Taarifa za uhakika ndani ya wiki iliyopita zinaonesha tofauti kabisa na kile anachokisema Rais Magufuli. Maambukizi na vifo vinaonekana kuongezeka kwa kiwango kikubwa mno.
Jana, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alifunga mpaka wa nchi yake na Tanzania ikiwa ni hatua ya kuzuia ongezeko la maambukizi. Hatua hiyo ilifuatiwa na serikali ya Zambia iliyofunga mpaka wake wiki iliyopita. Nchi zote hizi mbili, zinatoa ujumbe kuwa zimeona kitisho cha ongezeko la maambukizi ya COVID-19 kutoka Tanzania.
Taarifa za kina kuhusiana na ugonjwa wa COVID-19 zinahitajika kabla wananchi hawajaunga mkono hatua ya kufunguliwa kwa shule na kuendele kwa shughuli za michezo. Watu wetu hawastahili kutumbukizwa katika lindi kubwa la maambukizo kutokana na uzembe wa serikali. Uwazi usio na shaka unahitajika kila siku iendayo kwa Mungu. Rais Magufuli anapaswa kutoka huko Chato alikojificha na kuja kuongoza Serikali katika kutoa taarifa na takwimu za kila siku juu ya COVID-19. Atueleze mara kwa mara juu ya mipango ya kiuchumi, afya na elimu inayochukuliwa na serikali yake katika janga linalotukabili.
Tungeweza kukubaliana na hoja ya kufunguliwa shule watoto wetu waendelee na masomo, michezo na ligi ziendelee, na watalii waendelee kuingia, lakini tunahitaji kuwa na hakika kuwa mazingira ni salama kiasi cha kutosha kuyaruhusu hayo. Rais Magufuli hawezi kuishia kusema tu kwamba "Tanzania ni salama". Tunahitaji uthibitisho. Tunahitaji pia kufahamu mipango iliyopo ya kuendelea kupima na kufuatilia wenye dalili na maambukizi, na jitihada za serikali kwa jamii kuishi na mazoea mapya ya kuachiana nafasi kati ya mtu na mtu.
Chama chetu kinakubaliana na Rais Magufuli kuwa tunapaswa kushirikiana na majirani zetu katika mapambano haya. Lakini kwa kauli yake kwa jambo hili, anapaswa kueleza kwa nini hakuhudhuria kikao cha hivi karibuni cha SADC, chombo anachokiongoza kama Mwenyekiti. Vile vile kwa nini hakuungana na wenzake katika kikao cha wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.
Tunatarajia tutapata maelezo kuhusiana na haya. Vilevile, juu ya hatua anazochukua kuwasiliana na Viongozi wenzake wakuu wa nchi, kuhakikisha Tanzania inakwenda bega kwa bega na ndugu zetu wa nchi zinazotuzunguka.
Kwa sasa, hapana budi kuweka mbele UWAZI. Rais Magufuli anapaswa kubeba dhima kuu ya uongozi. Hilo ni deni kubwa analodaiwa na Watanzania.