LOLIONDO: UPORAJI ARDHI YA WANANCHI USITISHWE, WANANCHI WATENDEWE HAKI. Dorothy Semu.
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI: KUHUSU MAPIGANO LOLIONDO.
JUNE 12, 2022
Utangulizi:
Ijumaa ya tarehe 10 Juni, 2022 ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii – Ndugu Juliana Mwakan’gwali tulitoa tamko la kulaani na kupinga kwa nguvu zote kile kilichokuwa kinaendelea katika tarafa za Loliondo na Sare. Hii imefuatiwa na taarifa za taharuki kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha picha na video za vurugu, milio ya risasi na mabomu ya machozi. Aidha, picha zilizoonyesha baadhi ya wananchi waliodaiwa kujeruhiwa kwa risasi na kukatwa na vitu vyenye ncha kali. Tuliweka wazi kuwa taarifa ile ilikuwa ya awali ili tuweze kujipa nafasi ya kufuatilia na kupata usahihi wa taarifa na athari halisi zilizojitokeza kutokana na mapigano hayo.
Tumesikitishwa sana, kubaini ukweli kwamba siku ya Ijumaa tarehe 10 Juni 2022 katika Kijiji cha Loliondo kulitokea mapigano kati ya askari wa jeshi la Polisi dhidi ya wananchi kutoka katika vijiji 14. Taarifa zinaonyesha kuwa Juni 7, 2022 vikosi vya ulinzi viliwasili Loliondo kwa magari mengi na silaha. Jeshi la polisi, FFU, mgambo, na watu waliovalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania walionekana wakielekea kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 linalokusudiwa kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba.
Hali hiyo ilipelekea wanavijiji kujawa hofu na kuona ni mwendelezo wa jaribio la Serikali kuwapora ardhi yao. Usiku wa kuamkia tarehe 10 Juni, 2022 kikosi hicho kilianza kusimika vigingi katika ardhi ya Kijiji cha Ololosokwan. Vigingi hivyo vikipandwa vinarasimisha kuingiza ardhi ya vijiji kwenye pori la akiba.
Mapema asubuhi ya tarehe 10 wanavijiji walikusanyika na kujaribu kuingilia kati zoezi hilo. Kwa mujibu wa mashuhuda, hapo ndipo askari walipowatawanya wanavijiji kwa mabavu wakitumia risasi. Mapigano hayo baina ya Jeshi la Polisi na wanakijiji, yalipelekea kujeruhi wananchi wapatao 14; miongoni mwao wanawake ni wanane (8) na vikongwe wawili (2) na askari polisi mmoja ameuwawa.
Aidha, tunaelekeza masikitiko yetu makubwa kwa kauli za upotoshi kutoka kwa viongozi wa Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waziri Mkuu Ndugu Kasim Majaliwa Majaliwa na Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwasasu wamethubutu kupotosha ukweli kwa kukanusha mbele ya Bunge letu tukufu kuwa hapakuwa na taarifa za uvunjifu wa amani na vitisho dhidi ya wananchi wa Loliondo. Vilevile, kauli ya Spika ya kuishauri Serikali kuwashughulikia wananchi waliotoa taarifa kuhusu uwepo wa matukio hayo, inaonyesha dhahiri kuwa Bunge letu limeendelea kuwa tawi la Serikali na kutetea kila jambo linalofanywa na Serikali bila kujali athari wanazozipata wananchi. Limekuwa sio Bunge la wananchi ama chombo cha kuisimamia Serikali.
Kwa nini mivutano hii?
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa muda mrefu, eneo lote la tarafa ya Loliondo na sehemu ya tarafa ya Sale linatambulika kama Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000.
Tangu mwaka 2013, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa na azma ya kupunguza ukubwa wa eneo la Pori Tengefu la Loliondo kutoka Kilomita za Mraba 4,000 hadi 1,500 na kupandisha hadhi kutoka pori tengefu hadi kuwa pori la akiba. Hivyo ni dhahiri kuwa Wananchi waliopo katika Vijiji kumi na nne (14) vilivyo ndani ya Kilomita za Mraba 1,500 zilizotengwa kwa ajili ya uhifadhi kama nilivyovitaja, watatakiwa kuondoka katika maeneo haya.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, katika hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo Juni 3, 2022 alionyesha azma ya Serikali kuendelea kumega eneo la pori tengefu la Loliondo kwa kupandisha hadhi kwenda kuwa pori la akiba. Huku akifahamu kuwa kuna kesi iliyofunguliwa na vijiji vinne vya Loliondo kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki.
Aidha, itakumbukwa kuwa tarehe 25 Mei, 2022 Wawakilishi wa wafugaji kutoka vijiji 14 vya Loliondo walimkabidhi Waziri Mkuu taarifa iliyoandikwa na vijiji kuhusu tishio la Serikali kupora ardhi ya vijiji vyao na mapendekezo ya namna bora ya kutatua mgogoro huo wa tangu mwaka 1993. Waziri Mkuu, aliahidi, pamoja na mambo mengine, kukutana na wafugaji hao wa Loliondo.
Serikali, haijasikiliza wananchi hawa, matokeo yake imewajibu kwa mabomu ya machozi na mirindimo ya risasi za moto kwenye makazi yao.
Serikali inadharau Mahakama,
Serikali inafahamu kuwa tarehe 22 Juni 2022 Mahakama ya Afrika Mashariki, iliyoko Jijini Arusha, itatoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na vijiji vinne mwaka 2017.
Jitihada za wananchi wa Loliondo na Sale hazikukomea kutafuta mwafaka kwa kujadiliana na viongozi wa Serikali bali kwenye vyombo vya sheria. Mnamo Septemba 2017 vijiji vinne kati ya 14 vilifungua shauri namba 10 la mwaka 2017 dhidi ya Serikali ya Tanzania kupinga mlalamikiwa kuwahamisha kwa nguvu wafugaji, kuua mifugo, kuchoma moto nyumba, kutesa wanavijiji na kuwatoa katika ardhi ya vijiji vyao. Vijiji vilivyofungua kesi ni Ololosokwa, Oloirien, Kirtalo na Arash.
Vijiji hivyo pia vilifungua shauri namba 15 la mwaka 2017 kuiomba mahakama kuizuia Serikali kuacha kufanya jambo lolote katika eneo hilo hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa. Septemba 25, 2018 mahakama iliamuru Serikali kusubiri hukumu ya kesi ya msingi.
Kilichotokea Loliondo jana na juzi ni dharau ya wazi kwa mahakama. Mahakama ya Afrika Mashariki ipo kwa mujibu wa Mkataba unaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kudharau mahakama ni kosa la jinai na inaharibu kabisa dhana halisi ya utawala bora.
Mapendekezo Yetu:
ACT Wazalendo kutokana na hali tuliyoibainisha hapo juu tunatoa mapendekezo ya namna ya kumaliza mivutano na uvunjifu wa haki za binadamu unaoendelea Loliondo.
1. Kwanza, tunaitaka Serikali isitishe mara moja zoezi la kuweka alama za mipaka (vigingi) katika vijiji vyote vinavyoizunguka Pori Tengefu la Loliondo kwa ajili ya kulimega hadi Mahakama ya Afrika Mashariki itakapotoa hukumu.
2. Pili, tunaitaka Serikali kuunda Tume huru ya uchunguzi itakayokuwa na uwakilishi wa Jamii ya Kimasai itakayochunguza matukio ya vurugu zilizotokea tarehe 10 Juni 2022. Ni muhimu tume hii kuwa na uwakilishi wa Jamii ya Kimasai ili ifanye uchunguzi wa nini hasa kilitokea siku hiyo, ukweli kuhusu vifo vya raia, Polisi na majeruhi, uhusika wa wafugaji wa nchi jirani ya Kenya na uvunjifu mwingine wa Haki za Binaadamu katika eneo hilo. Uchunguzi wa Tume hii uje na nini kifanyike ili kuondokana kabisa na mgogoro huu wa Loliondo.
3. Tunataka Maafisa na Askari waliohusika kuendesha operesheni hii iliyosababisha uvunjifu wa haki za raia wachukuliwe hatua za kinidhamu na washitakiwe.
4. Serikali itumie njia ya majadiliano na ushirikishwaji ili kutafuta suluhu ya changamoto zote. Serikali ikae na wafugaji na wananchi wanaoishi katika vijiji hivi kutafuta suluhu.
5. Tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusitisha azma ya kupandisha ardhi ya vijiji kuwa Pori la Akiba ili kulinda haki za wenyeji ambao ni ardhi yao. Na hii siyo kwa Loliondo pekee bali kwa nchi nzima. Kwa mujibu wa Wildlife Conservation Act Na.5 ya 2009 sehemu ya 16 ilimtaka waziri aondoe Mapori Tengefu vijijini.
Hitimisho:
Ni wazi kwamba, suala la Loliondo ni la muda mrefu, mbinu ya kutowashirikisha wafugaji Jamii ya Kimasai katika kukabiliana na changamoto, linainyima Serikali kupata mtazamo mbadala. Pia kasi ya kupanuliwa kwa maeneo ya hifadhi za wanyamapori kama hifadhi za taifa, mapori tengefu, mapori ya akiba, na maeneo ya hifadhi za jamii ambayo kwa pamoja yanazuia kuendelezwa kwa maeneo ya wakulima na wafugaji imeendelea kutengeneza migogoro mingi nchini. Ni muhimu Serikali wakati wote kuzingatia haki na maslahi ya wazawa.
Ahsante sana!
Imeandaliwa na:
Dorothy Manka Jonas Semu
Waziri Mkuu Kivuli – ACT Wazalendo
[email protected]
12 Juni, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter