Tunachokisimamia

Ilani ACT 2020: Uhuru, Haki na Demokrasia

Ilani ACT 2020: Uhuru, Haki na Demokrasia

Watanzania hawakupigania uhuru kutoka kwa mkoloni ili waje watawaliwe kikoloni kwa kigezo cha ‘kuleta maendeleo’. Uhuru wa kila Mtanzania, ni haki na msingi wa Taifa la Tanzania. Kwetu sisi ACT wazalendo, Uhuru wa msingi wa Watu ni suala halina na halitakuwa na mjadala kwani kazi hiyo imekwishafanywa na Waasisi wa Taifa kupitia Uhuru wa Tanganyika wa Mwaka 1961, Uhuru wa Zanzibar wa Mwaka 1963 na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964. Hivyo tutachukua hatua stahiki kurejesha Uhuru wa Watu, Haki za msingi na Demokrasia madhubuti.

Ndani ya siku 100 za kwanza tangu Serikali itakayoongozwa na ACT Wazalendo na vyama washirika kushika madaraka itachukua hatua zifuatazo;

1. Itapitia na hatimaye Itafuta Sheria zote zinazobana, kuminya na kufifisha haki na uhuru wa Watanzania kujieleza na kutoa maoni, zikiwemo, Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya vyombo vya habari, Sheria ya Takwimu, kanuni ya maudhui ya mtandao na sheria nyingine kandamizi.
2. Itafuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya habari, na kutengeneza sheria, kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sekta ya habari.
3. Itaunda Kamisheni ya vyombo vya habari ambayo itaratibu sekta ya habari na maadili ya vyombo vya habari. Kamisheni hii itakuwa huru, na yenye kujitegemea, Serikali itakuwa ni mmoja tu ya wadau wa kamisheni lakini si miliki wa kamisheni hii.
4. Itahakikisha vyombo binafsi vya habari vinakuwa na haki sawa ya kupatiwa taarifa na kuripoti habari kutoka Serikalini.
5. Itahakikisha vyombo vyote vya habari, vya umma na vya binafsi, vinakuwa na haki sawa ya kupatiwa matangazo ya Serikali.
6. Itahakikisha vyama vya wanahabari vinawezeshwa kusimamia haki na maslahi ya wanachama wao bila hofu wala woga.
7. Italinda uhuru na haki ya mtu mmoja mmoja, Asasi za Kiraia, Jumuiya za kijamii na Kitaaluma, pamoja na makundi mbalimbali ya jamii kukutana, kuungana, kushirikiana na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na miongozo yao bila kuvunja Katiba ya nchi.
8. Itafanyia marekebisho sheria kandamizi ya Jeshi la Polisi Tanzania na huduma saidizi sura ya 322, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kifungu cha 43 (3), (4), na (6), inayotoa mwanya wa wazi kwa polisi kuzuia uhuru wa kujumuika bila sababu yoyote ya msingi, hivyo kukengeuka Katiba yetu ya nchi ya 1977 ibara ya 20 (1) inayoruhusu Uhuru wa Kukusanyika,
9. Itaundwa Tume ya Majaji itakayoongozwa na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa itakayochunguza vitendo vyote vya Utekaji, Watu kupotea na mauaji yote yasiyo na maelezo yaliyotokea kati ya mwaka 2015-2020 na vitendo vya Watu kubambikiwa Kesi na hata kuhukumiwa.
10. Kufuatia Taarifa ya Tume ya Majaji, kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokutwa na makosa, kufuta rekodi ya jinai kwa watu waliobambikiwa Kesi na kuhukumiwa vile vile kulipa fidia kwa familia zote zitakazokuwa zimeathiriwa na vitendo husika.

Rudi kwenye ilani

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK