UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO KUHUSU RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23. #KAZIINAENDELEA KUFUJA FEDHA ZA UMMA
Utangulizi
Jumatatu tarehe 15 April 2024 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles Kichere alitoa taarifa yake ya Ukaguzi wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 Bungeni baada ya kuikabidhi kwa Rais tarehe 28 Machi mwaka huu.
ACT Wazalendo tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini. Katika uchambuzi wetu, tumeona zipo hoja nyingi za ukaguzi zinajirudiarudia mwaka hadi mwaka.
Uchambuzi huu wa CAG 2022/23 unaibua picha ya jumla kwamba Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia ni mwendelezo wa Tunaendelea kuona Kazi inaendelea kufuja fedha za umma.
Aidha, katika uchambuzi wa mwaka 2019/20 na 2020/21 tuliibua hoja 20 kutoka katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ikiwa hoja kumi kwa kila mwaka kwa lengo la kutaka uwajibikaji wa Serikali kwenye hoja hizo. Zipo zilizofanyiwa kazi kama tulivyoonesha kwenye uchanbuzi wetu wa mwaka jana.
Maeneo kumi (10) muhimu katika Uchambuzi wa Ripoti ya CAG mwaka 2022/23.
Kama ambavyo tumekuwa tukifanya kila mwaka, uchambuzi wetu mwaka huu utajikita kwenye mambo kumi (10) ambayo tunaona ni muhimu Watanzania kuyatambua na tutayatolea mapendekezo ili yaweze kuchukuliwa hatua.
Katika uchambuzi wetu tumebaini CAG ameibua hoja nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi. Baadhi ya hoja hizo zitazingatiwa kwenye uchambuzi wa bajeti wa kila wizara ya Serikali utakaofanywa na Wasemaji wetu wa kisekta.
1. Kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali na hatari zake kwa Taifa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya ukaguzi wa Akaunti ya Deni la Taifa na kuonyesha ukuaji wa kasi wa deni la taifa na viashiria vya hatari kwa deni la Serikali. CAG ameeleza kuwa Deni la Serikali hadi tarehe 30 Juni 2023 lilikuwa Shilingi trilioni 82.25 ambalo ni Ongezeko Shilingi trilioni 10. 94 sawa na 15% kutoka mwaka wa Fedha uliopita.
Uchambuzi wetu wa CAG kuhusu Mwenendo wa deni la Serikali ni kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali inatishia maendeleo ya watu, uwezo wa nchi kujihudumia na kusababisha ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na deni (debt driven growth).
Kasi ya ukuaji wa Deni ya Serikali ya awamu wa Sita chini ya Rais Samia kwa miaka miwili tumeshuhudia ongezeko ambalo halijawahi kutokea tangu kupata Uhuru katika Nchi yetu. Amekopa zaidi kwa shilingi trilioni 17.7 kutoka shilingi trilioni 64.52. Huku uchumi ukiendelea kuchechemea kwa ukuaji wa asilimia 5.2
Jedwali; Mwenendo wa Deni la Serikali kwa awamu mbalimbali za Serikali
JINA LA RAISI MIAKA KIASI KILICHOKOPWA KIASI CHA DENI LA SERIKALI.
Jakaya Kikwete 10 Trilioni 29.7 Trilioni 33.5
John Mgufuli 6 Trilioni 31.3 Trilioni 64.5
Samia Hassan 2 Trilioni 17.75 Trilion 82.25
Athari za Mwenendo wa Deni la Serikali zinaangukia kwenye mabega ya wananchi. Mathalani kwa mwaka wa fedha 2022/23 Makusanyo ya Ndani ya kodi, yasiyotokana na kodi na makusanyo ya serikali za mitaa yalikuwa Sh. trilioni 26.515 huku matumizi kwa ajili ya kuhudumia deni la Serikali ilikuwa shilingi trilioni 9.1. Hii ina maana kuwa 34.3% ya kila tulichokuwa tunakusanya kilienda kulipa deni la Serikali.
Mwenendo wa kukua kwa deni linaathari zifuatazo;
a) Nchi inatumia sehemu kubwa ya makusanyo yake kwenda kuhudumia deni badala ya kutoa huduma kwa wananchi walalahoi. Ukitazama taarifa za Benki Kuu zinaonyesha kila mwezi tunatumia bilioni 900 kwa ajili ya kulipa deni la Serikali, kati ya fedha hizo deni la ndani ni wastani Bilioni 600.5
b) Ongezeko la mikopo ya Biashara yenye masharti ya muda mfupi Serikali inalazimika kuingia sokoni kukopa zaidi ili kulipa madeni (hatifungani) yaliyoiva.
c) Ukopaji wa Ndani; Serikali na Sekta binafsi kugombania fedha jambo linalopelekea kuiminya sekta binafsi kupata mikopo kutokana na taasisi zinaona zinafaidika kwa rahisi kuikopesha Serikali kuliko sekta binafsi
d) Ongezeko la utitiri wa kodi, tozo, ushuru kwa wananchi.
e) Kucheleweshewa kwa malipo ya mafao na pensheni za wastaafu ambao ni wanufaika/ wanachama kutokana na fedha nyingi ambazo Serikali haijazilipa kwa taasisi hizo
Jambo hili linaumiza sana wakati wananchi wakibebeshwa mzigo huo, tunashuhudia ubadhirifu na upotevu mkubwa wa fedha unaofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi bila kuchukuliwa hatua za kiuwajibikaji. Badala yake viongozi wanaendelea kulitafuna taifa kwa kujinunua magari ya kifahari, kujiongezea posho, safari za nje na mishahara.
Pili, kwa mujibu wa CAG Serikali bado ina orodha ya mikataba ya mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.6 bila kupokea fedha za mikataba hiyo. Hii ni hoja ambayo imekuwa ikijitokeza kila mwaka kwa muda mrefu.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo;
i. Ili kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali, haswa Deni la Nje, kutokana na kushuka kwa mauzo yetu nje na kuporomoka kwa shilingi dhidi ya dola, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye ‘hedging’ ya Deni la Nje ili kuwa na uhakika wa thamani ya fedha itakayotumika muda wote kuhudumia Deni hilo.
ii. Serikali izibe mianya ya upotevu fedha na matumizi mabaya yanayongeza maumivu kwa wananchi.
iii. Tunaitaka Serikali kufanya mapitio ya mikataba yote ya mikopo ili kufuta mikataba ambayo haitekelezeki na ile inayotekelezeka ipokee fedha na kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.
2. Madai ya wafanyakazi Sh. bilioni 36.47 na michango yao (sh. bilioni 856.78 kutowasilishwa kwenye Mifuko ya hifadhi ya Jamii.
Ripoti ya CAG ya mwaka 2022/2023 imeonesha madai ya shilingi bilioni 36.47 ya watumishi wa Umma katika halmashauri na serikali za mtaa 54. Madai hayo yanajumuisha malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi, stahiki za wastaafu na posho za kisheria. Mchanganuo wa madai ya watumishi hao ni ufuatao;
MADAI KIASI
Malimbikizo ya mishahara 11,420,214,782
Madai mengine likizo, kujikimu, safari, uhamisho, posho za kisheria 24,341,616,670
Wastaafu 708,111,184
Kutokulipwa kwa madai haya kunaongeza ugumu wa maisha kwa wafanyakazi ikizingatia tayari gharama za bidhaa muhimu zinaendelea kupanda kila uchao.
Vile vile, ucheleweshwaji wa malipo ni kinyume na kanuni ya utumishi wa umma inayoelekeza mfanyakazi yeyote wa Serikali pale anapopandishwa daraja au kuteuliwa kwenye nafasi ya kiwango cha juu, alipwe malipo ya nyongeza ya mshahara yanayostahili.
CAG anathibitisha jinsi ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kuwathamini wafanyakazi wa umma nchini. Hii inapelekea kushusha morali ya watumishi na kuondoa ufanisi katika utendaji na kuwahudumia wananchi.
Aidha, CAG amebainisha kiasi cha Shillingi billion 856.78 cha michango ya wafanyakazi kutowasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSSF, PSSSF na WCF). Mifuko ya hifadhi ya jamii kushindwa kukusanya michango inadhofisha uwezo wake wa kuhudumia wanufaika. Mathalani kiasi cha shilingi milioni 708.1 ambacho ni madai ya wastaafu kimeshindwa kulipwa kwa zaidi ya miaka minne.
ACT Wazalendo tunaitaka hatua zifuatazo kuchukuliwa ili watumishi na wastaafu walipwe stahiki zao;
i. Tunaitaka Serikali na waajiri binafsi kuheshimu matakwa ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi.
ii. Pia, tunaitaka Serikali kulipa malimbikizo ya madai yote ya watumishi na wastaafu.
3. Ubadhirifu na upotevu wa Shilingi Trilioni 3.14 fedha za umma.
Ripoti ya CAG mwaka 2022/23 imeendelea kuonesha uzembe mkubwa unaofanywa na Serikali uliosababisha upotevu wa makusanyo na mapato katika wizara, idara na taasisi za Serikali, Serikali za Mitaa, Miradi ya maendeleo na Mashirika ya umma.
Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG mwaka huu tumeona kwa mara nyingine vitendo au maamuzi yenye viashiria vya ubadhirifu wa fedha za umma katika utekelezaji wa miradi na majukumu mbalimbali ya wizara, taasisi za Serikali na Mashirika ya umma.
Hoja za ubadhirifu na upotevu wa fedha za makusanyo zina jumla ya thamani ya shilingi trilioni 3.14. Mchanganuo wa hoja na thamani yake ni kama ufuatao;
a) Serikali za Mitaa na Halmashauri zimeonesha upotevu wa shilingi bilioni 167.8
b) Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zina upotevu wenye thamani ya shilingi bilioni 103.32
c) Gharama zinazotokana na ucheleweshaji na kutelekezwa kwa miradi ya maendeleo zina jumla ya thamani ya shilingi bilioni 744.1
• Dosari za kiusanifu za TANROADS kwenye miradi ya Barabara 6 wenye thamani ya shilingi bilioni 130.51
• Mradi wa BRT shilingi Bilioni 28.05
• Bwawa la kufua umeme la Mwl. Nyerere wenye thamani ya shilingi bilioni 327
d) Mashirika ya umma yana hoja zenye thamani ya shilingi trilioni 2.23
Taarifa ya CAG inathibitisha tena tatizo sugu la Serikali kuendelea kupoteza na kutumia vibaya fedha za umma bila hatua za uwajibishaji kuchukuliwa.
ACT Wazalendo tunataka
i. Watu wote waliohusika katika ubadhirifu na uzembe uliopelekea upotevu wa fedha za umma wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
ii. Tunatoa wito kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali. Bunge lisipotekeleza wajibu wake kikamilifu ndio maana nchi yetu inashuhudia matumizi mabovu na ufujaji wa fedha bila hatua kuchukuliwa kila mwaka.
4. Fedha kutumika bila kupitishwa Mfuko mkuu wa Hazina ni mwanya wa Ufisadi
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameendelea kubainisha ukaidi wa Serikali kutumia fedha kinyume na katiba ya nchi. Kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/18 tulionyesha kuna fedha za Serikali ambazo zimetumika bila kufuata utaratibu wa kikatiba, ambao unailazimu Serikali kupitisha mapato na matumizi yake kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina.
Katika Mwaka 2022/2023 Jumla ya Matumizi yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.2 yalifanyika bila kupita Mfuko Mkuu. Kwa mujibu wa maelezo ya CAG, sehemu kubwa ya fedha hizi zinatokana na fedha zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutoka kwa wadau wa maendeleo. Fedha hizi za miradi zinaonekana katika vitabu vya Bajeti lakini CAG hazioni kuingia mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake ni kinyume cha Sheria
Matumizi ya aina hii licha ya kuwa ni kinyume na katiba na sheria za nchi, huwa ni kichaka cha kuficha ubadhirifu kwani kutumia fedha namna hii kunamnyima CAG kufanya kazi yake ya Udhibiti wa Fedha za Umma.
i. ACT Wazalendo tunamtaka Waziri wa Fedha na Mipango aheshimu Katiba na Sheria katika matumizi ya fedha ili kutotoa mwanya wa ufisadi kwa fedha za umma.
ii. Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inafanya usuluhishi sahihi wa taarifa za fedha zilizotolewa kwa Wizara mbalimbali na fedha zilizopokelewa moja kwa moja kwenye maendeleo katika miradi. Hazina iweke mahesabu sawasawa ili kuhakikisha ‘credibility’ ya taarifa zake.
5. Mbolea ya ruzuku kutowafikia wakulima
CAG katika ripoti ya ufanisi wa usimamizi wa shughuli za kilimo ameonyesha kuwa wakulima wengi nchini hawajapata mbolea zenye ruzuku licha ya Serikali kutenga wastani wa shilingi bilioni 150 kila mwaka.
ACT Wazalendo tulitoa mapendekezo ya kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei za pembejeo (mbolea) ikiwemo kuweka ruzuku ili kushusha bei na upatikanaji wake. Mpango wa ruzuku ulibeba matumaini makubwa kwa wakulima kwa matarajio ya kupunguziwa gharama na kuhakikishiwa urahisi wa upatikanaji.
CAG ameonesha kuwa wakulima milioni 2.55 kati ya milioni 3.4 waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku (sawa na 75%) hawakupata wala kutumia mbolea kupitia mpango wa ruzuku licha ya kuwa na sifa ya kupata mbolea hiyo ya ruzuku.
Aidha, CAG amebainisha kuwa Wafanyabiashara 1,712 kati ya 4,346 waliosajiliwa (sawa na 41%) katika programu ya ruzuku hawakuuza wala kusambaza mbolea ya ruzuku .
Halmashauri 41 kati ya 181 hazikupata kabisa mbolea ya ruzuku, kitendo kilichosabisha usumbufu kwa wakulima kusafiri umbali mrefu kufuata mbolea.
ACT Wazalendo kwa hatua za uwajibikaji tunataka
i. Serikali itueleze fedha za ruzuku zimepelekwa wapi ikiwa wakulima hawajanuifa nayo?
ii. Tunaitaka Serikali kuingiliakati mfumo wa uagizaji na usambaziji kwa kuiwezesha kibajeti Kampuni ya taifa ya Mbolea (TFC) kuagiza nje na kusambaza mbolea nchini. Kwaajili ya kuongeza uwezo wa usambazaji wa mbolea unaotokana na kulegalega kwa waagizaji na wasambazaji binafsi.
iii. Tunaitaka Serikali irejeshe mfumo wa uagizaji wa Pamoja wa mbolea
iv. Serikali illipe kwa wakati madai ya wasambazaji wa mbolea.
v. Kwa hatua ya kudumu, kuondoa utegemezi wa mbolea kutoka nje, kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili watu waweze kujenga viwanda vya kuzalisha mbolea nchini na kuimarisha uzalishaji kwa viwanda vilivyopo.
6. Tatizo la uagizaji, uingizaji na usambazaji wa mafuta nchini.
Kwa muda tumeshuhudia Changamoto ya Kupanda kwa gharama ya mafuta, uagizaji wa pamoja na usambazaji wa mafuta. Hii imepelekea kunaongeza sana Gharama za maisha, na Uchumi, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa Nauli za mabasi na Dalaladala nchini. CAG amefanya Ukaguzi wa ufanisi wa kiutendaji na uagizaji wa mafuta na hizi ni miongoni mwa hoja alizoibua;
a) Nchi haina hifadhi ya Taifa ya Petroli, CAG anaonesha kama Taifa kukosa hifadhi ya Petroli ya mkakati unaiweka nchi katika hatari ya kuwa na uhaba wa nishati wakati wa shida, CAG ameonesha kuwa Wizara haikuandaa mpango wa dharura wa Petroli kama unavyohitajika kisheria kwa takriban miaka 8 kutoka 2015-2023
b) Uwezo mdogo wa Miundombinu mafuta nchini, CAG anaonesha kwamba kuna Bomba Moja tu linalotumika kuingiza mafuta Tanga, mtwara na Dar es salaam na Bomba hilo moja ndio hutumika kusafirisha Petroli na Dizeli mtawalia, baada ya kusafirisha petrol linasafishwa ili kupitishwa Dizeli, Bomba hili limetumika kuanzia 2012 ambapo lilitumika kusafirishia Metric Tone 250,000 sasa linapitisha 650,000.
Serikali ya CCM inafanya mchezo na Suala hili nyeti, sisi tunaona ni lazima kuweka mkazo mkubwa sana kwenye eneo hili hasa ukizingatia mambo kadhaa yanaweza kuteteresha Usambazaji wa Mafuta Duniani kama vile, migogoro ya kieneo (vita mashariki ya kati), majanga, vikwazo vya kiuchumi kwa baadhi ya nchi, kupanda na kushuka kwa thamani ya dola na kuadimika kwa dola kunaweza kusababisha kupanda sana au kutopatikana mafuta kwa wakati na kuacha uchumi wetu mashakani.
i. ACT Wazalendo Tunataka Serikali ijenge uwezo wa Miundombinu ya kisasa na Usiamaizi wa hifadhi ya Mafuta nchini, tuwe na angalau hifadhi ya Mafuta ya Miezi mitatu.
ii. kuelekeza nguvu hiyo katika Kuwekeza kwenye matumizi ya Gesi Asilia kama nishati mbadala.
iii. Serikali iboreshe Miundombinu ya kupokelea, na kusambazia Mafuta nchini, ijenge Bomba kubwa na la kisasa la kupokelea Mafuta katika bandari zetu.
Serikali imepanga kuwanyima Fursa watoa huduma wazawa katika Miradi ya Gesi na Mfuta nchini (Local content)
Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ilipaswa kufanya utafiti wa msingi wa uwezo wa soko la watoa huduma wa ndani na ushindani ambapo utafiti ulitakiwa kuwa umemalizika ifikapo tarehe 30 Juni 2023 lakini hadi sasa haukufanyika. utafiti huu ni kwa ajili ya kuwasaidia wazawa kupata nafasi ya kutoa huduma katika miradi ya Gesi asilia wa LNG na Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki.
ACT Wazalendo Tunazitaka mamlaka husika zifanye haraka utafiti huo haraka ili kuweka mazingira wezeshi kwa watanzania kupata nafasi ya kutoa huduma katika miradi husika, Tunaendelea kupigania Taifa la Wote, Maslahi ya wote, tunataka Rasilimali za Tifa hizi zinufaishe watu wote hivyo ni lazima watambulike.
7. Usimamizi mbovu wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi)
CAG amebaini kuwa kuna usimamizi mbovu kwa wakala wamabasi yaendayo haraka (DART)ambayo ipo chini ya OR-TAMISEMI, katika ripoti yake ametoa hoja tatu kubwa zinazothibitisha uzembe katika uendeshaji wa Mradi.
Kukamilika kwa miradi ya Awamu ya pili na kutotoa huduma, Mradi wa Bilioni 217.48 wa kutoka Katikati ya Jiji hadi mbagala umekamilika kwa 98.86% lakini hautoi huduma.
DART Kukalia bidhaa za Bilioni 3.43 za mifumo ya kukusanya Nauli, CAG ameonesha kuwa DART ilinunua Kadi janja (Smart cards) za Bilioni 1 na mifumo mingine ya TEHAMA ya kukusanyia nauli ya Bilioni 2.43 vimetelekzwa.
Utoaji wa Huduma usioridhisha, CAG ameonesha katika Mabasi 210 ya mkataba Mabasi 132 (63%) yalikuamabovu na hayatoi huduma na kwamba yanahitaji Bilioni 2.1 ya matengenezo.
Hoja zote alizotoa CAG ni hoja zinazotokana na Uzembe wa kiutendaji na kimenejiment na zina harufu ya Uhujumu Uchumi. Hii inasababisha kukosekana kwa thamani halisi ya fedha na kutotatua tatizo la usafiri jijini Dar es salaam.
Badala ya kurekebisha masuala tumemsikia Waziri wa OR-TAMISEMI ameona Suluhu ni mwekezaji Binafsi na ameipa miezi saba DART kupata mwekezaji binafsi, na tayari tumesikia kuwa tayari mwekezaji kutoka UAE ameshapatikana kuendesha huduma za mwendokasi. ACT Wazalendo tunaona uzembe na usimamizi mbovu wa mashirika ya Umma hauwezi kutatuliwa kwa kugawa miradi kwa watu binafsi, kufanya hivyo hakutatui matatizo.
Uchambuzi wetu unaona kuwa pesa iliyotumika kutengeneza mradi ni pesa za mkopo ambazo zinalipwa na watanzania wote, uzoefu unaonesha kuwa Nchi nyingi miradi ya usafiri ndani ya majiji zinaendeshwa na Majiji husika au serikali mfano ni Jiji la Berlin, Tokyo, Singapore, NewYork (NewYork City Depertment of Transportation), London (transport for London), Toronto (Toronto transit Commission) kutaja kwa uchache.
ACT Wazalendo Tunapendekeza yafuatayo;
i. Mfumo wa Kielekroniki wa kukusanyia nauli uliotelekezwa, ufungwe maramoja na uanze kutumika.
ii. Bodi ya wakurugenzi ya DART ivunjwe yote na kuundwa upya, kwa kuzingatia wataalamu wa sekta ya hiyo ambayo itauendesha mradi kwa faida.
iii. Waziri wa OR-TAMISEMI ajiuzulu kwa kushindwa kuisimamia DART na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa.
iv. Tunamsihi DPP kufanya uchunguzi wa kijinai kubaini wote waliohusika kuhujumu Mradi wa mabasi ya mwendokasi Dart na kuwafikisha mahakamani.
8. Mradi wa Bwawa la kuzalishia umeme la Mwl. Nyerere
Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) limekuwa likiguswa na hoja za ukaguzi kila mwaka. Kuanzia mwaka wa fedha 2019/20, 2020/21, na 2021/22 zimejitokeza hoja kuanzia eneo la kitalaam masuala ya usanifu, ufuatiliaji wa sheria, udhaifu wa kiusimamizi, ulipaji wa gharama za ziada na masuala ya manunuzi.
Ripoti ya CAG 2022/23 imeendelea kuonyesha bado kutofanyiwa kazi hoja zake za huko nyuma na hasa kutotolewa kwa fedha za CSR shilingi bilioni 270 asilimia 3% ya fedha za mradi. CAG ameonesha mkandarasi wa bwawa la mwalimu Nyerere hajatoa fedha hizi zilizopaswa kupelekwa katika miradi ya kijiamii kwa wananchi wa Rufiji ambao mradi unajengwa katika eneo lao.
Aidha, hoja kubwa inayojirudia ni kuchelewa kwa Mradi kwa zaidi ya miaka miwili sasa kitendo kinachosababisha nchi yetu kumlipa Mkandarasi malipo ya ziada yenye thamani ya shilingi bilioni 327.
Ukiachilia, gharama tunayolipa kama taifa kutokana na ucheleweshwa huu. Tumeona katika siku za hivi karibuni kumekuwa na changamoto juu ya uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini. Katika mazingira ambayo bwawa limepokea maji ya kutosha (limejaa) lakini kinu cha kuzalishia umeme kilichofunguliwa ni 1 kati mitambo 9. Kwahiyo umeme unaozalisha ni Megawati 235 pekee kati ya Megawati 2115 zilizotarajiwa.
Katika hali hii ya mshangao, Wizara ya Nishati kupitia TANESCO imefungulia maji ambayo yameenda kusababisha maafa makubwa kwa wakazi wa Rufiji na Kibiti. Maji ambayo yangeweza kutusaidia kuzalishia umeme wa kutosha na kuzuia athari za mafuriko yamegeuka kuwa laana na majuto kwa wananchi wanaozungukwa na Mradi.
Hivyo basi, ucheleweshaji na uzembe mkubwa katika usimamizi wa Mradi huu umeligharimu taifa letu sio tu fedha zilizoteketea kwa kulipa ziada na maisha ya watu kutokana na mafuriko.
ACT Wazalendo tumeona udhaifu ulioibuliwa na CAG wa serikali kuamua kutoa ukandarasi wa usimamizi wa Ujenzi wa mradi wa bwawa la mwalimu Nyerere kwa taasisi ya serikali yenyewe umegharimu mali na maisha ya watu wa Rufiji. Tunaitaka serikali iwajibike kwa uzembe na iwalipe fidia wananchi waliopata hasara Rufiji kwa haraka.
9. Udhaifu katika Usimamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Unaweka rehani Afya za wanachama
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Serikali (CAG) kwa mara nyingine katika ukaguzi
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter