Kuporomoka Bei ya Korosho, Serikali Iingilie Kati Kuwaokoa Wakulima

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA
Kuporomoka kwa bei ya korosho; Serikali iingilie kati kuwanusuru Wakulima na kuhami uchumi wa Wananchi.

1. Utangulizi,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kufuatiwa na mwenendo usioridhisha wa bei ya korosho unaotokana na taarifa za minada ya Korosho ghafi kwa mwaka 2022/2023. Hali hii imesababisha wakulima kugomea kuuza korosho zao ingawa makusanyo ya korosho katika ghala za minada yakiendelea.

Sisi, Viongozi wa ACT Wazalendo baada ya kufuatilia kwa karibu sana mwenendo huo tumeona tulizungumzie suala ili kuwanusuru Wakulima wa korosho kuingia kwenye lindi la umaskini. Kutokana na hali tutaenda kuzungumzia mambo manne. Mosi, kipi kimepelekea kupunjwa kwa bei kwa wakulima. Pili, tutaelezea mwitikio wa bodi ya korosho kwenye kukabiliana na hali hiyo. Tatu, athari zitakazojitokeza ikiwa hatua madhubuti za kuhami au kuwanusuru wakulima hazitachukuliwa. Mwisho mapendekezo ya kukabiliana na changamoto ya kuporomoka kwa bei za korosho.
Mnamo tarehe 21 Oktoba 2022 minada ya korosho ilianza rasmi; ambapo minada ilifanyika katika vyama vikuu vya TANECU ambapo ilitangazwa bei ya chini kuwa ni shilingi 1,630 na bei ya juu shilingi 2,011. Wakati katika Chama cha MAMCU (mnada ulifanyika Mtandi B Tandahimba na Chingulungu Masasi) bei ya chini ilikuwa shilingi 1,800 na bei ya juu ilikuwa ni shilingi 2,000.

Aidha, kwa mkoa wa Lindi minada ilianza tarehe 22 Oktoba, 2022 ambapo ulifanyika chama kikuu cha Lindi Mwambao katika Halmashauri ya Mtama ambapo bei ya chini ilikuwa shilingi 1,507 na bei ya juu ilikuwa shilingi 1,900. Vilevile, mnamo tarehe 23 Oktoba 2022 ulifanyika Chama Kikuu cha RUNALI Kijiji cha Ndomondo katika Wilaya ya Nachingwea. Katika mnada huo bei ya chini ilikuwa shilingi 1,480 na bei ya juu ilikuwa shilingi 2,200.
Katika minada yote iliyofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2022 wakulima walikataa kuuza korosho kutokana na kutoridhika na bei zilizotolewa na wanunuzi ambazo ni wazi zinaenda kudidimiza wakulima.

2. ACT tumebaini nini?
Ndugu Waandishi wa habari
Kwanza, pamoja na soko la korosho kushuka kidogo kwa wastani asilimia 0.3 utitiri wa kodi na tozo kwenye zao la korosho limeongeza mzigo na kupelekea kumpunja zaidi mkulima. Wakati watanzania wanajua korosho imenunuliwa kwa bei ya juu ya shilingi 2,200 na bei ya chini ya shilingi 1,480 (kwa mujibu wa minada iliyofanyika Lindi na Mtwara), lakini uhalisia haupo.
Uchambuzi wetu wa bei halisi ya korosho ambao tumeupata baada ya kujumlisha bei ya minadani na fedha ambazo mnunuzi anakatwa kwa kila kilo moja ya korosho anayoinunua (indirect charges). Kwa msimu wa mwaka huu 2022/2023, makato kwenye kila kilo moja ya korosho zipo kama ifuatavyo;
Makato ya gharama za Biashara:

i. Usafirishaji shilingi 120
ii. ICD shilingi 120
iii.Vibali shilingi 10
iv. Kushusha mzigo shilingi 10
v. Provisional income tax shilingi 70
vi. Tozo ya kupakia mzigo shilingi 10
vii. Deni la gunia 80


Tozo au makato ya Serikali:
i. Makato ya maendeleo ya zao la korosho (pembejeo) shilingi 110

ii. Ushuru la kusafirisha korosho ghafi nje (Exporty levy) ambayo ni sawa na asilimia 15 ya FOB shilingi 380
iii. Makato mengine shilingi 50
iv. Ushuru wa Bandari Shilingi 100


Ndugu Wanahabari,
Jumla ya makato haya ambayo mkulima amebebeshwa kwa mgongo wa mnunuzi kwa kilo moja ya korosho ni shilingi 1113. Hii ni sawa na kusema, kama makato haya yasingekuwepo, bei ya korosho ingeongezeka kwa shilingi 1113 kwa kila kilo moja ya korosho. Ukijumlisha bei inayoonekana kwenye minada ya shilingi 2200 na hii ambayo serikali imemnyonya mkulima ya shilingi 1113, inafanya bei halisis ya korosho inayonunuliwa Minadani kuwa shilingi 3313.
Pili, sababu nyingine ni baadhi ya Wafanyabiashara kukubaliana bei ya kununulia korosho kabla ya muda mnada(Syndicate).
Tatu, baadhi ya watumishi kuanzisha makampuni madogo ya uwakala wa kununuwa korosho na kutumia nafasi zao za kupata taarifa kwa urahisi wakiwa ndani ya utumishi wa Serikali na kukandamiza bei ya korosho
Nne, Wafanyabiashara wakubwa kutojitokeza sokoni kwa kuwa wanawatumia Wafanyabiashara wadogo kupitia VIKAMPUNI walivyoviandaa kuwakusanyia korosho hatua ambayo kwao ni salama zaidi kwa pesa zao.
Aidha pamoja na kutangazwa kwa bei ya juu kuwa Shilingi 2011 uhalisia ni korosho chache sana itanunuliwa kwa bei hiyo, kwa mujibu wa taarifa za mnada ni wastani wa tani 170 pekee ndio zitanunuliwa kwa bei hiyo. Hivyo, mzigo mkubwa utanunuliwa kwa wastani wa shilingi 1600 hii sio sawa kabisa, inapaswa tuzamwa na kupigwa kilele na kila mpenda maendeleo.
Ndugu Waandishi wa Habari,


3. Serikali inasemaje?
Katika hali hii ya kuporomoka kwa bei, illitegemewa Serikali kupitia, bodi ya korosho Tanzania, Wizara ya Kilimo kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa wakulima wa korosho. Kinyume chake bodi ya korosho kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi ametoa maneno ya dhihaka na kejeli kuwa wakulima kama hawataki kuzua korosho zao hakuna atayewalazimisha kwa kuwa ni bei ya soko la dunia. Kauli hii inaonyesha kupuuza hoja na malamimiko ya wananchi yanayotokana na uhalisia wa gharama za uzalishaji, thamani ya shilingi na mfumuko wa bei za bidhaa zingine.
Serikali ilianza kushambulia zao la korosho kutokana na mgawo wa pembejeo. ACT Wazalendo tulieleza changamoto ya mwenendo wa usambazaji na mgawo wa pembejeo kwa wakulima wa korosho kwenye mikoa ya Ruvuma (Tunduru), Lindi na Mtwara; Ambapo kinyume na ahadi ya serikali ya kuleta pembejeo ya bure, ya kutosha na kwa wakati, hali ilikuwa tofauti mno. Jambo lililopelekea kupunguza kwa uzalishaji wa zao la korosho. Kuporomoka kwa uzalishaji na anguko la bei ya korosho inaenda kumdidimiza zaidi mkulima.
Ndugu wanahabari, tumeona ni muhimu pia kueleza watanzania kuhusu hili pia kwani ukweli ni kuwa, zao la korosho linashuka uzalishaji mwaka hadi mwaka toka tani laki 3 mwaka 2017/18 hadi tani laki 2 mwaka 2021/2022
Kushuka huku kwa uzalishaji, ambako pia kwa mwaka huu makusanyo halisi hatutarajii kuvuka tani laki 2 kutokana na hali halisi iliyopo mashambani, kunatokana pamoja na mambo mengine, utaratibu usiofaa wa pembejeo, kucheleweshwa kwa pembejeo, mgawo kiduchu kwa baadhi ya maeneo, pembejeo zisizozingatia hali ya hewa ya eneo, usambazaji wa pembejeo feki, pamoja na ugawaji wa pembejeo za mchicha na nyanya kwenye zao la korosho.

4. Mapendekezo ya ACT Wazalendo;
Hali ya Mwenendo wa soko la korosho ikiachwa iendelee itapunguza kipato cha wakulima na kuwaingiza kwenye ufukara. Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo kinatoa wito kwa serikali kuchukua hatua zifuatazo:

A: Hatua za haraka
1. Serikali ipunguze utitiri wa kodi, ushuru na tozo mbalimbali ili kumnusuru Mkulima wakati anatesekana bei isiyoridhisha
 Ifute ushuru wa shilingi 110 inayoitwa ya maendeleo ya korosho huku ukweli ukiwa ni fedha za kulipia pembejeo zinazoitwa za bure kwani tayari serikali ileile iliwatangazia watanzania kupitia bunge na sharia ikapitishwa ya kurejesha fedha za export levy asilimia 50 kwa wakulima
 Iondoshe ushuru wa gunia shilingi 81
 Iondoshe shilingi 20 kwa watunza maghala.
 ifute ongezeko la asilimia 100 ya ushuru kwa bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko toka shilingi 2 hadi shilingi 4 kwa kilo moja
2. Serikali ipeleke haraka muswada wa sharia kupunguza makato ya export levy toka asilimia 15 ya FOB hadi asilimia 9 (single digit) kuhami bei ya soko na bodi ya korosho iharakishe mchakato wa kuandaa mapendekezo kwenye kikao kijacho cha wadau kutazama kama bado haya makato yana tija kwa wakulima.
3. Serikali itoe ruzuku ya kufidia soko la korosho ya shilingi 200 kwa kila kilo moja (subsdies) kama ilivyofanya kwenye mahindi huko songea mwaka 2021/2022 wakati soko limeyumba ili kumuokoa mkulima

B: Hatua za Muda wa Kati
1. Serikali iandae taarifa za wakulima (ukubwa wa mashamba) katika kutimiza ahadi yake ya kugawa pembejeo bure kwa wakulima kulingana na mahitaji halisi. Serikali iimarishe mfumo wa usambazaji kupitia vyama vya ushirika vya korosho (AMCOS).

2. Serikali itoe taarifa za uhakika mapema kuhusu upatikanaji wa pembejeo badala ya kutoa taarifa za hadaa. Kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakijinunulia pembejeo wenyewe. Ni bora serikali ieleze wazi juu ya uwezo wake ili wakulima waweze kujiandaa mapema kwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kununua pembejeo

3. Serikali iweke wazi hatua zilizochukuliwa dhidi ya Wafanyabiashara waliokamatwa na pembejeo bandia, ili kuondosha wasiwasi wa wananchi.


C: Hatua za Muda Mrefu
1. Ni muda mwafaka wa kuanza kutazama upya muundo wa vikao vya wadau wa zao la korosho ambao ndio hupitisha makato haya kwa wakulima. Mchakato wa kupata wawakilishi upoje wawakilishi wa wakulima ni asilimia ngapi ya wajumbe wote? Ni nani hasa msemaji wa wakulima?

2. Kufungamanisha sekta ya korosho na hifadhi ya jamii ili kupitia fao la bei kuweza kuweka uimara wa bei za mazao na pembejeo. Fao la bei litalinda ustawi wa wakulima wa korosho na kuwaepusha na hasara iwapo bei ya korosho ya msimu huu itaanguka tofauti na msimu uliopita.

3. Serikali ifanye haraka kuweka vivutio vya kuanzisha viwanda vya kupungua korosho nchini

Mwisho;

Ndugu wanahabari, sisi kama chama tumetimiza wajibu wetu. Tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuchukua hatua stahiki kumnusuru mkulima anayezama kwenye umasikini ambao serikali imeshiriki kumfukarisha mkulima.
Imetolewa na;
Ndugu Mtutura Abdallah Mtutura,
Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Isihaka Rashid Mchinjita
Mwenyekiti wa Mkoa-Lindi
ACT Wazalendo

Alphonce Andrew Hittu
Mwenyekiti Mkoa – Mtwara
ACT Wazalendo

26.10.2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK