Muhtasari wa Uchambuzi wa Chama cha ACT Wazalendo kuhusu Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 Aprili 10, 2023.

Muhtasari wa Uchambuzi wa Chama cha ACT Wazalendo kuhusu Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022
Aprili 10, 2023.

UTANGULIZI
Ndugu Wanahabari,

Ndugu Viongozi wa ACT Wazalendo mliopo hapa.

Nikiwa Kiongozi wa ACT Wazalendo, wiki hii nilijisikia fahari kubwa. Mimi na viongozi wenzangu tumepigiwa simu na kutumiwa jumbe za kila aina na Watanzania wa kawaida kabisa, Wabunge, Waandishi wa Habari na hata baadhi ya Viongozi wa Vyama vingine vya Upinzani, kutuuliza ni lini tutafanya uchambuzi wa ripoti hii.
Tumejijengea utaratibu wa kuwa chama cha kisiasa cha masuala na sasa tumeanza kuvuna matunda ya utamaduni wa kisiasa tulioanza kuujenga kuliko wakati mwingine wowote kwenye maisha yangu ya kisiasa.
Sasa nimeona kwamba siasa za masuala ya msingi yanayowakabili Watanzania ndizo siasa ambazo watu wetu wanazitaka. Napenda kuwaahidi Watanzania kwamba ACT Wazalendo, In Shaa Allah, tutaendelea kubaki kwenye njia hii na hatutahama maana kuna tija kubwa.

HABARI NJEMA!
Kabla sijaingia kwa undani kuhusu ripoti ya mwaka huu, naomba kwanza nianze na habari njema. Habari njema ni kwamba uchambuzi wetu huu ambao tumekuwa tunaufanya mara kwa mara, huwa unasikilizwa na kufanyiwa kazi. Kwa hiyo hapa hatupigi maneno matupu. Baadhi ya mambo tuliyopendekeza katika miaka miwili iliyopita na tayari yamefanyiwa kazi ni:
• Mapendekezo yetu kuhusu uchunguzi wa uporaji wa Ofisi ya Mwendesha Mashataka (DPP) uliofanywa kupitia makubaliano ya kukiri kosa (Plea Bargain);
• Kugeuza madeni ya Shirika la TANESCO na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuwa mitaji; na
• Kulipwa kwa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii; yote yamefanyiwa kazi.

HOJA MAHUSUSI KWENYE UKAGUZI WA MWAKA HUU 2021/2022
Kwa kawaida, uchambuzi wa ACT Wazalendo hujikita katika hoja kubwa 10 tunazoziona za msingi zaidi katika mwaka unaohusika wa ukaguzi. Mwaka huu tunaendelea na utaratibu wetu huo kama kawaida;


1. Hatari ya Mfuko wa Bima ya Afya
Ripoti ya CAG imebaini matatizo makubwa kwenye Mfuko wa Bima ya Afya. CAG kwa mara nyingine tena ameonyesha kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaendelea kupata hasara ambapo katika mwaka huu wa ukaguzi, 2021/2022, hasara ilikuwa shilingi bilioni 205. Ikumbukwe kuwa mfuko ulipata hasara ya shilingi bilioni 104 mwaka 2020/21, hivyo hasara imeongezeka maradufu na ina maana kumuelemea mwananchi.
CAG amebaini yafuatayo kuhusu NHIF. Kwanza wafanyakazi wamejikopesha na kusuasua kulipa kiasi cha shilingi bilioni 41.42. Yaani watu wanachangia fedha mfuko halafu wafanyakazi wake wanatumia fedha hizo kujikopesha kufanyia mambo yao mengine.
Kwa mwenendo huu, ni wazi mfuko wa NHIF unakwenda kufa katika muda mfupi. Kuunusuru mfuko huu tunapendekeza mambo mawili;
Mosi kubadilishwa kwa Bodi na Menejimenti ya NHIF ambapo vyombo hivyo havina mbinu mbadala za kuendeleza mfuko huo na kubadilishwa kwa sheria nzima ya Bima ya Afya. Na pili ni kuunganishwa kwa mfumo wa Bima ya Afya na ule wa Hifadhi ya Jamii kama ambavyo tumekuwa tukipendekeza siku zote.

2. Deni la Taifa
CAG amefanya ukaguzi wa Akaunti ya Deni la Taifa na kueleza kwamba hadi Juni 30, 2022 lilikuwa Shilingi trilioni 71 ambapo ni ongezeko la 11% kutoka deni la shilingi trilioni 64.5 lililo ripotiwa mwaka 2020/21. Uchambuzi wetu unaotokana na Ripoti ya CAG unaonyesha kuwa katika mwaka huu wa ukaguzi Serikali ilichukua mikopo ya ndani kwa 30% zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Vilevile mikopo ya nje yenye masharti nafuu iliyochukuliwa na Serikali ilikuwa 33% zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge. Mwenendo huu unaonyesha Serikali kutojali na kudharau mamlaka ya Bunge. Tunaitaka Serikali kuheshimu Bunge na kufuata sheria ya Bajeti.
3. Upotevu usiokwisha wa Mabilioni ya Fedha za Mikopo kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu zinazotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ripoti hii imeibua hoja zenye thamani ya Shilingi Bilioni 97.59 kuhusu mikopo hii. ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Mikopo kwa Vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu itolewe kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii ambapo fedha hizi zitakuwa ni mchango wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wananchi wenye sifa watakaoingia kwenye Skimu husika. Tukitekeleza mfumo huu kwa miaka mitano tutakuwa tumejenga Skimu ya Hifadhi ya Jamii yenye thamani ya shilingi trilioni 2.1 yenye wanachama zaidi ya milioni 3 wenye Fao la Matibabu.
4. TANROAD haikujenga barabara hata moja kwa mwaka 2021/2022
CAG amebainisha katika ripoti yake ya ukaguzi kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilishindwa kutekeleza bajeti yake yote ya mwaka 2021/2022 licha ya kutengewa na Bunge bajeti ya shilingi trilioni 2.9. Tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe;
Moja, baada ya CAG kuthibitisha kuwa Waziri wa Miundombinu Prof. Makame Mnyaa Mbarawa alisema uongo Bungeni kwa kukana taarifa hii, Mheshimiwa Waziri awajibike kwa kujiuzulu na kuliomba radhi Bunge. Mbili, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS ajiuzulu nafasi yake au Rais amfukuze kazi mara moja kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.
5. ATCL kukodisha ndege kutoka TGFA
CAG ameonyesha mapungufu, hasara na hoja kadhaa za ukaguzi zinazohusu Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). CAG ameonyesha kuwa mwaka 2021/22, ATCL walipata hasara ya shilingi bilioni 35 kutoka hasara ya shilingi bilioni 36 ya mwaka 2020/21.
Uchambuzi wetu unaonyesha kwamba hasara inayopata ATCL kwa sehemu kubwa inatokana na mfumo wa umiliki wa ndege. Mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. Ndege zote zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za walipa kodi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL. Tunapendekeza ATCL imilikishwe ndege zote inazo kodishiwa kutoka TGFA.
6. Kuhusu Vishikwambi (Tablets) vya Sensa ya Watu na Makazi
CAG katika ukaguzi wake mwaka 2021/2022 amebainisha dosari katika mchakato wa manununuzi wa Vishikwambi 150,000 vilivyotakiwa kutumika kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
ACT Wazalendo tunapendekeza TAKUKURU kwa kushirikiana na Polisi wafanye uchunguzi wa kijinai katika mchakato mzima wa manunuzi ya vishikwambi vya sensa na wakati uchunguzi huo unaendelea watu wote waliohusika na mchakato wa manunuzi hayo wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi.
7. Mapungufu Makubwa katika Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi Awamu ya II.
Katika Ripoti ya Mwaka 2021/2022, CAG ametoa hoja mbili kubwa za ukaguzi kuhusu Mradi wa Ujenzi wa miundombinu ya Mabasi ya Mwendokasi Dar es Salaam (DART); kwanza ni ujenzi kutokidhi ubora wa viwango na pili matumizi ya dizeli badala ya gesi kwenye mabasi ya mradi huo.
Kuhusu eneo la dizeli, CAG amebaini kuwa TPDC imeingia gharama ya ujenzi wa miundombinu kujaza gesi asilia kwenye mabasi ya mwendokasi bila ya kuwa na mkataba na DART. Kwa mujibu wa CAG, DART waligoma kuingia mkataba na TPDC kwa ajili ya kubadilisha magari kutoka mfumo wa mafuta kwenda gesi kwa madai kuwa wameingia mkataba wa miaka 12 na kampuni ya kuuza mafuta ya dizeli.
Hoja hii ya mkataba wa miaka 12 haina mashiko na ni kichaka cha ubadhirifu. Taarifa tulizonazo zinaonyesha kwamba DART wanatumia wastani wa lita 30,000 za diseli kuendesha huduma ya usafiri kwa siku. Hii ni sawa na kutumia shilingi milioni 91 kila siku, sawa na shilingi bilioni 33 kwa mwaka mzima. ACT Wazalendo tunaitaka DART kuingia mkataba mara moja na TPDC kubadilisha mabasi ya mwendokasi kutoka kutumia diseli na kutumia gesi asilia (CNG).

8. Uzembe wa Usimamizi Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere
CAG ameendelea kuhoji uzembe wa Serikali kushindwa kusimamia utekelezaji wa wajibu wa kampuni kuendeleza jamii (Corporate Social Responsibility- CSR). Kampuni inayotekeleza mradi huu ilipaswa kutekeleza mpango ulioandaliwa na Serikali wa miradi mbalimbali ya kijamii yenye thamani ya shilingi Bilioni 270. Hadi mwezi Disemba 2022, takribani miaka minne tangu mradi uanze, mpango huo haujatekelezwa. ACT Wazalendo inapendekeza Mawaziri wa Nishati na Madini na TAMISEMI wasimamie na kuhakikisha makubaliano ya Mkataba yanatekelezwa kuanzia mwaka wa fedha unaoanza Julai 2023 ili wananchi wafaidike na hio CSR.

9. Manunuzi katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati (SGR)
Katika Ripoti yake ya mwaka unaoishia Juni 30, 2022, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya ukaguzi wa kiufundi katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa, SGR. CAG na ameibua hoja nyingi katika ukaguzi huu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 957 (Shilingi Trilioni 2.2).
Hoja hizo ni masharti ya mkopo kutoka Benki ya Standard Chartered ya Uingereza kwenda kwa Serikali, kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa SGR kipande cha 3 na 4 na kuongezeka kwa gharama za ununuzi wa vichwa na mabehewa ya treni ya SGR.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Serikali ilipokea mkopo kutoka Standard Chartered wenye masharti ambayo yalisababisha gharama za ujenzi kuongezeka kwa shilingi trilioni 1.7. Gharama za ujenzi kwa kipande cha 3 na 4 ziliongezeka kwa kiasi cha dola milioni 1.3 na milioni 1.6 mtawalia.
ACT Wazalendo inapendekeza kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Kamati Teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa kina wa masuala haya matatu yaliyoibuliwa na CAG katika taarifa yake ya mwaka huu.
10. Bilioni 212 za UVIKO-19
Kufuatia athari mbaya kwenye uchumi zilizotokana na ugonjwa wa Uviko -19, Serikali ilikopa kiasi cha shilingi trilioni 1.24 kutoka IMF kwa ajili ya kukabiliana na athari hizo. Ripoti ya CAG imeibua hoja nyingi zinazoonyesha matumizi mabaya ya fedha hizo zilizopelekwa kwenye wizara mbalimbali za serikali upande wa Bara na hata Zanzibar. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika katika ubadhilifu wa fedha hizi.

HITIMISHO
Uchambuzi wa Ripoti ya CAG tulioufanya umeangalia maeneo 10 tu tuliyoyachagua kutokana na umuhimu wake. Hata hivyo hoja za ukaguzi katika ripoti nzima ni nyingi sana – nyingine mpya na nyingine zikiwa mwendeleleo wa makosa ya ya miaka ya nyuma, na ambazo nyingi zake pia hazijafanyia kazi yoyote ile.
Ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi kurekebisha makosa ya nyuma bila woga ili kuliokoa taifa na urathi (legacy) wa maamuzi ya ovyo yaliyowahi kufanywa huko nyuma? Tuonavyo sisi, mambo ni yaleyale, yakifanywa na watu walewale na bila shaka yoyote na chama kilekile.
Serikali ya Rais Samia ina mtihani mmoja tu, nao ni kusafisha urathi (legacy) wa maamuzi ya ovyo ya nyuma na kujenga mfumo madhubuti wa taasisi ambao utazuia ubadhirifu wa fedha za umma kwa faida kubwa ya uhai wa taifa, ili kuweza kufikia ndoto ya kuwa na taifa la wote kwa maslahi ya wote. Tunamsihi Rais achukue hatua hizo.

Ahsanteni Sana.


Kabwe Z. Zitto Ruyagwa
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
Aprili 10, 2023
Dar es Salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK