Rais Magufuli, UMETUFUNZA. Zitto Kabwe

Kwa Heri John Magufuli, Buriani Tingatinga

Zitto Kabwe
26 Machi, 2021.

Imenichukua karibu wiki nzima kuandika, japo kidogo, kukuaga Rais Magufuli. Unajua kwanini ninapata ugumu kuandika japo napenda sana kuandika tanzia kiasi huwa nawaza nani ataandika tanzia yangu na ataandika nini.

Lakini pia imenichukua uzito kuandika kwa sababu ya kuchoka. Kuchoka sababu ya vifo vingi sana.

Tangu mwaka umeanza vifo vimekuwa vingi sana. Wazee wetu wengi wametangulia mbele ya haki. Mwenyekiti wangu wa Chama Maalim Seif Sharif Hamad alitangulia mbele ya haki mwezi mmoja tu kabla yako kutokana na maradhi ya Korona. Tofauti na viongozi wengine, Maalim aliweka wazi maradhi yake na sisi kama chama tulitangaza hadharani hilo ili Watanzania wachukue tahadhari.

Watu ambao nilikuwa nawaona kama Wazee wangu, Walimu wangu na Washauri wangu kama Prof. Benno Ndulu walitangulia mbele ya haki wiki chache kabla yako. Nawe pia ulipoteza mtu wako wa karibu katika kazi, Balozi John Kijazi mwezi mmoja kabla ya umauti kukufika. Hakika robo ya kwanza ya mwaka 2021 imekuwa mtihani mkubwa kwa nchi yetu. Tumepoteza watu wengi sana, na wengi kutokana na ugonjwa wa COVID-19 yaani Korona.

Nimepata nguvu leo kukuaga Rais kwa sababu licha ya machungu mengi moyoni mwangu nina kumbukumbu nzuri nawe. Nilipopata ajali wakati wa kampeni ulikuwa tayari kutoa kila msaada ili niweze kupona. Ulinipa faraja nikiwa hospitalini Maweni Kigoma na pia Aghakan Dar es Salaam kwa kunipigia simu mara kwa mara kunijulia hali. Ninaamini ulikuwa unaniombea kupona ili kuendelea na kazi zangu ambazo kubwa hasa ni kukukosoa kisera. Hukupenda kukosolewa, lakini pia naamini ulikuwa umeshazoea kupopolewa nasi. Wakati mwingine uliamini nakuchukukia binafsi. Wasaidizi wako walikuwa wanasema. Hapana. Sikukuchukia. Sikukubaliana tu na namna yako ya kuendesha nchi yetu.

Rais, mara kadhaa niliamua kukushauri ama hadharani au faragha kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yetu. Mara nyingi hukuchukua ushauri huo. Haikuwa lazima uchukue ushauri wangu kwani wewe ulikuwa na taarifa nyingi zaidi kuliko Mtanzania mwingine yeyote. Mara chache ulipochukua ushauri nilifarijika. Kwa mfano ulipokwenda Benki Kuu na kuamua kurejesha akaunti ya madeni Benki Kuu nilikupigia simu kukueleza sio sawa. Utarudisha EPA. Ulinisikiliza kwa makini na siku ya pili ukamwita Gavana Ndulu kubadilisha maamuzi yako. Nilifarijika sana kwani uamuzi wako ulikuwa unairudisha nchi yetu nyuma katika masuala ya usimamizi wa Fedha za Umma.

Rais, umetufunza mengi katika muda ambao umeongoza nchi yetu. Umetufunza uthubutu wa kufanya maamuzi. Umetufunza ujasiri wa kusimamia unachoamini. Hata hivyo umetufunza umuhimu wa Taasisi katika Jamhuri yetu. Miaka sita ya uongozi wako imetuonyesha kuwa mtu mmoja anaweza kufanya lolote atakalo bila kujali lolote. Hili funzo ni lazima tulifanyie kazi ili akitokea kiongozi mwingine kama wewe asiweze kufanya atakalo. Mara kadhaa ulichukua maamuzi ya kuvunja Katiba yetu. Nilipoamua kwenda Mahakamani kukupinga kumwondoa kazini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kukushinda katika hatua za awali kwa Mahakama kutoa Uamuzi kuwa Rais anaweza kushtakiwa, ukapeleka sheria Bungeni kuwanyima haki Watanzania kukushtaki.
Hii haipaswi kutokea tena Tanzania. Umetufunza.

Rais, ulichukua uongozi wa nchi yetu demokrasia ikiwa imeshamiri. Demokrasia ndani ya Vyama vya Siasa na miongoni mwa vyama vya siasa. Hata ndani ya chama chako kulikuwa na demokrasia kubwa. Miaka sita ya uongozi wako hakuna aliyekuwa anaweza kusimama kukupinga ndani ya chama chako. Uliteua unayemtaka hata kama hana historia ya Chama chako. Kwa sisi wa Upinzani ulihakikisha tunasagwa. Ulitumia Polisi na Mahakama na baadaye Tume ya Uchaguzi kurudisha nchi kwenye mfumo wa Chama kimoja. Uliona Demokrasia ni kero kwako. Hili pia ni funzo kubwa. Kwamba tunapaswa kujenga vyama vyetu kuwa imara kuzuia mambo kama haya kutokea tena. Uhuru haupatikani kwenye kisahani cha fedha, Mwalimu Nyerere alipata kusema. Umetupa funzo kubwa.

Rais, dhamira yako kwa Tanzania siwezi kuishuku. Sikuwahi kuwa na mashaka na mapenzi yako kwa nchi yetu. Ulitaka Tanzania ipige hatua kubwa za maendeleo japo tulitofautiana kuhusu dhana ya maendeleo ni nini haswa. Kwako wewe miradi mikubwa mikubwa ya Umeme, Madaraja, Reli, Madege, majengo ya vituo vya afya na kadhalika ndio ilikuwa tafsiri ya Maendeleo. Hakika ulijitahidi kujenga nchi. Kila mtu anakupongeza kwa hilo.
Lakini Rais, hukujitahidi kujenga Taifa. Watakaofuata baada yako hawana budi kujielekeza kujenga Taifa hata kama ni muhimu kumalizia miradi yako ya kujenga Nchi. Bila Taifa lenye watu waliostaarabika, wenye upeo na ujuzi, nchi haiwezi kudumu. Msingi wa Nchi ni Taifa. Miaka sita ya wewe kujenga Nchi lazima ifuatwe na miaka zaidi ya kumi na sita ya kujenga Taifa. Taifa ni Watu na Tunu zake.

Tingatinga, John Pombe Magufuli, hatukukubaliana kwenye mambo mengi. Ni kawaida ya wanadamu kutokubaliana. Ni kawaida katika demokrasia kupingana kwa mawazo. Miaka sita ya Uongozi wako kuna mambo yalitokea Tanzania nisingependa kuyaona yakitokea tena. Watu kupotea hovyo, Wabunge kupigwa risasi hadharani na kutofanyika uchunguzi wowote, kuvunja vunja misingi ya Utumishi wa Umma kwa kuteua wanasiasa katika madaraka ya Utumishi wa Umma, kuvuruga Uchaguzi na kuwanyima haki wananchi kuchagua viongozi wanaowataka, raia kunyang'anywa pasipoti zao za kusafiria, watu wasio na hatia kubambikiwa kesi na kukaa gerezani miezi mingi kama sio miaka na hali ya watu kuishi kwa hofu. Kwa kuwa naamini haya yote hayatatokea tena Tanzania baada yako, nimekusamehe duniani na akhera, Fi Dunia, Wal’Akhera!

Rais John Pombe Magufuli, wakati tunakuhifadhi leo katika nyumba yako ya milele kijijini kwako Chato Mkoani Geita, ninakuombea kwa Mungu ailaze roho yako mahala pema. Mungu akupunguzie adhabu ya kaburi. Mungu akusamehe dhambi zako zote. Pumzika kwa Amani.

Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama (Party Leader) cha ACT Wazalendo.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK