Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ivunjwe. WanaNgorongoro washirikishwe ipasavyo.

TAARIFA JUU YA SUALA LA KUHAMISHA WAFUGAJI WA JAMII YA MAASAI KATIKA HIFADHI YA NGORONGORO
UTANGULIZI

Ndugu Wanahabari,

Ngorongoro ni eneo la shughuli mtambuka. Kiutawala ni Tarafa mojawapo ya wilaya ya Ngorongoro yenye vijiji 25 na Kata 11. Kiuhifadhi, eneo hili linasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa matumizi mseto ya Uhifadhi, Maendeleo ya Jamii na Utalii. Eneo hili limekuwa gumzo kubwa kwa muda mrefu kuhusu ufanisi wa matumizi ya ardhi mseto.

Wahifadhi kwa upande moja wamekosoa wazi wazi kuwa huu mfumo mseto wa matumizi ya ardhi umeshindwa kustawisha uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii kwa pamoja.

Kwa kudhihirisha hoja yao hii, wahifadhi wamewekeza taaluma na raslimali nyingi katika tafiti mbalimbali zinazoegemea uhifadhi zaidi huku zikikwepa tafiti zinazoelezea ujuzi asilia na maendeleo ya jamii na kusababisha hitaji la kubadilisha sheria ya mamlaka ya hifadhi na mapendekezo ya mpango mbadala wa matumizi ya ardhi unaopendelea zaidi uhifadhi kwa madai ya ukuaji na ongezeko la watu na mifugo.

Hii imepelekea kugawa jamii ya Ngorongoro katika makundi mawili – wakazi wenyeji na wahamiaji haramu huku mapendekezo haya yakielekea zaidi katika kupunguza idadi ya watu ndani ya eneo hili.

Kwa upande wa pili, jamii ya Ngorongoro imekuwa ikilalamika kuwa tafiti hizo na mbadiliko ya sheria ikiwemo mapendekezo ya matumizi ya ardhi yamefanyika bila kuwashirikisha na bila kuzingatia tafiti juu ya uhusiano wa ustawi wa eneo la Ngorongoro na maisha asilia ya jamii ya wafugaji katika eneo hilo.

Jamii ya Ngorongoro imeilaumu mamlaka hiyo kwa kushindwa kusimamia ipasavyo mfumo mseto wa matumizi ya ardhi na kuishia kutuhumu jamii na kusababisha uharibifu wa eneo la hifadhi.

Pia inatuhumu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutowekeza na kutozingatia tafiti za kitaalamu juu ya namna mahusiano ya uhifadhi yanavyotegemea jamii ya wafugaji katika uwepo wake. Hii ni pamoja na kushindwa kutafiti ukaribu wa wafugaji na wanyama pori na mahusiano yao ya kila siku na jamii ya wafugaji.

Ndugu waandishi,

Mgongano huu wa kimatazamo umekuwa chanzo cha sintofahamu ya muda mrefu kati ya jamii na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Jamii imelalamika kutengwa katika usimamizi wa eneo hili na kuonekana kama waharibifu badala ya wadau muhimu na pengine wa lazima katika kufanikisha usimamizi wa eneo lenyewe.

Jamii ya wafugaji wakazi wa eneo hili kwa muda mrefu sana, wameomba kushirikishwa katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya usimamizi wa eneo, kushirikishwa katika tafiti mbalimbali na utengenezwaji wa mpango wa kusimamia eneo zima maarufu kama GMP (General Management Plan). Juhudi za jamii kuomba kushiriki katika kutambua na kutatua changamoto zinazoikabili Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zilionekana kugonga mwamba kwa muda mrefu.

1. HISTORIA

Eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ni ardhi inayomilikiwa kimila na wafugaji. Kuna vijiji 25 ndani ya eneo hilo ambavyo hadhi zao siyo tofauti na vijiji vyote Tanzania.

Mwaka 1958 Serikali ya kikoloni ya Tanganyika iliwahamisha kimabavu Wamaasai kupisha kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye ukubwa wa Km za mraba 15,000 WaMaasai walibakiwa na eneo dogo (8,100 km2), la iliyokuwa ardhi yao, yaani NCA. Pamoja na hayo wafugaji hao wanatumia ardhi hiyo na wanyamapori na watalii.

Serikali ya Kikoloni iliahidi mwaka 1958 kuwa haitawahamisha tena wa Maasai kutoka Ngorongoro. Mwaka 1975 sheria ya Ngorongoro iliunda Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) – Game Parks Miscilleneous Amendment Act 1975 na kuipa hadhi ya mtu kisheria aneyeweza kushtaki na kushtakiwa kwa jina lake, mamlaka yenye kazi/majukumu (Functions) baadhi ni kama yafuatayo;

a. Kuhifadhi na kuendeleza Maliasili katika Hifadhi

b. Kuhamasisha utalii na kuendeleza miundombinu ya utalii ndani ya Hifadhi.

c. Kulinda na kuendeleza maslahi ya Watanzania, Jamii ya Maasai wanaojishughulisha na ufugaji ndani ya Hifadhi
Lakini tangu kuanzishwa kwake Mamlaka ya Ngorongoro imekuwa katika mgogoro mkubwa na jamii ya wafugaji wanaoishi katika hifadhi hiyo.

Matatizo ya sasa ya Ngorongoro yanatokana hasa na Sheria ya 1975. Sheria hii ni chanzo cha matatizo kwa kutekelezwa lakini pia kwa kutotekelezwa.

2. MASUALA (ISSUES)

Ndugu waandishi wa habari,

Masuala na changamoto zinazowakabili Wamasai waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ni kama ifuatavyo;

Mosi, ni Mamlaka Makubwa ya NCAA mamalaka haya ni makubwa yanaifanya Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro kuwa kama ni nchi ndani ya nchi. NCAA ina Mamlaka ya kutunga Sheria (legislative powers).

Mamlaka ya kitawala na kipolisi (Executive and police powers) kama vile kukamata mali, mifugo, mamlaka ya kukamata watu (arrest) bila warranti, kuingia kwenye ardhi ya mtu n.k. Mamlaka ya Kimahakama (Quasi- Judicial) na Mamlaka Mtambuka ndani ya hifadhi NCAA, Rais, Tamisemi, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Ardhi. Katika Mamlaka haya wananchi hawashirikishi wala kushiriki.

Pili, ni Kukosekana kwa haki za Ardhi na uhakika wa miliki ya Ardhi. Wanavijiji katika vijiji 25 wana haki ya Ardhi kama walivyo watanzania wengine (customary right of occupancy) tofauti na mamlaka zinavyopotosha, sheria za ardhi zinawapa haki hiyo na wananchi wa Ngorongoro wana haki ya ulinzi wa kikatiba wa ardhi na mali zao. Lakini tumeshuhudia kwa miongo 4 sasa kila wakati wananchi wakitishwa kuhamishwa kwa nguvu kutoka kwenye ardhi yao na mamlaka husika.

Tatu, ni Kukosekana kwa Haki ya Kushiriki na Kushirikishwa katika maamuzi. Muundo wa sasa wa Bodi ya Mamlaka hautoi nafasi ya wananchi kushiriki katika maamuzi. Mhifadhi ana mamalaka zaidi na bodi yake.

Nne, ni Kukosekana kwa Haki ya kujiendeshea Shughuli za Maisha (Right to livelihood) – kuzuia Kilimo cha vibustani, Mifugo kukamatwa, nk

Tano, Kukosekana kwa Uhuru wa Kujihusisha/kujiunga (Freedom of Association).

Sita, Kukosekana kwa Uhuru wa Kukusanyika (Freedom of Assembly).

Saba, Kukosekana kwa Uhuru wa Kujieleza (Right to Freedom of Expression) Ambapo kumekuwa na matukio ya waandishi wa habari kukamatwa, kuzuiwa. Sambamba na hilo watafiti kunyimwa vibali vya kutafiti na kuingia kufanya mahojiano na wakazi wa ngorongoro.

Nane, Ongezeko la shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na hoteli na magari. Kuna hoteli lukuki Ngorongoro zilizojengwa kwenye maeneo tete ikiwemo Ukingo wa Kreta ya Ngorongoro. Zingine zimejengwa kwenye mapario ya wanyamapori na mifugo.

Tisa, Kukosekana kwa uhakika wa chakula ambalo ni jukumu la mamlaka.

Kumi, Ukosefu wa uhakika wa Maji ambalo ni jukumu la Mamlaka.

Kumi na Moja, Ubovu wa Barabara na miundombinu yake.

Kumi na Mbili, Ukosefu wa huduma za Afya kama Zahanati na Vituo vya Afya.

Ndugu Wanahabari,

Masuala hayo kwa kiasi kikubwa unaona yanahusiana na Mamlaka na majukumu ya Mamlaka ya Ngorongoro kutumika vibaya au kutotekeleza majukumu yao sawasawa. Wananchi kwa upande wao wana jukumu la kulinda wanyama pori na uhifadhi.

Tofauti na mengi mliyoyasikia katika majuma haya mawili, wananchi wa Ngorongoro wameendelea kuwa ni wahifadhi namba moja na hili linathibitishwa kwa idadi ya wanyama katika hifadhi hasa Faru weusi ambao wamebaki katika Hifadhi hii pekee wakati walikuwepo katika hifadhi zote.

Pia madai yanayotolewa na Mamlaka, Wabunge na baadhi ya watu kuwa wananchi hao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi ni kichekesho kwa sababu wanaotakiwa kutoa huduma hizo ni Mamlaka ya Ngorongoro kwa mujibu wa Sheria.

Mamlaka imeshindwa kutekeleza majukumu yake na badala ya kulaumiwa na kulazimishwa kutoa huduma hizo inawatupia lawama wananchi.

3. MAPENDEKEZO
Ndungu Waandishi,

ACT wazalendo inatoa mapendekezo yafuatayo ili kufikia Ngorongoro Endelevu;

Pendekezo la Kwanza:

Tunapendekeza Kuwe na Majadiliano (Dialogue) ya pande mbili kati ya Serikali (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) kwa upande mmoja na Jamii yaani wawakilishi wa wenyeji wanaoishi ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa upande wa pili.

Majadiliano haya yafanyike kwa namna ifuatayo;
Hatua ya kwanza; Utambuzi na uchambuzi yakinifu wa pamoja wa changamoto zilizopo ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Wizara ya Maliasili na Utalii iitishe mkutano wa wadau wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro utakaohusisha pande mbili kwa idadi sawa yaani,
• Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
• Wawakilishi wa wenyeji wanaoishi ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mkutano huu utakuwa jumuishi na utahudhuriwa na washiriki kutoka Serikalini (pamoja na taasisi zake muhimu) na jamii kwa uwakilishi watakaoufanya wenyewe. Washiriki wa mkutano huu kwa upande wa jamii wajichague wenyewe kulingana na makundi wanayotoka (self-selection).

Inamaanisha kuwa washiriki wachaguliwe na kila kundi wanalowakilisha. Lazima kuwepo na wawezeshaji wawili (mmoja atokane na jamii ya Ngorongoro na mwingine Serikalini) watakaondesha mkutano huo ili kuwezesha ukusanyaji wa maoni.

Katika mkutano huu wa awali, washiriki watatumia fursa hii ya kukutana pamoja kubainisha na kukubaliana juu ya masuala yanayohitaji kuzungumziwa au kujadiliwa ambayo washiriki wanaona kama changamoto zinazokabili eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro katika sekta za maslahi ya jamii, uhifadhi na utalii.

Katika mkutano huu, pia washiriki wote kwa umoja wao watapendekeza na kuunda Timu ndogo yenye wajumbe wenye idadi sawa kati ya Jamii na Serikali waliochaguliwa na kundi lao kuandaa Hadidu za Rejea. Wajumbe wa Timu hii watawajibika kwa chombo/kundi lililowachagua.

Hatua ya Pili; Kuunda Timu ya Kuandaa Hadidu za rejea na Kukubaliana mambo ya msingi katika hadidu za rejea.
Tunapendekeza kwamba kabla ya kazi ya kukusanya maoni au baada ya kukubaliana juu ya hoja za msingi za changamoto za Ngorongoro, pande hizi mbili yaani Serikali pamoja na wananchi kwa pamoja watengeneze hadidu za rejea zitakazosaidia kuthibitisha changamoto zilizotambuliwa katika kikao cha pamoja kilichozungumziwa katika hatua ya kwanza hapo juu. Timu iundwe yenye uwakilishi sawa wa wajumbe waliochaguliwa na kila upande ili ikatengeneze hadidu za rejea.

Pamoja na kwamba timu hii iliyoteuliwa itatengeneza hadidu za rejea, tunapendekeza na kutoa angalizo zifuatazo:

a) Hadidu za rejea zinazopendekezwa zirejee na kuzingatia HOJA zilizoibuliwa na kukubaliwa kwenye mkutano wa wadau;

b) Hadidu za rejea zizingatie mchakato wa kidemokrasia na wa kisheria kukusanya taarifa kwa kuitisha mikutano halali kutoka Halmashauri ya Wilaya, vijiji, viongozi wa jadi, Mamlaka za Wilaya Jirani, makundi maalum kama vile wanawake na vijana, na taasisi za kiraia za wafugaji.

c) Utengewe muda maalum wa uandishi wa hadidu za rejea ili ziwasilishwe tena kwa wadau kwa ajili ya uthibitisho.

d) Tunapendekeza kuwa, uitishwe mkutano wa pili wa wadau wenye lengo la kupitia na kuridhia hadidu za rejea na iwe na wenyeviti wenza wawili na watoa taarifa wawili kutoka kila upande

Baada ya wadau kuridhia hadidu za rejea, watapendekeza na kuunda timu ya kutembelea jamii, kukusanya na kuchakata maoni na baadaye kuandika ripoti ya mwisho. Timu hii itakayoundwa kwenye mkutano wa pili wa wadau itakuwa na wenyeviti wenza wawili kuwakilisha Jamii na Serikali. Aidha, tunapendekeza kuwa makundi yote mawili wakilishwa washiriki katika hatua zote za mchakato. Tunashauri kuwa utengwe muda wa kutosha kufikia jamii, kukusanya, kuchakata maoni, kuandika ripoti na kuwasilisha kwa wadau.

Hatua ya Tatu; Mkutano wa wadau kupitia na kuridhia ripoti ya mwisho.
Kuwepo na mkutano wa wadau kupokea na kuridhia ripoti. Mkutano huu utanguliwe na mikutano ya ngazi za vijiji, na Baraza la Wafugaji ili kuruhusu makundi yote ya jamii kupata ufahamu wa kina na kuridhia yaliyomo katika ripoti. Hata hivyo, ripoti itakuwa halali ikiwa itathibitishwa (validation) na wadau wote wa lazima na kutiwa saini na kuidhinishwa na wenyeviti wote wawili. Hakuna maamuzi yoyote yatakayofanywa bila makubaliano ya pande zote mbili (Jamii na Serikali).

Pendekezo la pili;

Tunapendekeza Mamlaka ya Uteuzi itengue uteuzi wa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro Daktari Freddy Manongi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hadi kupelekea Wakaazi wa Hifadhi ya Ngorongoro kukosa huduma muhimu kama maji safi na salama, chakula, barabara na huduma za afya.

Pia Kumekuwa na malalamiko ya Wamasai waishio ndani ya hifadhi juu ya Unyanyasaji wanaofanyiwa kwa amri ya Mhifadhi. Ikumbukwe kuwa Bwana Manongi ameshatimiza miaka 60 ya kustaafu toka mwaka 2021, ni wakati muafaka sasa akapumzishwa. Ni vema wakati wa majadiliano Jamii ikafanya majadiliano chini ya uongozi mpya.

Pendekezo la tatu;

Tunapendekeza kwa Mamlaka ya Uteuzi kuwa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ivunjwe kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake na kuishauri serikali ipasavyo juu ya Hifadhi hii.

Pendekezo la Nne;

Tunapendekeza Serikali iachane na Mapendekezo yote yaliyotolewa katika Ripoti ya Matumizi Mseto ya Ardhi ya Ngorongoro yaani The Report on Multiple Land Use Management Plan ikiwa ni pamoja na pendekezo la kuondoa watu katika hifadhi ya Ngorongoro. Ripoti hiyo iliandaliwa bila ushirikishwaji wa Jamii ya Wamaasai waishio Hifadhini na wadau wa uhifadhi.

Pendekezo la Tano;

Tunapendekeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ivunjwe na badala yake iundwe Kampuni yenye kumilikiwa kwa Ubia kati ya Wananchi Waishio Ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na Serikali. Wananchi wamiliki 51% na Serikali 49%. Uendeshaji wa kampuni hii uwe mikononi mwa Serikali.

Mwisho;
Chama cha ACT Wazalendo, tunapenda kutumia fursa hii kwanza kuwaomba radhi jamii yote ya Wamaasai hasa wale waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lugha chafu, dhihaka, kejeli, dharau na kutweza, iliyotumika wakati wa sakata hili.

Tumeshuhudia ndani ya Bunge, kwenye vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii jinsi mjadala juu ya suala hili ulivyokosa staha dhidi ya Wamaasai

Tunakemea vikali lugha na kauli hizo. Tunaomba vyombo vya habari viandike au kutoa taarifa kwa weledi na kuhoji watu wenye weledi juu ya jambo hili na sio kila mtu anayejitokeza bila kuangalia rekodi za mtu huyo. Vyombo vya habari vifuate misingi ya taaluma yao ya habari.

Kuhusu Wabunge na Bunge la Jamhuri ya Muungano, tunaomba wananchi mfuatilie hoja zao, kauli zao dharau zao na kejeli zao ili ifikapo muda muafaka 2025 mfanye maamuzi sahihi kadri ya mnavyoona.


Imetolewa na:

Bonifasia Aidan Mapunda
Msemaji Sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi
ACT Wazalendo
15 Februari, 2022.
Dar es salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK