MAELEKEZO YA OFISI YA KATIBU MKUU KUHUSU JANGA LA VIRUSI VYA KORONA (COVID-19) KWA VIONGOZI NA WANACHAMA WA ACT WAZALENDO NCHI NZIMA

Ndugu Viongozi na Wanachama wa ACT Wazalendo, awali ya yote napenda kuwapa pole nyingi kwa msiba mzito uliotukuta kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wetu wa Chama Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aipokee roho ya kiongozi wetu na kuiweka mahali pema peponi, Amina.

Tarehe 21 Januari 2021 Ofisi yangu ilitoa maelekezo maalumu kwenu yakihimiza kila mmoja wetu kuchukua tahadhari na hatua za kujilinda na kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya virusi hatari vya Korona kufuatia mlipuko wa awamu ya pili unaoendelea kote ulimwenguni. Tangu tulipotoa maelekezo hayo hadi sasa, janga hili limeendelea kutugharimu kwa kuchukua uhai wa wapendwa wetu kila siku ya Mungu. Tumempoteza Mwenyekiti wetu wa Chama kutokana na janga hili. Watu wengi nchini wanaugua na kuendelea kupoteza maisha kila siku.

Chama chetu pamoja na wadau wengine tumefanya jitihada mbalimbali za kuitaka serikali kuchukua hatua za kiuwajibikaji zinazopendekezwa chini ya miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwemo kutambua na kulichukulia janga hili kwa unyeti na udharura unaostahiki ili kuokoa maisha ya Watanzania, lakini ni wazi serikali haijali. Serikali haitaki kutambua rasmi uwepo wa tatizo. Inakwepa uwajibikaji juu ya suala hili. Tunachoshuhudia kutoka kwa serikali na viongozi wake wenye dhamana ni kukwepa uwajibikaji.

Mawaziri wa Afya wanahamasisha umma kujielekeza katika matumizi ya njia za kienyeji ambazo hazina ithibati kitaalamu na kitabibu juu ya usalama na ufanisi wake wa kukabiliana na virusi vya Korona. Sisi kama Chama tunaitazama na kuichukulia hali na vitendo hivi vya mawaziri na mamlaka zenye dhamana kuwa yenye mzaha mkubwa kwa maisha na uhai wa Watanzania. Serikali imeamua kutelekeza maisha ya wananchi katikati ya janga hatari linalopukutisha uhai wetu.

Hapana shaka tena hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 ndani ya nchi yetu ni ya kutisha. Hii inathibitishwa na kiwango cha vifo tunachokishuhudia.

Kwa hatua hii, Ofisi ya Katibu Mkuu inaelekeza ifuatavyo;-

•Viongozi na Wanachama mnasisitizwa kuendelea kuzingatia njia za kitaalamu zenye ithibati ya kisayansi katika kujikinga na kuwakinga wengine. Kwa waliobainika kuambukizwa, kuwahishwa hospitali ili kupata matibabu. Kila mmoja wetu tuendelee kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, na pia kuepuka misongamano.

•Kila Kiongozi au Mwanachama ambaye amempoteza ndugu yake kwa kifo kinachotokana na dalili za Covid-19, atoe taarifa kwa Katibu wa Chama wa Kata. Makatibu wa Majimbo wakusanye taarifa zote kutoka kwenye Kata na kuzifikisha katika Chama ngazi ya Mkoa. Ofisi ya Katibu Mkuu itakusanya taarifa hizo zilizotoka nchi nzima kwa Makatibu wa Chama wa Mikoa. Maagizo haya yasimamiwe na kufanyika vizuri.

•Chama kitatumia taarifa hizi kuchukua hatua muhimu za kuiwajibisha Serikali kwa uzembe wake wa kutowajibika ipasavyo na kusababisha vifo vya Watanzania.

Pamoja na Salamu za Chama: ACT Wazalendo, Taifa kwanza leo na kesho.

 

Ado Shaibu
Katibu Mkuu
ACT Wazalendo
22 Februari, 2021.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK