MIAKA 30 YA VYAMA VINGI NCHINI: NAFASI YA VYAMA VYA SIASA NA HATMA YA MAPAMBANO KUTETEA MASLAHI YA UMMA

Miaka 30 ya Vyama Vingi Nchini: Nafasi ya Vyama vya Siasa na Hatma ya Mapambano Kutetea Maslahi ya Umma.

Na. Dorothy Jonas Semu,

Tanzania inatimiza miaka 30 tangu kurejeshwa rasmi kwa siasa za vyama vya vingi nchini. Ambapo Julai, 1992 serikali ya Tanzania iliweka wazi kurejesha mfumo wa siasa za vyama vingi, kisha mwaka 1995 ulifanyika uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vya upinzani.

Andiko hili ni muendelezo wa utamaduni wa kutathmini mwenendo na mchango wa vyama vingi ambapo wadau, wachambuzi na wataalam mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao katika kupima mwelekeo, kuelezea historia, mafanikio na changamoto zinazoukumba mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu kurejeshwa kwake tena.

Ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba ndani ya miaka hii 30, mchango wa siasa ya vyama vingi hususani vyama vya upinzani umesaidia kuleta urari (balance) wa madai na matarajio ya wananchi dhidi ya vitendo vya watawala kuhusu haki za kiuchumi, kijamii na kiraia. Mfumo wa vyama vingi kwa sehemu kubwa umetoa mchango katika uendeshaji wa siasa, mifumo ya chaguzi, kutengeneza majukwaa ya kujadiliana, kubishana na kukosoana.
Mfumo wa vyama vingi, umesaidia kuwaleta wananchi pamoja na kuamsha hamasa ya kufuatilia mwenendo, kauli, matamko ya viongozi, sera na sheria mbalimbali nchini. Uzoefu na ushahidi wa kihistoria pia unaonyesha kuwa hata siasa za kibunge zilionyesha kukua na kuondoa siasa za uadui ambapo wabunge kutoka vyama vya upinzani walitumia bunge kuibua mijadala ya kitaifa kupitia vikao rasmi vya Bunge na kuikosoa Serikali bila kupepesa macho.

Ipo mifano mingi mikubwa imeandikwa na wachambuzi mbalimbali kama vile hoja za mgodi wa Buzwagi, uliowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Ndg. Zitto Zuberi Kabwe mwaka 2007, tuliona namna ulivyoibua mijadala katika jamii juu ya rasilimali za madini na hatima ya taifa letu kwa ujumla. Kutokana na hoja hiyo Serikali ilifanya mabadiliko ya sheria za madini mwaka 2010.

Vilevile, hoja za kashfa za Richmond na Tegeta Escrow nazo zilishikiliwa kwa sehemu kubwa na vyama vya upinzani hadi kupelekea mabadiliko makubwa, kuwajibika kwa Viongozi na hata kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Ndugu Edward Lowassa.

Aidha, yapo mabadiliko ya sheria yaliyokuwa yanaonekana kuwakandamiza wananchi, Serikali imekuwa ikipata upinzani mkubwa kutoka vyama vya siasa. Kwa ufupi, katika kutazama historia ya vyama vingi (1992), ni wazi kuwa vyama vya upinzani vimekuwa jukwaa la kutoa upinzani kwa sera, sheria, maamuzi na vitendo vinavyofanywa na Serikali vikizingatia maslahi ya wananchi.

Kisha, Kuingia kwa Magufuli 2015-21:

Tangu kuasisiwa kwa siasa za vyama vingi, kama wengi wanavyopenda kuita ‘siasa za mageuzi’ kulikuwa na mwelekeo wa ukuaji mzuri wa uendeshaji wa siasa na vyama vya siasa. Ushiriki wa wananchi kwenye siasa na uongozi, ulikuwa unapiga hatua mbele mwaka hadi mwaka, changamoto zilizokuwepo wakati siasa za vyama vingi ziliporejeshwa tena, zilikuwa zinatatuliwa kutokana na maoni ya wadau mbalimbali. Vijana na wanawake ambao kwa sehemu kubwa walikuwa hawavutiwi na siasa za vyama, taratibu hali hiyo ilianza kufifia. Hadi kufikia mwaka 2015, kama nchi tulipiga hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia.

Mfano uwiano wa wabunge wanawake kwa wanaume katika uchaguzi wa mwaka 2015, ulifikia asilimia 36. Aidha, kabla ya kuingia Rais John Magufuli tuliona kuimarika kwa majukwaa ya kujadiliana, uhuru wa kutoa mawazo na vyombo vya habari kuripoti habari na taarifa za kisiasa.

Hali ilikuwa tofauti, baada ya kuingia madarakani Rais John Pombe Magufuli, kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa, ambapo ilianza kwa kuruhusu wanasiasa waliochaguliwa kwenye maeneo yao ya uwakilishi pekee na baadaye ikaondolewa kabisa. Kukamatwa na kufunguliwa kesi za kubumba kwa viongozi wa kisiasa katika ngazi mbalimbali, kushambuliwa kwa risasi za moto, kutishiwa kuuwawa n.k

Rais Magufuli aliweka wazi kabisa azma yake ya kufuta mfumo wa vyama vingi vya upinzani nchini, ambapo wasaidizi wake walimsaidia kutafsiri kisheria na kutekeleza kwa mabavu. Licha ya mapungufu katika sheria zilizokuwa zinaendesha siasa, Rais Magufuli aliona haziwezi kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kumaliza upinzani na kutokomeza siasa ya vyama vingi. Hivyo, katika utawala wake alifanya mabadiliko ya sheria kuanzia sheria ya vyama vya siasa, kanuni za uchaguzi, sheria ya huduma ya vyombo vya habari, sheria ya Takwimu na zaidi kuruhusu vitendo visivyowekwa kisheria dhidi ya wapinzani.

Miaka 6 chini ya Serikali ya awamu ya tano, tulishuhudia kuporwa kwa chaguzi, chaguzi zilikuwa kama majukwaa ya mateso, maumivu au uwanja wa vita. Wanasiasa wa upinzani waliteswa, waliumizwa, walisababishiwa vilema vya kudumu na wengine kukimbia nchi kabisa.

Chaguzi za mwaka 2019 (Uchaguzi wa serikali za Mitaa) na 2020 (Uchaguzi Mkuu wa Urais, Ubunge na Udiwani), hazikuwa chaguzi huru, sawa na za haki; kama wengi tunavyoita ‘uchafuzi’. Mbaya zaidi, zilijengwa kauli na hoja zilizopelekea kufifisha nafasi na mchango wa siasa ya vyama kwenye maendeleo. Siasa ilijengewa dhana na kuonekana ni kikwazo cha Maendeleo.

Makala hii hailengi kuelezea utawala wa Rais Magufuli na maendeleo ya siasa za vyama vingi (nafikiri ni kazi ya wakati mwingine). Lakini, hakuna mtu anayeweza kuelezea au kuzungumzia mfumo wa vyama vingi nchini bila kuangazia kipindi hiki muhimu ambacho kimerudisha nyuma siasa za nchi miaka 30 nyuma.

Leo tunapoadhimisha miaka 30 ya vyama vingi, ni kama tunajipanga kuanza tena mfumo wa vyama vingi vya siasa. Madai ya vyama vya siasa leo ni zaidi ya kipindi ambacho Tanzaia iliporejesha tena mfumo huu mwaka 1992; Madai ya kufanya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, sheria za uchaguzi, sheria za Jeshi la Polisi (vifungu vinavyohusu, ushiriki wa Polisi kwenye Siasa).

Ni matarajio yangu kwamba, kipindi cha miaka 6 iliyopita kimetoa funzo kubwa kwa viongozi wa nchi wa sasa na wa baadaye katika kuendesha siasa, kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano wa watu kwenye kuleta maendeleo. Vitendo vyote vilivyorudisha nyuma siasa za vyama vingi, havipaswi kuenziwa na kuimarishwa. Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha uelekeo tofauti na mtangulizi wake kwa kuanza kufanya mabadiliko kwenye mifumo ya sheria, hatua ambayo ni muhimu kwa ustawi na muendelezo wa sheria Rafiki kwa demokrasia yetu.

Siasa ya Vyama Vingi na Nafasi ya Wanawake katika Siasa:

Mara kadhaa linapozungumziwa suala ya wanawake na siasa, huwa inalinganishwa na uongozi, uanaharakati wa wanawake na wanasiasa wanaozungumzia uwakilishi wa wanawake kwenye uongozi kama vile ni ushirika wa wanawake kwenye siasa.

Historia inatukumbusha kwamba ushiriki wa wanawake kwenye siasa nchini, siyo wa kutiliwa shaka hata kidogo, kwani wanawake wameshiriki tangu wakati wa mapambano ya kupigania uhuru wa nchi, baada ya uhuru na wakati wa siasa za mageuzi.

Katika vipindi vyote wanawake wanashiriki kwa namna tofauti tofauti lakini miaka ya hivi karibuni nafasi ya wanawake imebadilika kwa kuwafanya washirika wa kimaamuzi.

Tafiti na maandiko mbalimbali yanaonyesha uwepo wa tatizo la kukosekana kwa usawa wa kijinsia ndani ya vyama vya siasa nchini. Ingawa hivi karibuni pamekuwa na mifano ya wanasiasa wanaotumika kama kielelezo cha mafanikio ya wanawake katika masuala ya siasa hususan katika uongozi. Kuwepo kwa Rais Samia Suluhu Hassan kunachora mstari wa juu wa mafanikio ya ushirika wa wanawake kwenye siasa za Tanzania.

Hoja na mifano hii inapuuza ukweli na uhalisia uliopo, kwa kuwa mifumo ya uchaguzi na siasa Tanzania kwa kiasi kikubwa ina vikwazo vingi kwa wanawake kwenye mashindano ya ndani ya vyama na baina ya vyama.

Zipo tafiti kadhaa zilizofanyika miaka ya hivi karibuni zinazoonyesha kwamba hakuna chama cha siasa nchini ambacho kimefikia usawa wa kijinsia katika ngazi ya kufanya maamuzi.

Uzoefu unaonyesha kwamba, kadri mazingira ya kisiasa yanavyokuwa magumu ushiriki wa wanawake kwenye siasa unakuwa hafifu zaidi na ushiriki wao kwenye uongozi kuwa mdogo zaidi. Mtu yeyote anayependa wanawake na kutaka mageuzi ya siasa kwa kuongeza idadi ya wanawake kwenye vyombo vya maamuzi katika ngazi mbalimbali wajibu wake ni kupigania kubadili mazingira ya sasa ya kisiasa ambayo hayawavutii wanawake ama sio rafiki kwao.

Pili, ushiriki wa wanawake kwenye siasa unapaswa kwenda mbali zaidi ya kuangalia idadi ya wanawake kwenye viti vya Ubunge, Udiwani na serikali za mitaa bali kwenye uamuzi wa vyombo vingine ndani ya vyama vyetu vya siasa.

Ninashukuru kuwa kiongozi kwenye Chama cha siasa (ACT Wazalendo) ambacho kinajali na kuzingatia nafasi ya wanawake kwenye ngazi za uamuzi ndani ya chama. Mwaka 2015 wakati naingia kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama Katibu wa Sera na Utafiti wa Chama nilikuta Sekretarieti ikiwa na asilimia 38 ya wanawake na Mwenyekiti wa Chama alikuwa mwanamke. Asilimia ya wanawake kwenye Sekretariet ilipanda hadi kufikia 43 mwaka 2017 wakati nikiwa Katibu Mkuu wa Chama. Mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Chama katika Kuunda kamati ya Kuisimamia Serikali ambayo inaundwa na Wasemaji wa Kisekta 42. Wanawake ni 21 na wanaume 21 sawa na asilimia 50 kwa 50.

Pamoja na jitihada hizi zilizopo kwenye Chama, bado haiondoi ukweli mchungu kuwa wanawake wanapewa nafasi ndogo sana kwenye siasa zetu. Sehemu ya sababu hizo zinaelezwa ni kutokana na mila na desturi, lakini kama nilivyoeleza awali, mfumo wa siasa za uhasama, uteswaji, unyanyasaji na ukandamizaji yanawakimbiza wanawake wengi.

Zipo tafiti zinaonyesha licha ya kuongezeka kwa uwiano wa wabunge wanawake dhidi ya wanaume Bungeni (2015) bado unyanyasaji wa kijinsia unazidi kukithiri mitandaoni, mitaani na ndani ya vyama vya siasa.

Tunapoadhimisha miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi, tunapaswa kupigania mazingira bora ya kufanya siasa, kuongeza ushirika wa wanawake ndani ya vyama, kwenye vyombo vya Serikali na dola kwa ujumla.

Siasa na Maendeleo ya Watu:

Katika eneo la kwanza nilijaribu kuelezea kwa kiasi gani vyama vingi vya siasa vimechangia kuleta madiliko ya msingi katika nyanja mbalimbali ambayo kimsingi ni katika kutanua huduma za watu na kuleta maendeleo ya wananchi. Lakini umri wa siasa za vyama vingi na kasi ya maendeleo ya watu vinakimbiana, hapa tunaweza kujiuliza kama kweli vyama vyetu vinatumika kuibua mijadala, hoja na mitazamo inayosaidia kusukuma mbele jitihada za wananchi? Au ni mapambano ya vyama vya siasa huku vikiangusha matumaini ya wananchi? Ni muhimu kuweka wazi kuwa siasa za masuala zinahitaji mambo kadhaa; kwanza, uvumilivu wa kisiasa, ambapo vyama vitajadiliana, kubishana na kuafikiana au kupishana kwa hoja. Pili, ufasaha wa kimtazamo na kiitikadi, kama mtajadiliana, kubishana na kuzungumza kwa hoja itakuwa ni rahisi kujijenga katika mitazamo na itikadi; ambazo ndio dira ya uelekeo wa kisiasa. Tatu, utamaduni wa siasa za ushindani badala ya siasa hodhi.

Tanzania ya sasa inakosa sifa hizo hapo juu na ni muhimu kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya vyama vingi, kutafakari kwenye maeneo hayo.

Imetolewa na:

Ndugu Dorothy Semu,
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalaendo – Bara
Waziri Mkuu Kivuli wa Baraza la Wasemaji wa Kisekta
01 Julai, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK