Mwaka wa misukosuko; chungu kwa wanyonge, raha kwa vibonge

Hotuba ya Waziri Mkuu Kivuli juu ya miezi 10 ya Kamati ya kuisimamia Serikali ya ACT Wazalendo;

Mwaka wa misukosuko; chungu kwa wanyonge, raha kwa vibonge

1. Utangulizi
Mnaelewa kuwa tupo katika siku za kumalizia mwaka, taasisi mbalimbali zinatumia fursa hii kuelezea, kujitathmini na kupanga mipango mipya kuelekea mwaka mpya. Mtakumbuka kuwa Mwezi Februari mwaka huu (2022) chama Chetu, ACT Wazalendo kiliunda chombo cha kuisimamia Serikali kilichoitwa Kamati ya kuisimamia Serikali ya wasemaji wa kisekta ambayo inafanana na Baraza la Mawaziri Kivuli. Tangu mwezi Februari 2022, Kamati hii imekuwa ikifanya kazi zake hivyo kimekuwa chombo mbadala wa Serikali kwa kumulika, kufuatilia, kukosoa na kuzalisha mapendekezo ya kimtazamo, kifikra na kisera juu ya maamuzi na utendaji wa Serikali na vyombo vyake tanzu.

Awali, tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kabisa kwa vyombo vya habari kwa mchango wenu wa kuzibeba hoja zetu na kuzifikisha kwa umma kwa kipindi chote cha miezi 10. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wasemaji wetu ambao wamefanyakazi bila kuchoka na kujitolea kwao kwa hali na mali ili kutekeleza majukumu tuliyopewa na chama. Kwa muda wa miezi 10 tumefanikiwa kutoa matamko rasmi (Oficial statements) ya kiuchambuzi yapatayo 95 na Mkutano na Waandishi wa habari 31 na ziara za wasemaji wa kisekta (Mawaziri Vivuli) saba (7); Ziara ya Waziri Mkuu Kivuli kwenye vyombo vya Habari; Ziara ya Mawaziri Vivuli wa Kilimo, Biashara na Nishati kwenye Mikoa ya Kusini, Ziara ya Waziri Kivuli wa Madini kutembelea Wachimbaji wadogo Geita; ziara ya Waziri Kivuli wa Biashara na Viwanda kutembelea ajali ya moto Soko la Karume; Ziara ya Waziri Kivuli wa Maji na Mazingira kufuatilia maendeleo ya Mradi wa visima vya maji Kimbiji na Kigamboni; Ziara ya Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Makazi katika kata ya Bunju na Wazo.

Mwisho tunawashukuru wadau wote ambao kwa namna moja au nyingine wamesaidia kufanikisha majukumu yetu.
Leo tarehe 28 Desemba 2022 tutaenda kuzungumzia mambo tuliyopigania, tuliyofanikiwa na hatua tutakazozichukua kwenye masuala yenye mwendelezo.


2. Hoja na mambo tuliyopigania kwa mwaka 2022
A: Mwenendo wa uchumi na hali ya maisha ya watu
Kilio cha wananchi tangu mwaka jana mwishoni (Mwezi Disemba, 2021) ni kuwepo kwa mfumuko wa bei za bidhaa muhimu jambo lililopelekea kupanda kwa gharama za maisha:
Mosi, tumeshuhudia kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa kutoka Shilingi 2,510, Shilingi 2,412 na 2,212; na kufikia 3310 kwa petroli, 3380 kwa diseli.
Pili, bidhaa za chakula kama vile maharage, mafuta ya kula, sukari, unga na mchele vimepanda zaidi ndani ya mwaka mmoja. Vilevile, kupaa kwa pembejeo za kilimo na mbolea, baada ya kupaza sauti na kutoa mapendekezo kwa Serikali kuweka ruzuku kidogo imeshuka.
Tatu, kupanda kwa vifaa vya ujenzi kama vile saruji, bati, nondo
Tatu, wakati tunashuhudia kupanda kwa gharama za maisha kwa upande mmoja, upande mwingine tunaona kutetereka kwa bei za mazao ya kilimo kama vile tumbaku na korosho.
Tatu, tulisimama kidete kuishauri Serikali katika kukabiliana na majanga ambayo yalikuwa na mchango wa kuathiri maisha ya watu. Ajali ya treni iliyotokea Tabora, ajali ya ndege iliyotokea Kagera, ajali ya moto uliojitokeza katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Pamoja na matukio yaliyofutana ya ajali za moto kwenye masoko ya wafanyabiashara wadogo. matukio ya kuungua kwa masoko yaliwashtua wengi, kwa namna matukio hayo yanavyojitokeza kwa kufuatana na muda wa ajali (usiku).
Hivyo, ACT Wazalendo tulitoa msimamo na mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuleta unafuu kwa wananchi. Tulitoa pendekezo la kupunguza tozo, ushuru na kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ambazo ni muhimu kwa maisha ya watu kama vile mafuta ya kula, sukari, ngano na mafuta ya petroli na diseli; na kuongeza uzalishaji wa chakula na mahitaji muhimu kwa nchi yetu huku Serikali kuongeza umakini wa kudhibiti soko holela la nje (usafirishaji wa chakula nje) kwa ajili ya kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa za chakula.
Licha ya hapa na pale Serikali ilitekeleza baadhi ya mapendekezo tuliyowahi kutoa japo sio kwa ufanisi na kwa usahihi kama vile ilitoa ruzuku ya mafuta na mbolea, kuondoa kodi kwenye mafuta ya kula na kupunguza tozo za miamala ya kieletroniki (Simu na Benki).
Mwenendo wa mfumuko wa bei (gharama za maisha) bado unazidi kupaa na hali ya maisha ya watu itakuwa mbaya zaidi mwaka 2023. Hivyo, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuweka mikakati ya kuhami maisha ya watu na kujiandaa kukabiliana na hali hiyo na kuwaandaa wananchi kuongeza uzalishaji na angalau kukidhi mahitaji ya ndani.

B: Miswada ya Sheria na kanuni zilizoenda BungeniKatika kuisimamia Serikali ipasavyo, ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Wasemaji wa kisekta ya kuisimamia Serikali tulifuatilia, kuchambua, kukosoa na kutoa mapendekezo yetu kuhusu miswada kadhaa iliyowasilishwa Bunge na Serikali;

i. Muswada wa Bima ya Afya kwa wote
Serikali iliwasilisha kwa mara ya kwanza Bungeni muswada wa Bima ya Afya kwa wote mwezi Septemba 2022, pamoja na nia njema ya Serikali ya kutaka kupanua wigo wa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kuingizwa kwenye mifumo ya bima, maudhui ya muswada huo yalikuwa na mapungufu mengi sana. Tatizo tuliloliona ni kuwa sehemu ya wananchi walio sekta isiyo rasmi wasingeweza kumudu gharama za bima hiyo kutokana na viwango vya juu vilivyowekwa. Pia kiuchambuzi na uhalisia muswada ulikuwa unaimarisha na kukuza madaraja ya kupata huduma bora kama ilivyo sasa, kwa wasio na uwezo na wenye uwezo.
Pia, mfumo wa uchangiaji kutokuwa na uhakika na endelevu, uliwekeza kwenye kutumia mabavu kwa kuzuia watu kupata huduma zingine kama njia ya kuwavutia wananchi kujiunga na Bima ya Afya.
Sisi, ACT Wazalendo kwa kutambua changamoto ya afya, hususani gharama za matibabu zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wengi. Kutokana na umaskini, wengine hawana kipato cha uhakika kinachoweza kuwahakikishia wanapokuwa na magonjwa kumudu gharama hizo, wachache sana (ambao ni watumishi wa Serikali na wengine kwenye Sekta binafsi rasmi) ndio wenyewe uhakika wa matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa au bima zingine.
Wananchi wengi wanatumia fedha kutoka mifukoni mwao wanapougua au kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHIF) ambao haukidhi matarajio kutokana na mapungufu mengi sana.
Sisi, tuliupinga Muswada ule kwa sababu ulikuwa hauendi kuondoa matatizo ya msingi kwenye upatikanaji wa huduma bora za afya kwa usawa na kwa uhakika. Muswada ungeenda kuwadumbukiza zaidi kwenye umaskini Watanzania maana ulikuwa na mapendekezo ya gharama za juu kwa kaya moja Shilingi 340, 000 kila mwaka.
Tuliwaeleza tatizo la afya ya Watanzania halitokani na kukosa matibabu tu bali ni mazingira hatarishi ya kazi, watu kukosa vipato vya kueleweka, masikini kuendelea kuwa maskini zaidi, wazee kutopatiwa mahitaji yao ya msingi, umaskini wa chakula na kipato.
Mfumo utakaoimarisha afya ya watanzania na kuwezesha kugharamia matibabu kwa watu wote nchini ndio jawabu la kuimarisha afya na kukabiliana na changamoto za gharama za matibau. Sisi tulipendekeza mfumo wa hifadhi ya jamii kwa watu wote ambao ndani yake ungetoa fao la bima ya afya watu wote.
Hatimaye Muswada uliondolewa rasmi Bungeni, tunatumai sasa kama wadau tutasikilizana ili kuboresha zaidi.
ii. Kanuni ya Kikotoo cha Mafao ya Uzeeni
Serikali ilirejesha kanuni ya mafao iliyopigiwa kelele mwaka 2019 na kuifanyia marekebisho madogo sana. Kiukweli, ACT Wazalendo tulipambana kuhakikisha kanuni hizo zisipitishwe na Bunge kwa kutoa mapendekezo mbadala kupitia Kamati hii ya wasemaji wa kisekta.
Uamuzi wa Serikali kutangaza Kanuni mpya uliweka kikotoo cha 1/580 badala ya 1540, pia malipo ya mkupuo ya mafao (kiinua mgongo) ya mtumishi aliyestaafu atalipwa kwa asilimia 33 badala ya 50% iliyokuwa inatumika kabla, umri wa kuhudumiwa mstaafu ni miaka 12.5 badala ya miaka 15.5.
Tulionyesha uchambuzi wa athari za kutumia kikotoo kipya chenye marekebisho madogo tu ya asilimia kutoka 25 hadi 33 na kuacha maeneo mengine kama yaliyovyo, namna yatakavyoenda kumpunja mstaafu. Kwa uchambuzi tulioufanya inaonyesha dhahiri kuwa;
 Kikotoo cha 1/580 kinaenda kupunguza mafao ya mtumishi aliyestaafu ya mwaka kwa asilimia 6.9

 Pia, kinapunguza malipo ya mkupuo (lumpsum) ya kiinua mgongo kwa asilimia 50.5 ukilinganisha na kanuni za awali.
 Vilevile, kinafupisha umri wa kuhudumiwa mstaafu kwa takribani miaka mitatu kutoka miaka 15.5 ya awali hadi 12.5
 Kwa kutumia ukokotozi wa wastani wa miaka mitatu ya mshahara wa juu badala ya kiwango cha mshahara wa mwisho kutashusha mafao ya wastaafu kwa asilimia 7.08
 Mwisho, kutakuwa na ongezeko kwenye posho ya kiinua mgongo ya kila mwezi kwa asilimia 24.7 lakini kwa kukokotolewa jumla ya mafao atakayepokea kwa miaka 12.5 yanaongezeka kwa asilimia 0.6 pekee kutokana na kufupishwa kwa miaka mitatu tofauti na awali.
Kutokana na matatizo ya kanuni za mafao tulizipinga kanuni hizi, kwa kuwa tunaamini Mfumo wa Hifadhi ya Jamii unapaswa kusaidia kulinda maisha ya watu na kutoa uhakika wa kuishi vizuri unapokutwa na majanga au kupoteza uwezo wa kufanya kazi kwa namna yoyote ile. Hatupaswi kuwaadhibu wazee wetu kwa kukubali kanuni kandamizi zinazoenda kuwapunja mafao yao na kufupisha muda wa kuwahudimia kwa kuwakadiria kifo mapema zaidi. Aidha, hatukukubaliana na uamuzi wa serikali kuwabebesha wastaafu mzigo wa gharama kwa makosa ya utendaji mbovu wa menejimeti za mifuko na madeni ya serikali.
Lakini Serikali haikutusikiliza iliendelea na kanuni zile na matokeo yake hata mwaka haujafika tunasikia kelele za wafanyakazi, juzi tu hapa tumewasikia Chama cha Walimu wanalipigia kelele. Sisi, tulitahadharisha na tunaendelea kuikumbusha Serikali muda upo wa kurekebisha makosa hayo.
iii. Muswada wa huduma za Habari
Muswada huu unaenda kuongeza kitanzi cha uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari. Tuliungana na wanahabari kupaza sauti kuhakikisha muswada huu unarekebishwa. Hii ni kazi ambayo tutaendelea nayo mwaka 2023.
iv. Utawala bora (kupigania Sheria za mageuzi ya kisiasa)
Kama nchi tulipitia wakati mgumu kidemokrasia kwa takribani miaka sita (6) ACT Wazalendo tuliamua kuongoza umma ili kuhakikisha kama taifa tunafanya mageuzi ya kidemokrasia na uendeshaji wa siasa zetu. Kwa muda wa miezi kumi, tumekuwa mstari wa mbele kupigania mageuzi ya Sheria ya Jeshi la Polisi ili kulifanya kuwa ni Jeshi linalotumia weledi, kujali wananchi badala Jeshi la mabavu dhidi ya raia. Tulifanya uchambuzi na kutoa mapendekezo yetu wakati wa uchambuzi wa bajeti, ili Serikali izingatie athari za kibajeti zitakazotokana na mchakato wa mageuzi ya Jeshi la Polisi.
Aidha, tulipiganaia mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi ili kuifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa huru kwa kuajiri wafanyakazi wake yenyewe na kusimamia chaguzi zote nchini ikiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Tunaendelea kushuhudia chaguzi ndogo zinazoendelea nchini (Bara na Zanzibar) zikiwa bado zimegubikwa na changamoto zile zile zilizotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Tangu ripoti ya kikosi kazi imekamilika hatuoni hatua za utekelezaji, ni rai yetu kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inashughulikia masuala ya sera na sheria za kiuchaguzi kuanza kufanyia kazi mapendekezo ya taarifa ya kikosi kazi
Hivyo basi, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali itoe ratiba ya utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi hatua kwa hatua ili itakapofika mwezi April mwakani (2023) miswada ya Sheria mpya ya vyama vya Siasa, Sheria mpya ya uchaguzi na marekebisho ya Sheria ya mchakato wa Katiba mpya iwe imesomwa kwa mara ya kwanza Bungeni.

C: Hatua, kauli na maamuzi ya Serikali
Eneo jingine ambalo Kamati ya kuisimamia Serikali ya ACT Wazalendo imeifanyia kazi kwa ufanisi ni kumulika hatua, kauli na maamuzi ya Serikali ambayo kwa namna moja ama nyingine zinaathiri mielekeo ya kijamii na nchi kwa ujumla.
Baadhi ya mambo tuliyoyasimamia ni pamoja na kupinga uamuzi wa Serikali kuwaondoa kwa nguvu na vitisho wananchi jamii ya wafugaji katika maeneo ya Loliondo na Ngorongoro ili kulinda haki na usalama wa umiliki wa ardhi kwa wazalishaji wadogo wadogo nchini. Tumepaza sauti na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na migogoro ya ardhi nchini; mathalani shinikizo la kufuta vijiji 25 katika wilaya ya Mbaralali.
Aidha katika migogoro ya ardhi tumeshuhudia vilio vya wananchi kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji kwenye maeneo ambayo hayajawahi kuwa na mivutano hiyo hususani Mikoa ya Kusini. Tulitahadharisha hali ya mapigano ya wakulima na wafugaji yanahatarisha amani ya nchi yetu. Migogoro hii ni bomu litakalo lipuka siku za usoni. Serikali ilipe uzito unaostahiki suala hili ikiwemo kuwa na Wakuu wa Wilaya wenye uwezo mkubwa wa kutatua migogoro kwa njia ya amani badala ya watumiaji wa nguvu za dola.
Lakini kauli na hatua zinazochukua na Serikali hivi sasa zinaweza kuongeza tatizo zaidi. Hivyo, rai yetu viongozi wawekeze nguvu kwenye kuleta mshikamano kwa kusimamia mipango shirikishi ya ardhi, kushughulikia watendaji na viongozi wote wanaopokea rushwa, kutoza fidia za uwongo ili kupora haki za wakulima; na Jeshi la Polisi lisimamiwe vya kutosha kushughulikia matukio ya kihalifu na uhujumu wa mali za wakulima
Vilevile, tulisimama kupigania mchakato wa ukodishwaji wa kitengo cha makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuitaka Serikali kutoipatia tena mikataba Kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena (TICTS). Hatimaye, mwezi huu Serikali imetangaza kutoipatia tena mikataba TICTS kwa kushindwa kufanya kazi.

D: Hoja kuhusu Bajeti ya Serikali Kuu na Ripoti za Mkaguzi Mkuu (CAG)
Kuiachilia utamaduni wetu wa kuchambua Bajeti ya Serikali Kuu mwaka huu kupitia Kamati ya Kuisimamia Serikali ya ACT Wazalendo. Tulifanya uchambuzi wa Bajeti za kila Wizara na kutoa hoja mbalimbali. Kwa ufupi baadhi ya hoja ni kuwa;
 Serikali ijielekeze kubuni vyanzo vingine vya mapato (non-tax revenue) vitakavyosaidia kugharamia Bajeti ya Serikali kuliko kuongeza tozo na ushuru kwa wananchi wanyonge. (Iondoe tozo mpya za miamla ya Simu na Benki, kupunguza tozo kwenye bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kula, petroli, Diseli, ngano na sukari pamoja na Mbolea ili kukabiliana na mfumuko wa bei).
 Serikali ipunguze uwiano wa mikopo ya kibiashara kwa deni la Serikali mpaka kufikia asilimia 20 ya deni lote.
 Kukua kwa gharama za kuhudumia Deni la Serikali hadi kufikia 22% ya Bajeti ya Serikali kutahatarisha na kudumaza uboreshaji wa huduma kwa wananchi.
 Kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma
 Fedha za ushuru wa kuuza korosho nje (Export Levy) zirudishwe kwa wakulima
 Serikali isimamie mgao wa fedha za Muungano kwa usawa na kwa mujibu wa kanuni.
 Waajiriwa wenye kima cha chini cha Mshahara (chini ya 420,000) wasitozwe kodi ya PAYE
 Kutunga sheria ya kurejesha utaratibu wa makato ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu wa asilimia 8 iliyokuwepo awali.
Kwa upande wa hoja zetu kutokana na uchambuzi wa ripoti ya CAG baadhi yake ambazo zinaendana na Mwenendo wa Bajeti ni; Serikali kutolipa madeni ya ndani ya wazabuni kwa wakati zinazorotesha uchumi wa nchi. Kutoshughulikiwa kwa hoja za ubadhirifu wa fedha za umma Serikali inawabebesha mzigo mzito wananchi wa madeni. Madai na madeni ya Mashirika ya umma yalipwe kwa mkupuo. Hali mbaya ya kifedha ya Mashirika ya PSSSF na NSSF ni mzigo kwa wafanyakazi na wastaafu.
Kwa sehemu kubwa hoja tulizozitoa Serikali haijazifanyia kazi ndio maana hali yetu kama nchi bado tunachechemea.

E: Mambo ya Nje
Tuliungana na wanajumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha Mradi wa bomba la Mafuta ghafi la Uganda na Tanzania unaendelea kwa kupinga na kulaani uamuzi wa Bunge la Ulaya la kushinikiza Serikali hizi mbili kusitisha.
Pia, kuitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingilia kati na kuchukua hatua za utatuzi wa amani mzozo wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mwisho, kuunga mkono watu wa Sahara Magharibi katika mapambano yao ya kujikomboa kwa kupinga kauli za Rais mpya wa Kenya Ndg. William Ruto kutaka kusitisha uwakilishi wa Saharawi katika nchi ya Kenya.

Hitimisho;
Ndani ya mwaka mmoja wa utendaji wa Baraza Kivuli, tumefanikiwa kuwa sauti ya kutetea haki na maslahi ya Wananchi; tumeweza kuzuia muswada mbovu wa Bima ya afya kwa wote, kuishinikiza Serikali kutoa ruzuku kwenye Petroli na Diseli, tulipigania Serikali kutoa ruzuku kwenye pembejeo (mbolea) ili iweze kushuka bei, tulipagania kuondolewa kwa tozo za miamala ya simu na tozo mpya miamala ya kibenki (ingawa Serikali ilipunguza tu).
Lakini kwa tathmini yetu bado hatua zilizochukuliwa na Serikali zinaweza kusema zimetoa maumivu makubwa kwa walalahoi wa nchi hii. Ni muhimu kwa Serikali kuongoza nchi kwa maslahi ya wote, bila kuacha kundi fulani nyuma kwa maslahi ya kundi jingine.

Ndg. Doroth Jonas Semu
Waziri Mkuu Kivuli
ACT Wazalendo
28 Desemba 2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK