Tunachokisimamia

Kujenga Utajiri wa Jamii kupitia Ushirika wa kisasa

Ilani 2020: ACT Wazalendo Kujenga Utajiri wa Jamii kupitia Ushirika wa kisasa

Kuongezeka kwa tofauti za kipato huku matajiri wakizidi kunufaika na mifumo ya kiuchumi iliyopo pamoja na ukosefu wa ajira kunazidi kushika kasi duniani na Tanzania ikiwemo. Hii inaamsha ari ya kufikiri njia mpya za kuleta usawa wa kimapato. Njia mojawapo ya kupata suluhu ya matatizo haya ni kwenda kwenye chanzo -- kurekebisha mfumo wa uzalishaji, ukusanyaji kodi na mgawanyo wa keki ya Taifa.
 
Kwa mantiki hio, ni vyema kutumia mfumo wa kujenga uchumi unaohusisha Jamii nzima. Wananchi wanaweza kushiriki katika umiliki wa mali kupitia Vyama vya Ushirika, Jumuiya za Wananchi au Serikali za Mitaa. Chama cha ACT Wazalendo kimeanzisha Azimio la Tabora lenye lengo hilohilo -- kuchochea wananchi kushika hatamu za uchumi. Vyama vya Ushirika vya Wananchi vitawezesha wananchi kumiliki njia za uzalishaji, usambazaji na masoko. 
 
Kufikia mwaka 2018 kulikua na Vyama Ushirika 10,990 vyenye wanachama milioni 2.5 (sawa na 5.% ya watanzania). Vyama hivi hasa SACCOs vinasaidia sana wanachama wao kupata mikopo midogo ya biashara, kusuluhisha matatizo ya dharura na kijamii n.k. ACT Wazalendo itaimarisha zaidi Ushirika ili kuwezesha wananchi kumiliki uchumi wao kwa njia zifuatatazo:
 

  • Itaweka mazingira ya kisera na kuwekeza katika ushirika utakaomilikiwa na wanaushirika kwa ajili ya maendeleo yao. Ushirika wa wakulima, wafugaji na wavuvi utakakuwa ni nyenzo ya wanaushirika kujiunga na hifadhi ya jamii, kupata bima ya afya, makazi yenye hadhi na staha, kuwekeza kwa pamoja, kusimamia bei na mauzo ya mazao yao nakadhalika,
  • Itawezesha kisera na kisheria kuunganishwa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji na masoko makubwa ya nje ya nchi kupitia vyama vyao vya ushirika na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo. Zaidi, tutahakikisha kunakuwa na ushindani baina ya wafanyabiashara ili wakulima wapate bei nzuri kwa mazao yao,
  • Itaondoa unyonyaji unaofanywa na madalali (middlemen) kwenye soko la mazao, kwa kuimarisha mfumo wa taarifa ya masoko ya mazao, kwa kutumia mifumo ya TEHAMA itakayowezesha wakulima kuuza mazao yao moja kwa moja kwa mtumiaji kwa njia ya mtandao. Serikali pia itahusika kikamilifu kwenye hifadhi ya mazao na kuanzisha mfumo wa soko la bidhaa (commodities exchange), ambao utashirikisha  wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika.
  • Pale ambapo madalali ni lazima kwa sababu za kihistoria, kiuchumi na kimazingira, Serikali itahalalisha udalali wa asili (Mfano Kangomba) kwa kuurasmisha.
Rudi kwenye ilani

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK