Hotuba ya Ndg. Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo katika mazishi ya Maalim Seif Sharif Hamad

Ndugu Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar;

Ndugu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Ndugu Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;

Ndugu wanafamilia, waombolezaji wenzangu, mabibi na mabwana.

Assallaam Alleykum!

Ndugu waombolezaji wenzangu;

Tarehe 17 Februari, 2021 imeingia katika moja kati ya siku za huzuni kubwa kwa Taifa letu la Tanzania. Ilikuwa ni siku ya simanzi kwa wananchi wote wa Tanzania hususan wananchi wa Zanzibar. Ni siku ambayo iliiacha Zanzibar na simanzi kubwa kwa kuondokewa na mwana mwema wake, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Msiba huu sio tu ni msiba mkubwa kwa Zanzibar, bali pia ni msiba mkubwa kwa Chama chetu cha ACT-Wazalendo na wapigania demokrasia wote kote nchini na nje ya mipaka ya nchi yetu. Hakika hili ni pigo kubwa sana!

Ndugu waombolezaji wenzangu;

Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa ni baba wa demokrasia ya vyama vingi nchini; mlezi wa vijana wanaochipukia katika siasa za vyama vingi; muumini mkubwa wa ustawi wa wananchi wa Zanzibar na mpambania haki za wananchi wote bila kujali itikadi, mbari au imani zao.

Kwetu sisi ACT-Wazalendo, tumempoteza mtu muhimu sana katika malezi ya kisiasa na mshauri wetu mahiri. Tumempoteza mshauri na mpatanishi kwenye vikao vya chama chetu na mtu aliyetupa ujasiri mkubwa wa kusonga mbele hata pale ambapo tulikaribia kukata tamaa kutokana na madhila na mazingira magumu ya kisiasa katika siku za hivi karibuni.

Kila tulipokaribia kukata tamaa au kukatishwa tamaa, tumekuwa tukijikumbusha mapito magumu aliyoyapitia Maalim Seif Shariff Hamad katika mapambano ya kudai haki, heshma na ustawi wa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kila tulipojikumbusha mapito ya Maalim Seif Shariff Hamad,tunajiona bado tunayo nguvu kubwa ya kusonga mbele zaidi katika mapambano ya kudai haki na ustawi wa wananchi wenzetu.

Madhila yote aliyopitia, miaka yote aliyotumikia jela, kejeli zote alizofanyiwa, uongo wote aliozushiwa na hila zote alizofanyiwa; Maalim Seif Shariff Hamad, aliendelea kusimama imara na kutetea haki za wananchi. Hakika, Maalim alikuwa kioo na kiigizo chetu kisiasa!.

Ndugu waombolezaji wenzangu;

Pamoja na ajali mbalimbali za kisiasa alizokutana nazo wakati wa uhai wake, Maalim Seif Shariff Hamad, hakuwahi kukata tamaa, kuyumba wala kuyumbishwa katika jambo aliloliamini, yaani HAKI. Badala yake alisimama imara na kusonga mbele. Leo hii tunapojumuika kutoa heshma zetu kwa nguli huyu wa siasa za nchi hii, ni kwa heshma ya misingi aliyoisimamia, yaani HAKI na ustawi wa wananchi. Kama tunayo namna bora zaidi ya kumuenzi Maalim, basi ni kusimamia haki sawa kwa watu wote! na kupambania ustawi wa wananchi wenzetu.

Aliyaishi maneno yake aliyoyasema mwezi Desemba mwaka 1987 katika viwanja vya Tibirinzi Pemba kwa miaka 34 mpaka umauti ulipomkuta. Aliwaambia Wazanzibari “Nipo nanyi sasa hivi, ninawaahidi kuwa nitakuwa nanyi nikiwa ndani ya Serikali au nje ya Serikali. Nitakuwa nanyi nikiwa ndani ya chama au nje ya chama”. Kwa miaka 34 tangu atamke maneno haya hajawahi kuwa mbali na wananchi. Hivi leo tunampumzisha, simanzi ya Taifa zima la Zanzibar ni ushahidi kuwa huyu ni mtu wa Watu, Mtu wa maneno yake.

Hakuna maneno yanayotosha kumwelezea Maalim kwani Maalim ni zaidi ya maisha. Ni mpigania uhuru wa zama za sasa ambaye aliamini katika Uhuru kama msingi muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania. Alikuwa mjuvi wa maneno lakini pia wakati mwengine alikuwa zaidi ya maneno. Alichukua hatua ilipobidi.

Maalim Seif Sharif Hamad aliipenda sana nchi yake, alipenda amani na zaidi ya yote aliishi kwa Amani! Kinyume na nadharia zilizojengwa na baadhi ya watawala wa Afrika kuhusu vyama vya upinzani kwamba eti vinavuruga amani; Maalim Seif Shariff Hamad aliwafundisha watawala hao somo la amani kwa vitendo.

Maalim alikuwa tayari kusamehe baadhi ya mambo ambayo katika hali ya kawaida yasingesameheka, lakini kwa mapenzi yake kwa wananchi na kwa amani ya nchi yake, alilazimika kusamehe na kusonga mbele.

Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa na kifua kipana chenye uwezo wa kutunza mambo yote, mema kwa mabaya. Kutokana na uwezo wake huo aliojaaliwa na Maulana, aliweza kufanya maridhiano bila kikwazo. Yote hii ilitokana na mahaba yake makubwa kwa wananchi wenzake na zaidi ya yote kwa nchi yake. Ni mwanasiasa ambaye amefanya ama Miafaka au Maridhiano na kila Rais wa Zanzibar tangia Mfumo wa Vyama vingi uanze hapa nchini. Huyu ni Nguzo ya Zanzibar iliyoridhiana na Zanzibar yenye maridhiano kwa hakika ni Zanzibar yenye Maendeleo.

Ndugu waombolezaji wenzangu;

Waliomwona Maalim kwenye runinga au kusikia sauti yake kwenye radio alivutia na kuhamasisha. Tuliokaa naye kwenye vikao, kuishi naye, kupata ushauri wake, kusikiliza simulizi zake za maisha na uzoefu wake alivutia zaidi na kuhamasisha zaidi. Hapatakuwa na Maalim mwengine. Hakuna Mtu ambaye tutasema huyu ndiye Maalim ajaye. Hakuna. Lakini Maalim alifundisha uongozi. Alifunda Viongozi.

Ametuachia wosia mahususi wa namna gani ya kuendeleza harakati za kuimarisha demokrasia na kuhimiza maridhiano.

Siku moja kabla ya kukutwa na tatizo lililosababisha umauti wake nilizungumza na Maalim Ofisini kwake. Pamoja na mambo mengine, alinisisitiza sana kuhakikisha kuwa vyovyote iwavyo Chama chetu kinakuwa mstari wa mbele kuimarisha maridhiano. Sikujua kumbe alikuwa ananiaga. Nafahamu kuwa siku hiyo alikutana pia na Mawaziri wawili wa Serikali ya Zanzibar. Sijui wenzangu hao wosia wao ulikuwa nini.

Kwa hakika mwisho wa Maalim duniani sio mwisho wa mawazo na fikra zake bali ni mwanzo wa kutekeleza maono yake kwa aina ya Zanzibar aliyopenda kuijenga pamoja na Wazanzibari wote.

Tunapojiandaa kumpumzisha Maalim Seif Shariff Hamad jabali la siasa za Zanzibar, tunayo matumaini makubwa sana kwamba maono yake ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika yatatimia muda si mrefu sana kutoka sasa. Aidha, umoja wa kitaifa utaendelea kuenziwa na haki kwa kila Mzanzibari kutolewa bila ubaguzi.

Sisi ACT-Wazalendo tutaendelea kutoa mchango wetu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuhakikisha ndoto ya Maalim Seif Shariff Hamad ya kuleta ustawi wa Zanzibar, Haki kwa Wazanzibari na Umoja wa Wazanzibari haizimiki.

Kwangu mimi binafsi sina maneno ya kueleza kwa heshima hii niliyopata ya kumsitiri Mzee wangu. Kwamba katika maisha yake yote ya kisiasa Maalim amenipa nafasi ya kumzika ni wajibu mkubwa ambao nimepewa na naupokea wajibu huu kwa unyenyekevu mkubwa.

Nawahakikishia Wananchi kwamba “Nilikuwa nanyi nikiwa na Maalim, NINAWAAHIDI kuwa nitakuwa nanyi baada ya Maalim. Nitakuwa nanyi Chama chetu kikiwa ndani ya Serikali au Nje ya Serikali. Nitakuwa nanyi kuimarisha chama chetu na kuitetea Zanzibar muda wote popote In Sha Allah”.

Nimalizie maelezo yangu kwa maneno ya Allah katika Aya ya mwisho ya Surat Yasin FASUBHANA LADHI BIYADIHI MALAKUUTU KULLI SHAYN WALAIH TURJAUUN.
“Basi ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu;na kwake yeye atarejeshwa”

Inna Lillah, Wainna Illahi Rajjiuun;

 

Zitto Kabwe
Kiongozi wa Chama
18 Februari, 2021.
Zanzibar.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK