HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA UTAMADUNI, SANAA, UBUNIFU NA MICHEZO- ACT WAZALENDO NDG. WEBIRO S. WASSIRA KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2022/23.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA UTAMADUNI, SANAA, UBUNIFU NA MICHEZO- ACT WAZALENDO NDG. WEBIRO S. WASSIRA KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2022/23.

Utangulizi
Kufuatia taarifa ya utekelezaji wa mujukumu na mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2022/23 iliyowasilishwa leo tarehe 06 Juni, 2022 Bungeni na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohammed O. Mchengerwa (Mb.) ambapo itajadiliwa kwa siku moja pekee na hatimaye Bunge litaidhinisha jioni ya Leo. Sisi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tumeisoma, kuichambua na kuimulika ili kuona kwa namna gani inaakisi matarajio na matamanio ya wananchi na wadau wa sekta hii.
Aidha, kupitia uchambuzi wetu, tumeweza kutoa mapendekezo kuhusu maeneo ya vipaumbele ambayo tunaona yanafaa kuwa sehemu ya mipango na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka huu wa fedha na kwa miaka inayofuata. Katika kufanya hivyo, hotuba hii ya Msemaji wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa ACT Wazalendo Ndg. Webiro Wassira imebaba hoja sita (6) kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2022/23.
1. Ukosefu wa soko la uhakika wa bidhaa za sanaa ya ubumifu.
Katika nyakati tulizonazo kazi za ubunifu kama vile uhunzi, uchongaji, uchoraji, uvumaji na ubunifu wa mitindo ya mavazi ina mchango mkubwa sana katika kuinua maisha na vipato vya wanajamii. Uchumi wa kiubunifu una utajiri wa kibiashara na pia kiutamaduni. Uchumi wa sanaa ya ubunifu huchangia zaidi ya 6.1% kwenye pato la taifa la kimataifa (GDP), wastani wa kati ya 2% na 7% ya Pato la Taifa duniani kote. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN, 2021), tasnia za uchumi wa ubunifu huzalisha mapato ya kila mwaka ya zaidi ya dola za Marekani trilioni 2 na huajiri karibia watu milioni 50 ulimwenguni. Takriban nusu ya wafanyakazi hawa ni wanawake, na tasnia hii inaajiri watu wengi wenye umri wa miaka 15-29 kuliko sekta nyingine yoyote.
Mchango wa sekta hii, unasababisha Serikali duniani kote kujikita katika kukuza na kuendeleza uchumi wa kiubunifu kama sehemu ya mikakati ya mabadiliko ya kiuchumi na juhudi za kuhamasisha mafanikio na maisha bora. Hali ipo tofauti kwa Tanzania, Takwimu zinaonyesha kuwa Mwaka 2020, shughuli za kiuchumi za sanaa na burudani zilikuwa na ukuaji hasi wa asilimia 4.4 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 11.2 mwaka 2019 kutokana na Janga la Uviko 19. Huku Mchango wake katika Pato la Taifa umeendelea kuwa asilimia 0.3. Mchango wa sekta ya sanaa na burudani kwenye ajira ni asilimia 0.1 ya nguvu kazi iliyoajiriwa.
Hali ya uzalishaji wa kazi za sanaa kama vile filamu, muziki, uchongaji na ususi imekuwa ikiongezeka, ingawa bado kuna changamoto zinazoikabili tasnia hii ya sanaa. Pamoja na mchango wake katika jamii, bado nchini kwetu wasanii wa sanaa ya ubunifu hawatazamwi kwa jicho la umuhimu, wanakabiliwa na changamoto ya uhakika wa masoko ya kazi zao. Soko la ndani la bidhaa za sanaa za Kitanzania ni dogo kiasi cha kutokuwa na tija ya kuongeza kipato na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Wakati huo huo kuna fursa ndogo zaidi katika soko la nje.
Ndio maana Sisi, ACT Wazalendo tuliamua kutazama sekta hii kama ni sekta muhimu katika nchi yetu. Katika Ilani ya Uchaguzi 2020 tuliweka azma ya kuimarisha ubora na kutafuta soko la nje kwa kazi za ubunifu kama uhunzi, uchongaji, uchoraji na bidhaa zingine zitokanazo na kazi za mikono. Hii ingewezekana kwa kuweka mifumo mizuri ya kisera na uwekezaji katika soko la sanaa na michezo, Serikali yetu kupitia wizara husika itafanya uwekezaji wa kina kwenye kuimarisha, kuinua na kutengeneza ajira zenye tija zisizopungua laki tano kwenye soko la sanaa na buruduni na mnyororo wake wa thamani.

Aidha, kuna changamoto ya soko la uhakika kwa kazi za filamu. Kwanza, tunatambua jitihada zilizofanywa na kampuni ya Azam Media katika kuhakikisha soko kwa sekta ndogo ya filamu (tamthiliya), lakini bado ipo changamoto kubwa sana juu ya soko la uhakika kwa kazi za filamu.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kujenga kumbi za maonyesha ya sinema na kumbi za matamasha katika kanda za kusini (Mtwara), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mara, Mwanza), Kaskazini (Tanga na Kilimanjaro) na Magharibi (Kigoma na Rukwa) ili kupanua masoko na fursa kwa wasanii.
Pia, Kufanya shughuli za kukuza (promoting) na kutangaza kazi za sanaa za ubunifu za wasanii wanaochipukia kupitia Televisheni ya Taifa, Redio na Magazeti.
2. Usimamizi na mgawanyo wa mirabaha ya kazi za sanaa:
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia taasisi yake ya COSOTA ina jukumu la kusimamia masuala ya Hakimiliki katika kazi za sanaa na ubunifu ikiwemo kukusanya na kugawa mirabaha kwa wadau wa kazi hizo. Vilevile, taasisi hii ina jukumu la kutunza rejista za kazi, usanii na vyama vya watunzi, wasanii, wafasiri, watayarishaji wa sauti zilizorekodiwa na watangazaji na wachapishaji.
Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu juu ya usimamizi na mgawanyo wa mirahaba ya kazi za sanaa. Mambo yanayolalamikiwa ni pamoja na wasanii kutonufaika na mifumo ya mirabaha, kutokuwepo kwa ushirikishwaji wa wadau katika ukokotoaji wa manufaa yanayotokana na mirabaha. Aidha, mgawanyo wa mirabaha kutogusa makundi yote yanayobeba kazi za ubunifu (kwa sasa inatolewa kwa wanamuziki pekee). Pia, kukosekana kwa uwazi katika mchakato wa ugawaji wa mirabaha. Kwenye tangazo la ugawaji wa mrabaha lililotolewa mwezi Januari 2022, halikutaja kiasi cha mirabaha iliyokusanywa kati ya mwaka 2019 na 2021, na mirabaha hii bado haijagawanywa kama sheria inavyotaka.
Kutokana na malalamiko haya kutoka kwa wadau hususani wasanii wenyewe, ni wazi kuwa Serikali haitoi kipaumbele na umuhimu wa kumaliza malalamiko yanayotolewa na wadau wa sanaa. Katika, hotuba ya mwaka huu serikali haijajielekeza kuona namna itakavyoenda kukabiliana na changamoto hiyo ya muda mrefu. Serikali kila wakati inaahidi kushughulikia na kusimamia mirabaha ili kufanya mnyororo wa thamani ya kazi za sanii unawanufaisha wazalishaji na wabunifu, lakini katika utekelezaji hauoni matokeo yake.
ACT Wazalendo tuitaka Serikali kuwashirikisha wadau wote katika ukokotoaji, ukusanyaji na mgawanyo wa mirabaha ya kazi zote za ubunifu (hususani, muziki na filamu) ili kuwafanya wasanii kuelewa.
Aidha, Serikali iisimamie COSOTA ili kuhakikisha utendaji wake unaendeshwa kisheria, uwazi na ushirikishwaji, pia COSOTA iweke mkakati Madhubuti wa kutoa elimu ya Hakimiliki na hakishiriki za kazi za sanaa kwa wasanii na watunzi isisubirie wakati wa migogoro pekee.
3. Kutokuwepo kwa maktaba (Gallery) na kumbi za maonyesho ya sanaa za uchoraji, upakaji rangi, ufumaji na uchongaji.
Sanaa ya uchoraji, uchongaji, ufumaji na upakaji rangi ina kuwa kwa kasi sana nchi. Licha ya kukua huko bado wasanii hawa hawana fursa zilizoratibiwa na kuonyesha sanaa zao na kuhifadhi bidhaa zao ambao kila mtu au mteja atayetaka kuona au kununua kazi zao aweze kuwafikia kwa urahisi.
Kwa sasa wanafanyakazi kama sehemu ya burudani au kupata faida kidogo, soko kubwa wanalolitegemea ni watalii wageni (kutoka nje ya nchi). Maonyesho ya bidhaa yao kwa sehemu kubwa wanafanya katika makusanyiko ya semina za mafunzo, warsha, matukio na ghafla za kiserikali bila ya kuwa na jitihada za kitaasisi, wanafanya wasanii binafsi. Mwenendo huu unarudisha nyuma sanaa ya ubunifu.
Serikali, sambamba na kuanzisha kumbi za sinema na maonyesho ya sanaa za kuigiza ni muhimu kutoa fursa za kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya uhifadhi na maonyesho ya kazi za sanaa ya uchoraji, ufumaji, uchongaji na uhunzi.
4. Uendelezaji na ukuzaji wa sanaa na michezo kitaaluma
Sanaa na michezo huchukuliwa kuwa ni kimbilio la vijana na watu wengi kama sehemu ya kujipatia kipato. Pamoja ya kuwa wengi wa waliopo kwenye sanaa na michezo wamesukumwa na vipaji walivyonavyo. Uendelezaji wa tasnia hizi katika nchi yetu bado ni mdogo sana, wanajamii huchukulia michezo na sanaa kama mambo ya nyongeza katika shughuli za mwanadamu. Mchango wake katika Nyanja ya kiuchumi haujafahamika vizuri, ndio maana hata Serikali haichukulii michezo na sanaa kama chanzo muhimu cha kukuza na kuinua mapato ya nchi yetu (pato la taifa), kwa sasa huchangia kiasi kidogo zaidi cha wasatani wa asilimia 0.3 ya pato la taifa.
Hivyo, serikali haichukui juhudi za makusudi kuendeleza tasnia hizi mbili, mathalani kuna vyuo vikuu viwili tu viwavyotoa elimu ya shahada ya muziki na filamu (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma), vyuo vingine vinatoa ngazi ya astashahada na stashahada, TASUBA na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya. Idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwenye vyuo hivi hazidi wanafunzi mia sita kwa ngazi zote kuanzia astashahada, stashahada na Shahada ya kwanza.
Kwa hali ilivyo, ni wazi kuwa juhudi za kuendeleza tasnia ya sanaa na michezo ni ndogo sana, jambo ambalo linapelekea uzalishaji wa kazi za sanaa kuwa zenye viwango hafifu ukilinganisha na nchi zingine. Jambo pekee linaloifanya wasanii kuingia kwenye sanaa na michezo ni vipaji, jambo ambalo bila kuviendeleza vinapoteza ufanisi na tija.
Tunaishauri Serikali kuongeza vyuo vya sanaa vitakavyowaandaa wasanii na wataalamu wengi wenye ujuzi katika fani mbalimbali za michezo ili kuifanya tasnia hii kuwa ya kitaaluma na kukuza vipawa na vipaji vya wasanii na wanamichezo na kuongeza idadi ya udahili kufikia angalau wanafunzi elfu kumi kwa mwaka. Vilevile, Serikali kupitia bodi ya filamu na Basata iwe ina andaa programu za mafunzo kwa wasanii waliopo ili kukuza na kuendelea vipawa vyao.
Aidha, serikali itekeleze azma yake ya kuanzisha shule za michezo (Sports Academy) angalau kwa kuanzia shule tano (5) za kikanda kwa mwaka huu.
5. Mfumo hodhi wa soko la filamu na muziki, unaua vipaji, kunyonya wasanii na kuharibu ubora wa kazi za sanaa (Muziki na Filamu).
Tasnia ya kazi za ubunifu hususani muziki na filamu kwa muda mrefu imekuwa ikielezwa kwa namna gani inavyohodhiwa na watu wachache ambao kwa sehemu kubwa ndio uamua kazi za sanaa zinapaswa kuwaje. Wahusika wanaohodhi kazi za sanaa ni wale wanaohusika na usambazaji na urudufishaji (utengenezaji na uzalishaji) pamoja na waendeshaji na wamiliki wa vyombo vya habari (redio na runinga). Kama ilivyo dhana ya uhodhi (ukiritimba), wasanii wanalazimika kutayarisha kazi, kufuata utaratibu kulingana na sera (mitazamo, maamuzi na fikra) za Wafanyabiashara au vyombo vya Habari. Katika hali kama hii wasanii wengi wamekuwa wakinyonywa jasho lao kwa kuingia mikataba inayowanufaisha zaidi wafanyabiasha wakuzaji (promoters) kwa vigezo vya gharama ukuzaji wa majina.
Aidha, tatizo la ubora wa kazi za kibunifu linaathiriwa zaidi nchini Tanzania na mfumo wa soko hodhi. Muundo wa tasnia ya filamu na muziki nchini kwetu, umeparaganyika yaani badala ya kuanza na ubunifu kuelekea kwenye usambazaji, kwetu mfumo unaanza na usambazaji ili kupanga ubunifu. Kwa maneno mengine ni kuwa mitazamo, maamuzi na uzoefu wa Wafanyabiashara wa kazi za sanaa (wasambazaji) ndiyo yanayoongoza mchakato mzima wa utayarishaji uchukue sura gani- hivyo suala la ubora linapangwa na mfumo wa soko badala ya wazo (ubunifu).
Mfumo hodhi wa soko la sanaa unachagua nani aweje na sio kukuza vipaji na vipawa vya vijana, mfumo ndio unachagua kazi zipi zitangazwe hata kama zimefanywa kwa viwango visivyo na ubora. Upo Ushahidi wa kuwepo kwa makundi ya wasanii (filamu na muziki) kwa upande mmoja wapo wanaooneka kushikwa mikono na vyombo vya habari na wasambaji wa kazi za sanaa(“wasanii maarufu”) na kwa upande mwingine, wapo wasanii wasiopewa fursa sawa kusambazwa na kupigwa kazi zao kwenye vituo vya redio na runinga (watu wengine huwaita “wasanii marufuku”), jambo linalopelekea kuzia fikra na vipaji vipya au kuminya fursa kwa watu wengine walio nje ya mfumo huu hodhi.
Katika hali kama hii ukimya wa Serikali katika kuweka mikakati na hatua za kibajeti, inafanya kubariki mifumo inayoua vipaji na kukandamiza wasanii wa nchii hii. Serikali kupitia taasisi zilizo chini yake inao wajibu wa kuratibu, kusimamia sanaa na michezo ili kutoa fursa kwa watu wote kulingana na vipawa vyao.
ACT Wazalendo, tunaishauri Serikali kuanzisha Mamlaka ya tasnia za ubunifu (muziki na filamu) ili kuhakikisha kazi zinaendelea kutengenezwa na kusambazwa (kulifikia soko) kwa usawa.
6. Uhaba wa viwanja bora vya michezo na ukosefu wa maeneo ya mapumziko na burudani nchini.
Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 2009 inaonyesha umuhimu wa kukuza na kuendeleza michezo ni pamoja na ubora wa viwanja vya michezo. Hivyo, kwa mujibu wa sera hiyo, Serikali katika ngazi zake zote, kwa kushirikiana na wananchi inapaswa kuhakikisha kwamba vinakuwepo viwanja bora na vya kutosha na kumbi bora na za kutosha. Aidha Serikali, inatakiwa kusimamia utengaji wa maeneo maalumu kwa ajili ya viwanja vya michezo na kumbi mbalimbali.
Hali ilivyo sasa katika nchi yetu inasikitisha sana, Serikali na chama chake (CCM) imepora viwanja vya umma na maeneo yote ya wazi nchini. Viwanja vingi vilivyoporwa havijaendelezwa, vipo chini ya viwango (havina hadhi ya mashindano ya kimataifa. Upungufu wa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa unashusha thamani na hadhi ya michezo ya mpira wa miguu, pamoja na kupoteza fursa mbalimbali za kuandaa mashindano ya kimataifa. Kwa sasa tuna viwanja viwili pekee vinamilikiwa na serikali vyenye hadhi ya kimataifa (Uwanja wa uhuru na uwanja wa taifa wa Benjamin William Mkapa).
Aidha, miji yetu haina maeneo ya maalumu ya kwa ajili ya michezo na burudani kwa watoto na watu wazima. Maeneo mengi ya umma yamevamiwa na Serikali ya chama cha Mapinduzi imeyauza kwa wanaoitwa wawekezaji. Umma wa watanzania umekosa kabisa maeneo kwa ajili ya mapumziko, kufanyia mazoezi na kwa ajili ya kujiburudisha. Hatuwezi kukuza michezo katika nchi wakati hatuna maeneo kwa ajili ya michezo hiyo.
ACT Wazalendo katika Ilani yetu ya Uchaguzi 2020 tuliweka azma ya kurudisha serikali maeneo ya wazi yaliyoporwa, na kutenga maeneo mapya ya wazi kwa ajili ya michezo na mapumziko. Pia, ACT Wazalendo tuliahidi kuiingia ubia na vikundi vya wanawake na vijana katika kuhakikisha maeneo ya wazi yanatumika kwa ajili ya burudani, starehe pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana. Ni wakati sasa Serikali kuchukua mawazo haya ili kuinua hadhi ya sekta ya michezo kwa kuboresha viwanja vyetu vyote nchini.
Aidha, tunaishauri Serikali kuunda Mamlaka ya viwanja vya Michezo ili kujenga, kuendeleza na kutunza viwanja vya michezo kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi.
7. Maslahi na haki za wanamichezo nchini.
Sekta ya michezo ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa vikapu na ngumi imetoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri. Michezo hii sasa imefikia hadhi ya kuwa michezo ya kulipwa ambayo mchezaji hucheza kwa kulipwa chini ya mkataba maalumu ambao hukubalika kati ya mmilikaji na mchezaji. Kutokana na hatua ambayo Tanzania imeshafika katika baadhi ya michezo ya ridhaa hususani mpira wa miguu na ili kuweka misingi thabiti katika uendelezaji wa vipaji na maslahi ya wachezaji ni muhimu kuweka mfumo elekezi wa viwango vya malipo (Salary scales).
Wachezaji wa mpira wa miguu hususani timu za wanawake na timu ndogo zinazoshiriki ligi kuu wanalipwa viwango vidogo sana. Si ajabu kuwakuta wachezaji kwenye baadhi ya timu hawana uhakika wa kulipwa mishahara kwa mwezi licha ya kuwa kima cha chini cha mshahara kuwa kidogo zaidi, kwa maeneno mengine ni kuwa wachezaji wengi hawana mishahara inayoeleweka na yenye uhakika. Maslahi ya wachezaji hayapaswi kuishia kwenye kusimamia kupatikana kwa mikataba kwa kila mchezaji bali unapaswa kwenda mbali zaidi kwenye malipo ya haki na yenye kujikimu kimaisha kulingana na kazi hiyo.
Vilevile, kwa upande wa mabondia (michezo ya ngumi), kwa miaka ya hivi karibu kupitia Azam Media wamejitahidi kukuza na kutangaza mchezo wa ngumi na hivyo kupata ufuatiliaji na mashabiki wengi sana, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Pamoja na mafanikio haya madogo bado maslahi ya mabondia wetu ni madogo sana. Pamoja na maslahi haya, bado michezo hii haijafungamanishwa kwenye mifumo ya hifadhi ya jamii, wachezaji wanaweza kupata maradhi wao au wategemezi wao. Pia, michezo hii, huwa watu wanastaafu mapema hawana mfumo ya pensheni (Mafao ya uzee).
ACT Wazalendo tunapendekeza kuwepo kwa utaratibu wa kisheria wa kuwa na kima cha chini cha mishahara kwa wachezaji wote wazawa wanaoshiriki ligi kuu na mashindano mingine yenye hadhi inayofanana na ligi kuu bila kuathiri malipo ya bonasi na ushindani.
Aidha, Serikali kupitia vilabu vya mpira viweke utaratibu wa kuwaunganisha wachezaji na mfumo wa hifadhi ya jamii ili waweze kupata mafao ya uzee na matibabu wanapokutwa na majanga.
8. Ushiriki mdogo wa wanawake na watu wenye ulemavu kwenye michezo ya ngumi na mpira wa kulipwa.
Changamoto za kimila kongwe zinazokandamiza wanawake, zina mchango mkubwa kwenye kuamua ushirika wa wanawake katika sekta ya michezo hususani ngumi na mpira wa miguu. Historia inaonyesha kuwa wanawake wa Tanzania hawakuwa wakishiriki kikamilifu katika shughuli za michezo na mazoezi ya viungo, ushiriki wao huonekana kwenye kuhudhuria (kushangilia). Hata wale waliobahatika kucheza katika ujana wao kabla ya kuolewa, hujikuta wanalazimika kujitoa katika michezo mara wanapoolewa. Licha ya mabadiliko madogo tunayoshuhudia miaka ya hivi karibu takribani miongo miwili ya kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake kwenye mpira na ngumi.
Bado kama nchi, tunapaswa kuwekeza, kuendeleza na kuhamasisha zaidi wanawake waweze kushiriki. Michezo hivi sasa ni ajira, wanawake wengi wapo mtaani hawana ajira licha ya kuwa wanaweza kuwa na vipawa na vipaji.
Vilevile, kwa upande wa watu wenye ulemavu kutokana na hali yao wanaoneka hawana uwezo wa kushiriki kwenye shughuli za michezo. Tunaihasa Serikali Kuanzisha vyama vya michezo na mazoezi ya viungo kwa ajili ya wanawake; kutoa upendeleo wa makusudi kwa wanawake kushika nafasi za uongozi wa michezo aidha kupata nafasi za mafunzo na utaalamu katika Nyanja ya michezo
Hitimisho:
Hotuba ya bajeti ya wizara ya utamaduni sanaa na michezo, pamoja na ufinyu wake utengaji wa fedha unaelekezwa zaidi kwenye fungu la kawaida na matumizi mengineyo kuliko kwenye miradi ya Maendeleo. Kwa kufanya hivyo, uendelezaji wa sekta ya utamaduni na michezo kuwa hafifu sana. Wasanii na wanamichezo wanapiga hatua kwa jitihada zao wenyewe bila Usimamizi kutoka kwa Serikali. Ni muhimu kwa Serikali kuachana na utamaduni huu, michezo ni ajira na ina mchango mkubwa sana kwenye kutoa ajira na pato la taifa. Mapendekezo tuliyoyatoa katika kila hoja yanabeba azma ya kufanya mageuzi kwenye wizara hii.
Webiro Wakazi Wassira
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo- ACT Wazalendo
06 Juni, 2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK