TAREHE 16/2/2021
JANA Tarehe 15/2/2021 Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam lilitoa taarifa ya kumkamata Askofu mwamakula kwa madai ya tuhuma ya kosa la kuhamasisha Maandamano nchi nzima kwa lengo la kudai kupatikana kwa Katiba Mpya nchini.
ACT-Wazalendo inalaani na kupinga kitendo hicho cha Jeshi la Polisi kumkamata Kiongozi wa kiroho na Kijamii aliyejitolea kuhamasisha kwa njia za amani uwepo wa Mabadiliko ya Katiba ya Nchi itakayotoa fursa ya kuwa na TUME HURU YA UCHAGUZI.
1. Askofu Mwamakula amehamasisha kufanya “MATEMBEZI YA HIARI” ambayo ni haki yake ya Kikatiba kama Mtanzania, Jeshi la Polisi halijaeleza ni Sheria ipi imevunjwa kwa kuandaa matembezi ya Hiari? Katiba ya Nchi Ibara ya 20(1) inaeleza kuwa;
“Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani,…”
2. Kama Jeshi La Polisi linadai kwamba Matembezi ya Hiari ni Maandamano yasiyokuwa na Kibali, walijuaje kama Askofu Mwamakula asingetoa taarifa rasmi ya kufanyika kwa matembezi hayo kwa Jeshi la Polisi? Kuhamasisha kufanyika kwa matembezi ya hiari kunahitaji kibali cha Polisi?
3. Madai ya Askofu Mwamakula yamekuwepo tangu mwezi wa Disemba, 2020 si jambo la siri wala lenye nia ovu kama inavyotaka kuaminishwa na Jeshi la Polisi, aidha, ni nani aliyepata taharuki hiyo inayoelezwa na Jeshi la Polisi? Watanzania wanahitaji Katiba Mpya na Tume Huru itakayoheshimu misingi ya haki, demokrasia, uhuru wa kujieleza na kujumuika, haki za binaadamu na utawala bora.
4. Kuendelea kumshikilia Askofu Mwamakula kwa kutekeleza haki yake Kikatiba ni kosa kisheria. ACT-Wazalendo inalitaka Jeshi la Polisi kumuachia Askofu na kuacha kujituma kufanya kazi za Kisiasa zinazopora uhuru na haki zilizotolewa na Katiba ya Nchi.
5. Utaratibu uliotumika kumkamata Askofu Mwamakula (ni kitendo cha utekaji) na si utaratibu wa Kisheria wa kumkamata mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria. Jeshi la Polisi halipaswi kuingilia Uhuru wa kuabudu na kudhihaki hadhi ya Kiongozi wa Kiroho (Askofu) kwa kudai eti “anayejiita Askofu...” ili mtu atambulike na Jeshi la Polisi ni Sheikh au Askofu Jeshi linatumia ithibati ipi? Jeshi la Polisi halipaswi kuhoji juu ya Cheo chake cha Kidini kwa mujibu wa imani yake.
Ibara ya 19 (1),(2) imeeleza kuhusu Uhuru wa mtu kuamini dini atakayo;
(1)“Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.”
(2) “Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu ya binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”
6. ACT Wazalendo inaunga mkono “Matembezi ya Hiari” yaliyoitishwa na Askofu Mwamakula, Madai ya uwepo wa TUME HURU YA UCHAGUZI na Katiba Mpya ni ajenda endelevu ya Watanzania wapenda Haki na Demokrasia isiyoweza kuzimwa kwa vitisho na mamlaka yeyote ile iwayo.
ACT Wazalendo inalitaka Jeshi la Polisi kumuachia Askofu Mwamakula na kuacha ukandamizaji wa Haki za Kikatiba na kamwe Jeshi la Polisi lielewe kuwa kukuza Uchumi hakuwezi kupatikana kwa kuwa na mfumo mbovu wa Kiuchaguzi na Kiutawala usiozingatia HAKI NA DEMOKRASIA.
JANETH JOEL RITE
KATIBU IDARA YA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA
ACT WAZALENDO-TAIFA.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter