Maazimio ya Kamati Kuu ya ACT Wazalendo iliyokutana 21 Januari 2023

TAARIFA KWA UMMA


MAAZIMIO YA KAMATI KUU MAALUM YA ACT WAZALENDO

Jana tarehe 21 Januari 2022, Kamati Kuu ya ACT Wazalendo ilikutana kwenye Kikao Maalum kilichofanyika katika ukumbi wa Juma Duni Haji, Makao Makuu ya Chama jijini Dar as Salaam kujadili hali ya Kiuchumi na Kisiasa nchini.

Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu imetoka na maazimio yafuatayo;-

1. Hali ya Kisiasa na Kiuchumi Nchini:

i) Kamati Kuu baada ya kupokea Taarifa ya Hali ya Kiuchumi nchini ambayo inaonesha hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu na kushamiri kwa migogoro ya ardhi, imetoa maelekezo kwa Kamati ya Wasemaji wa Kisekta (Baraza Kivuli la Mawaziri) kufanya uchambuzi wa kina wa hali ya nchi kiuchumi na hatua za kuchukua kuukwamua na uwasilishwe kwa umma na Kiongozi wa Chama Ndg. Zitto Kabwe.

ii) Kamati Kuu imetoa maelekezo kwa Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe kukamilisha uundwaji wa Kamati ya Kuisimamia Serikali kwa upande wa Zanzibar ili kuiwajibisha Serikali ya Zanzibar na kupaza sauti ipasavyo dhidi ya hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wa Zanzibar.

iii) Kamati Kuu ya ACT Wazalendo inazitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kuweka wazi kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya Ripoti za Vikosi Kazi vya Demokrasia.

iv) Kamati Kuu ya ACT Wazalendo inaitaka Serikali iweke wazi lini mchakato wa Katiba Mpya utaanza, hasa hatua muhimu za kupitiwa upya kwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Constitutional Review Act) na Sheria ya kura ya maoni; kuitishwa kwa Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa kuhusu Katiba (National Consultative Conference); kuundwa kwa Kamati ya Wataalam (Committee of Experts) wa kuandaa rasimu ya Katiba na kupigwa kwa kura ya maoni.

Aidha, Kamati Kuu inazitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, ziweke bayana kalenda na mchakato wa uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi. Kamati Kuu ya ACT Wazalendo inataka maelezo ya kina kuhusu uundwaji wa Kamati ya Uteuzi ya Wajumbe wa Tume za Uchaguzi NEC na ZEC (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Mkurugenzi na Wajumbe) na upatikanaji wa Wajumbe hao.

v) Kamati Kuu inamtaka Rais wa Zanzibar Ndugu Hussein Mwinyi kufanya maamuzi juu ya masuala yaliyoachwa kwenye Kikosi Kazi cha Zanzibar baada ya mashauriano na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Masuala hayo ni kuhusu kura ya mapema na mfumo wa kupatikana kwa Kamati ya Uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

2. Kuhusu Mwelekeo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK)

i) Kamati Kuu ya Chama imepokea Ripoti ya maoni ya wanachama na viongozi kuhusu mwelekeo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kisha imeyatafakari, kuyachambua na kuyafanyia maamuzi. Kamati Kuu imeelekeza Maamuzi hayo yawasilishwe kwa Barua rasmi kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, pamoja na kunakiliwa kwa Barua hiyo kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

ii) Kwa vile Chama kilipokea taarifa kutoka kwa wawakilishi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yamerejesha mahusiano mazuri na Zanzibar kutokana na uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Kamati Kuu imewaagiza viongozi wakuu wa Chama kuonana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na serikali zao kuwaeleza mwenendo wa sasa usioridhisha wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

iii) Kamati Kuu inamtaka Rais wa Zanzibar Ndugu Hussein Mwinyi kuweka wazi Ripoti ya Kikosi Kazi alichokiunda kushughulikia masuala ya demokrasia Zanzibar, kama ambavyo Ripoti ya Kikosi Kazi cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekwa wazi kwa umma na inapatikana kwenye tovuti. Penye nia ya dhati, masuala yanayogusa maslahi ya umma huwekwa wazi. Hakuna sababu inayohalalisha kufichwa kwa Ripoti ya Kikosi Kazi Zanzibar.

iv) Kwa kuwa kwenye vikao mbalimbali Rais wa Zanzibar Ndugu Hussein Mwinyi amekuwa akieleza kuwa hoja za maridhiano zitatekelezwa kwa ufanisi atakapochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Kamati Kuu imeweka muda wa utekelezwaji wa makubaliano baina ya Rais Mwinyi na Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad waliyoyafanya kabla ya ACT Wazalendo kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tunataka utekelezaji kwa vitendo wa Hoja Tatu zilizowasilishwa kwa Rais Mwinyi.

Mbali na hoja ya kuachiwa huru viongozi wa ACT Wazalendo waliokuwa mahabusu au wameshikiliwa kwa njia nyingine ambayo imetekelezwa, Kamati Kuu inataka hasa utekelezajwaji wa hoja ya kufanyika uchunguzi huru wa kimahakama (Independent Judicial Inquiry) kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kuwapatia fidia wahanga wa uchaguzi huo na kufanyiwa mapitio na mabadiliko mfumo wa uchaguzi na Mahakama wa Zanzibar.

3. Kuhusu Mikutano ya Hadhara:

Kamati Kuu ya Chama imeidhinisha Programu ya Mikutano ya Hadhara ya Kitaifa ya ACT Wazalendo itakayofanyika nchi nzima katika awamu mbalimbali.
Katika awamu ya kwanza, Programu ya Kitaifa ya Mikutano ya Hadhara inajumuisha Mikoa na maeneo ya Dar es salaam, Unguja, Pemba, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Selous, Tabora, na Kigoma kwa ratiba ifuatayo;-

1. Dar es Salaam 19 Februari 2023

2. Unguja 26 Februari 2023

3. Pemba 04 Machi 2023

4. Tanga 08 Machi 2023

5. Pwani 09 Machi 2023

6. Lindi 10 Machi 2023

7. Mkoa wa Kichama Selous 12 Machi 2023

8. Tabora 14-15 Machi 2023

9. Kigoma 16-18 Machi 2023

Awamu ya Pili ya Programu ya Mikutano ya Hadhara ya Kitaifa itatangazwa baadaye.

Ajenda kuu zitakazotawala na kuongoza mikutano ya ACT Wazalendo ni hali ya maisha ya Wananchi na Mageuzi ya Mifumo ya Kidemokrasia nchini.

Kamati Kuu imeelekeza kuwa mbali na ajenda nyinginezo muhimu, Mikutano ya Hadhara ya Chama pia itumike kutambulisha Ahadi za Chama chetu (ACT BRAND PROMISE) kwa Watanzania na Wazanzibari ambapo Chama kitachambua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi, namna watawala wameshindwa kuzitatua na kuonyesha sera mbadala za ACT Wazalendo kutatua changamoto hizo.

Chama kitazindua kaulimbiu yake mpya tarehe 18 Februari, 2023 jijini Dar es Salaam na tarehe 25 Februari, 2023 Zanzibar. Mkutano wa uzinduzi wa Mikutano ya Hadhara utafanyika Viwanja vya Mbagala Zakhem Dar es Salaam na kauli mbiu hiyo kutambulishwa rasmi kwa Watanzania. Vilevile, kaulimbiu ya Zanzibar itatambulishwa rasmi kwa Wazanzibari huko Nungwi tarehe 26 Februari, 2023.

Ado Shaibu,
Katibu Mkuu,
ACT Wazalendo,
22 Januari, 2022.
Dar es Salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK