June 21, 2020 7:40 PM

MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA ACT WAZALENDO

Jana tarehe 21 Juni 2020, Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imekutana kwenye kikao chake cha kawaida kwenye ukumbi wa Lamada uliopo Ilala Jijini Dar es salaam chini ya Mwenyekiti wake Ndugu Maalim Seif Sharif Hamad.

Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Chama ilipokea na kuijadili kwa kina Ripoti ya Sekretarieti ya Chama kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kisha kutoa maazimio/maelekezo mbalimbali kama ifuatavyo;

 

1. Kuchukua na kurejesha fomu za ugombea wa Udiwani, Uwakilishi, Ubunge na Urais.


Kamati Kuu imefungua rasmi pazia la mchakato wa uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi Mkuu 2020. Zoezi la kuchukua, kujaza na kurejesha fomu litafanyika kuanzia tarehe 01 Julai 2020 hadi tarehe 13 Julai 2020.


Tarehe 11 Julai itakuwa ni kikao cha Kamati Kuu, tarehe 01 Agosti 2020 itakuwa ni kikao cha Halmashauri Kuu na mchakato utahitimishwa tarehe 02 Agosti 2020 kwa Mkutano Mkuu wa Taifa kuwapitisha wagombea urais wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Hivyo basi, ninapenda kuchukua fursa hii kuwatangazia wanachama wote wa ACT Wazalendo wenye nia ya kugombea kwenye nafasi za Udiwani, Ubunge, Uwakilishi na Urais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakachukue fomu ifikapo tarehe 01 Julai 2020 hadi 13 Julai 2020.


2. Kupinga rushwa kwa vitendo.


Kamati Kuu imesisitiza umuhimu wa ACT Wazalendo kuendeleza utamaduni wake wa siku zote wa kupinga rushwa kwa vitendo kwa kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya rushwa havipewi nafasi kwenye mchakato mzima wa uteuzi wa wagombea kupitia ACT Wazalendo. ACT Wazalendo haitamvumilia mwanachama yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa kwenye zoezi la uteuzi wa wagombea wake.

Idara ya ACT Amani imeagizwa kuchunguza na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mgombea wa kila nafasi. Atakayebainika kushiriki vitendo vya rushwa ajue fika kuwa hana nafasi ya kuteuliwa kugombea kupitia ACT Wazalendo. Mbali na kupoteza sifa ya kuteuliwa kuwa mgombea, mwanachama atakayebainika kushiriki vitendo vya rushwa, pia atachukuliwa hatua nyingine kali za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama.


3. Mchakato wa Uchaguzi kuzingatia misingi ya ACT Wazalendo.


Kamati Kuu imewaagiza wasimamizi wote wa mchakato wa uchaguzi wa kila ngazi kuhakikisha kuwa uteuzi wa wagombea wa ACT Wazalendo unafanyika kwa kufuata misingi ya Chama; uhuru, haki, usawa na uwazi ili kusimamia demokrasia kwa vitendo kama ulivyo utamaduni wa ACT Wazalendo.


4. Ushirikiano na vyama vingine makini vya Upinzani.


Kamati Kuu imewapongeza viongozi wakuu wa Chama kwa jitihada wanazozifanya kuimarisha ushirikiano baina ya vyama vya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020. Kamati Kuu imeridhia Chama kufanya mazungumzo ya ushirikiano na vyama makini vya upinzani ili kuingo'a CCM madarakani na kuleta mabadiliko yatakayowaletea Watanzania maendeleo.

Hitimisho:


Kamati Kuu ya Chama imesisitiza msimamo wa Chama kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2020 utakuwa wa kufa na kupona. Chama kitahakikisha kinaulinda ushindi wake kwa mbinu zote halali na kwa gharama zozote.


Ado Shaibu
KATIBU MKUU

22 Juni, 2020.
Dar es salaam.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK