Migogoro ya Ardhi Nchini, Serikali ni sehemu ya tatizo.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

Migogoro ya ardhi nchini; Serikali iache udalali wa kupora na kuuza ardhi za Wananchi.
1. Utangulizi,
Changamoto ya migogoro ya ardhi nchini zinazidi kuwa kubwa kila uchao, ipo migogoro kati ya wafugaji na wakulima, Wananchi dhidi ya Serikali, Wananchi dhidi ya wawekezaji kwa nyakati zote waathirika ni Wananchi, wao ndiyo wanaopoteza haki zao za kutumia ardhi. Mara kadhaa tumeshuhudia mauaji, mapigano, kufukuzwa na kuondolewa kwa wananchi kwenye ardhi zao. Pamoja na migogoro kuwa mingi nchini, kasi ya utatuzi ni ndogo sana na kwa maneno mengine njia za utatuzi hazifanyi kazi kwa ufanisi.
Sisi, ACT Wazalendo tunaamini ardhi inabaki kuwa rasilimali muhimu kwa nchi yetu ambayo kwa sehemu kubwa (65%) watu wake wanajishughulisha na kilimo, uchimbaji, na ufugaji ambao hutegemea ardhi kwa ajili ya kupata mahitaji muhimu ya kila siku. Wakulima na wafugaji ndiyo huzalisha chakula kinacholisha taifa hili, huingiza fedha za kigeni na kutoa ajira. Kwa hiyo ardhi ni roho (uhai) ya taifa letu.

Kutokana hali hii ya kukithiri kwa migogoro ya ardhi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi tunakusudia kuelezea hali halisi ya migogoro, vyanzo (viini) vya migogoro, msimamo wa ACT Wazalendo kwenye kukabiliana na changamoto hizo na mapendekezo ya hatua zinazopaswa ili kumaliza kabisa migogoro.
2. Serikali na uwekezaji; kuongezeka kwa Migogoro ya ardhi
Katika kufuatilia migogoro kuhusu ardhi nchini tumebaini inajitokeza zaidi baina ya wakulima na wafugaji kutokana na ufinyu wa maeneo au kukosekana kwa mipango bora ya ardhi. Migogoro ya wananchi na wawekezaji; Migogoro ya ardhi kati ya wananchi (jamii) na Serikali kupitia taasisi zake, uchukuaji wa maeneo kwa jina la hifadhi, ranchi ya taifa, vyombo vya ulinzi na usalama (Jeshi la wananchi na Magereza) Serikali imekuta inachochea na kuzalisha migogoro na mwisho wake hupelekea migogoro ya mipaka baina ya vijiji au miongoni mwa wanavijiji.
Uchambuzi wetu unaonyesha wazi kuwa migogoro inatokana na dhana iliyojengwa kuona kwamba ardhi ni mtaji au bidhaa. Kwa mtazamo huu, ardhi inachukuliwa kwamba inapaswa kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji kwa jamii. Ndio maana tunashuhudia Serikali ya CCM inapora ardhi kutoka kwa wananchi wazawa kwa ajili ya wawekezaji au inachukuliwa kutoka kwenye miliki ya vijiji au wanavijiji ili kupatiwa mtu mmoja atakayetumia kwa ajili ya kupata faida.
Aidha, ukiritimba katika umiliki wa ardhi (ardhi kuwekwa kwenye mikono ya Rais) na hivyo Serikali kujipa mamlaka ya mwisho katika kutwaa, kudhibiti na kumiliki ardhi.


Matokeo ya dhana na mifumo hii ni kuzalisha migogoro ambayo huishia kwenye mauaji, kupora au kuwanyang’anya wananchi ardhi. Vilevile, wananchi wamekuwa wakilazimishwa au kulazimika kuhama katika ardhi zao ili kupisha uwekezaji wa Serikali au watu, taasisi na makampuni binafsi.
Orodha ya migogoro, eneo la ardhi lenye migogoro na idadi ya watu walio ondolewa kwenye ardhi ni kubwa na inazidi kuongezeka nchini. Lakini kwa leo tutaenda kuzungumzia maeneo manne (4) ambayo yanatishia uhai wa uzalishaji nchini kutokana na migogoro au uporaji;

A: Mgogoro wa Ardhi Bunju (Chasimba)
Tarehe 28 Septemba 2022 tulitembelea Kata ya Bunju na kukutana na baadhi ya wakazi wa Chasimba, Chatembo na Chachui ambao wako kwenye tishio la kuondolewa kwenye makazi yao kutokana na mgogoro wa ardhi dhidi ya Kampuni inayoendesha kiwanda cha Saruji cha Twiga (Tanzania Portland Cement Company-TPCC).
Mgogoro wao unatokana na uamuzi wa Serikali kubinafsisha kiwanda cha Saruji kilichokuwa kinamilikiwa na shirika la umma la saruji (Saruji Corporation) mwaka 2001. Wakati Serikali inabinafsisha eneo hilo tayari wananchi hao walikuwa wanaishi kwenye sehemu ya ardhi hiyo na kuitumia kwa ajili ya shughuli nyingine. Kwa maneno mengine, Serikali iliuza kiwanda na wananchi waliokuwa wanaishi hapo. Kuanzia hapo mwekezaji huyo alifanya majaribio ya kuwaondoa wakazi hao na kufikia mwaka 2010 azma yake ilikaziwa na hukumu ya Mahakama ya Rufaa kwa kuwaamuru wananchi kuondoka au kuondolewa kwenye eneo hilo.
Pamoja na historia ndefu ya mivutano iliyodumu kwa miaka 15, mwaka 2015 Serikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi Ndg. William Lukuvi, Mwekezaji wa kiwanda cha Twiga na Wakazi wa Chasimba walifikia muafaka na kumaliza mgogoro na kutangazwa Bungeni mwaka 2016. Mwekezaji alikubali kutoa eneo lenye ukubwa wa hekta 243 kati ya 922.55 alizokuwa anazimiliki. Kutokana na zoezi la uthamini la mwaka 2012 eneo hilo lilikuwa linakaliwa na kaya 4,090 ambapo ilikadiriwa kuwa na watu 20,450 lilibadilishwa rasmi kuwa eneo la makazi kutoka kuwa eneo la machimbo (madini).
Makubaliano hayo yalienda na masharti ya kuwataka wananchi kusitisha shughuli za kuchimba mawe, kugonga kokoto au kuchimba mchanga. Aidha, wananchi walitakiwa kulipia malipo ya mbele ya kupata hati (Premium) ambayo ilikuwa shilingi laki moja. Serikali kwa upande wake ilitakiwa kusimamia kamati ya pamoja ya kupima, kupanga na kumilisha ardhi (kutoa hati). Vilevile, Serikali iliahidi kushughulikia masuala ya kuwaunganisha wananchi na huduma za jamii kama vile umeme na maji. Kwa upande wa Muwekezaji pamoja na kukubali kuiachia sehemu ya ardhi aliahidi kutekeleza wajibu wa kampuni kwa jamii kwa kujenga miundombinu ya barabara, maji na shule.

Baada ya muda wa miaka 6, Mwezi Machi mwaka 2021 aliyekuwa Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi alifika tena Chasimba na kuwataka wakazi hao kulipa fidia ya ardhi kwa mita moja ya mraba Shilingi 6,419 kinyume na makubaliano ya awali yaliyowataka wakazi hao kulipia hati. Hapo ndio hofu, vitisho na usalama wa ardhi za wakazi hao zilipoanza tena kutishiwa.
Hali ilikuwa tete zaidi kuanzia mwezi Machi Mwaka 2022 ambapo wananchi waliamriwa kuondolewa ikiwa hawajalipa fidia hiyo. Pia, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitangaza kwamba itakapofika tarehe 1 Novemba 2022 Serikali itajitoa kuwadhamini wakaazi (kwa maneno yake ‘wavamizi’) wasipolipa fidia hiyo. Vinginevyo wataondolewa kwa nguvu. Mwezi Oktoba kulikuwa na matangazo ya mara kwa mara mtaa kwa mtaa kuwasisitiza wananchi hao kulipa kabla ya Novemba jambo lililoongeza taharuki zaidi. Hadi sasa wananchi walioshindwa kulipa hicho kinachodaiwa kuwa ni fidia ni wanakaya 3,800 kati ya kaya 4,090. Serikali, ili kujenga uhalali wa operesheni ya kuwaondosha, inawaita wakazi hawa kuwa ni wavamizi.

Hoja za wananchi:
i. Hakuna makubaliano ya wananchi kulipa fidia hiyo; pia hawakushirikishwa ikiwa kuna fidia wanatakiwa kulipa kwa ajili ya ardhi yao waliyokuwa wanaishi hata kabla ya muwekezaji,
ii. Serikali haijatekeleza wajibu wake wa kurasimisha eneo hilo hata kwa watu ambao walisha lipa malipo ya hati,
iii. Serikali inaungana na mwekezaji kuwapora wananchi haki zao,
iv. Serikali isimamie makubaliano ya mwaka 2015 ambapo kila upande ulipaswa kutekeleza wajibu wake.
ACT Wazalendo katika uchunguzi wetu tumeona kwanza ni wazi kuwa Serikali inataka kurekebisha makosa yake kwa kuwabebesha mzigo huo wananchi. Pili, ni wazi kuwa hoja ya fidia ya ardhi imekuja baada ya miaka sita na bila ushirikishwaji wa wananchi. Tatu, Serikali haijatekeleza wajibu wake wa kusimamia makubaliano. Hivyo basi, tunaungana na wananchi wa Chasimba, Chatembo na Chachui kuhakikisha haki za ardhi kwa wakazi hao haziporwi na mwekezaji pamoja na Serikali. Aidha, tunaitaka Serikali imlipe fidia mwekezaji kama ilivyoahidi wakati wa makubaliano mwaka 2015. Vilevile, iache kuwaita wakaazi hao ni wavamizi.

B: Mgogoro wa ardhi Mbarali
Oktoba 25, 2022 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Ubaruku, Mbarali alitangaza kuvifuta vijiji vitano (5) na vitongoji 41. Uamuzi huu umeibua vilio na malalamiko kutoka kwa wananchi ambao kwa wao ardhi ndio uhai. Vijiji vilivyofutwa ni Iyala, Kalambo, Luhanga, Msanga na Madundusi. Uhamisho huo pia umevigusa vitongoji vitatu katika kijiji cha Lualaje wilayani Chunya vyenye idadi ya watu 21,252.
Madai ya Serikali ni kuwa imeamua hivyo ili kupisha eneo la hifadhi ya bonde la Usangu kwa lengo la kutunza na kulinda ardhi oevu pamoja na vyanzo vya kupokea na kutiririsha maji katika mito mbalimbali.
Sisi ACT Wazalendo tunaona kuwa uamuzi huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa tangazo la Serikali Namba 28 la mwaka 2008, ambalo msingi wake ni kupanua eneo la Hifadhi ya Ruaha ili eneo la Bonde la Usangu lijumuishwe ndani yake. Tangazo hili lililenga kuvifuta vijiji 28 vya Wilaya ya Mbarali, Mbeya ili kusudi eneo lake liingizwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ilipandishwa hadhi kutoka pori la akiba mwaka 2006. Jambo lililopelekea kuongeza ukubwa wa eneo la hifadhi kwa kumega eneo la uzalishaji wa kilimo na ufugaji. Hatua ambayo ilipingwa kwa nguvu zote na wadau mbalimbali.
Kwa hiyo, zoezi la kuwahamisha wakulima na wafugaji (kwa kuvifuta vijiji 5) wilaya ya Mbarali linajirudia tu, sio jaribio jipya lakini msingi wa kuwaondoa ni uleule kutaka kupanua eneo la hifadhi. Na hata hivyo, vijiji vingine vitaenda kuondolewa siku za usoni.
Hoja za kupungua au kukauka kwa maji kwenye mto Ruaha Mkuu ni hila tu kwani ukweli ni kwamba kwa majira ya kiangazi mito mingi nchini hupungua maji au mengine hukauka kabisa. Vile vile, hoja ya kulinda uhifadhi imejengeka katika mtazamo wa chuki dhidi ya wananchi hao kuona kuwa hawana uwezo wa kushiriki kwenye uhifadhi wa mazingira yao isipokuwa kuondolewa. Pia, ukweli ni kuwa kilimo cha mpunga hulimwa maeneo ya bondeni msisitizo unapaswa kuwa kuzingatiwa sheria za utunzaji wa mazingira na sio kuwahamisha.

Mchango wa wakulima hawa kwenye uchumi wa taifa ni muhimu sana kama ilivyo kwa sekta ya uhifadhi na sekta ya uzalishaji wa umeme. Inahitajika hekima ya kiuongozi kuzingatia uhai na usalama wa upatikanaji wa chakula, hatima ya wakulima na wafugaji na maslahi ya taifa kwa upana wake.
Kutokana na vilio vya wananchi kupoteza ardhi yao na kama wasipoungana vijiji vingine vinaingizwa kwa hoja hizi hizi, tunaitaka serikali kuchukua hatua zifuatazo;

i. Serikali isitishe zoezi la kuwahamisha wananchi hao badala yake itumie njia shirikishi za kuhakikisha utunzaji wa mazingira na kilimo chenye kuendeleza uhifadhi. Wananchi washirikishwe kwenye kutafsiri mipaka, kuweka alama na kukamilisha malipo ya fidia kwa wale watakaonekana kuvuka mipaka ya awali mwaka 2001.
ii. Serikali isaidie kuimarisha na kuboresha mifumo ya kilimo cha umwagiliaji wa kisasa ili kuhakikisha kilimo kinaendelea na mazingira yanahifadhiwa.
iii. Ili kuongeza umakini wa utunzaji wa utajiri wa bonde hili Serikali iongeze ukomo wa kulima karibu na mto kufikia mita 120 kila upande kama walivyopendekeza wakulima wenyewe.
iv. Ili kulinda kiwango cha maji yanayotiririka mto Ruaha Mkuu, wakulima wa Mbarali waruhusiwe kufanya Kilimo msimu wa masika, ili maji yaliyopo yaendeleze mtiririko kwa ajili ya viumbe wengine kwenye mto huo.
Upanuzi wa maeneo ya hifadhi na kupandishwa kwa hadhi kwa maeneo hayo, kumeongeza kasi ya migogoro ya ardhi kwa kuwa yanamega maeneo yanayotumiwa na wananchi kwa ajili uzalishaji, makaazi au shughuli za kijamii. Ni muhimu sana kuzingatia mahitaji ya kijamii kuliko hoja zingine.

C: Mapigano ya wakulima na wafugaji Kilwa na Kilombero
i. Wakulima na Wafugaji Kilwa
Wilaya ya Kilwa kwa asili tangu uhuru inakaliwa na wakulima wa mazao na ufugaji wa kawaida. Kuhamishiwa kwa jamii za wafugaji katika miaka ya 2012, kumeanza kuliweka eneo la wilaya hiyo kwenye orodha ya wilaya zinazoibuka kwa migogoro ya wakulima na wafugaji. Kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka huu imefanya jumla ya wakulima 12 wameuwa kutokana na mapigano. Hofu inazidi kuongezeka, uhasama unakua zaidi, majeruhi wa mapigano hayo kwa idadi inafikia watu 16 ndani ya mwaka mmoja.
Katika ziara ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo mwezi Januari na Julai 2022 katika kata kumi alikutana na tatizo la mapigano, mivutano na migogoro katika ya wakulima na wafugaji limechomoza kuwa kero inayotishia amani, usalama na ustawi wa wananchi. Kata ambazo tatizo hilo limeonekana kuwa na tishio zaidi ni Kikole ambayo ina Vijijini vinne (Migeregere, Kikole, Ruhatwe ) kati ya vijiji hivi vyote hali ya migogoro ni mbaya zaidi hata kufikia hatua ya kutangaziana vita. Kata ya Likawage, Nanjirinji na Mandawa nazo zinafuata. Wananchi wanaeleza kwa namna gani watendaji wa Serikali, wenyeviti wa vijiji kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya wanavyopuuza Sheria ya Ardhi kwa kutowashirikishi na kuwasikiliza wanavijiji juu mipango bora ya ardhi.
Kwa sehemu kubwa, matatizo ya migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Kilwa imepandikizwa na watawala kutokana na ukweli kwamba Lindi ipo ardhi ya kutosha kwa ajili ya Kilimo na hata Ufugaji. Uamuzi wa Serikali kuwaruhusu wafugaji kwenye ardhi ya Kilimo bila kuwashirikisha wanavijiji wenyewe ni kupandikiza mapigano yasiyo ya lazima.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali: Kwanza kuwasikiliza wanavijiji na kuwashirikisha kwenye mipango bora ya matumizi ya ardhi ya vijiji. Pili, kusimamia utekelezaji wa mpango ulioamuliwa na vijiji vyenyewe na sio kulazimisha kama inaendeshwa hivi sasa katika vijiji vingi.

Tatu, Serikali kama imeamua kuwaleta wafugaji wawawekee mazingira mazuri ya kufugia kwa kujenga malambo ya kunyweshea mifugo na kutengea maeneo ya malisho. Utaratibu wa sasa unasababisha vurugu, wanalisha kwenye mashamba ya wakulima, wananywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinahudumia wanavijiji.
Nne, tunaitaka TAKUKURU kuchunguza mienendo ya wenyeviti, watendaji na watumishi wa halmashauri ya Kilwa.
Tano, kuwachukulia hatua watendaji au wahusika wote walioshiriki kuwaingiza wafugaji kwenye ardhi za vijiji ambavyo havijaruhusu wafugaji.

ii. Mapigano ya Wakulima na Wafugaji Kilombero
Tarehe 23 Oktoba 2022 kulitokea mgogoro wa kati ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Ikwambi Wilaya ya Kilombero, Morogoro. Mapigano hayo yalisababisha vifo vya watu wawili. Uhaba wa ardhi ya kilimo na ufugaji kutokana na maeneo makubwa kugaiwa kwa wawekezaji na hifadhi za wanyamapori pamoja na ukuaji wa miji unaomeza ardhi za vijiji, ndio chanzo. Pia, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi vijiji sio shirikishi hivyo kipaumbele hutolewa kwa matumizi mengine kama ya uwekezaji na uhifadhi na matokeo yake makundi ya wafugaji na wakulima hukosa ardhi.

3. Mapendekezo ya Jumla
ACT Wazalendo tunaona malalamiko na vilio hivi vya wananchi vinapaswa kutafsiri katika utungaji wa Sera na Sheria za Ardhi zitakazomlinda mwananchi, tofauti na sasa ambapo msukumo wa urasmishaji wa ardhi unabebwa na malengo ya kibiashara. Hivyo tunapendekeza mambo yafuatayo;
i. Serikali iharakishe na kukamilisha zoezi la kupima, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano na mivutano.
ii. Mamlaka za Halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushugulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi
iii. Vilevile, mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji yaimarishwe, kusimamiwa na kujengewa uwezo ili yaweze kushugulikia, kuamua na kutatua masuala ya ardhi katika maeneo yao kwa wakati.

Imetolewa na:

Ndugu: Bonifasia Aidan Mapunda
Msemaji wa kisekta Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi,
ACT Wazalendo
Twitter: @BonifasiaMapunda
11 Novemba, 2022.
Dar es Salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK