Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Malawi uchaguzi ulipangwa kurejewa upya, na vyama vya upinzani viliunganisha nguvu pamoja na kuunda Muungano ulioitwa 'Tonse' kukabiliana na mkakati wa 'wagawe uwatawale' uliokuwa ukitumika na serikali ya chama tawala.
Wakati uchaguzi mkuu wa Tanzania ukiwa mbioni kufanyika hapo baadaye mwezi Oktoba, upinzani nchini Malawi inatupatia somo lililo bayana. Kwamba, serikali dhalimu na za kiimla zinaweza kuangushwa vibaya pale upinzani unapounganisha nguvu huku vikishirikiana na asasi hai za kiraia zinazosimamia maslahi ya wananchi.
Hili ni jambo la muhimu sana kwa Watanzania katika kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.
Ushindi wa Ndg. Chakwera wa kiti cha urais ni fursa muhimu na adhimu kwa demokrasia ya bara zima la Afrika.
Wakishirikiana vizuri katika muungano wao wa 'Tonse' wameweza kutuma ujumbe mzito kuhusu mapambano ya haki na uhuru na ni jukumu letu wengine kuchukua na kufuata mfano huo wa Malawi ili kuleta mabadiliko katika uongozi wenye kufuata misingi ya Uhuru na Katiba hapo mwezi Oktoba.