ni shilingi Bilioni 660 kwa mwaka tangu 2013/14 – 2021/2022. Kwa kutumia mgawo huu wa 4.5% Zanzibar inaidai Serikali ya Jamhuri ya Muungano Jumla ya Shilingi trilioni 5.94 kama mgawo wake wa Mapato ya Muungano yanayozidi Matumizi ya shughuli za Muungano.
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kufanya tathmini mpya ya mgawo na kulipa madeni yote inayodaiwa na Zanzibar.

HITIMISHO:
Jitihada za kupambana na uharibifu wa mazingira na utunzaji wake katika nchi yetu bado zina mapungufu makubwa katika kufanikisha azma ya kuweka mazingira salama na safi kwa weledi. Hii inaenda sambamba na udhibiti wa taka za aina zote, kuhakikisha miradi ya maendeleo inasimamia mazingira, usimamizi wa fedha na utunzaji wa mazingira, na utekelezaji wake, pamoja na utekelezaji wa Sera ya mazingira kama inavyoainishwa, na usimamizi wa sheria ya mazingira. Mazingira ni swala mtambuka linalohusisha takribani sekta zote za jamii chini ya wizara mbalimbali za serikali ambazo zinafanya kazi kwa kuingiliana mfano wizara ya maji, kilimo, utalii, uvuvi, madini, viwanda na biashara. Pia ipo haja ya Serikali kuungana na nchi nyingine duniani zinazochukua hatua za maksudi kulinda mazingira kwa kusimamia sera na sheria zenye malengo ya muda mrefu.
Ili Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uendelee kwa maridhio ya watanzania wote na amani idumu kwa vizazi vijavyo, ipo haja ya Serikali kuacha kufunika kero za Muungano kwa kuhakikisha kuna usawa kwenye maeneo ya muungano. ACT Wazalendo inaamini kwenye Muungano wenye haki, usawa na unaohakikisha maendeleo ya watanzania wote.

Imetolewa na:
Esther Thomas
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Mazingira
ACT Wazalendo
28.04.2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK