Uchunguzi wa 'Plea Bargain' Jaji Biswalo Mganga Awajibishwe
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Uchunguzi wa akaunti ya Fedha za makubaliano ya kukiri kosa (Plea bargaining); Jaji Biswalo Mganga awajibishwe!
Utangulizi:
Kuibuka tena kwa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ndg. Charles Kichere zinazohusu kuendelea na uchunguzi wa akaunti ya fedha zilizokusanywa kutokana na utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa ‘plea bargaining’ na ripoti yake kutarajiwa kutolewa mwezi Machi 2023 imechochea mjadala na kuzalisha mapendekezo tofauti tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali nchini.
Mnamo mwaka wa 2019, Bunge lilitunga Sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) ambayo iliweka utaratibu wa makubaliano maalumu katika kesi ya jinai kati ya Mwendesha Mashtaka na Mshitakiwa. Kupitia utaratibu huu mshitakiwa anakubali kosa moja au zadi katika makosa aliyoshitakiwa nayo ili apate nafuu ya kesi hiyo.
Itakumbukwa kuanzia mwaka 2017 lilizuka wimbi la Serikali kushiriki uporaji dhidi ya mali za watu, wakiwemo wawekezaji kupitia kesi za kubambikiwa za Uhujumu Uchumi. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) ilianza kutaifisha fedha za watu bila ya kuwepo kwa Sheria ya ‘plea bargain’. Baada ya malalamiko ndipo sheria ikatungwa. Kwa muda wa miaka 4 tumeshuhudia watu wengi wakiporwa mali zao ili kupata uhuru wao.
Katika uchambuzi wetu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesbabu za Serikali (CAG) wa mwaka jana (2021) tulisema kuwa CAG amekuta kuna fedha kiasi cha shilingi bilioni 51.521 kutokana na kesi zilizomalizika katika Mahakama mbalimbali kwa kipindi cha miaka 6. Kwa mujibu wa CAG fedha hizi hazikutumika kwa sababu ya kukosekana kwa sheria na kanuni za matumizi yake.
Wakati watanzania wakisubiri Ripoti ya Ukaguzi wa fedha na utaratibu wa kesi zilizohitimishwa kwa kufuata sheria ya makubaliano ya kukiri kosa, ili kujiridhisha na taratibu zote na kubaini kiasi halisi kilichokusanywa kutokana na utaratibu huo, ni muhimu hatua za uwajibishaji zichukuliwe ili kulinda heshima ya Ofisi ya Umma.
ACT Wazalendo tunapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa;-
1. Rais aunde Tume ya Majaji ili kupitia malalamiko ya watu wote ambao walilipishwa fedha kwa mtindo wa kukiri makosa na kulipa fedha Serikalini.
2. Wale watakaobainika walilazimishwa kukiri makosa warejeshewe fedha zote zilizoporwa wakati wa kubambikiwa makosa mbalimbali kwa utaratibu wa ‘plea bargaining’.
3. Jaji Biswalo Mganga ajiuzulu mara moja ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
4. Jaji Kiongozi asimpangie kazi Mhe. Jaji Biswalo Mganga hadi uchunguzi utakapokamilika na kujua hatma ya maamuzi ya uchunguzi wa fedha za Plea Bargain.
Imetolewa na:
Ndg. Victor Kweka
Msemaji wa Sekta ya Katiba na Sheria
Twitter: @Advocate_Kweka
ACT Wazalendo
17 Oktoba, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter