Tunachokisimamia

Mambo 30 kutoka kwenye ilani yetu

Mambo 30 MUHIMU kutoka Ilani ya ACT Wazalendo 2020 Kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

 1. Kufuta Sheria zote zinazobana, kuminya na kufifisha haki na uhuru wa Watanzania kujieleza na kutoa maoni, zikiwemo, Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya vyombo vya habari, Sheria ya Takwimu, kanuni ya maudhui ya mtandao na sheria nyingine kandamizi. Watu wote walioonewa kwa kubambikiwa kesi na kuthibitishwa hivyo na Tume ya Majaji itakayoundwa ndani ya siku 100, watalipwa fidia na kufutiwa rekodi zao za Jinai.
 2. Kuimarisha taasisi za kusimamia uwajibikaji kama Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT), Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kwa kuhakikisha mchakato wa uteuzi wa wakuu wa Taasisi hizo unaidhinishwa na Bunge baada ya uteuzi wa Rais. Jeshi la Polisi litafanyiwa marekebisho makubwa kutoka Police Force kuwa Police Service. Itamrejesha kazini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad ili kumaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba.
 3. Kufufua mchakato wa Katiba Mpya na kuwashirikisha Watanzania katika uundwaji wake. Itaboresha Muundo wa Muungano ili kuwa na Muungano wa Usawa, wa Haki na wenye Kuheshimiana, na kusimamia uundwaji wa muundo wa Serikali tatu. Watanzania watakuwa na Haki ya Uraia pacha.
 4. Kufuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kulipa Ada ya Masomo (Tuition Fee), Fedha za Vitabu (Stationeries), na gharama za Mafunzo kwa Vitendo (Field Studies/Internship) kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye Chuo Kikuu. Kutunga Sheria kuhakikisha kuwa Mikopo ya Elimu ya juu itakuwa ni kwa ajili ya gharama za kujikimu tu (Meals & Accomodations). Kufuta mikopo yote ya wahitimu wote watakaoingia mikataba maalum na Serikali ya kufanya kazi kwa miaka mitatu mfululizo katika maeneo ya pembezoni na yenye mazingira magumu ya kazi, kwa zile sekta mahsusi (Mfano Utabibu na Ualimu, Maafisa Ugani kwa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi nk). Kurasmisha na kulipia mafunzo kwa vitendo (paid internship), kwa fani zote kwa kipindi kisichopungua miezi sita ili wanafunzi wote wapitie mafunzo kwa vitendo kikamilifu, vilevile kuweka utaratibu wa kutumia matokeo ya mafunzo kwa vitendo katika utoaji ajira ili kuhimiza wanafunzi kuona umuhimu wa mafunzo kwa vitendo. Itaweka vivutio maalum vya kikodi kwa makampuni binafsi yatakayotoa nafasi kwa vijana waliohitimu kufanya mafunzo kwa vitendo.
 5. Kuboresha mfuko wa Bima ya Afya kwa kuunganisha na mifumo ya Hifadhi ya Jamii, ili kila Mtanzania anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya Afya moja kwa moja. Kwa mfumo huu, mfuko wa Bima ya Afya utaweza pia kupata fedha kwa wakati na kulipa watoa huduma kwa wakati. Bima ya Afya ni haki ya kila Mtanzania. Itaisimamia kikamilifu haki ya kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya yenye kumpa kinga ya matibabu bila kujali hali yake ya kiafya (wakati wa kujiunga na bima).
 6. Kuwekeza kiasi cha  shilingi Trilioni 10 ndani ya miaka mitano, wastani wa Shilingi Trilioni 2 kwa kila mwaka, kwenye kumaliza kabisa tatizo la maji safi na salama kwa Wananchi. Hii ni pamoja na kujenga na kupanua miundombinu ya maji safi na maji taka. Fedha hizi zitatoka kwenye Mapato ya Ushuru Maalumu wa Maji kwenye kwenye matumizi ya Mafuta ya Petroli.
 7. Kurejesha Mradi wa Gesi Asilia (LNG Plant) kwa kuharakisha mazungumzo na wawekezaji na kuondoa vikwazo vyote ili kuwezesha nchi yetu kuwa mzalishaji mkubwa wa gesi katika Afrika, kuongeza ajira kutokana na viwanda na huduma na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo nje ya Gesi Asilia.
 8. Kupunguza michango kwenye hifadhi ya jamii kutoka asilimia ishirini (20%) ya sasa mpaka asilimia kumi na mbili (12%), kwa mchanganuo wa asilimia tisa (9%) kuwa mchango wa akiba ya hifadhi ya jamii, asilimia mbili (2%) kuwa mchango wa Bima ya Afya, na asilimia moja (1%) kuwa mchango wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF).
 9. Kutengeneza ajira zenye tija milioni kumi (10) ndani ya miaka mitano. Ajira million tano (5) kutoka kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo, ajira million 2 kutoka sekta rasmi na ajira milioni 3 kutoka sekta isiyo rasmi.
 10. Kurekebisha sera za kodi ili kuirejesha katika hali yake ya kawaida sekta ya Utalii pamoja na mnyororo wake ambayo imeathirika sana na janga la COVID 19. Marekebisho hayo yatahusisha kutoa ruzuku kwa Kampuni za Utalii na kulinda Ajira za Wafanyakazi wa Sekta ya Utalii.
 11. Kuwekeza kwenye Ujenzi wa miundombinu ya Maeneo ya Utalii ili kufungua vivutio vipya na kuvifanya kufikika kwa urahisi na kwa usalama. Itawezesha Sekta Binafsi kuongeza vyumba vya mahoteli kwenye vivutio vya Utalii. Itaanzisha kampeni Maalumu ya kufikisha Idadi ya Watalii Milioni 5 watakaoingia nchini ifikapo Mwaka 2025. Itatumia sekta ndogo za Michezo na Burudani kimkakati kama nyenzo za kukuza Utalii nchini.
 12. Kusimamia kuhakikisha kuwa Uwekezaji wa eneo la kiuchumi la Bagamoyo unatekelezwa. Kuimarisha Bandari ya Mtwara ili kuhudumia korido ya maendeleo ya Mtwara (Mtwara Corridor), ambayo inahusisha mradi wa Mchuchuma na Liganga na Usafirishaji wa Bidhaa kutoka na kwenda katika nchi ya Malawi na kaskazini mwa nchi ya Msumbiji. Vilevile, Kuufanya Mji wa Mtwara kuwa kituo cha huduma kwa miradi ya uwekezaji wa mafuta na gesi, kusini mwa Tanzania na Kaskazini mwa Msumbiji.
 13. Kubadili mfumo wa umiliki ili uwekezaji kwenye madini kuwa ni kwa utaratibu wa kugawana mapato (Production Sharing Agreement) kati ya mmiliki na mwendeshaji (Contractor). Itaweka kisheria utaratibu wa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye madini kutoa idhini ya mradi wa uchimbaji madini kabla ya kuanza kutekelezwa (Free Prior Informed Consent). Itaweka mkazo kwenye miradi ya uchimbaji madini ambayo ina faida kubwa ya fungamanisho, miradi mikubwa miwili ya kipaumbele itakuwa ni Mradi wa Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa, mkoani Njombe, na mradi wa Kabanga Nickel wilayani Ngara, mkoani Kagera.
 14. Kusimamia kukamilika kwa uwekezaji wa mradi wa Mchuchuma na liganga kuzalisha bidhaa za chuma, madini ya vanadium na madini mengine, umeme wa makaa ya mawe na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
 15. Kusimamia Ujenzi wa mabwawa makubwa 5 ya kuzuia mafuriko na kujenga skimu kubwa za umwagiliaji zenye jumla ya hekta 1,000,000.
 16. Kutekeleza Ujenzi wa miradi ya maji nchi nzima kuhakikisha kila mtanzania anapata maji safi na salama kutoka mapato ya ushuru wa mafuta na kwa kutumia mfumo wa “development finance” ili kumaliza kabisa tatizo la maji safi na salama.
 17. Kuwezesha Ujenzi wa barabara ya korosho (cashew ring road) – Nangurukuru – Liwale – Nachingwea – Masasi – Newala – Tandahimba – Mtwara – Lindi - Nangurukuru kutoka mapato ya ushuru wa korosho kwa kutumia mfumo wa “development finance” ili kufungua wilaya zinazolima korosho. Vile vile kufungua Wilaya ya Liwale kwa kufungua barabara za Songea-Liwale na Liwale-Morogoro.
 18. Kusimamia uwekezaji wa eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo ili kuifanya Tanzania kuwa kituo cha usafirishaji wa majini katika Afrika na eneo la maziwa makuu, kuongeza ajira na mapato ya fedha za kigeni.
 19. Kusimamia kukamilika kwa Uwekezaji wa kinu cha kuchakata gesi asilia (LNG) ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni, ajira na maendeleo ya viwanda nchini.
 20. Kusimamia kukamilika kwa Uwekezaji wa mradi wa uchimbaji madini ya Nikeli katika eneo la Kabanga, wilayani Ngara, mkoani Kagera.
 21. Kufanya uchambuzi wa kina kwa miradi inayoendelea sasa, kama vile mradi wa Reli ya Kati (SGR), Mradi wa Umeme wa Maji Mto Rufiji (Nyerere|Stiglers Gorge), na Ufufuaji wa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL), kwa kutumia wataalamu wa ndani na wa nje, kuhusu namna bora ya kutekeleza miradi mikubwa kwa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma, kwa kuzingatia muda wa miradi husika kuanza kuzalisha mapato ya kulipia madeni ya ununuzi/ujenzi wake. Lengo la uchambuzi huu ni kuiondoa Serikali kwenye angalau 50% ya gharama za utekelezaji ili kuelekeza rasilimali fedha kwenye miradi ya huduma za jamii, kama elimu, maji na afya, na kwenye miradi itakayochochea maendeleo ya watu, kama kilimo cha umwagiliaji.
 22. Kujenga mazingira ili kukuza shughuli za uchumi, kupanua wigo wa kodi na kuingiza watu wengi zaidi kwenye kulipa Kodi ili kufikia lengo la uwiano wa mapato ya Kodi kwa Pato la Taifa (Tax/GDP ratio) kufikia 25% ifikapo mwaka 2025.
 23. Kuweka vivutio vya kikodi ili kuwezesha sekta binafsi kujenga miundombinu wezeshi na muhimu kwa mfumo wa ubia. Hii itaipa Serikali pumzi ya kujielekeza kwenye kutoa huduma muhimu kwa Wananchi, kuepuka kuongeza Deni la Taifa na kukuza Sekta Binafsi.
 24. Kutunga sera za kikodi ili kuhami sekta ya Utalii na mnyororo wake ambao umeathirika sana na janga la Covid 19. Hii ni pamoja na kulinda Ajira za Wafanyakazi wa Makampuni ya Utalii kwa kutoa ruzuku kwa kampuni zote zitakazoendeleza mikataba na Waajiri na kuruhusu Wafanyakazi waliokosa kazi kulipwa Fao la kukosa Kazi kutoka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
 25. Kuweka vivutio vya kibajeti na kikodi kwenye Miradi yote ya Kilimo cha Umwagiliaji na Viwanda vyote vya kuongeza thamani ya mazao ya Kilimo.
 26. Kuweka muundo mzima wa makato kutoka kwenye mapato ya waajiri na wafanyakazi ili kuchochea matumizi kwenye uchumi, kwa kupunguza PAYE kima cha chini  mpaka asilimia nane (8%) kutoka asilimia tisa (9%) ya sasa.
 27. Kufanya marekebisho ya Tozo ya kuongeza Ujuzi (Skills Development Levy) kwa kupanua wigo wa makusanyo kuhusisha sekta ya Umma na kushusha kiwango cha malipo mpaka 2% tu.
 28. Kupunguza makato ya Bima ya Afya, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi WCF mpaka asilimia kumi na mbili (12%) kutoka asilimia ishirini na tatu (23%) ya sasa. Hivyo kupunguza jumla ya makato kutoka asilimia thelathini na mbili (32%) ya sasa mpaka asilimia ishirini tu (20%).
 29. Kuimarisha sheria ya kuzuia ukwepaji wa Kodi wa Makampuni ya Kimataifa ili kuokoa Mapato sawa na 5% ya Pato la Taifa ambayo yanapotea kupitia mbinu za kihasibu zinazofanywa na Multinational Corporations. Kuwezesha hili Serikali itaingia mikataba ya kimataifa inayosadia mataifa kuzuia ukwepaji wa kodi.
 30. Ilani hii imetoa ahadi ambazo zitahitaji Fedha ili kutekelezwa. Jumla ya Shilingi Trilioni 130 zitatakiwa kuwekezwa nchini ili kutekeleza miradi mikubwa Fedha za Uwekezaji huu mkubwa na uendeshaji wa Serikali kwa ujumla zitatoka maeneo yafuatayo:
 • Uwekezaji wa Sekta Binafsi katika Miradi ya Mchuchuma na Liganga, Kinu cha kuchakata Gesi Lindi, Kabanga Nickel, Vinu za kuzalisha Umeme kutoka Gesi Asilia na Eneo la Uchumi la Bagamoyo. Hii ni miradi itakayoingiza nchini Fedha za Kigeni (FDI) na kuongeza uwezo wa Nchi kupata mapato ya ndani. Wajibu wa Serikali utakuwa ni kuweka mazingira mazuri na sera zinazotabirika (stable fiscal regime).
 • Gharama za Elimu Ufundi na Elimu ya Juu zitatokana na Tozo ya kuongeza ujuzi ( Skills Development Levy ) ambayo baada ya marekebisho ya kupanua wigo wa walipaji itakuwa na uwezo wa kukusanya shilingi Bilioni 470 kila Mwaka na kuongezeka kulingana na kuongezeka kwa shughuli za Uchumi Nchi.
 • Gharama za Ujenzi wa Miradi ya Maji zitagharamiwa na Tozo Maalumu ya Matumizi ya Mafuta ya Petroli. Serikali itachukua Mkopo nafuu wa Muda mrefu wa Shilingi Trilioni 10 kutoka Benki za Maendeleo ili kutekeleza mradi mara moja na Mapato ya ‘fuel levy’  yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa. Tozo ya shilingi 200 kwa kila lita ya Mafuta itazalisha Jumla ya shilingi Bilioni 700 kila Mwaka zinazoweza kutumika kulipa mkopo wa muda mrefu wa miaka 15.
 • Gharama za Ujenzi wa Barabara ya Korosho (Cashew Ring Road) zitalipiwa na 50% ya Mapato ya Ushuru wa Korosho (exports levy) ambapo Serikali itachukua mkopo nafuu wa muda wa kati ili kupata fedha za ujenzi wa barabara hiyo mara moja na mapato ya exports levy yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa. Ushuru wa Korosho unakadiriwa kuingiza mapato ya zaidi ya shilingi Bilioni 245 kila Mwaka ambazo nusu yake inaweza kulipa mkopo wa barabara hiyo na barabara za Songea-Liwale na Liwale-Morogoro kwa muda wa miaka 10.
 • Gharama za Miradi mikubwa ya Umwagiliaji zitalipiwa kutoka uwekezaji wa skimu ya hifadhi ya jamii kwa Wakulima kama uwekezaji wa Skimu wa muda mrefu.
 • Gharama nyengine zote zitaweza kulipwa na Serikali kutokana na mapato ya ndani ikiwemo kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma ikiwemo madeni ya miaka 5 iliyopita, uboreshaji wa mfumo wa utoaji haki nchini (criminal justice system), kulipa madeni ya mapato ya Zanzibar kutoka mgawo wa mapato ya muungano ambao haukuwa ukilipwa kwa miaka yote ya nyuma na fidia kwa watu wote waliobambikiwa kesi katika utawala wa awamu ya tano.

Jiunge na ACT Wazalendo uwe sehemu ya mabadiliko Haya kwa Nchi yetu. Ilani Hii ndio pekee katika Ilani zote za Vyama ambayo imeonyesha Gharama za utekelezaji na wapi Fedha zitatoka kutekeleza.

Rudi kwenye ilani

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK