KC Zitto Kabwe Ashinda Kesi Mahakama Kuu: Mahakama Yasema Rais Magufuli Alivunja Katiba Kumuondoa Kazini CAG Prof. Assad

TAARIFA KWA UMMA

MAHAKAMA KUU YAAMUA KUWA RAIS ALIVUNJA KATIBA KUMUONDOA OFISINI PROF. MUSSA J. ASSAD KAMA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Nimefarijika kuwa leo tarehe 05/12/2022 Mahakama Kuu katika shauri la Zitto Zuberi Kabwe vs. Mwanasheria Mkuu na wenzie Shauri Namba 8 la 2020 mbele ya jopo la majaji watatu Masoud, Masabo na Kakolaki imetoa uamuzi kuwa Rais John Pombe Magufuli alivunja Katiba alipomuondoa Prof. Mussa J. Assad kama CAG.

Shauri hili lilikuwa linapinga sheria iliyotumika kutenguliwa kwa Prof. Mussa Assad kama CAG na kuteuliwa kwa Charles Kicheere. Mahakama Kuu imekubaliana na shauri hili kuwa sheria iliyotumika ni batili. Kwamba ukomo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali umewekwa na Katiba na Sheria iliyoweka muhula inapingana na Katiba. Prof. Mussa Assad alipaswa kuhudumu kama CAG mpaka umri wa kustaafu ufike kwa mujibu wa Katiba.
Nimefarijika sana kuwa Mahakama Kuu imesimama na Katiba katika shauri hili. Kwamba sasa haitatokea tena kwa Mtu mmoja Hata kama ni Rais kuamua tu kuvunja Katiba ya Nchi yetu atakavyo. Muhimu zaidi ni kwamba kwa hukumu hii ma CAG wote wajao katika Nchi yetu sasa wamelindwa rasmi kwa Uamuzi wa Mahakama.

Hata hivyo, Mahakama imekataa kukubali maombi yetu kuteuliwa CAG mwingine ilikuwa batili. Hili tutakwenda Mahakama ya Rufaa ili iweze kulitolea maamuzi. Kama kuondolewa kwa Prof. Assad ilikuwa batili ni dhahiri kuwa kuteuliwa kwa mtu mwingine kushika nafasi hiyo ilikuwa batili pia. Nimeshatoa maelekezo kwa mawakili wangu wakate Rufaa katika eneo hilo la hukumu.
Nachukua nafasi hii kuwashukuru sana mawakili wangu Rugemeleza Nshala na Nyaronyo Kicheere kwa kazi kubwa ya kuniwakilisha.

Vilevile, wakili Bonifasia Mapunda ambaye alikuwa wakili wa Prof. Assad katika kesi hii.
Kwa namna ya pekee natoa shukrani zangu kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadam (LHRC) chini ya Uongozi wa dada Wakili Anna Henga na Wakili Fulgence Masawe kwa msaada wao mkubwa katika shauri hili muhimu sana kwa nchi yetu.

Asanteni sana.

Zitto Kabwe
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
05 Disemba, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK