Kupanda kwa Nauli za Mabasi na Daladala: Serikali Isitishe Ongezeko la Nauli Mpya
LATRA kupandisha nauli za mabasi; Serikali isimamishe maamuzi ya kutumika kwa nauli mpya za mabasi na daladala nchini.
Jana tarehe 30 April 2022, Mamlaka ya udhibiti wa usafiri Ardhini (Latra) imetangaza nauli mpya za mabasi ya masafa marefu (yaendayo mikoani) na daladala (mabasi ya mijini) ambazo zimeonyesha kupanda kwa ongezeko la asilimia 11 kutoka sh. 36 kwa kilomita moja hadi sh. 41 kwa daraja la kawaida na daraja la kati limepanda kwa asilimia 6 kutoka kilomita 53 hadi 56. Huku nauli za daladala zimepanda kwa wastani wa shilingi mia moja. Mfano kutoka shilingi 400 hadi 500, 450 hadi 550 hadi shilingi 1,100. Hatua ya kupandishwa kwa nauli hizi kumetokana na shinikizo lililowekwa na chama cha wamiliki wa mabasi nchini (Taboa) wiki mbili zilizopita na kutishia kusitisha huduma hiyo kama serikali isingepandisha. Bei hizi za nauli zitaanza kutumia tarehe 14 Mei 2022.
ACT Wazalendo kimesikitishwa sana na uamuzi wa kupandisha nauli za mabasi na dalala nchini uliofanywa na serikali kupitia Mamlaka ya udhibitiwa usafiri wa Ardhini (Latra) kwa kuwa uamuzi hauzingatii mzigo mkubwa wanaobebeshwa wananchi kutokana na mabadiliko yoyote yanayotokea nchini na nje ya nchi. Serikali imeongeza kodi katika miamala ya simu kwa wastani wa zaidi ya asilimia mia moja. Wakati tunashuhudia ongezeko kubwa la gharama za maisha kutokana na kupanda kwa kasi kwa bei za bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kula, mchele, unga wa ngano na sukari. Serikali kukubali kupandisha nauli hizi ni kukubali kuwaumiza wananchi wake.
Ni dhahiri kuwa ongezeko la nauli za usafiri wa mabasi na daladsala zinaenda kuongeza athari kwa wananchi kwa kwenda kupandisha gharama za Maisha mara dufu na kuongeza kasi ya mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu nchini.
Sababu inayotajwa na wamiliki wa mabasi (Taboa) kushinikiza kupandisha bei ni kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na diseli, huku wadu mbalimbali tulipendekeza ili kuwanusuru wananchi dhidi ya kupaa kwa bei za mafuta serikali ishughulikie tatizo hilo,wapo baadhi ya wa bunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nao walitoa mapendekezo namna kushusha bei za mafuta, serikali haikusikiliza.
Serikali ya Tanzania tangu tumeanza kushuhudia kupanda kwa bei ya mafuta imechukua wajibu wa kikasuku wa kuweka matangazo tu na kuelezea vyanzo vya matatizo yaliyopo kwenye mataifa mengine yanavyotugusa badala ya kutafuta au kuchukua mapendekezo yanayotolewa kukabiliana na hali hii. Jambo ambalo linatisha na kuondosha matumaini ya wananchi juu ya namna serikali inavyowajibika katika kupigania ustawi wa maisha kwa watu wake, serikali inajipotezea uhalali na kupandikiza hofu na mashaka kwa wananchi.
Katika hali kama hii serikali ina machaguo mawili; Kuwaumiza wananchi kwa kuacha bei za vitu vipande bila kudhibitiwa au kuamua kuwalinda wananchi kwa kuingilia kati kwa namna tofauti. Katika hali kama hiyo ACT Wazalendo tunaendelea kutoa mapendekezo yetu namna ya kukabiliana na hali hii kuliko kuwaumiza wananchi.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo juu ya kupanda kwa anauli zambasi nchi.
1. Serikali isimamishe kwa muda angalau tozo ya Shilingi 500 kwenye mafuta.
Katika kila lita ya petroli, Diseli na Mafuta ya taa serikali isimamishe kuchukua shilingi 500 ili kukabiliana kupaa kwa bei. Tunafahamu kusimamishwa kwa tozo hiyo, kutaathiri bajeti ya serikali. Kiasi ambacho serikali itapoteza kwa muda wa miezi mitatu ni wastani wa Shilingi Bilioni 220 kwa mwezi, ambayo tunapendekeza kusimamisha kwa muda ununuzi wa ndege na Serikali ibane matumizi yake kufidia kufutwa kwa kodi.
2. Serikali ichukue sehemu yake ya akiba katika Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ili kufidia maeneo kwenye matumizi ya maendeleo ambayo yatakuwa yameathiriwa na kuondolewa kwa tozo hizo.
Serikali irudishe imani kwa wananchi na kuchukua hatua dhidi ya taasisi na watendaji ambao wametajwa katika ripoti ya CAG kuiba, kufuja mali na rasilmali za taifa zilizokua chini ya dhamana na usimamizi wao. ACT Maendeleo inaamini hili la kuzuia bei ya mabasi lisipande linaweza kufanyika kama Serikali itakuwa na nia ya kufanya hivyo ili kuzuia mzigo huo usiwaelemee wananchi na katika hili ACT Wazalendo itaedelea kulipazia sauti.
Imetolewa na;
Ndugu Ally Saleh
Msemaji wa Sekta ya Habari, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi
ACT Wazalendo
0715 430022
1 Mei 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter