KC Zitto Kabwe: Mapendekezo ya Kikosi Kazi cha Rais Yatekelezwe

Mageuzi ya Kidemokrasia: Tunataka Hatua za Utekelezaji wa Mapendekezo ya Taarifa ya Kikosi Kazi sasa.

Utangulizi

ACT Wazalendo tuliamua kuongoza umma ili kuhakikisha kama taifa tunafanya mageuzi ya kidemokrasia na uendeshaji wa siasa zetu. Ndio maana tangu awali, tulikubali kuingia kwenye mijadala ya aina yoyote ambayo ingeweza kuwa na mchango wa kubadilisha siasa zetu na kutoa ushirikiano kwa Rais Samia Suluhu Hassani kwenye azma ya kufanya mageuzi ya kisiasa nchini.

Hatukufanya hivyo kibubusa au kujisalimisha bali kutokana na tafakuri ya kina juu ya hali ya kisiasa ya sasa ambayo tuliona inatoa mwanga wa matumaini kwamba tunaweza kusukuma mabadiliko ya kisiasa.

Mathalani, kuwepo kwa fursa ya kukaa meza moja kujadiliana na Rais. Pili, kauli za Rais mwenyewe kuvitaka vyama kuwa na mwanzo mpya (hivyo, ameweza kukutana na vyama vya upinzani kujadiliana). Tatu, kuwepo kwa utashi kidogo wa kisiasa wa kufanya mabadiliko kadhaa.
Kutokana na fursa hiyo tulichukua hatua kadhaa za kusukuma mabadiliko ya kisheria ili kurejesha siasa kwenye hali yake ya kawaida badala ya kutegemea utashi pekee wa watawala. Hatua tulizozichukua kama chama ni pamoja na kushiriki vikao vya pamoja vya wadau wa siasa nchini kama vile Mkutano wa wadau wa Siasa uliofanyika Disemba 2021 ambao uliopelekea kuundwa kwa Kikosi kazi.
Pia, kuhuisha kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kama chombo cha majadiliano, kushiriki kwenye Mkutano wa Dodoma wa Mwezi April 2022. Vilevile, tumeshiriki kutoa maoni kwenye kikosi kazi juu ya katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, mageuzi ya Jeshi la Polisi, sheria ya vyama vya siasa na mageuzi ya siasa kwa ujumla.
Tangu ripoti ya kikosi kazi imekamilika hatuoni hatua za utekelezaji, ni rai yetu kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inashughulikia masuala ya sera na sheria za kiuchaguzi kuanza kufanyia kazi mapendekezo ya taarifa ya kikosi kazi. Tunapata wasiwasi mkubwa sana juu ya hatua za utekelezaji. Mfano kwa utaratibu wa kawaida wa kiserikali ilitarajiwa kwenye Mkutano wa Bunge uliopita ilitakiwa taarifa ya kikosi kuwasilishwa Bungeni kama hati ya kuwasilishwa mezani ili kutoa nafasi ya kila Mbunge kupitia`taarifa hiyo, lakini haikufanyika.

Hivyo, tunaitaka Serikali kuchukua hatua za utekelezaji kwa kuchukua hatua zifuatazo;
i. Mosi, Serikali itoe ratiaba ya utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi hatua kwa hatua ili itakapofika mwezi Juni mwakani (2023) tuwe na Sheria mpya ya vyama vya Siasa, Sheria mpya ya uchaguzi na marekebisho ya Sheria ya mchakato wa Katiba mpya.
ii. Tunatoa wito kwa asasi za kirai na vyama vya kijamii kutoa shinikizo kwa Serikali kuchukua hatua stahiki ili kueleta mageuzi nchini.
iii. kupitia majukwaa ya kisiasa kama vile baraza la vyama vya siasa na Kitupo cha demokrasia nchini kuanza mijadala katika ngazi ya mikoa na wilaya kuhusu mapendekezo ya kisheria ili kuhakikisha kwamba uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja na Uchaguzi Mkuu 2025 unakuwa huru na haki.
Hivyobasi, kwa kuhitimisha majukumu haya yanahitaji juhudi za makusudi na Utashi wa utekelezaji wa Waziri Mkuu wa Nchi kama Mkuu wa Shughuli za kiserikali Bungeni, Mkuu wa kisera na Mkuu wa shughuli za kisiasa kwa kuwa Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa ipo chini yake.

Imetolewa na;
Janeth Joel Rithe
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na umma.
ACT Wazalendo
18 Novemba 2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK