Hotuba ya Waziri Kivuli wa TAMISEMI na Maendeleo Vijijini wa ACT Wazalendo Ndg. Kulthum J. Mchuchuli kuhusu Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Hotuba ya Waziri Kivuli wa TAMISEMI na Maendeleo Vijijini wa ACT Wazalendo Ndg. Kulthum J. Mchuchuli kuhusu Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Utangulizi.
Ijumaa, tarehe 14 April 2023, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ndg. Angellah Jasmine Kairuki (Mb) aliwasilisha Bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24. ACT Wazalendo katika mwendelezo wake wa kuisimamia Serikali, kupitia Waziri Kivuli wa Sekta ya TAMISEMI na Maendeleo vijijini imefuatilia, imeisoma na kuichambua hotuba hiyo kwa lengo la kumulika na kutazama kwa kiasi gani inakidhi matarajio na matamanio ya wananchi katika kupata huduma na usimamizi wa rasilimali zao. Kupitia uchambuzi huu tunaonyesha maoni yetu kwenye maeneo saba (7) yenye mtazamo mbadala wa ACT Wazalendo kuhusu Hotuba ya Bajeti ya TAMISEMI, ambayo tunaona ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu na wananchi walio wengi.
Maeneo saba (7) ya uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara ya TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

1. Mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
Kwa miaka mitatu mfululizo mwenendo wa bajeti ya Wizara kwa ujumla wake inaonekana ikiongezeka kitakwimu. Kwa mwaka wa fedha 2021/22 bajeti iliyoidhinishwa na Serikali ilikuwa ni Shilingi Trilioni 7.6, mwaka 2022/23 bajeti ya Wizara ilikuwa shilingi Trilioni 8.5 na mwaka huu Wizara imeomba kuidhinishiwa na Bunge Shilingi Trilioni 9.1. Ingawa kumekuwa na ongezeko la kibajeti kila mwaka, katika mapitio yetu ya utekelezaji wa bajeti tumebaini kuna maeneo mengi hayatekelezwi vizuri. Maeneo hayo ni kama yafuatayo;

1.1 Kushuka kwa makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 Halmashauri ziliwekewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 1.01 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani. Hadi Februari, 2023 Halmashauri zimekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 625.31 sawa na asilimia 62 ya makisio kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/23. Mwenendo wa makusanyo haya ni anguko la asilimia 9 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi Bilioni 615.61 kati ya Shilingi 863.85 (ambayo ilikuwa ni asilimia 71 ya lengo) yaliyokusanywa kwa kipindi kama hiki katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22. ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali kuzuia mianya ya upotevu wa mapato na udanganyifu wa baadhi ya watendaji kwenye Halmashauri zetu ili kuzisaidia kufikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato yaliyowekwa.

1.2 Ufisadi mkubwa kwenye fedha za madarasa ya UVIKO 19
Katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliidhinishiwa fedha za nyongeza ya Shilingi bilioni 512.14 kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO - 19 (TCRP). Kati ya fedha hizo asilimia 90 zilielekezwa kwenye sekta ya Elimu kwa ajili kujenga miundombinu ya madarasa na vyoo vya shule. Wakati tunafuatilia utekelezaji wa bajeti kwa miaka iliyopita tumesikitishwa sana kuona kuwa fedha hizi zimekuwa na matumizi mabaya. Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/22 matumizi mabaya yamejionyesha kwenye maeneo kadhaa.
Mosi, Madarasa 138 yaliyojengwa katika Halmashauri za Wilaya 10 yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.2 yalikua hayatumiki hadi kufikia mwezi Disemba 2022.

Pili, CAG ameonyesha kuwa Halmashauri 36 nchini zimezidisha manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa madarasa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.02 ili watumishi wajinufaishe binafsi.
Tatu, vyumba vya madarasa 1,213 kiti ya 15,000 vilivyojengwa na fedha ya Mkopo wa UVIKO 19 havitumiki kutokana na kutokuwa na viti, madawati na meza. Mahitaji ni madawati 752, meza na viti 33,849 kutokana na mkandarasi kutotimiza vigezo vyake.
Nne, Halmashauri zimeongeza gharama za manunuzi ya vifaa vya ujenzi kwa shilingi bilioni 2.74. Hili tuliliona kwenye Halmashauri nyingine Wakurugenzi wakishiriki njama za kupandisha bei za vifaa kama vile saruji, bati na nondo. Hoja nyengine zinahusu kutofuatwa kwa sheria za manunuzi na usimamizi wa fedha ambazo kwa ujumla wake zinafikia thamani ya Shilingi bilioni 91.
ACT Wazalendo kwenye hoja hii ya matumizi mabaya ya fedha za mkopo katika ujenzi wa madarasa, tunarudia wito wetu kuwa hatua kali zichukuliwe kwa wasimamizi na maafisa masuuli wote kwenye Halmashauri zilizotajwa na ripoti hii.

1.3 Kucheleweshwa kwa ujenzi wa miundombinu ya Elimu na Afya
Katika taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2022/23 Waziri wa TAMISEMI ameonyesha hatua zisizorisha za utekelezaji wa baadhi ya miradi ya Miundombinu ya elimu na afya. Kutokana na uchambuzi wetu miradi hii imekuwa na hatua zisizoridhisha.

 Mradi wa nyumba za walimu: Serikali iliidhinishiwa bajeti ya Shilingi bilioni 55.57 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 809. Lakini hadi mwezi Februari, 2023 Wizara imepokea kiasi cha Sh. Bilioni12.4 tu ambayo imefanikisha kujenga nyumba 170, sawa na asilimia 21 tu.

 Matundu ya vyoo; Serikali ilipanga kujenga matundu 9,700 yenye thamani ya shilingi bilioni 10.37 katika vituo shikizi. Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri, imekamilisha kujenga matundu 576 pekee kwa muda wa mwaka mzima sawa na asilimia 5 pekee. Huku fedha zilizopokelewa ni Shilingi bilioni 5.45

 Ujenzi wa vyumba vya madarasa; Serikali ilipanga kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 1,911 kwa thamani ya Shilingi bilioni 23.2 lakini hadi kufikia mwezi Februari 2023 ni vyumba 404 pekee ndio vimekamilika.

 Programu ya Maji na Usafi wa mazingira (SRWW); Serikali ilipanga kutumia shilingi bilioni 53.38 kwa ajili kujenga vyoo katika vituo vya afya ukarabati wa majengo ya kujifungulia, miundombinu ya kunawia mikono, ujenzi wa visima vya maji na mashimo ya kondo la nyuma (Placenta Pit), kichomea taka na ujenzi wa matundu 6,634 ya vyoo katika shule za msingi 446. Lakini wizara imepokea Shilingi bilioni 23 tu.
Ni wazi kucheleweshwa kwa miradi hii huleta athari zaidi kwenye upatikanaji wa huduma za elimu na afya. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali isimamie kwa ukaribu utekelezaji wa miradi na kutoa fedha kwa wakati.

1.4 Ufinyu wa bajeti ya Elimu bila malipo kwa shule za msingi na Sekondari
Katika uchambuzi wetu wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 tulieleza kuwa nia ya Serikali ya kutoa elimu bila malipo kuanzia shule za msingi hadi sekondari ni nia njema inayopaswa kuungwa mkono. Na tuliweka wazi kuwa kisera sisi, ACT Wazalendo tunaona ni muhimu kwa Serikali kugharamia elimu kuanzia shule ya awali hadi Chuo Kikuu (shahada ya kwanza) ili kuondoa kikwazo kwa watoto wanaotoka kwenye familia masikini katika kupata elimu.
Lakini, utekelezaji wa Sera ya Elimu bila malipo ulioanza tangu mwaka 2016 licha ya kuwa na mafanikio ya kuongeza maradufu uandikishaji, utekelezaji wake umekuwa na changamoto za kibajeti. Katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23, Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliidhinishiwa jumla ya Shilingi Bilioni 346.49 kwa ajili kugharamia programu ya Elimu Msingi na Sekondari bila ada. Lakini hadi kufikia Februari, 2023 Shilingi Bilioni 235.75 zimepokelewa sawa na asilimia 68.04. Kusuasua kwa kutolewa kwa fedha hizi, kunaathiri uendeshaji wa shughuli muhimu za kuboresha elimu yetu.
Aidha, ruzuku ya uendeshaji (Capitation grants) kwa shule ni finyu sana. Viwango vilivyowekwa na Serikali kama ruzuku ambayo ni shilingi 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na shilingi 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kama ruzuku vimepitwa na wakati kutokana na uhalisia wa maisha na mabadiliko ya thamani ya shilingi kwa dola.
Hivyo, ni wazi kuwa ufinyu na ucheleweshwaji wa utekelezaji wa bajeti unaathiri kiwango cha ubora wa elimu na taaluma kwenye shule nyingi kutokana na kukosa uwezo wa kutimiza mahitaji muhimu ya kutoa elimu bora kama vile ukarabati wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na nyenzo za kujifunzia. Ndio maana tunaona kuibuka kwa wimbi kubwa la michango inayo elekezwa kwa wazazi kwenye shule mbalimbali nchini. Wazazi wanachangishwa fedha kwa ajili ya mitihani, vitabu, chakula, walinzi, ukamilishaji wa madarasa na kadhalika. Ni dalili za wazi ruzuku na bajeti ya Serikali haijitoshelezi kufikia lengo la kutoa elimu iliyo bora bali ni bora elimu.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza kiwango cha ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kwa kiwango cha shilingi 25,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Shilingi 58,000 kwa mwanafunzi wa sekondari. Aidha, Serikali ilipe fidia ya ada na michango mengine ili kuwezesha uendeshaji wa shule kwa kuwa tathimini zinaonyesha ruzuku hii haikutokana na tathimini ya gharama halisi za uendeshaji.

1.5 Usimamizi wa wajibu wa Makampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility)
Kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na. 12 ya mwaka 2002 imeweka miongozo ya kufuatwa na kampuni zinazofanya biashara na miradi nchini Tanzania kutenga fungu la wajibu wa kampuni kwa Jamii, katika nchi ya Tanzania kuna miradi mengi inaendelea lakini makampuni mengi hayatengi mafungu kama hayo. Hii ni kutokana na kuwa kuna kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa sheria kwa viongozi na watumishi katika nchini yetu.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo Miradi inaibuliwa na Kamati za Maendeleo za Jamii (Community Development Committee - CDC) na kupitiwa na Vijiji, Mitaa na Kata na kuwasilishwa Halmashauri na Mikoa kwa ajili ya uchambuzi na hatimaye Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi na kuridhiwa.
Katika ufuatiliaji wetu tumebaini kampuni nyingi hazitekelezi Sheria hii na jamii zinazopitiwa na miradi mbalimbali hazinufaikii ipasavyo na miradi hiyo huku faida kubwa ikiondoka bila kuacha athari chanya kwenye maeneo yao. Katika mpango wa bajeti wa Wizara 2023/24nSerikali imetaja baadhi tu ya makampuni makubwa ya Madini tu, lakini huu ukweli nusu juu ya Usimamizi wa Serikali kuhusu wajibu wa kampuni kwa jamii. Pia tumeona kuwa miradi hiyo sio shirikishi kwa jamii, moja ikiwa sababu ya wigo usio mpana.

Mathalani, katika ripoti ya CAG kwa miaka miwili inaonyesha kitendo cha Serikali kushindwa kuisimamia Kampuni inayojenga Bwawa la kufua umeme la Mwl. Nyerere- Rufiji kutoa mchango wa wajibu kwa jamii tunavyopata hasara kubwa. Kupitia Mradi huu tu Kampuni inatakiwa kutoa Shilingi Bilioni 270, ni fedha nyingi sana kuziacha zipotee tu ambazo ni zaidi ya robo ya makusanyo yote ya Halmashauri nchini.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kufanya mapitio ya sheria hiyo na kuweka kiwango maalum cha wajibu wa Kampuni kwa Jamii kwani jambo hili ni matakwa ya kisheria na sio hisani ya makampuni kwa jamii na kupanua wigo wa ushiriki wa makampuni yanayo wekeza nchini.

Pili, tunaitaka Wizara ya TAMISEMI kufuatilia na kutekeleza miradi yote kikamilifu kwa wakati wa miradi yote ya maendeleo inayotokana na Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (CSR)
Mwisho, tunaitaka Serikali kuishirikisha jamii inayohusika juu ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za CSR ili miradi inayotekeleza iwe na tija kwao na wajue thamani wanayopewa na makampuni, hii itasaidia kupunguzwa ubadhilifu kutoka ka baadhi ya watendaji na pia wenyeji kuwa walinzi wa miradi hiyo.

1.6 Ununuzi wa Magari kwa ajili ya Viongozi
Katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24, Ofisi ya Rais -TAMISEMI imetengewa Shilingi Bilioni 16.58 kwa ajili ya ununuzi wa magari 81 katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Sisi, ACT Wazalendo tunapinga maamuzi haya ya ununuzi wa magari ya kifahari kila mwaka. Wakati, ripoti ya ukaguzi ya CAG inaonyesha kuwa Mikoa 15 imelipa kiasi cha Bilioni 4.9 kwa ajili kuagiza magari lakini bado hajafika hadi tarehe ya ukaguzi na Halmashauri 29 zilimetumia kiasi cha bilioni 5.68 kuagiza magari ambayo hayajawasilishwa katika Halmashauri husika kwa muda usiopungua mwaka mmoja tangu malipo kufanyika. Sasa, Serikali badala ya kusimamia gari zilizoagizwa ziwasili wao watenga fedha zingine kuagiza magari mapya. Huu ni ufujaji wa fedha za umma.
Aidha, Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango iliagiza kupunguza matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi wa Serikali, lakini mpango huu unaonekana unaenda kinyume na kauli ya Serikali yenyewe. Wakati wananchi wanapiga kelele juu ya ubadhirifu wa fedha zao, bado TAMISEMI inaendelea na ufujaji wa fedha za umma?

2. Kukithiri kwa upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari
Tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari za umma linazidi kukua kutokana na jitihada ndogo za Serikali kuajiri. Katika uchambuzi wetu wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 tulieleza masikitiko yetu makubwa juu ya mwenendo usioridhisha wa Serikali katika kuajiri walimu ukilinganishwa na mahitaji. Bado tunaona Serikali imeamua kupuuza vilio vya wadau mbalimbali ili kuboresha elimu ya nchi hii.

Katika mwaka wa fedha 2022/23 aliyekuwa Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Innoecent Bashungwa aliliiambia Bunge kuwepo kwa upungufu wa walimu kwa shule za msingi kwa kiasi cha walimu 100,958 sawa na asilimia 36.7 ya mahitaji ya walimu 274,549 ambapo waliokuwepo ni 173, 591. Kwa upande wa sekondari kulikuwa na upungufu wa walimu 74,743 ikiwa mahitaji ni walimu 159,443 sawa na asilimia 46.7. Jumla ya upungufu wa walimu kwa shule za msingi na sekondari kwa mwaka jana (2022)

ulikuwa walimu 175,701.
Hali imeendelea kuwa mbaya zaidi hata kwa takwimu za mwaka huu, ambazo zinaonyesha upungufu wa walimu 186,325 kwa shule za msingi sawa asilimia 51.44 (mwaka jana ilikuwa asilimia 36.7) na upungufu kwa sekondari ni walimu 89,932 sawa na asilimia (51.5) ikilinganishwa na mwaka jana upungufu ulikuwa wa asilimia 47. Vilevile, mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa Shule za Msingi ni walimu 4,462 ambapo waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,945 sawa na asilimia 66. Kwa sasa, inafanya upungufu wa walimu kufikia walimu 279,202 kwa ajili ya shule za msingi, sekondari na zile za mahitaji maalum.
Lakini, inashangaza sana licha ya kuwa na mahitaji makubwa ya walimu mikakati ya ajira ya Serikali haiendani na upungufu mkubwa uliopo.

Mwaka wa fedha 2022/23 Serikali iliajiri walimu 9,800 tu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari na mwaka huu imeweka mikakati ya kuajiri walimu 13,000. Kwa mwenendo huu Serikali inatuambia kuwa itachukua zaidi ya miaka 20 kumaliza tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari ambao ni walimu 279,202.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza idadi ya ajira za walimu kwa mwaka hadi kufika walimu 30,000. Pia, Serikali irudishe utaratibu wa kutoa ajira za moja kwa moja za walimu kila mwaka. Wakati kuna vijana wengi sana takribani 123,000 waliohitimu ngazi mbalimbali waliosomea ualimu hatupaswi kusumbuliwa tena na tatizo la upungufu wa walimu katika shule zetu.

3. Kukosekana kwa Mazingira mazuri ya wafanyabiashara wadogo (Wamachinga).
Wizara ya TAMISEMI ina wajibu wa kuratibu shughuli za wajasiriamali na wafanya biashara wadogo. Sekta ya biashara na huduma imekaliwa kwenye sehemu kubwa na wafanya biashara wadogo maarufu kama Wamachinga. Kutokana na umuhimu wake katika kuajiri vijana wengi jambo hili ilipaswa kupewa kipaumbele na kuwekewa mazingira mazuri ili sekta iweze kukua na kuimarika. Lakini, tangu mwezi Julai 2021, tumeshuhudia kadhia kubwa inayo wakumba wafanya bishara wadogokufukuzwa maeneo ya miji, kubomolewa kwa vibandavyao, kuchomwa moto kwa vibanda na kuungua kwa masoko. Aidha, Serikali imesitisha kabisa mpango wa kuwatambua Wamachinga kama ilivyo ahidi kupitia Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Tamisemi katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2021/22

Mazingira ya wafanyabiashara wadogo (wamachinga, mamalishe, na wajasiriamali wengine) bado hayajawekewa mkakati wa kuondoa changamoto zao. Licha ya sekta ya biashara ndogo kuwa na mchango mkubwa sana nchini kwenye pato la taifa wastani wa asilimia 22 na mchango wake kwenye sekta ya ajira ni wastani wa asilimia 14 ya nguvu kazi nchini zinapatikana kwenye biashara ndogo.

Hali ya sasa wafanyabiashara hawaonekani wakilindwa kisheria au shughuli zao kutambulika kama halali kwenye mchango wa uchumi wetu. Kwa, kifupi wafanyabiashara wadogo hawachukuliwi kama injini ya maendeleo ya miji na majiji. Uamuzi wa kuwapanga wafanya biashara wadogo umetikisa uaminifu wao kwa taasisi za kifedha. Matukio kupunga ya moto kwa wafanyabiashara wadogo yamesababisha hasara kubwa sana kwa wafanya biashara.
Tunaitaka Serikali kusitisha operesheni za mara kwa mara kuwaondosha Wamachinga badala yake iwe na mipango ya miji itakayozingatia mahitaji ya makundi yote nchini, Wamachinga na Wafanya biashara wakubwa. Aidha, ujenzi wa miundombinu ya mbalimbali kama vile barabara mijini izingatie mahitaji ya Wamachinga.

4. Uhaba wa miundombinu katika Elimu ya msingi na sekondari
Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa bado kuna uhaba mkubwa sana wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari za umma, hususan linapokuja suala la vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, madawati, vitabu vya kiada na vyoo. Uhaba huu unapelekea kuwa na mazingira magumu ya kufundishia na kujifunzia na hivyo kushusha viwango vya ubora wa Elimu.

Hali ya upungufu wa miundombinu kwenye shule za umma inathibitishwa pia na tafiti, kwa mujibu wa takwimu za elimu (BEST), 2019; ni kwamba, kulikuwa na jumla ya matundu ya vyoo 175,732 kwa shule za msingi nchini. Kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo, wavulana 60 wanalazimika kutumia tundu moja la choo (1:60), ambapo uwiano unaotakiwa ni wavula 25 kwa tundu moja la choo (1:25). Wakati wasichana 56 wanatumiatundu moja la choo (1:52) uwiano unaotakiwa ni wasichana 20 kwa tundu moja la choo (1:20).

Ingawa kwa wastani tuliouona hapa, zipo shule zenye upungufu zaidi hadi wanafunzi 141 wanatumiat undu moja la choo. Pia, kuna upungufu wa vyumba vya madarasa takribani 95,557 kwa shule za msingi, vyumba vya madarasa kwa shule za msingi vilikuwa 121,022 na kufanya darasa moja kuwa na wanafunzi 84, ingawa zipo shule uwiano wa chumba kimoja cha darasa ni kwa wanafunzi 175 (1:175).

ACT Wazalendo kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 tuliweka namna ya kukabiliana na changamoto hizi, mathalan tuliahidi kujengamadarasa 24,000 kila mwaka ambapo bajeti yake wastani wa bilioni 448.
5. Benki sio suluhisho; Upotevu wa mabilioni ya Fedha za Mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu zinazotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 Halmashauri ziliidhinishiwa Shilingi Bilioni 76.02 kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu 5. Hadi Februari 2023, jumla ya Shilingi Bilioni 53.01 zilikusanywa ikiwa ni asilimia kumi ya mapato yasiyolindwa, kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 37.59 tu ndio zilipelekwa katika akaunti ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Hivyo, kutokana na fedha hizo, Halmashauri zimeweza kukopesha Shilingi Bilioni 31.9 kati ya Shilingi Bilioni 50.68 zilizotarajiwa kukopeshwa kwa kipindi hicho. Kwa ripoti ya CAG 2021/22 Fedha ambazo hazija rudiha ni Bilioni 88.42. Sasa Ofisi ya Rais -TAMISEMI imeanza maandalizi ya utoaji wa mikopo kupitia mfumo wa Benki.

ACT wazalendo tunafahamu kuwa Serikali inataka kuzipeleka fedha hizo katika mifumo ya kibenki. Sisi tunaona fikra hiyo inaenda kuleta matatizo zaidi kuliko msaada wa kuwakwamua vijana. Tunaona kabisa fedha hizi zinakwenda kuingia kwenye kundi na mifuko ya wachache, mifumo ya kibenki bado si rafiki kwa watu wengi masikini. Pia, mfumo ya kibenki itaongeza gharama za uendeshaji na utoaji wa mikopo hii kwani na benki zitahitaji kupata faida tofauti na ilivokua awali.
ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Mikopo kwa Vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu itolewe kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii ambapo fedha hizi zitakuwa ni mchango wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wananchi wenye sifa watakaoingia kwenye Skimu husika.

Kwa mfano katika mchango wa kila mwezi wa shilingi 30,000 kwa Skimu ya Hifadhi ya Jamii, mwananchi atachangia shilingi 20,000 na Mamlaka yake ya Serikali ya Mtaa itamchangia shilingi 10,000. Kwa mfumo huu tunaopendekeza Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu watapata mambo matatu. Nayo ni mikopo nafuu, Bima ya Afya kupitia Fao la Matibabu na Pensheni ya uzeeni watakapofika umri wa kustaafu.

Kwa pendekezo hili tutakuwa tumedhibiti upotevu wa mabilioni ya fedha, tumechochea utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwa wananchi wetu, kuongeza watu wenye Bima ya Afya nchini na kutoa mikopo nafuu inayolipika kwa Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu nchini kwetu. Kwa kutumia makadirio ya makusanyo ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa katika mwaka ujao wa Fedha, 2023/2024, jumla ya Watu 1,167,000 watafaidika na Skimu hii katika mwaka wa kwanza na Akiba itakayokusanywa na Skimu ya Hifadhi ya Jamii itakuwa ni shilingi Bilioni 420.

Tukitekeleza mfumo huu kwa miaka mitano tutakuwa tumejenga Skimu ya Hifadhi ya Jamii yenye thamani ya shilingi trilioni 2.1 yenye wanachama Zaidi ya milioni 3 wenye Fao la Matibabu.

Hivyo basi ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa 10% ya Mapato ya Ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zitolewe kwa Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu kupitia mfumo wa Hifadhi ya Jamii.

Aidha, tunawataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizokutwa na ubadhilifu wa fedha za umma wachukuliwe hatua kwa kusimamishwa kupisha uchunguzi na ikithibitika wamehusika wachukuliwe hatua za kisheria.

6. Ufinyu wa bajeti kwa wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA)
Kwa kuzingatia majukumu ya TARURA ambayo kwa sehemu kubwa yanahitaji fedha za kutosha kutekeleza wajibu huo kutokana na hali halisi ya barabara zetu. Kwa miaka minne mfululizo yaani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20, 2020/21, 2021/22 na 2022/2023 kiwango kilichoidhinishwa na kile kilichotolewa ni asilimia ndogo. Mathalani mwaka 2022/23 iliidhinishiwa kiasi cha sh. Bilioni 838.15 akati mwaka uliopita ilitengwa Bilioni 900. Mpaka Februari 2022 ilipokea kiasi cha Bilioni577.80 sawa na asilimia 69. Mwaka huu 2023/2024 TARURA inaomba kuidhinishiwa Shilingi Bilioni 710.31 kwa ajili ya kazi za miundombinu ya barabara kwa kiasi kilicho pungufu zaidi, licha ya kuongezewa majukumu.

Maendeleo ya barabara vijijini si mazuri, bado hali za barabara vijijini si nzuri, na tukijua kuwa ni vijijini ndio kuna uzalishaji, lakini hali ya barabara zake si nzuri, bado akina mama wanajifungua nyumbani ama njiani kutokana na miundombinu ya barabara kua mibovu.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali Ili kuchochea maendeleo vijijini na mamlaka za serikali za mitaa na Vijiji ni muhimu kuwekeza vyema kwenye miradi ya maendeleo vijiji kwa kuiongezea bajeti TARURA kuipatia vyanzo zaidi vya bajeti, ili kupanua mtandao wa barabara vijijini na kupeleka bajeti yote iliyopitishwa na kuisimamia vizuri TARURA.

7. Miradi ya Afya na Elimu kutegemea Fedha za nje.
Katika bajeti ya 2023/2024 Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa ameomba kuidhinishiwa programu mbalimbali za Afya na lishe zenye jumla ya thamani ya shilingi Bilioni 59.85 ambazo zote ni Fedha za nje, hakuna katika hotuba hiyo program au mradi wa Afya unaotokana na Fedha za ndani. Miradi iliyopangwa kutekelezwa kwenye ni kama ifuatavyo;

i. Mradi wa kuimarisha huduma za rufaa na ubora wa huduma za afya ya msingi Shilingi bilioni 44. 8
ii. Mfuko wa Pamoja wa Afya Shilingi bilioni1.6
iii. Programu ya kuimarisha Mifumo ya Afya inaombewa kuidhinishwa jumlaya Shilingi Milioni 654.28
iv. Mradi wa Udhibiti wa Magonjwa ya mlipuko na matukio yenye athari ya usalama wa Afya ya Jamii (GHSA- CDC) Shilingi Bilioni 3.7
v. Program ya kuboresha chakula na Lishe, inaombewa kuidhinishiwa jumla ya Shilingi Milioni 158.48
vi. Programu ya Mfuko wa Dunia wa Kupambanana UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (GlobalFund) Bilioni 8.7
vii. Mradi wa Usafi wa Mazingira (SRWSS): Shilingi Milioni741
viii. Programu ya Kuboresha Elimu Katika Shule za Sekondari (SEQUIP) Shilingi bilioni25.3
ix. Mradi wa uimarishaji wa ufundishaji na ujifunzaji (GPE-LANES II): Shilingi bilioni 1.0
x. Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (Primary Student Learning - BOOST) Bilioni 20.2
xi. Programu ya Uhamasishaji na Uchambuzi wa Sera (UNICEF) Milioni 609.1
xii. Mradi wa Usafi wa Mazingira (SRWSS): Shilingi milioni 333. 17

Miradi iliyotajwa hapo juu imepangwa kutekelezwa kwa kutumia fedha za nje tu. Tafsiri ya Mpango huu wa bajeti ni kwamba miradi hiyo siyo ya kipaumbele kwa kuwa fedha za nje sio za kutegemea kwa asilimia mia moja. Hii ni kutokana na uzoefu unaonyesha kwamba fedha za nje huchelewa sana kutolewa na wakati mwingine hazitolewi kabisa.

ACT Wazalendo tuna mashaka na vipaumbele vya Serikali kwa wananchi wake, masuala kama ya kinga na tiba kwa ngazi za TAMISEMI yanapaswa kwa kiasi kikubwa kutokana na mapato ya ndani ili kuweza kukabiliana na changamoto zozote za kidharura zinazokutokea huko nje, nchi yetu haipaswi kuwa tegemezi na kuwa muhanga kwa kiwango hiki.

Hitimisho
Katika uchambuzi wetu wa Bajeti ya TAMISEMI tumeonyesha maeneo saba lakini yamebeba jumla ya hoja kumi na moja (11). Bado tunaona ni yale yale kwenye Miundombinu ya Elimu na afya. Bado ni yale yale kwenye ukosefu wa ajira kwa vijana, ambapo tumeona upungufu mkubwa wa walimu nchini na hili litaendelea kuongeza muda zaidi wa kumaliza tatizo la walimu nchini. Bado ni yale yale kwenye upotevu wa rasilimali za umma kwenye Halmashauri zetu.

Imetolewa na;
Ndg. Kulthumu Jumanne Mchuchuli,
Twitter: @MchuchuliK
Waziri Kivuli TAMISEMI na Maendeleo Vijijini.
ACT Wazalendo
17 April 2024.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK